Hoja yangu tangu wiki iliyopita ni kuwakumbusha vijana kufahamu
vyema historia yao hasa kuhusu ukoloni na athari zake, ili wajipange
vyema kutumia fursa zilizopo na kuendeleza jamii zao.
Nilisema kuwa baada tu ya mkutano wa Berlin
uliofanyika Ujerumani mwaka 1885, bara lote la Afrika liliwekwa chini ya
utawala wa matapeli wastaarabu, wanaojulikana kama Wazungu kutoka
Ulaya.
Mtemi Zombwe |
Nilitaja baadhi ya athari za ukoloni kuwa ni
pamoja na mauaji makubwa, unyanyasaji, kupora utajiri wa Afrika, kugeuza
Waafrika kuwa vibarua wa dezo, ukatili, dhuluma, kuvuruga akili za
Waafrika na kuua mifumo ya viwanda na teknolojia iliyokuwa imeshamiri
katika jamii zetu.
Mbinu walizotumia kufanikisha utii na kuvuruga
akili za Waafrika ni kupandikiza dini za kigeni na mafundisho
mchanganyiko, huku wakinyang’anya ardhi za Waafrika, kuwaua ama
kuwatesa.
Waliendelea kuwapa utumwa wa kiakili na mitazamo
duni ili washindwe kufikiri vizuri. Wakawahimiza wawapende maadui zao
(ambao ni wao wazungu), wakawahimiza wasamehe saba mara sabini(ili
usihesabu viboko ulivyopigwa jana ukiwa uchi).
Waafrika wakaambiwa mila zao ni za kishetani (ili
wafuate mila za wazungu wawatawale kirahisi). Na wakacholewa sanamu ya
shetani mweusi inayotisha sana. Lakini malaika-wazungu, mitume-wazungu,
watakatifu-wote wazungu.
Waafrika wakaogopa! wakaacha mila zao njema
wakabeba mzigo wa mila za kishenzi zilizopakwa manukato ya kila aina ili
zinukie na zivutie. Hizi ndizo zinazowatesa dada zetu kutamani uzungu
kwa kuchubua ngozi zao, kudharau asili yao na hata uumbwaji wao.
Kila cha mzungu ni chema hata kama ni kinyesi na
kila cha Mwafrika ni kibaya. Hili likamomonyoa maadili ambayo hadi leo
tunayajutia. Wao kicheko!
Hata wasomi wakipelekwa Ulaya kwenda kupata
maarifa, hawarudi na maarifa. Wanarudi na utamaduni wa kizungu, ufisadi
wa kizungu, dharau za kizungu na ulevi wa kizungu. Maarifa wanayaacha
huko huko. Wanarudi vichwa vyeupe vimejaa uzungu-na tamaa ya utajiri
pasipo kufanyakazi.
Ndiyo maana kwa sasa tuna utawala wa kizungu,
mienendo ya kizungu, lugha za kizungu, dini za kizungu, miujiza ya
kizungu, nguo za kizungu, vyombo vya kizungu, na magonjwa ya kizungu.
Pia utamaduni wa kizungu, nyimbo za kizungu,
viboko vya kizungu, dawa za kizungu, ufisadi wa kizungu, rushwa ya
kizungu, taabu za kizungu, umasikini wa kizungu, Mungu wa kizungu na
manabii wa kizungu, matusi ya kizungu, hata uzinzi wa kizungu. Hizi
ndizo tunu za ukoloni tulizoachiwa.
Yaliyo mema ya Waafrika yakapotea, yakadharauliwa, yakabezwa na
mizigo ya laana ikavijaza vichwa vya Waafrika hao wachache waliokwenda
sambamba na mdundo wa mafunzo ya wazungu. Babu zetu wengi walipinga;
lakini mwenye nguvu mpishe.
Siyo kila kitu waliachofanya wakoloni ni kibaya
kwa Waafrika. La hasha! Yako mambo mengine mazuri kuigwa kwa kuoainisha
na mahitaji yetu.
Kwa mfano, jitihada ya kufikiri, kubuni na
kufanyakazi kwa bidii ni jambo jema linaloweza kuigwa. Ona kwa sababu ya
shida walizopata, walithubutu kuondoka kwao maelfu ya kilomita kuja
Afrika ambako hawakukuta pamba wala dhahabu zilizokuwa tayari. Bali
wakikuta misitu mikubwa mapori ya kutisha wanyama wengi na udongo wenye
rutuba.
Tena mapori mengi Waafrika waliyatumia kama kivuli
katika shughuli za unyago. Na misitu mingine ilitumiwa kama sehemu za
ibada na matambiko ya jadi.
Lakini wao wakakata nyasi na miti.Wakabuni
mashamba na uchimbaji wa madini yaliyokuwa chini ya ardhi, ambayo hata
Waafrika wenyewe hatukuyajua kama yapo. Wakathubutu kuchimba na kulima,
wakafanikiwa.
Hilo likawezekana wakazoa utajiri mkubwa
wakapekeka kwao. Bado huko huko kwao hawakuiacha pamba sebuleni, bali
wakabuni mitindo mbali mbali ya usokotaji wa nyuzi ambazo zilikuja
kutumiwa kuunda nguo za kila aina zilizouzwa kwao, Asia, Amerika na pia
kwetu Afrika.
Mpira uliolimwa Congo wakabuni matairi ya magari
wakapata pesa. Shaba waliichukua kwa wingi pale Zambia na Kongo wakabuni
nyaya za umeme wakafanikisha umeme ukawaka Waafrika tukafurahia. Je,
bila kufikri haya yangewezekana?
Hata wanasayansi wengi waliogundua kanuni na
fomula nyingi zilizotumika kutengenezea vitu kama magari, ndege hawakuwa
na vyeti vingi, bali kufikiri, kuthubutu na kubuni ndiyo siri ya
mafanikio. Walitumia muda wao mwingi kufikiri na kubuni kikamilifu hadi
wakaibuka na manufaa hayo makubwa yaliyoibadili dunia hii.
Kina Isaac Newton, Charles Darwin, Plato,Faraday,
Garileo, James Watt, Abbot Lambert na wengine wengi ni mifano ya
wafikirivu wakubwa ulimwenguni. Je, hawa walikuwa na digrii ngapi hadi
wakaweza kufikiri?
Wakati sisi tunaiga uzungu badala ya maarifa na
ubunifu, wenzetu Wachina na Wahindi wanaiga maarifa na ubunifu. Wachina
wanachukua karatasi wanapaka rangi, wanabuni aina za mikunjo na kukunja
karatasi linakuwa ua.
Wanaleta kwetu kama maua ya gharama sana.
Tunanunua! Tembelea kwenye masoko duniani kote, bidhaa za Wachina
zimetawala masoko, kutokana na kazi za wabunifu na watu wanaothamini
kazi na kufikiri.
chanzo. mwananchi
chanzo. mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni