Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 2 Oktoba 2013

Serikali kutoa ruzuku kwa shule binafsi

Serikali inatafakari uwezekano wa kutanua wigo wa kutoa ruzuku hadi kwa shule zinazomilikiwa na watu binafsi, ikiwa ni sehemu ya azma ya kuzipunguzia gharama za uendeshaji.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema hayo wakati akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba katika Shule ya St. Anne Marie Academy jijini Dar es Salaam jana.Alisema shule nyingi za binafsi zinafungwa kutokana na kushindwa kujiendesha miongoni mwa sababu kubwa ikiwa ni kupanda kwa gharama za uendeshaji.

Simbachawene alisema kuziacha shule binafsi `zife’ kutokana na sababu iliyo ndani ya uwezo wa nchi kuitatua, ni hasara kwa taifa na kwamba njia pekee ya kuzisaidia kwa kuzipa ruzuku ili ziweze kujiendesha.

Kwa mujibu wa Simbachawene, shule binafsi zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango cha elimu, hivyo kupunguza idadi na kasi ya Watanzania kupeleka watoto wao kusoma nje ya nchi.Alisema: "Ukiacha shule kama hii (St. Anne Marie) ikafa ni hasara kwa taifa, serikali inaangalia kuona namna bora ya kuzisaidia kwa kuzipatia ruzuku ili kuzipunguzia gharama za uendeshaji.”

Kwa upande mwingine, Simbachawene aliwaasa vijana kuwa makini katika kukabiliana na kuzishinda changamoto zilizo katika jamii, ikiwamo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na matumizi ama usafirishaji wa dawa za kulevya.

Meneja wa shule hiyo, Jasson Rweikiza, alisema serikali imekuwa na kigugumizi katika mambo mbalimbali katika sekta ya elimu, hali inayosababisha  kudumaa kwa sekta hiyo na watoto kukosa ufaulu mzuri.

Kwa mujibu wa Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, mpaka sasa mitaala ya elimu na sera za elimu hazipo wazi, hali inayosababisha walimu wakose mwongozo wa kufundishia.

Alisema wadau wa elimu hususani wamiliki wa shule binafsi, wanakabiliwa na kazi kubwa ya uendeshaji, huku kukiwa na changamoto kadhaa kama vile matumizi ya mitaala isiyoeleweka.

Pia alisema sera zinazohusiana na elimu hazipo wazi, na kutoa mfano kuwa sera haielezi kama ni kosa ama si kosa inapotokea kuwapo mwanafunzi asiyejua kusoma.
“Maendeleo hayawezi kwenda bila kuboresha sekta ya elimu...tunaiomba serikali isimame imara katika kuinusuru sekta ya elimu nchini,” alisema.

Rweikiza alisema wahitimu wa darasa la saba wanapaswa kuondokana na dhana inayowafanya kujiona wamemaliza shule, bali kiwango hicho kuwa msingi wa safari ndefu inayowakabili maishani.

ippmedia.com

Walimu 344 wafukuzwa kazi 2008- 2013

Walimu 344 nchini wamefukuzwa kazi kutoka mwaka 2008 hadi mwaka huu kutokana na makosa mbalimbali ikiwamo kuwapa mimba wanafunzi.Hayo yalisemwa na Katibu Msaidizi wa  Ajira na Maendeleo ya Watumishi (TSD), Christina Hape, jijini Dar es Salaam jana.

Hape alisema mwalimu anatakiwa kuwa kama mlezi wa wanafunzi, lakini suala la kuwapa mimba linapokuja ni kosa la jinai na kwamba ni lazima wapelekwe polisi kwa ajiri ya kuchukuliwa hatua.Kwa upande wake, TSD pamoja na Tume ya Utumishi wa Umma wanaweza kuwafukuza kazi walimu.

Alisema  katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2009 wamefukuzwa walimu  40, mwaka 2009 hadi 2010 walimu 20 , mwaka 2010 hadi 2011 walimu 13  na mwaka 2011 hadi  2012 walimu 11 walifukizwa.Aliongeza kuwa mpaka sasa walimu 84 walifukuzwa kazi baada ya kubainika makosa yao ya kuwapa mimba wanafunzi.

Hata hivyo, alisema ugumu unakuja pale wazazi wanapokosa kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kutohudhuria mahakamani na kuamua kulimaliza baada ya mtuhumiwa huyo kuwashawishi kwamba atamuoa binti yao.

Kwa upande wa makosa ya utoro kwa mwaka 2011 hadi 2012 walimu 152 na mwaka 2012 hadi 2013 walimu 157 walifukuzwa kazi .Alisema kwa wastani walimu wapatao 260 mpaka sasa wamefukuzwa kazi kutokana na utoro wa maeneo ya kazi.

Naibu Katibu Tume ya Utumishi wa Umma, Idara ya Utumishi wa Walimu, Edwini Mokongoti, alisema ili kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa masuala ya kiutumishi wakuu wa vyuo vya ualimu, vyuo vya maendeleo ya jamii, wakuu wa shule na walimu wakuu wanatakiwa kuwajibika katika kuwaelimisha walimu taratibu za masuala ya ajira katika maeneo mbalimbali ikiwamo kupandishwa vyeo, ajira na usajili.

Alisema pia wakuu hao watashughulikia makosa madogo madogo ya kinidhamu na kutoa adhabu, ambayo kwa mujibu wa kanuni namab 118 ya kanuni za utumishi wa umma ya mwaka 2003 zitakuw a, onyo, kusimamisha nyongeza ya mshahara kufidia hasara au sehemu ya hasara ambayo mtumishi itaisababishai serikali kutokana na uzembe wake.

ippmedia.com

mabunge ya wanafunzi yanawajengea wanafunzi uwezo wa kujieleza


Jumanne, 24 Septemba 2013

kurejea kwa elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne kwa shule kongwe

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Serikali imeanza kushughulikia utaratibu wa kurejesha utoaji wa elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne, katika baadhi ya shule kongwe nchini ili kurudisha ufaulu uliokuwepo na kuimarisha malezi ya watoto kuanzia elimu ya chini.

Jumamosi, 21 Septemba 2013

CCM yatoa miezi 6 kwa waziri wa Elimu kujiuzulu....Vinginevyo itamtimua kwa nguvu




CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kujiuzulu kwa kushindwa kulipa madeni ya walimu nchini.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pia ametoa muda wa miezi sita kwa Waziri huyo na Naibu wake Philip Mulogo kutekeleza hilo agizo hilo vinginevyo chama kitawatumia wabunge wake kuwatimua kwa nguvu.

Kwa mujibu wa taarifa za madeni zilizokusanywa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), hadi sasa walimu wanadai malimbikizo yao ya Sh bilioni 49 ambayo hajalipwa na Serikali.

Kinana alikuwa akihutubia mikutano ya hadhara jana katika wilaya za Bariadi na Busega.

Alisema CCM haiko tayari kuona walimu wakinyanyaswa wakati wana madai ya msingi.

Hivi sasa imejengeka tabia kwa baadhi ya mawaziri na watendaji wa wizara ya kuwadharau walimu na hata kuwanyanyasa huku wengine wakishusha utu na heshima ya walimu kwa kuwatukana, alisema.

Kinana ambaye yupo katika ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa alisema kwa mawaziri kushindwa kutatua kero za walimu, imefika wakati wahusika waondoke wenyewe na wasipofanya hivyo chama kitawaagiza wabunge wake wawafukuze kwa nguvu.

“Ninatoa muda wa miezi sita kwa Waziri wa Elimu na wasaidizi wake wakiwamo watendaji kuhakikisha wanalipa madeni ya walimu haraka. Haiwezeni hii ni nchi ya watu wote wakiwamo walimu wadharauliwe na hata kunyanyaswa kwa maneno ya matusi

“Hili hapana CCM haiko tayari kuona walimu kila siku wakipigwa danadana kutokana na uzembe wa watu waliokabidhiwa dhamana za kuongoza sekta ya elimu katika nchi yetu,” alisema.

MTANZANIA ilimtafuta Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch ambaye alisema hadi sasa madeni ya walimu yamefikia Sh bilioni 49 ambayo ni malimbikizo ya mishahara na mapunjo.

“Kila mara tunawaambia kuwa ni vema Serikali itafute Sh bilioni 100 katika fungu la dharura ili iweze kulipa madeni ya walimu na iachane nao lakini hawasikii,” alisema Oluoch.

Source: Mtanzania

Chikombe: Shule yenye walimu watatu wanafunzi 300

Nikiwa ziarani mkoani Lindi nafanikiwa kupita katika shule mbalimbali za msingi na sekondari. Lengo hasa lilikuwa ni kuangalia mazingira halisi ya shule hizo kama yanaweza kuleta tija kwa siku za baadaye?

Shule ya msingi Chikombe ndiyo kambi yangu ya kwanza katika ziara hii. Kwa kutumia usafiri wa pikipiki nafanikiwa kufika shuleni hapa saa tano asubuhi, nikitokea Lindi Mjini.

Mbele yangu ni uwanja mkubwa wa nyasi ukiwa na miti michache ya miembe. Kuna wanafunzi wachache wakiwa wamezagaa katika eneo hilo wakicheza mpira. Hii inaashira kuwa wako kwenye muda wa mapumziko.

Kadiri ninavyosogea nazidi kuwa karibu na majengo ya shule mbele yangu. Ni majengo mawili yenye hali tofauti. Moja ni jengo lenye madarasa mawili na ofisi moja ndogo ya walimu linaloonekana kuwa jipya kidogo.

Pia jingine ni jengo kuukuu lililojengwa kwa udongo na miti. Kwa kulitazama jengo hili unaweza kulifananisha na zizi la ng’ombe ama stoo ya kuhifadhia vifaa vya kilimo. Jengo hili lina vyumba vitatu vinavyotumika kama madarasa.

Upana wa chumba kimoja cha jengo hilo unaweza kuwa ni urefu wa madawati mawili na uchochoro wa kupita mtu mmoja katikati.

Wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza, la pili la tatu na la nne hutumia madarasa haya kama sehemu yao ya kusomea.

Kwa muda huu nilioingia nakuta wanafunzi wa darasa la kwanza wakiwa katika maandalizi ya kutoka shule.

Nafika kwenye ofisi ya walimu kwa ajili ya kujitambulisha na kupata mwenyeji wangu, ambaye ningepata mawili matatu kuhusiana na shule hiyo iliyo katika Wilaya ya Lindi Vijijini Jimbo la Mtama.

Mwalimu Hassan Halfan (54) ndiye alikuwa wa kwanza kukutana naye. Yeye ni mmoja kati ya walimu watatu katika shule hiyo. Kama ilivyo ada ya mgeni na mwenyeji alianza kwa kunipa historia ya shule yake.

“Shule ya Chikombe ilianza rasmi mwaka 2008 ikiwa na mwalimu mmoja ambaye ni mimi mwenyewe, nikiwa peke yangu niliweza kufundisha kwa miaka miwili bila usaidizi hadi mwishoni mwa mwaka 2009, alipokuja mwalimu mwenzangu,” alisema.

Mwaka 2010 idadi ya walimu iliongezeka na kufikia walimu watatu ambao tupo pamoja hadi hivi sasa.Changamoto kuu zinazoikabili shule hii

Kama ilivyo kwa shule nyingi zilizo katika Mkoa wa Lindi, Shule ya Chikombe inakabiliwa na matatizo lukuki kiasi cha kushindwa kujiendesha ipasavyo.Mradi pekee unaotegemewa katika shule hii ni ule wa shule ya awali, ambapo wazazi hulazimika kuwalipia watoto Sh300 kama ada ya mwanafunzi mmoja kwa mwezi.

“Pamoja na kuwekwa kwa kiasi kidogo cha ada, wazazi wanashindwa kuilipa na hivyo kuzidi kutupa wakati mgumu,” anasema mwalimu Halfani.

Anasema uchache wa walimu nalo ni tatizo linguine, ambapo walimu watatu waliopo wanalazimika kufundisha wastani wa vipindi 64 hadi 75 kwa wiki.
Jambo hili kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwapa mtihani walimu hao na hata kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

“Uchache wa walimu umekuwa ukikwamisha maendeleo ya shule yetu kwa kiasi kikubwa sana. Lakini ukiachikia mbali uchache huo, hapa shuleni kwetu kuna uhaba wa nyumba za walimu,” anasema.

“Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, tulilazimika kuwaondoa wanafunzi katika darasa moja ili kumpisha mwalimu mkuu ambaye alikuwa hana nyumba ya kuishi,” anasema mwalimu Halfan.

Jambo hilo lilisababisha msongamano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa, kwani madarasa manne yalilazimika kutumiwa na mikondo saba na wengine ilibidi wafundishiwe nje ya madarasa anasema mwalimu huyo.

Baada ya kuona ukubwa wa tatizo hilo, wanakijiji waliingilia kati na kwa pamoja walishirikiana kujenga nyumba moja ya mwalimu mkuu, ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kushiriki masomo darasani.
mwananchi.co.tz

Alhamisi, 19 Septemba 2013

wasichana 11 shule ya msingi wapata mimba

WASICHANA 11 wa shule ya msingi iliyo Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay, wamepatikana kuwa wajawazito. Wanafunzi hao wa Shule ya Msingi ya Rangenya, iliyo karibu na Ndhiwa mjini wanajumuisha msichana mwenye miaka kumi aliye katika darasa la saba. Wawili kati yao tayari wananyonyesha watoto baada ya kujifungua hivi majuzi.

Wasichana wawili wako katika darasa la saba, huku kukiwa na mmoja katika darasa la nne na mwingine darasa la tano.Duru za kuaminika zilisema waliohusika kuwapachika watoto hao mimba ni mwalimu aliyeajiriwa na Chama cha Walimu na Wazazi (PTA), waendeshaji boda boda na vijana wanaotoka katika vijiji vya karibu.

Mwalimu huyo ambaye ni jamaa ya mmoja wa walimu wenye vyeo vikuu shuleni humo alipelekwa hadi kituo cha polisi mwaka jana, kwa kudaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa wanafunzi aliye katika darasa la saba.

Shughuli katika shule hiyo zilisitishwa kwa muda Jumanne baada ya Mkuu wa Elimu katika wilaya hiyo Maurice Jayora, na maafisa wake walipowasili kuanzisha uchunguzi.
Maafisa hao walitumia saa kadha asubuhi kuhoji walimu na wanafunzi kuhusu tukio hilo.

Mkuu huyo wa elimu aligutushwa na hali kuwa wasimamizi wa shule hiyo hawajawahi kufahamisha afisi yake wala ile ya afisa wa elimu katika eneo hilo kuhusu matukio hayo.“Nataka ifahamike kuwa mimi na maafisa wangu, tulifahamu kuhusu tukio hili kupitia vyombo vya habari. Hata afisa wa elimu katika eneo hili hakujulishwa,” alisema.

Masomo

Alithibitisha kuwa baadhi ya wasichana walioathirika bado wanaendelea na masomo na wanasaidia kwenye uchunguzi.“Baadhi ya waathiriwa ambao bado wako shuleni wanatupatia habari muhimu zitakazosaidia kwenye uchunguzi tunaofanya,” alisema.

Juhudi za kukabiliana na matukio kama haya pamoja na kuozwa kwa wasichana wenye umri mdogo katika maeneo ya Ndhiwa na Homa Bay hazijafua dafu kutokana na ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa wazazi. Uchunguzi umebainisha kuwa wakati wowote wanaohusika wanapokamatwa, baadhi ya wazazi huingilia kati na kupendelea kutohusisha mahakama kutatua masuala hayo.

Naibu wa Kamishna wa Kaunti Geoffrey Omonding amekuwa akionya maafisa wa utawala kuhusu athari iliyopo ikiwa matukio kama haya yatapatikana kuwa yanatokea katika maeneo wanayosimamia.