Wakati Watanzania
wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013, imebaini kuwa Serikali
imetoa agizo kwamba wanafunzi wote waliofeli mtihani huo kuendelea na
masomo ya kidato cha tatu, huku wakisoma mafunzo ya kurudia mtihani wa
kidato cha pili.
Licha ya matokeo hayo kutotangazwa hadi sasa, imebainika kuwa waliofaulu
mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21 mwaka jana ni asilimia 62 tu,
asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili mwaka huu,
huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo kwa mara ya pili.
Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.
Uamuzi huo wa Serikali ni tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa Novemba 4, mwaka 2012, kwamba
kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo na
kwamba atakayefeli atatimuliwa.
Dk Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yatatumika
kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa
watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na
endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka
utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Gazeti hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16 mwaka huu na Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Profesa
Sifuni Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu nchini, wakiwamo maofisa elimu
wa mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (TAMONGSCO).
Katika barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa
wanafunzi watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na masomo ya kidato cha
tatu.
“Matokeo ya kidato cha pili yamepokewa na kufanyiwa uchambuzi ili kupata
taswira ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo imebaini kuwa watahiniwa
waliofanya mtihani na kufaulu ni sawa na asilimia 62 tu,” inaeleza
sehemu ya barua hiyo na kuongeza;
“Hali hii inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi watatakiwa kukariri
kidato cha pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara ya pili ambao ni
asilimia saba wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya mfumo rasmi.”
Barua hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 na
kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2014, wakati
awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa kufikisha alama 30
watatimuliwa.
“Wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi 39 wapewe mafunzo
rekebishi ‘Remedial class’ wakiwa kidato cha tatu,” inaeleza sehemu ya
barua hiyo.
Inaeleza kuwa uamuzi huo unawahusu wote wakiwamo wale walioshindwa kwa
mara ya pili, “Kwa maana hiyo hakuna mwanafunzi atakayerudishwa
nyumbani.”
Mwisho barua hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa inawapa taarifa
mameneja na wamiliki wa shule na seminari ili kusimamia utekelezaji wa
uamuzi kuhusu matokeo hayo.
Kauli ya wizara
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Profesa Mchome alisema, “Suala la wizara
kuagiza wanafunzi wote waliofeli kuendelea na masomo ya kidato cha tatu
mimi sijalisikia, ninachojua ni kwamba wapo watakaorudia.”
Alisema kuwa tayari wizara imeshapeleka taarifa za matokeo hayo na
uamuzi wa Serikali katika kila kanda nchini. “Kila shule ina taarifa
hizo. Wapo wanafunzi watakaorudia.”
Akizungumza kuhusu matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013 kutotoka mpaka
sasa alisema, “Ninachofahamu ni kwamba matokeo ya kidato cha pili
yameshawasilishwa katika kanda zote nchini.”
“Unajua matokeo ya kidato cha pili siyo kama matokeo ya darasa la saba,
kidato cha nne na sita. Matokeo ya kidato cha pili ni kama mwendelezo wa
tathmini ‘Continuous assessment’ kwa mwanafunzi, hutumika pia katika
mtihani wa kidato cha nne.”
Alisema ndiyo maana matokeo hayo hupelekwa katika shule husika. “Baada
ya kupelekwa katika shule husika, hapo ndipo inaweza kutolewa taarifa za
matokeo hayo pamoja na ufafanuzi.”
Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Dk Kawambwa na Naibu wake,
Phillip Mulugo ili kutolea ufafanuzi suala hilo, lakini simu zao za
mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.
Msimamo wa TAMONGSCO
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya kueleza kama
wanakubaliana na agizo hilo la Serikali alisema, “Inaonekana Serikali
haiko tayari kutekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).”
“Kama wizara inalazimisha wanafunzi walio na ufaulu mdogo kuendelea na
masomo katika mfumo wa vidato (formal education), lazima tutegemee kuona
wanafunzi wakifanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne.”
Alisema kuwa asilimia 98 ya wanachama wa chama hicho ni Watanzania
wazalendo kwamba hawapo tayari kutekeleza agizo la Serikali kwa sababu
siyo la kizalendo na limetolewa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa
ya kujiongezea umaarufu wa muda mfupi, huku Watanzania wakiogelea
kwenye dimbwi la umaskini unaotokana na ujinga.
“Wachache watakaosaliti msimamo huu watakuwa wamekubali kupoteza muda wa
vijana wetu huku wakijua kwamba watafika kidato cha nne, kupata daraja
sifuri na kuishia kuwa machangudoa, wauza dawa za kulevya, bangi, wizi
na vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema.
Alisema ili kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo yao;
“Mwanafunzi ambaye ufaulu wake utakuwa chini ya asilimia 45 aondolewe
katika mfumo wa elimu ya vidato (formal education) na kuingizwa katika
mfumo wa elimu ya ufundi mchundo (TVET - Technical education and
vocational education).”
Alisema wanachama wa Tamongsco wanamiliki vyuo 586 kati ya vyuo 750 vya
ufundi mchundo (VETA) na wanamiliki vyuo 1975 kati ya vyuo 1988 vya
ufundi stadi (technical institutes) ambavyo vinasimamiwa na Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi Stadi (NACTE).
“Vyuo hivi vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wote ambao wana ufaulu wa
chini ya asilimia 45 kuwaendeleza hadi chuo kikuu. Kikwazo pekee
kilichopo ni kwa Serikali kukubali kuchangia gharama za uendeshaji
wake.”
“Kikwazo hiki kitaondoka endapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
itakubali kutekeleza sera, sheria na kanuni za ushirikiano kati ya sekta
ya umma na binafsi (PPP) partnership) kama ilivyopitishwa na Bunge
mwaka 2010.
Kidato cha pili 2012
Katika mtihani huo mwaka 2012 wanafunzi 136,923 kati ya 386,271
waliofanya mtihani huo walifeli. Idadi ya waliofeli ilikuwa sawa na
asilimia 35.5, wakiwamo wasichana 74,020 na wavulana 62,903, waliofaulu
walikuwa wanafunzi 245.9,32.
CHANZO: Mwananchi
harakati za marafiki wa elimu musoma wasiliana nasi kwa namba +255755 650 075 au +255786 650 075 ni jukumu letu kuboresha elimu
HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni