Tumeghadhabishwa na hatua ya Serikali ya kuendelea kuficha Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mapema mwaka huu. Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba Tume hiyo iliundwa ikiwa ni hatua ya dharura kwa lengo la kutoa majibu ya haraka kuhusu sababu za wanafunzi wengi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana kufanya vibaya katika mtihani huo na kuamsha vilio kote nchini.
Katika matokeo hayo, watahiniwa 240,903 sawa na
asilimia 60.6 waliambulia sifuri, wakati watahiniwa 23,520 ambao ni
asilimia 5.16 wakiwa wamefaulu, huku watahiniwa wengine 103,327 sawa na
asilimia 26.02 wakiwa wamepata daraja la nne. Katika mtihani huo,
watahiniwa 397,136 walitoka katika shule mbalimbali, huku wengine 68,806
wakiwa wa kujitegemea.
Idadi kubwa ya wanafunzi hao kufeli mitihani kiasi
hicho lilionekana kama janga la kitaifa na ndiyo maana wananchi wa rika
zote, wakiwamo wabunge walipaza sauti wakiishinikiza Serikali itegue
kitendawili kuhusu sababu za matokeo hayo ya kutia fedheha na aibu kwa
taifa letu. Ndipo Serikali ilipounda Tume ya watu 15 Machi mwaka jana na
kuitaka kuwasilisha ripoti yake serikalini miezi mitatu baadaye.
Tume hiyo ilimaliza kazi yake katika muda
uliopangwa na kukabidhi ripoti hiyo Juni 15, mwaka huu. Jambo la
kushangaza ni kuwa, pamoja na kupita zaidi ya miezi minne tangu ripoti
hiyo iwasilishwe serikalini bado Serikali imeificha makabatini kwa
sababu inazozijua yenyewe. Habari zinasema kwamba Serikali inajua
umuhimu wa kuitoa ripoti hiyo hadharani haraka, lakini inasita kwa
sababu mengi ya matatizo yaliyoainishwa na Tume hiyo yanaonyesha bayana
kwamba Serikali pia ni sehemu ya tatizo.
Hata hivyo, tunapata shida kuelewa kwa nini
Serikali inaendelea kuatamia ripoti hiyo wakati ikijua kwamba Watanzania
wanasubiri ripoti hiyo kwa shauku kubwa kwa mategemeo kuwa, hatua za
kurekebisha makosa yaliyotokea zingechukuliwa na mamlaka zote husika kwa
kuwa muda siyo mrefu wanafunzi watafanya tena mitihani ya kidato cha
nne mwaka huu.
Ukimya wa Serikali unaendelea kusababisha madhara
mengine kadhaa, kwa maana ya baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo kuchoka
kuisubiri Serikali iweke hadharani ripoti ya Tume hiyo. Jana gazeti hili
lilichapisha habari kuhusu baadhi ya vipengere vilivyo katika ripoti ya
Tume hiyo, ambapo baadhi ya wajumbe waliounda Tume hiyo walisema katika
nyakati tofauti hivi karibuni kwamba waligundua mambo mengi
yanayodhihirisha udhaifu mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya elimu hapa
nchini.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wanasema sehemu
kubwa ya matokeo ya uchunguzi huo inajikita zaidi katika kulaumu Baraza
la Mitihani la Taifa (Necta) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), badala
ya kujielekeza zaidi katika kupendekeza nini kifanyike ili kurekebisha
mfumo mzima wa sekta ya elimu nchini ambao umedhihirika kuwa mbovu.
Tatizo hapa pengine ni muundo wa Tume hiyo yenye idadi kubwa ya
watumishi wa umma na wabunge wa chama tawala.
Wajumbe hao wamesema ripoti ya Tume hiyo ni ndefu
na ingefaa Serikali iiweke wazi sasa ili ifanyiwe kazi. Sisi tunaungana
na wajumbe hao kuishauri Serikali kufanya hivyo sasa. Madhara ya
kuendelea kuihodhi ripoti hiyo ni makubwa pengine kuliko Serikali
yenyewe inavyofikiri.
souce . mwananchi
souce . mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni