Mishahara ya viongozi tunaowachagua ni changamoto kupatikana kwa elimu ya bure nchini
HATIMAYE Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Zitto Kabwe, ameweka wazi mshahara wa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda.
Zitto ameutaja mshahara huo wa Pinda anayejitambulisha
kama ‘mtoto wa mkulima’ juzi mjini Mpanda na jana wilayani Sikonge
wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika ziara ya Kanda ya Magharibi
kwa ajili ya ujenzi wa chama.
Alisema Pinda anapokea jumla ya sh milioni 26, ambazo ni kiasi kikubwa kulinganisha na uchumi wa nchi.
Akichanganua alisema Pinda anapokea sh mil. 11.2 kama mbunge, sh mil. 8
kwa nafasi ya waziri na kiasi kinachosalia kufikia sh mil. 26 kwa
nafasi yake ya uwaziri mkuu.
Alisema sababu hiyo ya mishahara
mikubwa isiyokatwa kodi ndiyo huwafanya viongozi wa serikali ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wakali pale vyombo vya habari vinapotaka
kuwafahamisha wananchi namna watumishi wao wanavyojilipa.
“Nimeanza na mshahara wa waziri mkuu pia siku zijazo nitataja na wa
rais, kwa kuwa amesaini makubaliano na Serikali ya Marekani kuendesha
nchi kwa uwazi, na moja ya uwazi ni kwa muajiri kujua kiasi anachomlipa
mwajiriwa wake,” alisema Zitto.
Hatua ya Zitto imekuja baada ya
kuwapo mvutano mkubwa kuhusiana na kile kinachodaiwa ‘usiri’ wa
mishahara ya watumishi wa umma, wakati ni haki ya walipa kodi kujua kile
wanachowalipa walioomba kuwaongoza.
Kodi ya laini za simu
Akizungumzia sakata la kodi katika laini za simu, Zitto alisema CCM ina ajenda ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Alisema serikali baada ya kubaini watu wengi wanapeana taarifa kwa njia
ya ujumbe mfupi, hususan katika masuala ya kisiasa, wakaona njia sahihi
ya kudhibiti ni kuwatoza kodi ya laini ili kupunguza hatari ya
mawasiliano hayo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.
“Sikuwepo
bungeni wakati wabunge wa CCM wanapitisha kadhia hiyo ya kuwanyonya
wananchi, wenzangu wakaniambai tukasema hapana, kwa maana tuliona hii
leo kuna Watanzania wengi wasio na uwezo wa kuhudumia simu kwa kiasi cha
sh 1,000 kwa mwezi,” alisema Zitto.
Akijibu maswali ya
wananchi mjini Mpanda waliotaka kujua sababu ya kupunguza makali
bungeni, Zitto alisema hakuna makali yaliyopungua bali ni mitazamo ya
watu.
Alisema kwa kushirikiana na wabunge wenzake wa upinzani
wamekuwa wakisimamia hoja zenye manufaa kwa wananachi huku wabunge
wanaojipambanua kuwa majasiri kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wakiwaunga mkono wazi wazi.
Akiwa wilayani Sikonge, Zitto
alisema Watanzania hawawezi kujivunia uhuru huku mama zao, watoto wao na
wazee wao wakiwa hawana uhakika wa kupata huduma bora ya afya, elimu na
maji safi.
Alisema kwa sasa Tanzania ni taifa moja lililogawanyika katika nchi mbili za wenye fedha na wasio na fedha.
Alisema nchi ya wenye fedha, familia zao husoma katika shule bora,
zenye mazingira bora na walimu wazuri, hutibiwa katika hospitali zenye
hadhi na huduma muhimu na ikibidi nje ya nchi, huku nchi ya wasio na
fedha familia zao wakiishi kwa shida, kusoma katika majengo ya shule na
walimu wasiopata mishahara ya kuridhisha na hospitali zisizokuwa na
huduma muhimu licha ya kuchangia kiasi cha fedha kwa ajili ya bima ya
afya.
(chanzo Tanzania daima)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni