 |
| Mama mzazi wa binti muathirika wa ukeketaji akifafanua |
Mama mzazi wa binti muathirika wa ukeketaji akifafanua jambo huku akisikilizwa na binti yake.
Kuna mambo mengi anakumbukia msichana mwenye umri wa
miaka 12 yamemtokea maishani. Lakini tukio la siku hiyo, kuitwa na
mama yake mdogo, kisha kukamatwa kwa nguvu na kukeketwa linabaki kuwa
kovu lisilopona katika maisha yake. Ni ukatili uliopitiliza uliobadili
kabisa ndoto za maisha yake za kupata elimu.
Binti wa miaka 12 (jina linahifadhiwa) ni mtoto wa mwisho wa kike kati
ya watoto nane wa mzee Isaya na Mama Gyar Baa kutoka familia moja ya
kabila la Kimbulu.
Kabla hajakumbwa na mkasa uliobadilisha kabisa welekeo wa maisha yake,
alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne mwenye ndoto za kusoma hadi kufikia
ukomo wa maisha yake.
Hata hivyo, ndoto hizo zilizimwa baada ya kujikuta akilazimishwa
kukeketwa ikiwa ni ishara ya maandalizi ya kutafutiwa mume ili
aolewe.Tukio hilo la kikatili liliathiri maisha yake.
Makazi ya familia ya binti huyo ni katika kijiji cha Konje wilaya ya
Handeni mkoani Tanga, kilichopo umbali wa kilometa 16 kutoka Handeni
mjini.
Msichana huyo, anatoka katika familia ya wafugaji, yenye tabia ya
kuhamahama ili kufuata malisho, hasa nyakati za ukame ili kuhakikisha
kuwa mifugo yao haikosi chakula na maji.
Akisimulia kwa uchungu mkasa alioupata uliobadili kabisa uwelekeo wa
maisha yake, msichana huyo anasema siku hiyo ya Jumanne (hakumbuki
tarehe) aliitwa na mama yake mdogo (mama wa kambo). Aliitika na kutii
amri kwa kwenda kusikiliza alichoitiwa akiwa hana fununu kabisa ya
dhamira ya muitaji.
Anasema baada ya kufika nyumbani kwa mama yake huyo, alishangazwa
kumkuta dada yake anayemfuata (jina linahifadhiwa) akiwa amefungwa
mikono na miguu huku akilia kwa uchungu sana. Kilichomsikitisha zaidi ni
kuona jinsi ambavyo dada yake alikuwa akivuja damu nyingi katika sehemu
zake za siri.
Jambo hilo, lilimtisha sana Tansiana na kutokana na hamaki akapata wazo
na maamuzi ya haraka ya kukimbia kutoka nyumbani kwa mama yake mdogo
ili kujinusuru na hatari aliyoona kuwa inamkabili. Hata hivyo,
hakufanikiwa kutimiza matakwa yake.
“Nilishtuka sana, kumuona dada akilia huku damu zinamtoka kwa wingi
sana katika sehemu zake za siri. Lakini nilivyotaka kukimbia mama mdogo
na bibi yule niliyemkuta pale nyumbani ambaye sikufahamu ametokea wapi
wakanikamata na kunifunga mikono na miguu kwa kamba,” anasimulia
msichana huyo kwa masikitiko.
Baada ya kufungwa na kudhibitiwa kikamilifu ndipo bibi huyo asiyemfahamu
akachukua kiwembe na kumkata kwenye sehemu yake ya siri kwa namna
alivyojiridhisha na kusababisha atokwe damu nyingi kama ilivyokuwa kwa
dada yake.
“Wakati wananikata sikusikia maumivu sana kwa sababu nilikuwa na hasira
sana kwa kile kitendo nilichokiona amefanyiwa dada yangu…ndipo baada
ya kupita muda kama kama saa moja hivi nikaanza kusikia maumivu makali
sana kama roho inataka kutoka. Ndipo nikatambua namna gani watu wale
walivyo wakali. Nilikuwa nimefanyiwa unyama wa hali ya juu bila ya
ridhaa yangu. Nililia sana na kwa hakika nimemchukia sana huyo mama
mdogo na sijui kama nitamsamehe,” anasema.
Akikumbukia zaidi anasema kuwa “wakati wananifanyia unyama huo, mama
yangu mzazi alikuwa amesafiri kwenda Karatu na baba hakuwapo nyumbani.
Aliporudi alikuta tayari tumekeketwa.”
Anabainisha kwamba, ilimchukua takriban mwezi mmoja kuuguza kidonda
hicho hadi kupona. Aina ya matibabu aliyokuwa akipewa anasema kuwa, ni
kupakwa maziwa na mafuta ya taa mara mbili kwa siku.Yaani asubuhi na
jioni kama dawa ya kuponyesha jeraha hilo. Alipata msongo mkali wa
mawazo kuhusu tukio hilo baya kabisa na la ukatili wa kupindukia.
Baba yake, licha ya kutabua unyama waliofanyiwa, lakini hakuchukua hatua zozote dhidi ya wahalifu wale.
Anasema kuwa, miongoni mwa sababu walizoelezwa zilizolazimisha
wachukuliwe hatua hiyo kukeketwa ni watoto wa kike kuwafanya waachane na
vitendo vya uhuni kwa kile kinachodaiwa kuwa, wasipokeketwa wanakuwa na
tamaa kali ya kufanya mapenzi muda wote.
Hii ni kutokana na mila na desturi za kabila lao, kwamba iwapo binti
hatakeketwa, basi ni dhahiri kwamba hatapata mume wa kumuoa na hatakuwa
na heshima wala thamani anayostahili kupewa mwanamke kwenye jamii hiyo.
Kutokana na kitendo hicho, anasema kuwa ni dhahiri kwamba ameandaliwa
kwa ajili ya kuolewa, hata kama jambo hilo litafanyika litakuwa ni
kinyume cha ridhaa yake.
“Najua sasa hivi nasubiri tu kuolewa. Lakini ni kwamba watanilazimisha
tu lakini mimi mwenyewe sipendi…napenda sana kusoma… natamani sana
ajitokeze mtu wa kunisaidia katika hilo. Nipo tayari kabisa kwa hilo…na
baada ya kusoma cha kwanza nitakachofanya ni kuhakikisha nazuia mila hii
mbaya isiendelee kufanyika kwa wasichana wengine wa jamii hii. Kwa
kweli inauma sana…tunateseka sana jamani,” anasema msichana huyo huku
akibubujikwa machozi.
Msishana huyo, licha ya hatua ngumu ya maisha yake aliyopitia, lakini
ana matumaini kuwa, siku moja atakuwa mwanaharakati wa kutetea haki za
wanawake, na kupiga vita mila na desturi ambazo zimekuwa zikitumika
kumgandamiza mwanamke.
Aina hiyo ya maisha, ndiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kumfanya
msichana huyo kuwa miongoni mwa wale waliokosa fursa ya kupata haki yake
ya msingi hasa elimu. Alikuwa na ndoto za siku moja kupata elimu ili
uwe mwanga wa uhakika kwa maisha yake na jamii yake inayomzunguka.
Pamoja na kukabiliwa na changamoto hiyo maishani, lakini binti huyo
katika familia yake ana msimamo wa kupenda elimu na kujituma kwa kazi za
kifamilia na kwamba iwapo atatokea mfadhili yoyote atakayekuwa tayari
kumchukua na kwenda kumsomesha hata wazazi wake sasa wameutambua ukweli
huo na kuwa tayari kumruhusu aende akapate elimu.
“Kamwe sitasahau unyama huu…nikipata elimu lazima niwe mwanaharakati wa kupinga unyama huu ,” anasema.
Mama mzazi wa binti huyo aitwaye Gyar Baa Isaya anasema kuwa wakati
binti yake anakeketwa, alikuwa safarini na hakushirikishwa na mumewe
kuhusu kufanyika kwa kitendo hicho.
Kimsingi anasema, alikuwa anafahamu kuwa siku moja binti yake
atalazimika kufanyiwa mila hiyo kwa sababu ni utamaduni ambao hata yeye
ameupitia na hakuwa na mamlaka ya kuupinga, kwani kwa kufanya hivyo,
angeweza kumsababishia matatizo mtoto wake ikiwamo kutoolewa.
“Kusema kweli kwa mila za kwetu ili uonekane ni mwanamke ambaye
umekamilika ni lazima ukeketwe…vinginevyo hupati mume na unaweza kupatwa
na majanga makubwa ikiwamo binti kuanza tabia mbaya kabla ya wakati
wake…sasa watoto wangu wamelazimika kufanyiwa mila hiyo ingawa
hawakuridhika nayo kabisa,” anasema mama huyo.
Naye dada wa msichana huyo aliyeanza kufanyiwa ukatili huo, anasema
kuwa sababu kubwa ya mdogo wake kushindwa kuendelea na masomo licha ya
kuwa na ndoto za kufika mbali kimaisha ni ile hofu ya kuchekwa na
wenzake hasa wakati wa kuoga wakimuona amekeketwa.
“Unajua mnapokuwa rika moja mnakuwa hamuoneani aibu kabisa, hata kama
kuoga mtaenda wote, sasa wenzako wakikuona uko tofauti na wao kimaumbile
wanakushangaa na wengine wanakucheka. Hali hii nilipokuwa nikimwelezea
mdogo wangu ilichangia kumkatisha tamaa ya kusoma kwa hofu ya kuchekwa,”
anasema dada huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule
moja.
Hata hivyo anasema, kitendo walichofanyiwa kinadhihirisha udhalilishaji
kwa mtoto wa kike na kwamba licha ya baba yao kuwa ni miongoni mwa
wafugaji wenye tabia ya kuhamahama, lakini amedhamiria kuhakikisha kuwa
anamaliza masomo yake.
“Baba yetu ni miongoni mwa wafugaji wenye tabia ya kuhamahama makazi,
hali hii imetuathiri sana kielimu tena mimi ni nafuu kwa sababu naishi
kwenye hosteli za shule. Mdogo wangu ndiyo amerudi nyuma kwani hadi sasa
hasomi na aliishia darasa la nne,” anasema dada huyo.