harakati za marafiki wa elimu musoma wasiliana nasi kwa namba +255755 650 075 au +255786 650 075 ni jukumu letu kuboresha elimu
HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Jumatano, 19 Machi 2014
madarasa walimu na vitabu bado changamoto
Shule ya sekondari Tongoni mkoani Tanga ina majengo
mazuri, walimu 12, maabara, vitabu lakini kitaifa inashika
nafasi ya tatu kutoka mwisho katika matokeo ya kidato cha
nne mwaka jana.
Shule hiyo, ina walimu 12 wengi wao wakiwa na elimu ya
kiwango cha shahada ya elimu. Ina madarasa manane,
madawati kwa kila mwanafunzi, maabara na vitabu vya
kutosha.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 haijafaulisha
mwanafunzi hata mmoja kwa kiwango cha daraja la kwanza, la
pili wala la tatu. Daraja la kujivunia kwa shule hiyo kwenye
mitihani ya kidato cha nne ni la nne na sifuri kwa watahiniwa
wake.
Sasa shule hiyo ina wanafunzi wapatao 123 kati yao wasichana
ni 52 na wavulana 71.
“Ni wanafunzi watatu tu kati ya 47 walioweza kufaulu mtihani
wa kidato cha pili mwaka juzi … shule ikalazimika kuwatafutia
wanafunzi hao shule nyingine ili waendelee na masomo.
Waliobaki wakalazimika kurudia kidato cha pili,” alisema
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mfaume Juma.
Mwalimu Juma anasema mwaka jana, watahiniwa wa kidato
cha nne walikuwa 37 wanafunzi saba kati yao hawakupata
matokeo yao kwa kushindwa kukamilisha ada ya mtihani na 28
wakaambulia daraja sifuri. Ni wawili tu walipata daraja la nne.
“Mwaka jana wanafunzi 28 walipata daraja sifuri katika mtihani
wa kidato cha nne, saba matokeo yao yalizuiwa na Baraza la
Mitihani la Taifa kwa kushindwa kulipa ada ya mtihani,”
anasema Mwalimu Mkuu huyo.
Miongoni mwa changamoto zinazoikabili shule hiyo, Mwalimu
Mkuu anazitaja kuwa ni mwamko mdogo wa baadhi ya wazazi
kuhusu umuhimu wa elimu hasa ulipaji wa ada na michango ya
shule bado ni tatizo kubwa.
Hatua hiyo, anasema inasababisha shule hiyo kushindwa
kujiendesha kikamilifu asilimia 75 ya wanafunzi wanadaiwa ada.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa nyumba za walimu na
mabweni kwa wanafunzi. Asilimia 70 ya wanafunzi wa shule
hiyo huishi nje ya eneo hilo.
“Kutokana na ukosefu wa nyumba za walimu na mabweni kwa
wanafunzi baadhi ya wanafunzi wanachelewa kufika shule…
kuna wanafunzi wanaoishi katika kisiwa cha Mwarongo
ambacho ili kufika ng’ambo ya pili lazima wavuke kwa
mashua.Wakati mwingine hutegemea hali ya upepo wa bahari
siku ukivuma vibaya watoto wanashindwa kufika shuleni,”
anafafanua Mwalimu Juma.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wanasema, wamekuwa
wakishindwa kuhudhuria masomo kwa wakati au kuchelewa
hasa siku ambazo hali ya upepo wa bahari ukiwa mbaya.
“Mimi huwa naamka nyumbani saa 11 alfajiri, kuosha vyombo
na kuchota maji baada ya hapo najiandaa kwenda shule, lakini
ukifika Kivukoni ni lazima usubiri maji yajae ndiyo chombo
kiweze kuvuka.
Siku ambazo upepo ni mbaya mara kadhaa tulishawahi kuzama,
hali iliyotulazimu baada ya kunusurika turudi nyumbani badala
ya kwenda shule. Hii inatuumiza na kutuathiri sana
kimasomo,” anasema Mariam Hassan mwanafunzi wa kidato
cha kwanza shuleni hapo.
Naye Zuberi Hamid, mwanafunzi wa kidato cha tatu shuleni
hapo anasema, imekuwa ni kama kawaida kwao kutohudhuria
vipindi viwili vya kwa asubuhi kutokana na hali ya usafiri kuwa
ya mashaka na kimsingi hali hiyo imekuwa ni njia mojawapo
inayochangia kufeli masomo yao.
“Muda tunaoingia shuleni ni saa nne asubuhi unakuta vipindi
viwili vya mwanzo vimekamilika. Pia muda tunaotoka shule nao
hadi kuvuka na kufika nyumbani tunachelewa.Tukifika
nyumbani muda unakuwa umekwenda sana hata fursa ya
kujisomea inakuwa finyu sana, “ anasema Hamid.
Baadhi ya walimu wanasema , shule hiyo yenye walimu 12 kati
yao hakuna waliobobea katika masomo ya Biolojia, Fizikia na
Hisabati hali inayowalazimu wanafunzi kufanya mitihani ya
masomo hayo bila kufundishwa.
“Kwa sababu ya kutokuwa na walimu wa Physics,Hesabu na
Biology wanafunzi wanalazimika kufanya mitihani bila
kufundishwa masomo hayo hili nalo ni tatizo sana,” anasema
Thomas Simengwa, Mwalimu wa somo la Historia na Kiswahili
katika shule hiyo.
Omary Bushiri ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Tongoni
anakiri kuwepo mwamko mdogo wa wazazi katika uchangiaji wa
sekta ya elimu kijijini hapo sambamba na mmomonyoko wa
maadili kwa baadhi ya wanafunzi wa shuleni hiyo.
Bushiri ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya shule
hiyo, anasema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo
pamoja na mambo mengine ni mawasiliano duni kati ya
uongozi wa shule, wazazi na wanafunzi.
“Ni ukweli kabisa kwamba maendeleo ya shule ya sekondari
Tongoni yamekuwa yakididimia siku hadi siku lakini tatizo lipo
kwa pande zote tatu kwa maana ya uongozi wa shule,
wanafunzi, walimu na bodi ilishaomba uongozi wa shule
kuandalia mkutano na wanafunzi lakini hadi leo jambo hilo
halijafanyika ,“ anasema Bushiri.
Anasema lengo la Bodi ya shule kutaka kukutana na wanafunzi
wa shule hiyo ni baada ya kufahamishwa kuwa walimu
wamekuwa na tabia ya kutoingia darasani kwa wakati na
wengine kuishia njiani bila kufika shule na tabia nyingine
ambazo ni kinyume cha maadili ya wanafunzi.
“Wanafunzi walishalalamika kwamba walimu hawaingii darasani
kwa wakati….lakini si hilo tu, pia wanafunzi wenyewe wana
matatizo yao mengi tu ujana umewazidi na ndio maana tulitaka
kuzungumza nao,” anasema.
Anasema anashangaa wanafunzi kuchelewa shule kwa
kisingizio cha usafiri wa mashua wakati kuna boti
inayowasafirisha bila kikwazo chochote na kwamba hilo ni
tatizo na uzembe wa ufuatiliaji wa wanafunzi kati ya uongozi
wa shule na wazazi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tongoni, Luis Makame anasema
wakazi wa kata hiyo hawana mwamko katika uchangiaji wa
masuala ya elimu wakiamini kuwa elimu ya msingi inatosheleza
kuendesha maisha ya watoto wao.
“Kusema kweli, changamoto kubwa hapa ni uelewa wa wazazi
katika kuchangia sekta ya elimu.Wengi wanaamini kuwa, kila
mtoto ana riziki yake na kwamba elimu ya msingi inatosha
kabisa kuendesha maisha ya watoto wao ya kila siku, “ anasema
Makame.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi wa Kata ya Tongoni
wakizungumzia hali hiyo wanatupia lawama uongozi wa shule
na kusema kuwa umeshindwa kuwafuatilia wanafunzi wao na
baadhi wamekuwa na mienendo isiyofaa.
Selemani Sharif ni mmoja wa wazazi, ambaye anasema kuwa,
licha ya walimu kutoa malalamiko ya wazazi kutochangia ada
kikamilifu, lakini nao wameshindwa kusimamia uendeshaji wa
shule kwani hata wanafunzi nao wanalalamikia walimu
kutoingia madarasani kwa wakati.
“Sisi wazazi tunalaumiwa hatutaki kuchangia maendeleo ya
shule, lakini walimu nao wanalalamikiwa na wanafunzi
kutoingia madarasani na si hilo tu, uongozi wa shule
umeshindwa kusimamia tabia za wanafunzi wao ambao
tunawakuta vichochoroni wakati wa masomo na hiki kichaka
ndiyo gesti yao, walimu wanakuwa wapi wakati huo hata
wanafunzi wazurure ovyo,” anahoji Sharif.
Naye Mwajuma Mwanajumaa anaiomba serikali kufanya
mabadiliko ya uongozi wa shule hiyo kwa sababu wazazi
hawaridhishwi na matokeo ya shule hiyo.
“Shule hii wakati ikijengwa wananchi tuliichangia…kuitokana
na umuhimu wake kama kweli hatupendi elimu ilikuwaje
tulitoa nguvu zetu hadi ikajengwa…walimu na uongozi wa
shule umetukatisha tamaa sana… sasa ili twende vizuri
tunaiomba serikali iingilie kati suala hili,” anasisitiza
Mwanajumaa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga ambaye pia
ni Ofisa elimu Sekondari wa Jiji hilo , Bashiri Shelimo anasema
hatua ya kwanza itakayochukuliwa ni kuuondoa uongozi mzima
wa shule hiyo.
Shelimo anasema, hatua ya pili ni kuhamisha walimu wa shule
hiyo na kuwapeleka walimu wapya sambamba na kuunda upya
bodi ya shule hiyo.
Anasema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo hadi
kufikia katika hali hiyo mbaya ni uongozi mbovu uliodumu kwa
muda mrefu unaofanya kazi kwa mazoea.
“Nina miezi kadhaa tangu nilipohamia hapa lakini kwa
uchunguzi wangu wa awali nimeona kuna haja ya kuupangua
uongozi wa shule hiyo.
Bahati nzuri Mwalimu mkuu mwenyewe aliomba yeye na
makamu wake wapumzishwe na tukaona ni sababu za msingi ili
kuleta mabadiliko chanya kwenye shule ile,” anafafanua Ofisa
elimu huyo.
CHANZO: NIPASHE
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni