Chama
Cha Walimu Tanzania (CWT) kimeipa serikali siku 60 za kukamilimisha
madeni ya mishahara ya walimu ya Sh. bilioni 48 pamoja na kukamilisha
majadiliano ya mishahara ya walimu na chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa CWT,
Gratian Mukoba, wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu maazimio ya mkutano
mkuu wa Taifa wa walimu nchini uliofanyika mkoani Arusha Oktoba 28-29,
mwaka huu.
Mukoba alisema hatua hiyo ilifikiwa na chama hicho baada ya serikali
kukaa kimya kwa muda mrefu bila kutekeleza ahadi walizokiahidi chama
hicho juu ya madai ya walimu ya muda mrefu.
Alisema chama hicho kinaidai serikali zaidi ya Sh. bilioni 48, ambazo
serikali ili ahidi kuzilipa Septemba mwaka huu, lakini hawakufanya
hivyo badala yake ikasema inafanya uhakiki kwanza wa madai hayo ili
kukamilisha malipo hayo ambayo mpaka sasa hayajafanyika.
“Tuliendelea kukaa kimya tukisubiri serikali ikamilishe uhakiki wake
na kutoa taarifa ya madai ambayo walimu wanaidai, lakini bado haikufanya
hivyo, kwa hiyo na sisi baada ya kukaa kikao chetu cha walimu Taifa
tukaweka maazimio haya,” alisema Mukoba.
Alisema wanatarajia kukabidhi barua ya notisi kwa Katibu Mkuu
Kiongozi leo na hatua za kisheria zitafuata endapo serikali haitatimiza
hayo ambayo wameyaorodhesha baada ya siku 60 kumalizika.
Alisema, maazimio mengine waliyoyaandika kwenye barua hiyo ya notisi
ni serikali iwe imebadilisha muundo wa walimu na wakaguzi ndani ya siku
hizo 60.
Azimio lingine waliitaka
serikali kukamilisha majadiliano na chama cha walimu kuhusu mishahara ya
walimu ya mwaka ujao kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.
“Haya yote na mengine ambayo sijakuainishia tunayataka yatekelezwe na
serikali ndani ya siku hizi 60 tulizotoa na endapo serikali itaendelea
kukaidi basi hatua zaidi za kisheria zitafuata na tutatoa msimamo wa
chama kuwa nini kitafanyika,” alisema Mukoba.
NIPASHE lilimtafuta Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, jana ili kuzungumzia suala
hilo, lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.Hata Naibu Waziri,
Philip Mulugo, alipotafutwa simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.
ippmedia.com