Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 6 Februari 2014

makala kusoma kuhesabu tatizo kubwa kwa wanafunzi nchini

Tangu mwaka 2010, taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza kupitia mradi wake wa Uwezo, imekuwa ikifanya tafiti katika nchi za Afrika Mashariki zinazolenga kubaini uwezo wa watoto wa shule za msingi katika stadi za kusoma na kuhesabu.
Majaribio haya, yamekuwa yakihusisha masomo ya Hesabu na lugha za Kiswahili na Kiingereza kwa ngazi ya darasa la pili. Sampuli hujumuisha wanafunzi wa darasa la tatu na darasa la saba.
Sampuli ya washiriki
Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2010 watoto walioshirikishwa kwenye utafii huo walikuwa 37,683 mwaka 2011 wanafunzi 114,761 na mwaka 2012 wanafunzi walioshiriki ni 104,568.
Kwa upande wa kaya, mwaka 2010 zilishiriki kaya 18,952 mwaka 2011 zilikuwa kaya 59,992 na mwaka 2012 kaya. 55,191. Kwa wilaya, mwaka 2010 zilishiriki Wilaya 38, mwaka 2011 zilikuwa wilaya 119 na mwaka 2012 wilaya 126.
Shule zilizoshiriki kwenye utafiti uliofanyika mwaka 2010 zilikuwa ni 1,010 mwaka 2011 zilikuwa 3,709 na mwaka jana zikawa 3,624.
Mratibu wa Uwezo upande wa Tanzania, Zaida Mgalla anasema aghlabu majaribio hayo hutayarishwa kwa pamoja na wataalamu wa masomo kutoka vyuo vikuu, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na walimu wa masomo husika wa darasa la pili.
Matokeo 2010
Utafiti huu ulipofanywa mwaka 2010 ulionyesha kuwa, japo Kiswahili ni lugha inayozungumzwa kwa upana zaidi nchini, idadi kubwa ya watoto hawawezi kusoma kupitia lugha hiyo.
“Kwenye sampuli zetu, chini ya nusu (42.2 asilimia) ya watoto waliofanyiwa uchunguzi waliweza kusoma kwa hatua ya hadithi. Wakati watoto wote katika darasa la tatu wanapaswa kuweza kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, watoto chini ya mmoja kati ya watatu (32.7 asilimia) ndio wanaweza.
‘’Hata hivyo, hadi wanamaliza shule ya msingi, mtoto mmoja kati ya 5 hawezi kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, licha ya kumaliza miaka saba ya elimu ya msingi,”inasema sehemu ya utafiti huo.
Kwa upande wa Kiingereza, ripoti hiyo ya mwaka 2010 inaonyesha kuwa chini ya mwanafunzi mmoja kati ya 10 (7.7 asilimia) ndio anayeweza kusoma hadhithi ya Kiingereza ya ngazi ya darasa la pili

Wizara sita kufanyiwa tathmini `Matokeo Makubwa Sasa`

Mfumo  wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unatarajia kufanya tathmini katika wizara sita ili kuona ni kwa kiasi gani umefanya kazi na ripoti itakabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na kuwekwa kwenye mitandao.

Mtendaji Mkuu wa mfumo huo chini ya Ofisi ya Rais, Omari Issa, alisema tathmini ya mwaka mmoja itafanyika na taarifa kuwekwa wazi ili kila wizara ijipime na kuona kama imefikia malengo husika.

Alisema pia Februari 24, mwaka huu kutakuwa na mkutano na wafanyabiashara lengo likiwa ni kuwapa uwanja wa kueleza vikwazo vya kufanya biashara vilivyopo nchini kwa sasa ambavyo vinalalamikiwa.

Alisema chini ya mfumo huo ambao unmelenga kutatua matatizo yanayokwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo wengi wamesingizia kukosekana kwa fedha jambo ambalo alisema siyo kweli.

“Katika tathmini hiyo watabainisha matatizo ya wizara hadi wizara, mradi hadi mradi, uchambuzi wa kina utaonyesha nani apewe kiasi gani kwa ajili ya kutekeleza lipi…awali wizara ilikuwa inapewa kulingana na bajeti hata kama hawazitumii kwa wakati huo, lakini kwa sasa watapewa kulingana na utekelezaji,” alisema Issa.

Alisema mfumo huo umeweka utaratibu thabiti wa kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi katika maeneo ya kilimo, elimu, maji, nishati, uchukuzi na ufuatiliaji wa rasilimali, lengo likiwa ni kuwa na uwajibikaji wa kila mshiriki au taasisi katika utekelezaji wa miradi ya serikali ili kupata mafanikio haraka.

Kadhalika, Issa alisema mfumo umeanzisha kitengo cha kusimamia utekelezaji na ipo katika mchakato wa kuanzisha vitengo vya kusimamia utekelezaji katika ngazi za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ili kuongeza ufanisi wa kutekeleza miradi katika ngazi zote.

“Ili kufanikisha BRN, tunahitaji ushirikiano wa sekta binafsi ambayo italeta teknolojia, utaalamu wa menejimenti na mtaji, ili kuhamasisha ushirikiano huo tumeanzisha mchakato wa kurazinisha mfumo na taratibu za ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili tuhakikishe inatoa mchango wake stahili katika utekelezaji wa BRN,” alisema.

Alisema maeneo ya kimkakati ya kitaifa ni usambazaji wa maji salama vijijini ambako kwa kipindi cha miezi sita zaidi ya watu 300,000 wamepata maji, ulinzi wa chakula, elimu ya msingi na sekondari, kuimarisha usafirishaji wa bandari, reli na barabara katika kanda ya kati, upatikanaji na uzalishaji na utafutaji wa rasilimali fedha.
 

Jumatano, 29 Januari 2014

serikali kusambaza tabuleti shule za sekondari nchini

Serikali inakusudia kutoa maelfu kwa maelfu ya tabuleti za kufundishia masomo mbalimbali kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari nchini kama njia ya ubunifu zaidi, ya kisayansi na ya uhakika ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

Ili kufanikisha mpango huo, Serikali inakusudia kuingia ushirikiano na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Opportunity Education Trust ya Marekani ambayo jana ilizindua mpango wa majaribio wa utoaji wa tabuleti hizo kwa wanafunzi na walimu wao wa shule za sekondari nchini.

Mpango wa Serikali wa kusambaza tabuleti kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari ulitangazwa juzi na Rais Jakaya Kikwete, alipokutana na kuzungumza na Joe Ricketts, mwenye taasisi ya Opportunity Education Trust na mmoja wa matajiri wa Marekani.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete alimweleza kwa undani Ricketts hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali yake kupania na kuboresha elimu tokea mwaka 2006, hatua ambazo zimechangia kupanua kwa kasi na kwa kiwango kikubwa wigo wa utoaji elimu nchini na changamoto ambazo zimezuka kutokana na upanuzi huo mkubwa.

Rais Kikwete alisema baadhi ya changamoto hizo ni ukosefu wa walimu na hasa wa masomo ya sayansi na ukosefu wa vitabu vya kufundishia, changamoto mbili kubwa ambazo zinatatuliwa na matumizi ya tabuleti.

“Mbali na upanuzi mkubwa wa nafasi za wanafunzi kupata elimu ya ngazi mbalimbali, pia tumepanua sana ufundishaji wa walimu. Mwaka 2005, vyuo vyetu vyote vilikuwa vinatoa walimu 500 sasa tunatoa walimu 12,000 kwa mwaka. Hivyo, tunaamini kuwa katika mwaka mmoja ama miwili ijayo, tutakuwa tumemaliza tatizo la walimu wa masomo ya sanaa,” alisema.

Hata hivyo, alisema bado nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi.

"Tuna upungufu wa walimu 26,000 na kwa mwaka vyuo vyetu vyote vinahitimisha walimu 2,100 tu," alisema.

Chini ya mpango huo wa majaribio wa kusambaza teknolojia hiyo ya kisasa, taasisi ya Opportunity Education Trust inatoa tabuleti 1,100 kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa sekondari katika shule 33.

Ricketts alimwambia Rais Kikwete: “Hapa tunafanya majaribio na Tanzania ni nchi ya kwanza duniani miongoni mwa nchi ambazo tunaunga mkono mipango ya maendeleo kunufaika na mpango huo wa majaribio. Ni azma yetu kuwa baada ya kuwa tumefanya tathmini ya mafanikio na changamoto za hatua hii ya majaribio, tutaupanua mpango huu kushirikisha shule nyingi zaidi kwa kushirikiana na Serikali kwenye mpango wake mkubwa wa kusambaza teknolojia hii katika shule zote za sekondari hapa Tanzania.”

Ricketts na wataalam wake pamoja na maofisa wa Serikali walianza kutekeleza mpango huo jana kwa kutoa tabuleti kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Wama Nakayama iliyoko mkoani Pwani.

Baada ya hapo, shughuli hiyo itahamia Zanzibar na Pemba, kabla ya Ricketts na wataalam wake kutoa tabuleti kwa shule zilizoko mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kagera na Morogoro.

Shule zinazonufaika katika mpango huo ni za Serikali na binafsi na kwa kuanzia masomo ambayo yanapatikana katika tabuleti hizo ni Hesabu, Jiografia, Historia na Kiingereza.
 
chanzo ippmedia.com

Jumatatu, 27 Januari 2014

walimu wastaafu wa sayansi kupewa ajira tena

naibu waziri wa elimu philipo mulugo
Serikali imetangaza neema kwa walimu wastaafu wa somo la sayansi kujitokeza na kupeleka majina yao Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili waweze kupatiwa nafasi za kufundisha, kuziba pengo la ukosefu wa walimu hao nchini.

Hatua hiyo imechukuliwa ili kupunguza tatizo la upungufu wa walimu 26,000 uliopo hivi sasa hali inayoathiri zaidi wanafunzi wanaochukuwa masomo ya sayansi.

Hayo yalisemwa jijini Arusha na aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo siku moja kabla ya kuvuliwa wadhifa huo, wakati akizungumza katika mahafali ya tano ya chuo cha ufundi Arusha (ATC) ambapo jumla ya wanafunzo 256 walitunukiwa vyeti vya astashahada, stashahada na shahada ya kozi mbalimbali.

Alisema endapo walimu hao wastaafu hawatajitokeza, serikali itaingia hasara kubwa kutokana na kuajiri walimu wa fani hiyo kutoka nje ya nchi. Mulugo alisema serikali itawaombea kibali wizarani walimu wastaafu wa masomo ya sayansi watakaojitokeza  ili waweze kufundisha katika shule mbalimbali kwa kipindi cha miaka miwili na watakaopenda kuendelea hata kwa miaka 10 watakubaliwa.

“Tumekuwa tukitangaza sana kujitokeza kwa walimu wastaafu wa masomo ya sayansi nchi nzima kuleta majina yao wizarani ili waweze kupata ajira kwani tuna upungufu mkubwa sana, na tangu tutoe matangazo hayo wamejitokeza walimu wastaafu 96 tu, na hao hawatoshi bado tunawakaribisha sana popote pale walipo,” alisisitiza Mulugo.
 
Chanzo ippmedia.com

Jumamosi, 25 Januari 2014

Elimu bora; silaha ya kupambana na adui umaskini

Mwanahabari mkongwe, Othman Miraj anasema umaskini uliokithiri nchini ni suala lililogubikwa na mambo kadhaa yaliyosongamana.
Ni kwa sababu hiyo anasema ili kuumaliza umaskini, kunahitajika mipango na mikakati anuai, badala ya kuegemea katika kile anachosema dawa mujarabu ya aina moja.
“ Kuushinda umaskini ni kuwa na mkakati wa kuugawa utajiri wa Taifa, mifumo ya kisiasa duniani, kupigwa vita kwa ufisadi na kuwepo kwa mfumo mzuri wa elimu,’’ anataja baadhi ya mikakati ya kupambana na umaskini.
Mfumo bora wa elimu
Siyo Miraji tu, utafiti na uzoefu vinaonyesha elimu ni mojawapo ya silaha kubwa na muhimu siyo katika mapambano dhidi ya umaskini wa mtu mmojamoja, lakini pia katika maendeleo ya nchi kijamii na kiuchumi.
Wachambuzi wa sera na masuala ya kijamii, Elizabeth Missokia na Gervas Zombwe katika chapisho liitwalo ‘Hali ya Elimu Tanzania’, wanasema katika dunia ya leo, ili kila mtu aweze kuboresha maisha yake ni lazima awe na elimu.
Elimu ndiyo inayomwezesha mtu kujitambua na kujimiliki yeye mwenyewe, kuzikabili changamoto zinazomsonga, kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake
Wanaongeza kusema kuwa ndani ya utandawazi, elimu isiyotosheleza, tafsiri yake ni umaskini zaidi; wakati elimu zaidi tafsiri yake ni maisha bora zaidi.
Ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo ni lazima iwe elimu bora, ambayo inalenga kumbadilisha mtu na kumwezesha kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda kazi, kuwa na mwenendo mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na ya jamii, wanaongeza kusema.
Umuhimu wa elimu hasa kwa mabadiliko ya mtu binafsi kuelekea mafanikio ya kijamii,unadhihiri pia katika kauli maarufu ya aliyekuwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyesema:
“........elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya mtu. Ni kupitia elimu ndipo binti wa mkulima mdogo anaweza kuwa daktari bingwa, kwamba mtoto wa kibarua wa mgodini anakuwa mkuu wa mgodi na mtoto wa kibarua wa mashambani anakuwa Rais wa Taifa kubwa”.
Elimu bora ni ipi?
Kwa kawaida, mfumo wa elimu bora huzaa elimu bora na hii ndiyo aina ya elimu tunayoitaka Tanzania kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi wake.
Swali kuu ni; elimu bora ni ipi? Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ahmed Kiwanuka anasema elimu bora ni ile inayomkomboa binadamu na kumwezesha kuchangia katika jamii na taifa kwa kazi atakazokuwa akizifanya.
“Lengo la kupata elimu ni kumkomboa mtu kutokana na utumwa wa umaskini. Inatakiwa elimu imwezeshe mtu kutumia fikra zake kuendesha maisha mara baada ya kuhitimu masomo yake,” anasema
Akirejea maneno ya Mwalimu Julius Nyerere, anasema mwanafalsafa huyo aliyekuwa mtetezi mkubwa wa elimu aliwahi kusema kuwa ukombozi wa watu maskini utatokana na kusoma.
“Ukimwelimisha mtoto wa masikini, utakuwa umeisaidia familia yake, jamii na hata Taifa kutokana na mchango atakaotoa baada ya kuelimika,” anaeleza Dk Kiwanuka na kuongeza:
“Wasomi wetu wanatakiwa kujitoa kwa jamii kuhakikisha wanatumia elimu walioipata kwa ajili ya wengine.Taifa lolote linalotaka kuendelea lazima liwekeza zaidi katika elimu kwa kuwasomesha watu wote bila kuwabagua.”
Naye Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, anasema elimu bora ni ile inayozingatia mambo muhimu matatu, ambayo ni maarifa, ujuzi na mtazamo.
“Ukiwa na mambo hayo mwanafunzi atakuwa anajitambua na ataelewa maisha ni kitu gani. Ndivyo vitu vitakavyomwezesha kujua namna ya kuitumia elimu katika maisha ya kawaida katika jamii inayomzunguka,” anasema Mukoba.
Vikwazo vya elimu bora 
Licha ya kuwepo kwa juhudi kadhaa zinazofanywa na Serikali na wadau wengine wa elimu zinazolenga kuimarisha elimu nchini, bado sekta ya elimu inakabiliwa na vizingiti kadhaa vinavyohatarisha utoaji wa elimu na hata mustakabali wa sekta kwa jumla.
Tafiti na uzoefu vinaonyesha vikwazo vikubwa vya elimu nchini ni pamoja na taifa kukosa dira maalumu kuhusu elimu na aina ya mafunzo au maarifa, ambayo wanafunzi wanapaswa kufundishwa au kujifunza kutegemea mahitaji ya wakati uliopo.
Dira ni mwongozo wenye malengo yanayolinda utoaji wa elimu kwa manufaa ya nchi na mtu binafsi.


Changamoto nyingine zinazotajwa na wataalamu wa elimu kupitia utafiti wao ni kasoro za mitalaa, ikiwamo baadhi yake kuwa na masomo yasiyotoa ujuzi wa maana kwa wahitimu, hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Nyingine ni kuendelea kutumia lugha ya Kiingereza katika kufundishia shule za msingi, ambayo haifahamiki kwa wanafunzi na walimu wenyewe, uhaba wa walimu hasa katika masomo ya sayansi na hesabu, uwepo wa walimu wenye uwezo mdogo kitaaluma na kufundisha, uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na baadhi ya wanajamii kutojali elimu kwa watoto wao.

chanzo mwananchi

Mapenzi ya jinsia moja yalalamikiwa sekondari wasichana

Shule moja ya sekondari ya wasichana iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani,  imelalamikiwa na wanafunzi pamoja na wazazi kuwa mabinti wanajihusisha na vitendo vya ngono vya jinsia moja (usagaji).

Akizungumza na NIPASHE mmoja wa wazazi (jina linahifadhiwa)  alisema shule hiyo imepoteza sifa kwa kuwa kuna wimbi kubwa la wanafunzi wanaojihusisha na vitendo hivyo vya usagaji.

Alisema  mtoto wake alikuwa ameanza kidato cha kwanza mwaka jana na baada ya kumuandikisha ndipo baadhi ya watu walipomueleza kuwa shule hiyo kwa sasa ina sifa mbaya ya mchezo ‘huo mchafu.’

"Baada ya kuelezwa nikasema nitalifanyia kazi jambo hilo hivi karibuni katika kupekua madaftari ya mwanangu nakutana na kibarua cha mapenzi alichoandikiwa na msichana mwenzake niliumia sana na nilitumia nguvu kumbana bila hivyo asingeniambia," alisema

Alisema ilimbidi amhamishe binti yake na kujiunga na shule moja ya sekondari iliyopo mkoani Tanga kwa ajili ya kuendelea na masomo ya kidato cha pili mwaka huu.

Mzazi huyo alisema anashangazwa ni kwa nini hatua hazichukuliwi wakati suala hilo ni la hatari kwani watoto wao wataharibika kiakili pamoja na kimwili na wanaweza kuambukizana VVU na Ukimwi..

Alisema wakati mwanaye akisoma katika shule hiyo alikuwa akihudhuria vikao vya wazazi mara kwa mara na kwamba kila kikao walikuwa wakifukuzwa wanafunzi kutokana na mwenendo huo.

"Hili tatizo ni kubwa na kufukuzwa kwa mwanafunzi sidhani kuwa wanatatua tatizo nadhani hakuna usimamizi mzuri kwani wangeweza kudhibiti kwa haraka tatizo hilo kabla ya kuwa kubwa," alisema

Pia alisema ndugu yake imembidi amhamishe mwanae na kumtafutia shule nyingine kwa kuhofia binti yake  kurubuniwa kwani wanakuwa ni wadogo na hawaelewi chochote, hivyo inaweza kuwa rahisi kudanganywa na kuingia kwenye vitendo hivyo viovu.

Alisema kuwa hata kiwango cha ufaulu kwa sasa shule hiyo imeshuka kutokana na tatizo hilo kwa wanafunzi .

Hata hivyo, NIPASHE  ilizungumza na mwanafunzi mmoja ambaye anasoma katika shule hiyo kuhusiana na suala hilo ambapo alikiri kuwepo kwa jambo hilo na kueleza kuwa wanaofanya mchezo huo ni wa kidato cha tano na cha sita.

"Mimi hawajanifanyia ila najua wanaofanya mchezo huo ni wale walioko kidato cha tano na cha sita," alisema Pia kuna baadhi ya wazazi wengine wamekuwa wakilalamikia jambo hilo na kueleza kuwa ndugu zao imewalazimu kuwahamisha watoto wao kutokana na vitendo hivyo vinavyofanyika shuleni hapo.

CHANZO: NIPASHE

Jumatano, 22 Januari 2014

mabadiliko baraza la mawaziri kila mmoja na mtizamo wake

Hatimaye Baraza jipya la Mawaziri limetangazwa , tumeshuhudia mabadiliko katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo Naibu Waziri wa Elimu wa sasa ni Mh. Jenista Mhagama amechukua nafasi ya Mh. Philipo Mulugo. Wako watanzania wanayaona mabadiliko haya kutokuwa na tija huku wengine wakiamini mabadiliko yanaweza kutokea, wote wana sababu za msingi kabisa kuamini kile wanachoamini. Je mdau wa elimu ni mambo yapi Uongozi wa sasa unatakiwa kuyazingatia/kuyafanya ili kuhakikisha kiwango cha elimu nchini kinapanda na wanafunzi kote nchini wanapata elimu bora? Tafakari na tushikirikishane
 
chanzo haki elimu facebook page