Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatatu, 28 Desemba 2015

Shule ya kidato I - IV ina wanafunzi 45 tu

 Shule ya Sekondari Panzua iliyoko kata ya Panzua Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, ina jumla ya wanafunzi 45 wa kidato cha kwanza hadi cha nne.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka wilayani humo, Ofisa Kilimo wa kata hiyo, Muharami Makulika, alisema wanafunzi hao wanatoka katika vijiji saba vinavyoizunguka kata hiyo. Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Kibuyuni, Mkuruwili, Masanganya, Bupu kwa Wilaya ya Mkuranga na Kisarawe kijiji cha Malegele na Bwama.
 
Alisema takwimu za mwaka jana zinaonyesha shule hiyo ilikuwa na idadi ya wanafunzi 50 tu katika kidato cha kwanza hadi cha nne, jambo linalosababisha kufa kwa elimu katika kata hiyo, huku wengi wao ambao ni wa kike wakidaiwa kuolewa katika umri mdogo kutokana na wazazi na walezi kushindwa kuwasomesha.
 
Kwa mujibu wa Makulika, wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wamechangia kuhalalisha ndoa za wanafunzi hao kwa kisingizio cha kipato kidogo kila mwaka, wakati baadhi yao kutokuwa na mwamko kuhusu elimu kwa mtoto wa kike itakayomkomboa katika mnyororo wa umaskini kwa siku za baadaye.
 
Alisema wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, wamegeuka washawishi wakubwa kwa wanafunzi hao kufanya vibaya katika masomo yao ya kuhitimu darasa la saba kwa dhamira ya kufeli ili  wawaozeshe.
“Ni vigumu kutatua changamoto hii, labda ziingilie sekta binafsi kama taasisi inayopambana na masuala ya ndoa za utotoni kama Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa).
 
Ofisa kijiji wa kitongoji cha Kibuyuni katika kata hiyo, Idd Ummagala, alisema takwimu za mwaka jana zinaonyesha idadi ya  wanafunzi katika shule hiyo walikuwa 54 na wengi wao hawakuhitimu masomo yao kutokana na ndoa za utotoni.
 
Alisema takwimu hizo katika kipindi cha masomo cha mwaka huu, ni chini ya mwaka jana kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za ndoa za utotoni, hali duni ya wazazi na walezi. Kwa mujibu wa Ummagala, mkakati wa serikali kwa 2016, ni kuiboresha shule hiyo ili iwe ya bweni kwa lengo la kudhibiti wimbi la wanafunzi hao hususan wa kike wanaoangukia ndoa za utotoni.
 
 Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Sharifa Abdallah, alisema idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, wanatoka katika familia duni ambapo wazazi ama walezi wanaishi kwa kutegemea kilimo ambacho hawawezi kukihudumia. Alisema wanakijiji wengi wa kata hiyo, wanategemea fedha za kujikimu kupitia kilimo cha matunda, maharage na mahindi, wakati wanakabiliwa na idadi kubwa ya watoto katika familia, jambo linalochangia wengi wao kukatishwa masomo kutokana na rasilimali fedha.
 
“Pamoja na changamoto hiyo, lakini bado wanaume wengi hawana mwamko kuhusu elimu ya mtoto wa kike, badala yake wanaendekeza mila potofu za ndoa za utotoni huku wengine wakiona ufahari kuozesha mtoto katika umri chini ya miaka 18.
 
Takwimu hizo ni miongoni mwa shule chache za kata zilizoko vijijini zinazokabiliwa na idadi hiyo ndogo ya wanafunzi, lakini bado serikali imeshindwa kutoa adhabu au kuweka sheria inayosimamia haki zao  kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
 
chanzo. ippmedia.com