Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 22 Januari 2014

mabadiliko baraza la mawaziri kila mmoja na mtizamo wake

Hatimaye Baraza jipya la Mawaziri limetangazwa , tumeshuhudia mabadiliko katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo Naibu Waziri wa Elimu wa sasa ni Mh. Jenista Mhagama amechukua nafasi ya Mh. Philipo Mulugo. Wako watanzania wanayaona mabadiliko haya kutokuwa na tija huku wengine wakiamini mabadiliko yanaweza kutokea, wote wana sababu za msingi kabisa kuamini kile wanachoamini. Je mdau wa elimu ni mambo yapi Uongozi wa sasa unatakiwa kuyazingatia/kuyafanya ili kuhakikisha kiwango cha elimu nchini kinapanda na wanafunzi kote nchini wanapata elimu bora? Tafakari na tushikirikishane
 
chanzo haki elimu facebook page

Habari TATU KALI zinazohusu masuala ya Elimu nchini Tanzania zinazopamba katika vyombo vya habari tarehe 22 January 2014



1. Wanafunzi 11,000 katika mkoa wa DSM wamekosa nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza licha ya kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana. (Chanzo: Habari Leo)

2. Mkuu wa Wilaya ya Nzega ameagiza wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari wilayani humo waliokatishwa masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba, utoro n.k (Chanzo:Tanzania Daima)

3. VETA yaanzisha maabara za LUGHA katika vyuo vyake ili kuwezesha ufundishaji wa lugha za kigeni kwa ubora zaidi na kuondoa tatizo la watanzania kushindwa kujieleza kwa lugha za kigeni. ( Chanzo: The Guardian)
 
chanzo haki elimu page

Jumanne, 21 Januari 2014

waliofeli kidato cha pili kuendelea na masomo

Wakati Watanzania wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013, imebaini kuwa Serikali imetoa agizo kwamba wanafunzi wote waliofeli mtihani huo kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, huku wakisoma mafunzo ya kurudia mtihani wa kidato cha pili.

Licha ya matokeo hayo kutotangazwa hadi sasa, imebainika kuwa waliofaulu mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21 mwaka jana ni asilimia 62 tu, asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili mwaka huu, huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo kwa mara ya pili.

Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.

Uamuzi huo wa Serikali ni tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa Novemba 4, mwaka 2012, kwamba kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo na kwamba atakayefeli atatimuliwa.

Dk Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.

Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.

Gazeti hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16 mwaka huu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu nchini, wakiwamo maofisa elimu wa mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (TAMONGSCO).

Katika barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na masomo ya kidato cha tatu.

“Matokeo ya kidato cha pili yamepokewa na kufanyiwa uchambuzi ili kupata taswira ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo imebaini kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kufaulu ni sawa na asilimia 62 tu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza;

“Hali hii inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi watatakiwa kukariri kidato cha pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara ya pili ambao ni asilimia saba wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya mfumo rasmi.”

Barua hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 na kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2014, wakati awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa kufikisha alama 30 watatimuliwa.

“Wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi 39 wapewe mafunzo rekebishi ‘Remedial class’ wakiwa kidato cha tatu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.


Inaeleza kuwa uamuzi huo unawahusu wote wakiwamo wale walioshindwa kwa mara ya pili, “Kwa maana hiyo hakuna mwanafunzi atakayerudishwa nyumbani.”

Mwisho barua hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa inawapa taarifa mameneja na wamiliki wa shule na seminari ili kusimamia utekelezaji wa uamuzi kuhusu matokeo hayo.

Kauli ya wizara

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Profesa Mchome alisema, “Suala la wizara kuagiza wanafunzi wote waliofeli kuendelea na masomo ya kidato cha tatu mimi sijalisikia, ninachojua ni kwamba wapo watakaorudia.”

Alisema kuwa tayari wizara imeshapeleka taarifa za matokeo hayo na uamuzi wa Serikali katika kila kanda nchini. “Kila shule ina taarifa hizo. Wapo wanafunzi watakaorudia.”

Akizungumza kuhusu matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013 kutotoka mpaka sasa alisema, “Ninachofahamu ni kwamba matokeo ya kidato cha pili yameshawasilishwa katika kanda zote nchini.”

“Unajua matokeo ya kidato cha pili siyo kama matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na sita. Matokeo ya kidato cha pili ni kama mwendelezo wa tathmini ‘Continuous assessment’ kwa mwanafunzi, hutumika pia katika mtihani wa kidato cha nne.”

Alisema ndiyo maana matokeo hayo hupelekwa katika shule husika. “Baada ya kupelekwa katika shule husika, hapo ndipo inaweza kutolewa taarifa za matokeo hayo pamoja na ufafanuzi.”

Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Dk Kawambwa na Naibu wake, Phillip Mulugo ili kutolea ufafanuzi suala hilo, lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.

Msimamo wa TAMONGSCO

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya kueleza kama wanakubaliana na agizo hilo la Serikali alisema, “Inaonekana Serikali haiko tayari kutekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).”

“Kama wizara inalazimisha wanafunzi walio na ufaulu mdogo kuendelea na masomo katika mfumo wa vidato (formal education), lazima tutegemee kuona wanafunzi wakifanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne.”

Alisema kuwa asilimia 98 ya wanachama wa chama hicho ni Watanzania wazalendo kwamba hawapo tayari kutekeleza agizo la Serikali kwa sababu siyo la kizalendo na limetolewa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa ya kujiongezea umaarufu wa muda mfupi, huku Watanzania wakiogelea kwenye dimbwi la umaskini unaotokana na ujinga.

“Wachache watakaosaliti msimamo huu watakuwa wamekubali kupoteza muda wa vijana wetu huku wakijua kwamba watafika kidato cha nne, kupata daraja sifuri na kuishia kuwa machangudoa, wauza dawa za kulevya, bangi, wizi na vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema.

Alisema ili kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo yao; “Mwanafunzi ambaye ufaulu wake utakuwa chini ya asilimia 45 aondolewe katika mfumo wa elimu ya vidato (formal education) na kuingizwa katika mfumo wa elimu ya ufundi mchundo (TVET - Technical education and vocational education).”

Alisema wanachama wa Tamongsco wanamiliki vyuo 586 kati ya vyuo 750 vya ufundi mchundo (VETA) na wanamiliki vyuo 1975 kati ya vyuo 1988 vya ufundi stadi (technical institutes) ambavyo vinasimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Stadi (NACTE).

“Vyuo hivi vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wote ambao wana ufaulu wa chini ya asilimia 45 kuwaendeleza hadi chuo kikuu. Kikwazo pekee kilichopo ni kwa Serikali kukubali kuchangia gharama za uendeshaji wake.”

“Kikwazo hiki kitaondoka endapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakubali kutekeleza sera, sheria na kanuni za ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) partnership) kama ilivyopitishwa na Bunge mwaka 2010.

Kidato cha pili 2012

Katika mtihani huo mwaka 2012 wanafunzi 136,923 kati ya 386,271 waliofanya mtihani huo walifeli. Idadi ya waliofeli ilikuwa sawa na asilimia 35.5, wakiwamo wasichana 74,020 na wavulana 62,903, waliofaulu walikuwa wanafunzi 245.9,32.


CHANZO: Mwananchi

Ijumaa, 10 Januari 2014

Baba wa miaka 54 aoa mtoto wa miaka minane

Bunda. Polisi Wilaya ya Bunda, wanamshikilia baba mwenye umri wa miaka 54 kwa tuhuma kuoa mwanafunzi wa kike wa umri wa miaka minane.
Msimamizi wa Dawati la Jinsia katika Kituo Kikuu cha Polisi Bunda, Rita Charles alisema baba huyo mkazi wa Kijiji cha Nyaburundu wilayani Bunda alikamatwa jana akiwa anaishi na binti huyo (jina limehifadhiwa) kama mke wa nyumbani baada ya kutoa kishika uchumba kiasi cha Sh55,000 kwa wazazi wake.
Ilielezwa kuwa mwanaume huyo kabla ya kumwoa mtoto huyo aliyekuwa anasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Nyaburundu, alimchumbia kwa wazazi wake na kutakiwa atoe ng’ombe watano za mahari ndipo akatoa kishika uchumba hicho na mtoto huyo kuondolewa shule. “Tulifanikiwa kumkamata mwanamume huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema,” alisema Rita.
Alisema siku ya Mwaka Mpya, alichukuliwa na dada yake na kumpeleka kwa mume wake huyo ili aanze maisha ya ndoa.
Hata hivyo, alisema alipofika, usiku huo walilala kitanda kimoja wote watatu (baba muoaji, muolewaji na dada wa muolewaji) na kwamba mwanamume huyo alianza kufanya mapenzi na dada yake na baadaye akamgeukia ‘mkewe’ kuanza kumnyonya maziwa.
“Tulilala wote watatu na alifanya mapenzi na dada yangu, mimi akininyonya maziwa,” alisema mtoto.

chanzo. mwananchi

uandikishwaji wa wanafunzi darasa la kwanza baadhi ya mikoa kuna changamoto

Zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wapya wa darasa la kwanza mwaka huu limeanza na misukosuko ya aina yake. Baadhi ya maeneo nchini yamekumbwa na mgogoro mkubwa baina ya wazazi na walimu, chanzo kikitajwa kuwa ni pamoja na gharama ambazo kila mtoto hutakiwa alipiwe na wazazi wake kabla ya kupatiwa fursa ya kuandikishwa.

Taarifa zilizoripotiwa jana zilionyesha kuwa mjini Morogoro hali haikuwa shwari. Vurugu kubwa ziliibuka na mwishowe baadhi ya wazazi wanaodaiwa kuwa ni wenye itikadi tofauti za vyama walivaana mwilini.

Katika kisa hicho, inalezwa kuwa kila mzazi alitakiwa alipe walau Sh.50,000 ndipo kila mtoto aliyempeleka shuleni apate fursa ya kuandikishwa. Kwamba, baadhi ya wazazi wenye uwezo kifedha walilipia gharama hizo bila shida. Hata hivyo, wengine wakataka watoto wao waendelee kuandikishwa hata kama walikosa fedha hizo kwavile si sera ya serikali kuwabagua wananchi wake kwa kigezo cha pesa.

Inadaiwa kuwa sintofahamu hiyo ikakolezwa na itikadi za vyama baada ya mzazi mmojawapo anayedaiwa kuwa ni wa chama tawala kutetea ulipaji wa gharama hizo huku mwingine anayedhaniwa kuwa ni wa upinzani akipinga vikali. Mwishowe wawili hao wakavaana kwa nia ya kushikishana adabu. Walishindwa kukubaliana juu ya kutofautiana kwao.

NIPASHE hatukusudii kujadili ugomvi baina ya wazazi hao wa Morogoro. Na wala siyo lengo letu pia kuwa mahakimu na kueleza ni nani kati yao aliye sahihi. Bali, tunalichukulia tukio hili kuwa ni mfano wa kile kinachotokea katika maeneo mengi nchini.

Kwamba, katika kipindi hiki, baadhi ya walimu wakuu huwageuza wazazi kuwa mtaji. Huanzisha michango mingi kwa visingizio mbalimbali, lengo likiwa ni kuwakamua wazazi hadi tone la mwisho. Katika hili, sisi hatuoni kuwa ni sahihi. Siyo haki hata kidogo kuwabebesha wazazi mzigo mzito wa gharama za elimu kupitia rundo la michango inayoanzishwa kwa visingizio mbalimbali.

Kwa mfano, sisi tunaona kuwa kuwalazimisha wazazi kulipa Sh. 50,000 kwa kila mtoto ndipo haki ya kuandikishwa shule ipatikane siyo uamuzi sahihi. Tunaamini hivyo kutokana na ukweli kuwa mara zote, serikali yetu imekuwa ikisisitiza kuwa elimu ya msingi ni lazima kwa kila mtoto aliyefikisha umri wa kwenda shule. Tena, kadri ya ufahamu wetu, elimu hii hutolewa bure.

Abadan, michango ya aina yoyote ile haiwezi kuwa chanzo cha mwanafunzi wa darasa la kwanza kunyimwa haki yake ya kuandikishwa. Na ndiyo maana, kwa tukio la Morogoro, Mbunge wa Jimbo hilo aliingilia kati na kuwataka walimu kuwaandikisha watoto wote bila kujali kama wazazi wao wamelipa mchango wa Sh. 50,000 ama la. Ni kwa sababu elimu ya msingi ni ya lazima, na tena ni haki ya kila mtoto.

Isitoshe, kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali za elimu nchini, umri wa kuanza darasa la kwanza una ukomo wake. Kutomuandikisha mtoto aliyefikia umri wa kuanza shule ni kumpa adhabu asiyostahili kwani kuna uwezekano mkubwa wa kukataliwa katika mwaka unaofuata kutokana na kigezo cha kuwa na umri mkubwa. Matokeo yake, taifa litakuwa katika hatari ya kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika. Hili siyo jambo zuri hata kidogo.

NIPASHE hatupingi hatua ya wananchi kutakiwa kuchangia maendeleo yao, yakiwamo ya elimu. Hata hivyo, michango hii haipaswi kuwa chanzo cha kuongeza kwa idadi ya wasiojua kusoma na kuandika. Haipaswi vilevile kuwa chanzo cha kuligawa taifa kwa misingi ya wenye nacho na wasio nacho. Isitoshe, tunadhani kwamba sasa kuna kila sababu kwa viongozi wanaosimamia elimu kuingilia kati na kusimamia kwa vitendo kauli zao mbalimbali zinazosisitiza kuwa elimu ya msingi ni ya lazima kwa kila mtoto na kwamba, hakuna ada wala michango yoyote ya lazima.

Kuachia hali iendelee kuwa kama Morogoro ni hatari. Ni kuichafua serikali ambayo lengo lake zuri la kutoa elimu ya msingi bure linaelekea kutibuliwa na watu wachache walio na vipaji vya kubuni kila aina ya michango ili kuwakamua wazazi kwa maslahi yanayotiliwa shaka.

Michango mingi kama ya madawati, ya uji, ya ulinzi, ya nembo za shule na ya mitihani kwa shule za msingi haipaswi hata kidogo kutumiwa kwa maslahi ya wachache kwani athari za kuwa na taifa lililojaa watu wasiojua kusoma na kuandika ni kubwa sana na kamwe hazipimiki kirahisi.

Shime, michango hii katika uandikishaji wa wanafunzi wapya wa darasa la kwanza isitumiwe kubagua wasio na uwezo.

chanzo Nipashe

Alhamisi, 19 Desemba 2013

Waziri wa elimu adai yeye si waziri mzigo




Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ameamua kuvunja ukimya na kueleza kuwa yeye si waziri mzigo na wala hashtushwi na jina hilo kwani hawezi kuzuia maamuzi ya watu kumuita hivyo.

Dk. Kawambwa amesema yeye ni mchapakazi na tayari juhudi za kiutendaji katika wizara anayoiongoza zimeanza kuonekana.

Amesema kuwa suala la kuitwa waziri mzigo linatokana na yeye kuwa kioo na dira ya wenzake  katika wizara hiyo na hivyo majina kama hayo hayawezi kukwepeka na wala kuathiri utendaji wake na kujivunia kuwa yeye ni mmoja wa wasimamizi wa upatikanaji bora wa elimu hapa nchini.

 Waziri Kawamba aliamua kuvunja ukimya huo wakati akifungua kikao cha kazi cha maofisa elimu wa mikoa na halmashauri kinachojadili maendeleo ya elimu ya msingi hapa nchini pamoja na kufanya udahili wa pamoja katika matokeo ya darasa la saba.

"Kuna mtikisiko mkubwa katika wizara yetu na mengi yanasemwa wote mnasikia na Watanzania wanafahamu. Tupo katika safari nzito lakini ili gari liondoke, lazima kwanza litikisike, hivyo msiwe na wasiwasi tutafika salama tu," alisema Dk. Kawambwa.

Alisema anashangazwa kuitwa mzigo kwani kutokana na uwajibikaji wake katika wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, wamepata mafanikio makubwa hususani katika kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2013.

 Alisema kutokana na jitihada zake na kushirikiana na watendaji na wadau mbalimbali, kiwango cha ufaulu mwaka 2013 kwa wahitimu wa elimu hiyo ya msingi

kimeongezeka kutoka asilimia 31 mwaka uliopita hadi kufikia asilimia 50.61 mwaka 2013 ambao ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 19.89 ukilinganishwa na mwaka jana.

Waziri Kawambwa alisema jumla ya watahiniwa 844,938 walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi na kati yao 427,606 sawa na asilimia 50.61, wamefaulu kwa zaidi ya alama 100 kati ya 250 matokeo ambayo aliyaita ni mazuri.

Alisema kuwa kati ya watahiniwa hao waliofaulu, wasichana ni 208,227 sawa na asilimia 46.68 na wavulana ni 219,379 sawa na asilimia 55.01kitu ambacho kimeinua kiwango cha ufaulu.

Hata hivyo, alisema ufaulu huo bado haujafikiwa lengo la mpango wa Matokeo Makubwa Sasa la kufikia asilimia 60, lakini kutokana na jitihada na kipindi kifupi tangu mpango huo utangazwe, ni wazi kuwa kazi imefanyika na kustahili kupongezwa.

Jumatano, 18 Desemba 2013

Serikali yagomea CWT kuhusu kima cha chini cha mishahara


 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.Shukuru Kawambwa


Serikali  imesema haiwezi kuongeza vianzio vya mishahara kwa asilimia 53 kama Chama cha Walimu Nchini (CWT) kinavyotaka kwa kuwa fedha hizo ni zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Bungeni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso (Chadema).

Pareso alitaka kujua ni lini serikali italipa malimbikizo ya walimu yakiwamo yanayotokana na kupandishwa madaraja.

Pia alihoji serikali inapata kigugumizi gani kulipa nyongeza ya asilimia 50 ya mishahara kwa kadiri walivyokubaliana na CWT.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kufahamu mpaka sasa serikali imeshughulikiaje madai ya stahili za walimu hapa nchini.

Akijibu maswali hayo,  Dk. Kawambwa alisema serikali imejipanga kuondokana na madeni ya walimu.

Alisema zoezi linaloendelea hivi sasa ni uhakiki wa madeni ya serikali kwa ushiriki kikamilifu na CWT.

Hata hivyo, alisema madai ambayo CWT yaliyotaka nyongeza ya asilimia 53 kwa vianzia vya mishahara yanazidi bajeti ya mishahara yote ya watumishi wa serikali nchin.Kwa msingi huo alisema hakukuwa na namna ambayo serikali ingelipa.

Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikiongeza mishahara kwa walimu ambapo mpaka sasa imeshaongeza asilimia 30.9.

Aidha, alisema serikali na CWT wanaendelea na majadiliano kuhusiana na madai hayo ya walimu na tayari vikao vinane vimefanyika.

“Katika vikao hivyo, serikali iliahidi kutoa nyongeza ya wastani wa asilimia 14.62 ya vianzia vya mishahara ya walimu wakati CWT walishuka kutoka asilimia 100 hadi asilimia 53 ya nyongeza waliyokuwa wanadai,” alisema.

Chanzo Ippmedia.com