Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 23 Oktoba 2013

ripoti ya tume ya Pinda ni kitendawili haionekani




Tumeghadhabishwa na hatua ya Serikali ya kuendelea kuficha Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mapema mwaka huu. Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba Tume hiyo iliundwa ikiwa ni hatua ya dharura kwa lengo la kutoa majibu ya haraka kuhusu sababu za wanafunzi wengi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana kufanya vibaya katika mtihani huo na kuamsha vilio kote nchini.
Katika matokeo hayo, watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 waliambulia sifuri, wakati watahiniwa 23,520 ambao ni asilimia 5.16 wakiwa wamefaulu, huku watahiniwa wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wakiwa wamepata daraja la nne. Katika mtihani huo, watahiniwa 397,136 walitoka katika shule mbalimbali, huku wengine 68,806 wakiwa wa kujitegemea.
Idadi kubwa ya wanafunzi hao kufeli mitihani kiasi hicho lilionekana kama janga la kitaifa na ndiyo maana wananchi wa rika zote, wakiwamo wabunge walipaza sauti wakiishinikiza Serikali itegue kitendawili kuhusu sababu za matokeo hayo ya kutia fedheha na aibu kwa taifa letu. Ndipo Serikali ilipounda Tume ya watu 15 Machi mwaka jana na kuitaka kuwasilisha ripoti yake serikalini miezi mitatu baadaye.
Tume hiyo ilimaliza kazi yake katika muda uliopangwa na kukabidhi ripoti hiyo Juni 15, mwaka huu. Jambo la kushangaza ni kuwa, pamoja na kupita zaidi ya miezi minne tangu ripoti hiyo iwasilishwe serikalini bado Serikali imeificha makabatini kwa sababu inazozijua yenyewe. Habari zinasema kwamba Serikali inajua umuhimu wa kuitoa ripoti hiyo hadharani haraka, lakini inasita kwa sababu mengi ya matatizo yaliyoainishwa na Tume hiyo yanaonyesha bayana kwamba Serikali pia ni sehemu ya tatizo.
Hata hivyo, tunapata shida kuelewa kwa nini Serikali inaendelea kuatamia ripoti hiyo wakati ikijua kwamba Watanzania wanasubiri ripoti hiyo kwa shauku kubwa kwa mategemeo kuwa, hatua za kurekebisha makosa yaliyotokea zingechukuliwa na mamlaka zote husika kwa kuwa muda siyo mrefu wanafunzi watafanya tena mitihani ya kidato cha nne mwaka huu.
Ukimya wa Serikali unaendelea kusababisha madhara mengine kadhaa, kwa maana ya baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo kuchoka kuisubiri Serikali iweke hadharani ripoti ya Tume hiyo. Jana gazeti hili lilichapisha habari kuhusu baadhi ya vipengere vilivyo katika ripoti ya Tume hiyo, ambapo baadhi ya wajumbe waliounda Tume hiyo walisema katika nyakati tofauti hivi karibuni kwamba waligundua mambo mengi yanayodhihirisha udhaifu mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya elimu hapa nchini.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wanasema sehemu kubwa ya matokeo ya uchunguzi huo inajikita zaidi katika kulaumu Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), badala ya kujielekeza zaidi katika kupendekeza nini kifanyike ili kurekebisha mfumo mzima wa sekta ya elimu nchini ambao umedhihirika kuwa mbovu. Tatizo hapa pengine ni muundo wa Tume hiyo yenye idadi kubwa ya watumishi wa umma na wabunge wa chama tawala.
Wajumbe hao wamesema ripoti ya Tume hiyo ni ndefu na ingefaa Serikali iiweke wazi sasa ili ifanyiwe kazi. Sisi tunaungana na wajumbe hao kuishauri Serikali kufanya hivyo sasa. Madhara ya kuendelea kuihodhi ripoti hiyo ni makubwa pengine kuliko Serikali yenyewe inavyofikiri.

souce . mwananchi