Hukumu ya hivi karibuni ya
mahakama ya kikatiba imethibitisha kwamba shule haziwezi kuwafukuza
wanafunzi kwa kupata uja uzito.Lakini Afrika Kusini bado inang'ang'ana
kukabliana na suala hilo linalowaathiri wasichana 180,000 kila mwaka.
Daktari Jay-Anne Devjee ambaye ni mkuu wa afya
ya akina mama katika hospitali ya King Dinuzulu anasema kwa mara nyingi
hulazimika kuwazalisha wasichana kwa njia ya upasuaji, jambo
linaloongeza hatari ya kuvuja damu na kuhatarisha maisha ya wazazi hao.
Msichana mwenye umri mdogo zaidi
hapa ana umri wa miaka 14 na anaonekana kuzidiwa na uchungu wa uzazi
kiasi cha hata kushindwa kuongea.
Phumla Tshabalala, mwenye umri wa miaka 16,
anamshikilia mwanawe mchanga aliye na umri wa siku moja.Hii ni mara yake
ya kwanza kujifungua na anasema ana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kumlea
mwanawe peke yake.
Anaeleza hajamuona mpenzi wake kwa muda mrefu na
licha ya kumuarifu kwamba amejifungua, hakuna mtu kutoka familia ya
mpenzi wake aliyekuja kumjulia hali.
Anatoka katika familia maskini, Babake ndiye
anayeilisha familia. Yeye ni binti wa mwisho kati ya mabinti watatu na
wa kwanza aliyejifungua mtoto, jambo ambalo familia yake bado
haijalipokea vyema.
Inakisiwa kuwa kila mwaka wasichana zaidi ya
laki moja na themanini nchini Afrika Kusini hushika ujauzito. 180 kati
ya wengine 1000, hupata kuwa wajawazito. 36% ya wasichana wenye mimba
hufariki kila mwaka kulingana na takwimu za nchi hiyo wakati
wanapojifungua.
Mifuko yao ya uzazi huwa bado haijakuwa vyema
kiasi cha kubeba mimba na wengi huwa na wakati mgumu sana wanapojifungua
, kulingana na daktari Jay-Anne Devjee.
Phumla anapanga kurudi shuleni kwa wakati
muafaka ili aweze kufanya mtihani wa mwisho wa mwaka , lakini ana
wasiwasi kuhusu vipi atakavyoweza kutimiza majukumu yote mawili ya kuwa
mwanafunzi na mzazi pia.
Anasema laitani angesubiri hadi angekuwa mkubwa.
Lakini anajiona kuwa mwenye bahati kwa kuwa yeye na mwanawe ni wazima na wenye afya.
Madakatari wanasema kuna hatari ya kuzaa ukiwa
una umri mdogo. Kwa mujibu wa baraza la utafiti wa sayansi ya binaadamu,
viwango vya akina mama wanaofariki ni kubwa kwa wasichana kwa asilimia
36 ya vifo katika uzazi kila mwaka licha ya kwamba ni asilimia 8 pekee
ya vifo hivyo ndivyo vinavyoripotiwa.
Utafiti unaashiria kwamba wasichana wengi
hulazimika kuacha masomo ili kuwalea watoto wao na wengi wao hukosa
kurudi kusoma baadaye.
Maafisa wa elimu wanasema katika shule ya upili
wa Intshisekelo nje ya mji wa Durban, zaidi ya wasichana 20 walipachikwa
mimba katika nusu ya kwanza ya mwaka.
Maafisa nchini humo wana wasiwasi kwamba huenda
kushiriki kwa vijana katika ngono bila ya kinga kukaathiri vita dhidi ya
HIV/Ukimwi. Mwalimu mmoja anasema mimba ni miongoni mwa sababu kuu
pamoja na umaskini zinazochangia nusu tu ya wanafunzi wa kike kumaliza
shule.
Kwa mujibu wa sheria, shule hazipaswi kufichua
ni wanafunzi gani waja wazito na inasema baadhi ya wasichana huwa na
kibarua kigumu cha kificha matumbo yao yanayozidi kukuwa ikwemo kuvaa
nguo kubwa na pia kubeba mabegi yao ya shule mbele.
Sheria hiyo ya mwaka 1996 inasema wanafunzi
hawapswi kufukuzwa kwa kuwa ni waja wazito lakini shule zinasema
wanalazimika kuwafukuza kwa sababu hazijapewa mafunzo ya namna ya
kuwasaidia wasichana hao waja wazito.