
Nikiwa
ziarani mkoani Lindi nafanikiwa kupita katika shule mbalimbali za
msingi na sekondari. Lengo hasa lilikuwa ni kuangalia mazingira halisi
ya shule hizo kama yanaweza kuleta tija kwa siku za baadaye?
Shule
ya msingi Chikombe ndiyo kambi yangu ya kwanza katika ziara hii. Kwa
kutumia usafiri wa pikipiki nafanikiwa kufika shuleni hapa saa tano
asubuhi, nikitokea Lindi Mjini.
Mbele yangu ni uwanja mkubwa wa
nyasi ukiwa na miti michache ya miembe. Kuna wanafunzi wachache wakiwa
wamezagaa katika eneo hilo wakicheza mpira. Hii inaashira kuwa wako
kwenye muda wa mapumziko.
Kadiri ninavyosogea nazidi kuwa karibu
na majengo ya shule mbele yangu. Ni majengo mawili yenye hali tofauti.
Moja ni jengo lenye madarasa mawili na ofisi moja ndogo ya walimu
linaloonekana kuwa jipya kidogo.
Pia jingine ni jengo kuukuu
lililojengwa kwa udongo na miti. Kwa kulitazama jengo hili unaweza
kulifananisha na zizi la ng’ombe ama stoo ya kuhifadhia vifaa vya
kilimo. Jengo hili lina vyumba vitatu vinavyotumika kama madarasa.
Upana wa chumba kimoja cha jengo hilo unaweza kuwa ni urefu wa madawati mawili na uchochoro wa kupita mtu mmoja katikati.
Wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza, la pili la tatu na la nne hutumia madarasa haya kama sehemu yao ya kusomea.
Kwa muda huu nilioingia nakuta wanafunzi wa darasa la kwanza wakiwa katika maandalizi ya kutoka shule.
Nafika
kwenye ofisi ya walimu kwa ajili ya kujitambulisha na kupata mwenyeji
wangu, ambaye ningepata mawili matatu kuhusiana na shule hiyo iliyo
katika Wilaya ya Lindi Vijijini Jimbo la Mtama.
Mwalimu Hassan
Halfan (54) ndiye alikuwa wa kwanza kukutana naye. Yeye ni mmoja kati ya
walimu watatu katika shule hiyo. Kama ilivyo ada ya mgeni na mwenyeji
alianza kwa kunipa historia ya shule yake.
“Shule ya Chikombe
ilianza rasmi mwaka 2008 ikiwa na mwalimu mmoja ambaye ni mimi mwenyewe,
nikiwa peke yangu niliweza kufundisha kwa miaka miwili bila usaidizi
hadi mwishoni mwa mwaka 2009, alipokuja mwalimu mwenzangu,” alisema.
Mwaka
2010 idadi ya walimu iliongezeka na kufikia walimu watatu ambao tupo
pamoja hadi hivi sasa.Changamoto kuu zinazoikabili shule hii
Kama
ilivyo kwa shule nyingi zilizo katika Mkoa wa Lindi, Shule ya Chikombe
inakabiliwa na matatizo lukuki kiasi cha kushindwa kujiendesha
ipasavyo.Mradi pekee unaotegemewa katika shule hii ni ule wa shule ya
awali, ambapo wazazi hulazimika kuwalipia watoto Sh300 kama ada ya
mwanafunzi mmoja kwa mwezi.
“Pamoja na kuwekwa kwa kiasi kidogo
cha ada, wazazi wanashindwa kuilipa na hivyo kuzidi kutupa wakati
mgumu,” anasema mwalimu Halfani.
Anasema uchache wa walimu nalo
ni tatizo linguine, ambapo walimu watatu waliopo wanalazimika kufundisha
wastani wa vipindi 64 hadi 75 kwa wiki.
Jambo hili kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwapa mtihani walimu hao na hata kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
“Uchache
wa walimu umekuwa ukikwamisha maendeleo ya shule yetu kwa kiasi kikubwa
sana. Lakini ukiachikia mbali uchache huo, hapa shuleni kwetu kuna
uhaba wa nyumba za walimu,” anasema.
“Katika kipindi cha miezi
kadhaa iliyopita, tulilazimika kuwaondoa wanafunzi katika darasa moja
ili kumpisha mwalimu mkuu ambaye alikuwa hana nyumba ya kuishi,” anasema
mwalimu Halfan.
Jambo hilo lilisababisha msongamano wa wanafunzi
katika vyumba vya madarasa, kwani madarasa manne yalilazimika kutumiwa
na mikondo saba na wengine ilibidi wafundishiwe nje ya madarasa anasema
mwalimu huyo.
Baada ya kuona ukubwa wa tatizo hilo, wanakijiji
waliingilia kati na kwa pamoja walishirikiana kujenga nyumba moja ya
mwalimu mkuu, ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kushiriki masomo darasani.
mwananchi.co.tz