Walimu wa kike wa shule za msingi wilayani Ruangwa mkoani Lindi,
wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wa kike kutokana na wanafunzi hao
kuwachukulia waume zao kama kulipiza kisasi kwa adhabu wanayopewa na
walimu wao.
Kadhalika walimu wa kiume wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wakiume kwa hofu ya kuchomewa nyumba zao moto.
Mwalimu wa kike ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema
aliwahi kutoa adhabu kwa mwanafunzi wa darasa la tano ambaye
alimchukulia mumewe wa ndoa ili kumkomesha.
Alisema alimuonya mwanafunzi huyo bila mafanikio na kuamua kwenda kwa
Afisa wa Ustawi wa Jamii ambaye alisaidia kunusuru ndoa yake.
Alisema kutokana na hali hiyo walimu wote wa kike wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wa kike.
Utafiti wa kihabari uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania
(Tamwa), kuhusu ukatili, unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na
watoto, katika Wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi, umebaini kuwepo kwa hali
hiyo.
Chama hicho kinafanya utafiti wa kihabari katika wilaya kumi za Tanzania Bara na Zanzibar.
Akiongea na NIPASHE, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkata kata ya
Nandagala, Wilaya ya Ruangwa, Ismail Chikandanda, alisema kuna uadui
mkubwa kati ya walimu na wazazi kutokana na kutokupenda watoto wao
kupewa adhabu.
Chikandanda, alisema katika tukio moja wanafunzi walipigana, mwalimu
alimchapa mtoto aliyeanzisha ugomvi lakini baada ya kipindi mwanafunzi
alitoka darasani na kwenda kumuita bibi yake ambaye aliita wanakijiji
wakiwa na silaha kumtafuta mwalimu aliyemwadhibu mwanafunzi huyo.
Mwalimu wa kiume ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema
nyumba ilichomwa moto na wanakijiji baada ya kumwadhibu mwanafunzi wa
kiume.
Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya Msingi Ruangwa, Sharifa Hassan,
alisema kuwa tatizo kubwa linalowafanya wanafunzi kuwa na tabia mbaya
ni kutokana na ngoma za jando na unyago wanazochezwa na kujiona wako
sawa na wakubwa.
Afisa Elimu Kilimo na Ufugaji wa Wilaya ya Ruangwa Yussuf Chilumba,
alisema tatizo kubwa ni wazazi kutokuwa na mwamko wa elimu, kwani hata
wazazi wao hawakusoma hali inayowafanya kushindwa kusimamia maendeleo
yao ya elimu,
“Wazazi wanawaomba wanafunzi wao wasifanye mtihani vizuri ili wasifaulu
kwani watawapa shida ya kuwasomesha,” alisema Diwani wa kata ya
Nandagala, Wilaya ya Ruangwa, Adrew Chikongwe, alisema kuwa ugomvi kati
ya wazazi na walimu ameumaliza na kuanzia wakati huu kutakuwa na amani
na hali ya elimu itaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na kuwahimiza walimu
kuwafundisha kwa bidii watoto.
chanzo.Ipp media
harakati za marafiki wa elimu musoma wasiliana nasi kwa namba +255755 650 075 au +255786 650 075 ni jukumu letu kuboresha elimu
HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni