|
james mbatia |
Mbunge James Mbatia unajisumbua. Natambua uchungu ulio nao juu ya
kudorora kwa sekta ya elimu, na natambua uhitaji wako wa mabadiliko
katika sekta hii mapema inavyowezekana, lakini unajisumbua.
Sisemi kuwa ukate tamaa, na mimi sikati tamaa, ila naona unazungumza na
watu ambao hawawezi kuelewa maana ya kile unachosema na kuhimiza. Nataka
nieleza yafuatayo.
Mwaka jana ulipozungumza kuhusu mitaala, kuwa hakuna na kuwa sekta ya
elimu inaendeshwa mzobemzobe kama Waluguru ambavyo wangesema, na kuwa
vitabu vinavyotumika katika shule zetu havina uhakika wa ubora wake
walikubeza, walikutukana, walikutenga, na kukuona mzushi.
Lakini wiki mbili baada ya kuahirishwa kwa Bunge, matokeo ya mitihani
yakatoka, na kilichotokea, kuhusu kufeli kwa wanafunzi, Mungu tu anajua.
Mungu alikulipia na kuwaaibisha wale waliodhani kuwa ulikuwa mzushi,
na ukarabati uliofanyika kuhusiana na matokeo hayo, na unaondelea
kufanyika, sijui, ni suala la kuliombea taifa liondokane na pepo huyu
ambaye hataki sisi tulioko serikalini tusikilize mawazo ya wananchi
wenzetu.
Kuwa wananchi wenzetu wanapotushauri wanaonekana kuwa ni adui, na kuwa
lengo lao sio kujenga ufanisi katika kutoa huduma bali kwa waliotupigia
kura, bali kwa sababu wanataka kutujengea hoja tushidwe uchaguzi ujao.
Mbatia, unapokuwa na serikali ambayo wasiwasi wake ni kama itashindwa
uchaguzi wa miaka mitano ijayo, na sio kama miaka mitano ijayo watakuwa
na cha kuwaonyesha wananchi, katika orodha ndefu ya ahadi ndani na nje
ya ilani ya uchaguzi waliyoinadi, sidhani kama unachokisema kitaeleweka.
Tumeona mwaka 2011, mara baada ya uchaguzi malumbano yakaanza ndani ya
wanaserikali na walioko nje ya serikali, lakini wote wa chama kimoja,
wakifanya maandalizi ya uchaguzi wa 2015.
Vikundi vya uchaguzi wa 2010 havikuvunjwa, kwa kweli vikaimarishwa na
kampeni za uchaguzi kiaina zikaanza kwa makini kabisa, hadi walipoonyana
wenyewe kwa wenyewe, lakini wale wenye masikio magumu wanaendelea bila
kujali kitu.
Sasa hawa watu unapowaambia kuhusu kuimarisha sekta ya elimu unadhani
inawezekana kweli, mawazo sio katika huduma bali katika kufanikisha
chaguzi.
Mbunge Mbatia, maendeleo kwa wananchi kwa sasa, wewe unajua, sio kigezo cha kuchaguliwa. Hizo siasa zako ni za kizamani.
Sasa hivi unachaguliwa kwa sababu unaweza kutoa takrima, unaweza
kuwanunulia watu ubwabwa wakashiba, ukawanunulia watu t-shirts, kofia na
khanga, na kuwaimbisha nyimbo jioni wakala wakashiba.
Wananchi wa siku hizi hawaoni uhakiki wa utendaji wa walio madarakani
kama ni kigezo, bali uwezo wake wa kutoa rushwa kwa wapiga kura. Sasa
unapokuwa na uhakika wa kushinda kwa kutumia fedha na sio utendaji,
unaanzaje kufikiria kuboresha elimu.
Elimu haikuwa kwenye ajenda wakati wa uchaguzi, ilitamkwa majukwaani kwa
sababu mdomo haukosi cha kuzungumza ukikaa mbele ya kinasa sauti.
Kitu kingine ambacho unanishangaza James Mbatia ni kuwa huoni dunia
inakwendaje?. Fasheni siku hizi ni kuhakikisha kuwa watoto wanakwenda
kusoma nje, na kama ni ndani basi katika shule za watu wakubwa, na wewe
ukiwemo, nitashangaa kama haumo, kuwapeleka watoto kwenye English
Medium, au sijui International Schools.
Unashangaa, mimi hapa ni waziri wa elimu, ofisa elimu, mkurugenzi wa
elimu, mwalimu wa sekondari au mwalimu wa shule ya msingi, nimepewa
dhamana ya kuhakikisha kuwa elimu inaboreshwa, na tulidhani kigezo
kimojawapo ni kutuona sisi wenyewe tunawasomesha watoto wetu nje au
ndani, lakini katika shule za serikali.
Lakini aka! Sasa kama tuliopewa dhamana ya kuboresha elimu tunakwepa
shule zetu wenyewe, si ujue kuwa kuna jambo ambalo ni bovu tunaliona, na
hatusemi ila tunawahamisha watoto wetu. Watoto wa masikini wajua wapi
pa kuwapeleka wa kwao.
Kumeundwa kampeni kuwa wazazi wawagharimie watoto wao, badala ya
kuimarisha shule za serikali, wanahimiza kuanzisha shule za binafsi.
Hivi kama kweli serikali ina nia ya kuboresha elimu, hao wazazi ambao
wanalipa mabilioni ya fedha kwa ajili ya watoto wao, kama wangelipa
robo tu ya hizo fedha kwenye shule za serikali kama ada, na serikali
ikaweza kuboresha huduma na ubora wa, elimu, kungekuwa kweli na
malalamiko dhidi ya sekta ya elimu?
Tungewaokoa wazazi wangapi ambao wanalipa ada kwenye shule ambazo hazina
chochote ila utapeli. Lakini nadhani hatuwezi kufikiria kwa umakini.
Tunataka majibu rahisi kwa kitu kigumu, na hatutaki kufikiria kwa mkakati—strategically, bali kwa kuishi kama tulivyozoea.
Mbatia, tunahitaji kupungwa pepo huyu ambaye hataki kusikiliza vilio vya Watanzania kuhusu elimu.