Mmoja wa kina mama wenye watoto kisiwani Kome Mchangani akiwa katika mizunguko yake ya kila siku kisiwani humo hivi karibuni.
Wakati taifa likiendelea na mikakati mbalimbali ya
kuboresha elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN), hali ni tofauti kwa watoto zaidi ya 300 wanaoishi
katika Kisiwa cha Kome Mchangani kilichopo kwenye Ziwa Victoria, Wilaya
ya Sengerema mkoani Mwanza baada ya kutojengwa shule kwa zaidi ya miaka
30.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kwa zaidi ya wiki mbili kwenye kisiwa
hicho umebaini kuwa tatizo hilo halitokani na kuwapo kwa hamasa ndogo ya
elimu kwa wazazi wa watoto hao; bali ni matokeo ya utekelezwaji wa
Sheria ya Uhifadhi Misitu ya Mwaka 2002, katika kifungu cha 26
kinachokataza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa majengo ya
kudumu.
Kisiwa cha Kome Mchangani ni miongoni mwa visiwa vya Ziwa Victoria vilivyotangazwa na serikali kuwa hifadhi ya misitu.
Kiongozi wa wakazi na wafanyabiashara wa mazao ya samaki katika kisiwa
hicho, Tibenda Luhuya, aliiambia NIPASHE kuwa wamejitahidi kupigania
uwapo wa shule na huduma nyingine za jamii kisiwani humo kwa muda mrefu
lakini hakuna wanachoambulia zaidi ya kuambiwa kuwa sheria za nchi
haziruhusu.
"Tunaelezwa kuwa eneo lote la kisiwa (cha Kome) halitakiwi kuwa na
majengo ya kudumu na hivyo, serikali haiwezi kutujengea shule wala
zahanati kwa sababu kufanya hivyo ni kuvunja hizo sheria," alisema
Luhuya.
Hata hivyo, wakati shule na majengo mengine ya kudumu yakizuiwa,
serikali imeruhusu kuwapo kwa jengo la kudumu la vyumba vitatu ambalo
linatumiwa na Kikosi cha Usimamizi wa Fukwe (BMU).
"Bado tunaendelea kuisihi serikali kuwa itujengee shule kwa ajili ya
watoto wetu ambao wanaishia kuvua samaki tu na kukosa elimu ambayo ni
haki yao ya msingi," aliongeza.
Anasema kisiwa hicho kina wakazi zaidi ya 5,000 na kinahesabika kipo
katika Kijiji cha Buhama, Kata ya Nyakasasa, Tarafa ya Buchosa. Umbali
wa kutoka kisiwa hicho mpaka Kijiji cha Buhama ambako kuna Shule ya
Msingi ni zaidi ya kilomita tano.
Akieleza zaidi, Luhuya anasema kwa zaidi ya miaka 30 tangu wavuvi na
wafanyabiashara wa mazao yatokanayo na samaki walipoanza kuishi hapo
hawajawahi kuwa na shule na hivyo, baadhi ya wazazi hulazimika
kuwapeleka watoto wao kwa ndugu, jamaa na marafiki wanaoishi nje ya
kisiwa hicho ili wakasome.
Hata hivyo, anasema zoezi hilo limekuwa gumu kwa kuwa baadhi ya wazazi
wakishawapeleka huko (kwa ndugu zao), huwa wanawatelekeza na matokeo
yake watoto hao wanarudi wenyewe kwa kuomba nauli na wengine kuingia
ndani ya boti inazokwenda kisiwani humo bila ya kuwa na nauli.
WATOTO, WAZAZI WANENA
"Inaniuma sana kujikuta naishi bila kujua kusoma na kuandika. Wazazi
wangu ni wavuvi na wote hawakusoma. Lakini na mimi nitaishia kuwa mvuvi
nisiyejua kusoma na kuandika kama wao kwa sababu hapa kwetu (Kome)
hakuna shule," ndivyo anavyoanza kueleza mtoto mmojawapo kisiwani Kome
Mchangani, John (11).
Ibrahimu anasema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisikia kwamba kuna
harakati zinafanywa za kuiomba serikali iwajengee shule. Lakini hadi
sasa hakuna kilichofanyika na anaamini kuwa yeye na watoto wenzake wote
kisiwani humo hawatapata fursa ya kujua kusoma na kuandika.
"Mimi inaniuma sana kwa kutojua kusoma... huwa ninawaona baadhi ya watu
wanasoma magazeti na vitabu, hasa wanaotoka Mwanza kuja kununua samaki
huku kwetu. Lakini mimi sijui kusoma wala kuandika.Ninachokijua zaidi ni
kuvua na kufanya kazi ya kusomba dagaa kutoka ziwani kuwaleta nchi
kavu," anasema Ibrahim.
Mtoto aitwaye Yona, mwenye umri wa miaka 10, anasema kutokana na kisiwa
hicho kukosa shule, wazazi wake walimpeleka Mwanza mjini kwa rafiki yao
ili akasome huko, lakini hilo halikuwezekana kwa sababu huko
alikopelekwa, wenyeji hawakuipa shule nafasi na hata watoto wao (wa
wenyeji) hawakuwa wakienda shule.
''Sasa nimerudi kwa wazazi wangu hapa kisiwani. Nimekaa wala sijui kama
nitasoma... naendelea na kazi ya kibarua cha kusomba samaki kutoka
katika mitumbwi ya wavuvi nyakati za jioni,'' alisema.
Tatu Kipile ni mmoja wa wakazi wa kisiwa cha Kome Mchangani. Anasema
kuwa yeye ameshindwa kumpeleka shule mtoto wake anayeishi naye huko
kutokana na kukosa fedha za kumsafirisha kutoka kisiwani humo na
kumhudumia wakati anapokwenda kwenye eneo lenye shule.
"Nilihamia hapa (Kome) wakati mwanangu akiwa na miaka mitatu. Sasa ni
zaidi ya mwaka wa tano niko hapa. Ninapenda sana mwanangu asome, lakini
sina namna ya kufanya kwa sababu kisiwa hiki hakina shule na sina fedha
za kumpeleka kwenye maeneo ya mbali yaliyo na shule za msingi," alisema
mama huyo.
Hellen Cosmas alisema analazimika kumpangia chumba jijini Mwanza mtoto
wake mwenye umri wa miaka 10 ili apate fursa ya kusoma, ingawa anasema
bado kuna changamoto nyingi ya kutekeleza azima yake hiyo kwa sababu
hana mwangalizi maalum.
"Hivi sasa nimemrudisha hapa kisiwani (Kome) kwa sababu mazingira ya
kuishi Mwanza ni magumu. Hana mwangalizi na hivyo sasa niko naye hapa...
haendi tena shule," alisema Hellen.
Sara Machera bado hajabahatika kupata mtoto. Hata hivyo, alisema kuwa
hali iliyopo sasa ni ngumu kwa wazazi wa kisiwa hicho kutekeleza jukumu
la kusomesha watoto wao kwavile hakuna shule. Aliongeza kuwa watoto
wanaopelekwa kwa ndugu zao ili wasome ni kama huwa wanatelekezwa kwani
uangalizi huwa mdogo.
Neema Abel ambaye pia bado hajapata mtoto anasema watoto kisiwani humo
hukosa elimu kwavile hakuna shule na hivyo anaiomba serikali ifikirie
kuwajengea shule ili kuokoa mamia ya watoto walio katika hatari ya kuwa
wajinga, wasiojua kusoma wala kuandika.
VISIWA VINGINE
Tatizo la shule linalowakabilia wakazi wa kisiwa cha Kome Mchangani lipo
pia katika visiwa vingine kadhaa vilivyomo kwenye Ziwa Victoria.
Mwanamama Agnes Joseph, mkazi wa kisiwa cha Ikulu alisema kuwa yeye ana
watoto watano, na wote amewapeleka kwa mama yake ambako ni katika eneo
lisilokuwa la kisiwa wilayani Sengerema ili wasome.
"Huwa ninawatembelea kila baada ya miezi miwili na kuwaachia fedha za
matumizi... sitaki wanangu wakose fursa ya elimu," anasema Agnes.
Kiongiozi wa Kisiwa cha Ikulu Baharini, Juma, alisema watoto kukosa
elimu na kuishia kuwa wavuvi kwa sababu ya kukosekana kwa shule ni janga
kubwa kwao na taifa.
Alisema kwavile serikali inafahamu kwamba kwenye visiwa kuna mamia ya
watu ambao ni Watanzania halisi, inapaswa kuchukua hatua sahihi ya
kuwajengea shule.
Kiongozi wa Kisiwa cha Ito, Neema Elias, alisema eneo hilo lina wakazi
(wavuvi) zaidi ya 500, lakini hakuna shule kwa ajili ya watoto wao.
Aliongeza kuwa tatizo la watoto kukosa elimu kwa sababu ya serikali
kutokubali kujenga shule lipo pia katika visiwa vingine vingi miongoni
mwa visiwa 35 vilivyopo katika Ziwa Victoria, hasa kwenye eneo la Wilaya
ya Sengerema.
Alisema licha ya kukosekana shule katika eneo hilo, lakini pia wamepata
maagizo ya serikali kwamba kamwe hawaruhusiwa kuishi kisiwani humo
wakiwa na watoto wao.
"Hii siyo sawa. Wazazi wanapozaa watoto wanalazimishwa kuwaondoa watoto
kwa madai kwamba hakuna shule na tunatakiwa kuwapeleka kwa ndugu, jamaa
na marafiki walio katika maeneo yenye shule, nje kabisa ya visiwa.
Lakini hili limeshindikana... bado tunaishi na watoto wetu na matokeo
yake wanakosa elimu," anasema.
OFISA ELIMU, MBUNGE
Akizungumzia tatizo la kukosekana kwa shule, Ofisa mtendaji wa Kata ya
Nyakasasa, Mathayo Kanisiro alisema, eneo la visiwa hivyo ni msitu wa
hifadhi na kwamba serikali imeagiza pasijengwe nyumba wala jengo lolote
la kudumu.
Kanisiro alikiri kwamba hakuna namna ya kufanya, lakini amekuwa
akistushwa na ukubwa wa tatizo kwani watoto wanaoishi na wazazi wao
katika visiwa hivyo bila kupata haki yao ya msingi ya elimu imezidi
kuongezeka.
Diwani wa Kata ya Nyakasasa, Avoid Geogratias, anasema eneo hilo la
visiwa wanalokalia wavuvi na familia zao, lilitengwa kwa ajili ya
hifadhi ya mistu miaka mingi iliyopita na kwamba, awali, wavuvi
waliruhusiwa kuishi huko ili kulinda misitu huo dhidi ya watu waliokuwa
wanapasua mbao.
Naye, kama ilivyo kwa Kanisiro, alisema hana namna yoyote ya kuwasaidia
watoto hao ili wapate nafasi ya kusoma na kwamba, anajua kwamba watoto
wamezidi kuwa wengi kama wanavyoongezeka wazazi wao (wavuvi).
Ofisa Elimu wa Wilaya ya Sengerema, Juma Mwajombe, alisema kuwa siku za
nyuma kulikuwa na utaratibu wa wa wazazi kuchangishana fedha kisha
kuwapeleka watoto wao kusoma nje ya visiwa. Lakini mpango huo ulifikia
mwisho mwaka 2010 baada ya kutokea ajali ya kuzama kwa mtumbwi na
wanafunzi 18 walipoteza maisha.
"Baada ya kutokea kwa ajali hiyo, zoezi hilo lilisimamishwa na hadi sasa
watoto wengi wameendelea kuishi visiwani bila kupata elimu," alisema
Mwajombe, aliyeelezea wasiwasi mwingine kuwa huenda misitu itakuwa
hatarini kwa sababu baadhi ya wakazi wa visiwani wataona hakuna haja ya
kulinda misitu wakati watoto wao wakikosa elimu kwa kutojengewa shule
kwa sababu ya zuio litokanalo na sheria ya kulinda misitu.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Sengerema, Consolata Magaka, alisema
serikali inafahamu shida wanayopata wazazi na watoto walio kweney visiwa
kama Kome Mchangani, lakini hakuna namna ya kufanya.
Alisema serikali haiwezi kupeleka huduma za shule kwa kuwa wananchi hao
wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi wako aktika eneo la hifadhi ya
misitu.
Mbunge wa jimbo la Buchosa Wilaya ya Sengerema, Charles Tizeba,
aliiambia NIPASHE kuwa, kama kuna mwananchi anayetaka kuendelea kukaa
kisiwani (kama Kome) ambako ni hifadhi ya misitu, lazima amuondoe mtoto
wake huko na kumrudidisha alikozaliwa ili ampatie fursa ya kusoma.
Alisema hawezi kuwatetea wananchi wake hao kujengewa shule visiwani,
kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria ya misitu ambayo inakataza kuwapo
kwa majengo ya kudumu.
Akizungumza na NIPASHE, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Focus
Majimbi, alisema ni vigumu kujenga shule kwenye kisiwa cha Kome na
visiwa vingine vya hifadhi ya misitu kwani sheria inazuia maeneo hayo
(ya hifadhi ya misitu) kujengwa majengo ya kudumu. Aliitaja sheria hiyo
kuwa ni namba 14, ya mwaka 2002, kifungu cha 26.
Majimbi alikiri kwamba suala la ukosefu wa elimu kwa watoto ni baya na
lina athari kubwa. Alisisitiza kuwa, kwa kuzingatia sheria hiyo ya
hifadhi ya misitu, maeneo ya visiwa hivyo hayatakiwi kujengwa shule wala
jengo lolote la kudumu na kwamba serikali imeagiza kuhamisha watoto
wote walioko huko ili wakasome katika maeneo mengine.
Hata hivyo, amri hiyo ya serikali ya kutaka watoto wanaozaliwa huko
waondoshwe inakiuka sheria nyingine ya nchi; namba 21 ya mwaka 2009
ambayo inalinda haki za watoto wenye umri chini ya miaka 18.
Wilaya ya Sengerema ina ukubwa wa kilomita za mraba, 8,817 na kati ya
hizo, kilomita za mraba 3,335 ni nchi kavu sawa na asilimia 38 na
kilomita 5, 832 ni nchi kavu, sawa na asilimia 62.
Kwa mujibu sensa ya watu na makazi ya mwaka 2010, wilaya hiyo ina watu
662,166 na kati ya hao, wanaume ni 335,756 na wanawake ni 326,410.