Walimu 35,411 nchini wataajiriwa katika shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Watakaokaidi kwenda kuripoti katika mikoa ya pembezoni, hawataajiriwa na serikali.
Hatua hiyo imeelezwa kwamba imetokana na serikali kupokea maombi
mengi ya kazi kwa walimu, ambao mwaka jana hawakuripoti katika vituo
walivyopangiwa pembezoni mwa miji kwa kutegemea kuajiriwa na shule
binafsi, lakini hawakufanikiwa.
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
Selemani Jaffo alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) aliyetaka kufahamu serikali
inafanya nini kwa walimu waliopangiwa kwenda mikoa ya pembezoni, ikiwemo
Lindi na kwingineko, lakini hawakuripoti.
Jaffo alisema ni kweli kuna walimu wengi ambao hawakuripoti katika
mikoa ya pembezoni. Alisema si Lindi peke yake, bali na mikoa mingine,
ikiwemo Katavi na Kigoma.
Alisema kwa mwaka huu, wataajiri walimu 35,411, lakini ambaye
hataripoti katika mikoa hiyo na kuishia mijini tu, hawataajiriwa tena
serikalini, kama wanavyoomba tena baada ya kukosa katika shule binafsi