harakati za marafiki wa elimu musoma wasiliana nasi kwa namba +255755 650 075 au +255786 650 075 ni jukumu letu kuboresha elimu
HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ijumaa, 28 Machi 2014
mwanafunzi bingwa wa hisabati na ndoto za udaktari
Unapomuona kabla ya kuzungumza naye, ni rahisi kuamini
kwamba Sunday Mrutu (18) ana hulka ya usikivu, upole na
kutafakari kabla ya kutamka ama kuchukua hatua yoyote.
Ndivyo ilikuwa wakati nikijiandaa kumhoji, muda mfupi baada
ya uongozi wa Shule za St. Anne Marie za jijini Dar es Salaam,
kumtunukia Sh milioni tatu, kutokana na mafanikio yake
katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka jana.
Mkurugenzi wa Shule za St. Anne Marie, Jasson Rweikiza,
Uanamtaja Mrutu kuwa kati ya wanafunzi wawili wa shule hiyo
waliopata kati ya pointi saba na tisa za daraja la kwanza, yeye
(Mrutu) akiwa na pointi saba.
Kwa upande mwingine, Rwekiza akasema Mrutu alikuwa
miongoni mwa wanafunzi 10 bora nchi nzima, akishika nafasi
ya sita, wakati aliongoza katika utahiniwa uliofanywa na
Baraza la Mitihani, kama ilivyo kwa hisabati aliyopata alama 98
kati ya 100.
Rwekiza anasema matokeo hayo na mengine hususani
yaliyowahusisha wanafunzi 32 wa St. Anne na shule dada ya
Brilliant, waliopata daraja la kwanza, yanajenga heshima kwa
vijana hao na uongozi wa shule hizo.
Tayari uongozi wa St. Anne Marie, Brilliant Sunshine, zote
zikimiliwa na Rwekiza, zimetoa jumla ya Shilingi milioni 13.2
kwa wanafunzi waliopata daraja la kwanza.
Zawadi hizo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mkurugenzi
wa shule hizo, Rwekiza, kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha
nne mwaka jana.
Wanafunzi hao walipata kiasi tofauti cha fedha ambapo
waliofaulu kwa kati ya pointi 15-17 walikuwa 14 na
walizawadiwa Shilingi 200,000 kila mmoja.
Wengine na kiasi cha fedha alizopata kila mmoja ni 13
waliofaulu kwa kati ya pointi 13-14 (300,000), wanafunzi
watano waliofaulu kwa kati ya pointi 10-12 (500,000) na wawili
waliopata kati ya pointi 7-9 (1,000,000).
Hata hivyo, mwanafunzi aliyekuwa miongoni mwa wawili hao,
SundayMrutu alipewa zawadi tofauti kutokana na mafanikio
makubwa aliyoyapata katika mitihani hiyo.
Mwanafunzi huyo alizawadiwa Shilingi 1,000,000 kwa miongoni
mwa wanafunzi 10 bora nchini ambapo alishika nafasi ya sita
huku akiwa wa kwanza kwa upande wa wavulana.
Pia Mrutu alizawadiwa Shilingi 500,000 kwa kuwa wa kwanza
kwenye utahiniwa uliofanywa na Baraza la Mitihani la Taifa na
kiasi kama hicho kwa kuongoza katika somo la hisabati nchi
nzima, ambapo alipata alama 98.
Rwekiza, akasema ingawa fedha hizo zinaweza kuonekana kuwa
nyingi, lakini zitasaidia kuibua na kuhamasisha ari ya usomaji
kwa wanafunzi wa shule hizo na nyingine nchini.
“Tunalolifanya hapa kwa kutoa zawadi hizi za hamasa ni jambo
la kawaida kwa kila mwaka, lengo kubwa hapa ni kuhakikisha
watoto wetu wanaamini kwamba ahadi tunayowapa kuhusu
kusoma kwa bidii zinatekelezwa,” anasema.
Mrutu anathibitisha kwamba hisabati ni moja ya masomo
anayoyamudu darasani, hali hiyo ikichochewa na umakini,
usikivu na uelewa pindi mwalimu anapofundisha darasani.
“Hisabati inaaminika kuwa somo gumu sana, lakini ninaamini
kwamba kama mwanafunzi atakuwa msikivu, atatulia na
kufuata mafundisho ya mwalimu, itakuwa kinyume
chake….hisabati ni somo zuri na linaloeleweka kwa urahisi,”
anasema.
Mrutu anakumbuka namna alivyowafuatilia na kuwatii walimu
wake waliowahi kumfundisha hisabati, akiwataja kwa jina moja
moja kuwa Tarimo, Tino na Samuel.
Wakati Mrutu akisema hivyo, wanafunzi wa shule kadhaa za
sekondari wamekuwa wakilielezea somo hilo kama moja ya
masomo yanayowashinda katika kusoma na kufaulu.
KUHUSU UFAULU WAKE
Mrutu anasema hadi matokeo ya kidato cha nne yalipotoka na
kutaarifiwa kuhusu ufaulu wake, hakuamini kwa urahisi.
“Nilifuatwa nyumbani (bila kumtaja mtu aliyemfuata) na
kuambiwa kwamba nimefanikiwa vizuri sana kwenye mitihani
yangu,” anasema.
ANAPENDELEA UDAKTARI
Mrutu anasema pamoja na kuwa na uwezo unaomfanya
alimudu vyema somo la hisabati, kusudio lake ni kutaka
kusomea Udaktari.
“Ninajua hisabati ni somo muhimu lisilopewa kipaumbele sana
kwa madaktari, ila mimi nafsi yangu ni kuona ninasoma kufikia
kuwa Daktari wa binadamu,” anasema.
CHANGAMOTO KWA WANAFUNZI SHULENI
Mrutu, anasema ni jambo lililo wazi kwamba katika maisha ya
takribani miaka minne ya kusoma sekondari ya awali,
wanafunzi wanajenga urafiki na uhusiano wa karibu.
Hata hivyo, anasema kinachotakiwa kwa mwanafunzi ni kuweka
mipaka ya urafiki na uhusiano, kisha kusimamia dhamira, nia na
utashi vinavyomuongoza.
Anasema kukosekana kwa mipaka katika urafiki na uhusiano, ni
miongoni mwa vyanzo vya kuibuka tabia zisizofaa, nyingi kati ya
hizo zikitokana na kujifunza kunasababishwa na muingiliano wa
kirafiki ama kimahusiano.
“Sasa inapokuwa kwamba mpo marafiki wengi shuleni na
huwezi kuwakimbia, ni vizuri mwanafunzi ukajiepusha na kuiga
mambo, vinginevyo utajikuta unaachwa na wale uliokuwa
unawaiga, kwa maana kila mtu ana mbinu zake,” anasema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni