Mwanahabari mkongwe, Othman Miraj anasema umaskini uliokithiri nchini ni suala lililogubikwa na mambo kadhaa yaliyosongamana.
Ni kwa sababu hiyo anasema ili kuumaliza umaskini,
kunahitajika mipango na mikakati anuai, badala ya kuegemea katika kile
anachosema dawa mujarabu ya aina moja.
“ Kuushinda umaskini ni kuwa na mkakati wa kuugawa
utajiri wa Taifa, mifumo ya kisiasa duniani, kupigwa vita kwa ufisadi
na kuwepo kwa mfumo mzuri wa elimu,’’ anataja baadhi ya mikakati ya
kupambana na umaskini.
Mfumo bora wa elimu
Siyo Miraji tu, utafiti na uzoefu vinaonyesha
elimu ni mojawapo ya silaha kubwa na muhimu siyo katika mapambano dhidi
ya umaskini wa mtu mmojamoja, lakini pia katika maendeleo ya nchi
kijamii na kiuchumi.
Wachambuzi wa sera na masuala ya kijamii,
Elizabeth Missokia na Gervas Zombwe katika chapisho liitwalo ‘Hali ya
Elimu Tanzania’, wanasema katika dunia ya leo, ili kila mtu aweze
kuboresha maisha yake ni lazima awe na elimu.
Elimu ndiyo inayomwezesha mtu kujitambua na
kujimiliki yeye mwenyewe, kuzikabili changamoto zinazomsonga, kuyatawala
na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake
Wanaongeza kusema kuwa ndani ya utandawazi, elimu
isiyotosheleza, tafsiri yake ni umaskini zaidi; wakati elimu zaidi
tafsiri yake ni maisha bora zaidi.
Ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli
kimaendeleo ni lazima iwe elimu bora, ambayo inalenga kumbadilisha mtu
na kumwezesha kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda
kazi, kuwa na mwenendo mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na
ya jamii, wanaongeza kusema.
Umuhimu wa elimu hasa kwa mabadiliko ya mtu
binafsi kuelekea mafanikio ya kijamii,unadhihiri pia katika kauli
maarufu ya aliyekuwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson
Mandela aliyesema:
“........elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya
mtu. Ni kupitia elimu ndipo binti wa mkulima mdogo anaweza kuwa daktari
bingwa, kwamba mtoto wa kibarua wa mgodini anakuwa mkuu wa mgodi na
mtoto wa kibarua wa mashambani anakuwa Rais wa Taifa kubwa”.
Elimu bora ni ipi?
chanzo mwananchi
Kwa kawaida, mfumo wa elimu bora huzaa elimu bora na hii ndiyo
aina ya elimu tunayoitaka Tanzania kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi
wa wananchi wake.
Swali kuu ni; elimu bora ni ipi? Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ahmed Kiwanuka anasema elimu bora ni ile
inayomkomboa binadamu na kumwezesha kuchangia katika jamii na taifa kwa
kazi atakazokuwa akizifanya.
“Lengo la kupata elimu ni kumkomboa mtu kutokana
na utumwa wa umaskini. Inatakiwa elimu imwezeshe mtu kutumia fikra zake
kuendesha maisha mara baada ya kuhitimu masomo yake,” anasema
Akirejea maneno ya Mwalimu Julius Nyerere, anasema
mwanafalsafa huyo aliyekuwa mtetezi mkubwa wa elimu aliwahi kusema kuwa
ukombozi wa watu maskini utatokana na kusoma.
“Ukimwelimisha mtoto wa masikini, utakuwa
umeisaidia familia yake, jamii na hata Taifa kutokana na mchango
atakaotoa baada ya kuelimika,” anaeleza Dk Kiwanuka na kuongeza:
“Wasomi wetu wanatakiwa kujitoa kwa jamii
kuhakikisha wanatumia elimu walioipata kwa ajili ya wengine.Taifa lolote
linalotaka kuendelea lazima liwekeza zaidi katika elimu kwa kuwasomesha
watu wote bila kuwabagua.”
Naye Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT),
Gratian Mukoba, anasema elimu bora ni ile inayozingatia mambo muhimu
matatu, ambayo ni maarifa, ujuzi na mtazamo.
“Ukiwa na mambo hayo mwanafunzi atakuwa
anajitambua na ataelewa maisha ni kitu gani. Ndivyo vitu
vitakavyomwezesha kujua namna ya kuitumia elimu katika maisha ya kawaida
katika jamii inayomzunguka,” anasema Mukoba.
Vikwazo vya elimu bora
Licha ya kuwepo kwa juhudi kadhaa zinazofanywa na
Serikali na wadau wengine wa elimu zinazolenga kuimarisha elimu nchini,
bado sekta ya elimu inakabiliwa na vizingiti kadhaa vinavyohatarisha
utoaji wa elimu na hata mustakabali wa sekta kwa jumla.
Tafiti na uzoefu vinaonyesha vikwazo vikubwa vya
elimu nchini ni pamoja na taifa kukosa dira maalumu kuhusu elimu na aina
ya mafunzo au maarifa, ambayo wanafunzi wanapaswa kufundishwa au
kujifunza kutegemea mahitaji ya wakati uliopo.
Dira ni mwongozo wenye malengo yanayolinda utoaji wa elimu kwa manufaa ya nchi na mtu binafsi.
Changamoto nyingine zinazotajwa na wataalamu wa elimu kupitia
utafiti wao ni kasoro za mitalaa, ikiwamo baadhi yake kuwa na masomo
yasiyotoa ujuzi wa maana kwa wahitimu, hivyo kushindwa kukabiliana na
changamoto za kimaisha.
Nyingine ni kuendelea kutumia lugha ya Kiingereza
katika kufundishia shule za msingi, ambayo haifahamiki kwa wanafunzi na
walimu wenyewe, uhaba wa walimu hasa katika masomo ya sayansi na hesabu,
uwepo wa walimu wenye uwezo mdogo kitaaluma na kufundisha, uhaba wa
vifaa vya kufundishia na kujifunzia na baadhi ya wanajamii kutojali
elimu kwa watoto wao.
chanzo mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni