Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumanne, 22 Julai 2014

binti aliyekeketwa alilia shule

 Akiwa darasa la nne alikamatwa kwa nguvu..
Mama mzazi wa binti muathirika wa ukeketaji akifafanua 
Mama mzazi wa binti muathirika wa ukeketaji akifafanua jambo huku akisikilizwa na binti yake.
Kuna mambo mengi anakumbukia msichana mwenye umri wa miaka 12  yamemtokea maishani. Lakini tukio la siku hiyo, kuitwa na mama yake mdogo, kisha kukamatwa kwa nguvu na kukeketwa  linabaki kuwa kovu lisilopona katika maisha yake. Ni ukatili uliopitiliza uliobadili kabisa ndoto za maisha yake za kupata elimu.
 
Binti wa miaka 12 (jina linahifadhiwa)  ni mtoto wa mwisho wa kike kati ya watoto nane wa mzee Isaya na Mama Gyar Baa kutoka familia moja ya kabila la Kimbulu.
 
Kabla  hajakumbwa na mkasa uliobadilisha kabisa welekeo wa maisha yake, alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne mwenye  ndoto za kusoma hadi kufikia ukomo wa maisha yake.
Hata hivyo, ndoto hizo zilizimwa baada ya  kujikuta akilazimishwa kukeketwa ikiwa ni ishara ya maandalizi ya kutafutiwa mume ili aolewe.Tukio hilo la kikatili liliathiri maisha yake.
 
Makazi ya familia ya binti huyo ni katika kijiji cha Konje wilaya ya Handeni mkoani Tanga, kilichopo umbali wa kilometa 16 kutoka Handeni mjini.
 
Msichana huyo, anatoka katika familia ya wafugaji, yenye tabia ya kuhamahama ili kufuata malisho, hasa nyakati za ukame ili kuhakikisha kuwa mifugo yao haikosi chakula na maji.

Akisimulia kwa uchungu mkasa alioupata uliobadili kabisa uwelekeo wa maisha yake, msichana huyo anasema siku hiyo ya Jumanne (hakumbuki tarehe) aliitwa na mama yake mdogo (mama wa kambo). Aliitika na kutii amri kwa kwenda kusikiliza alichoitiwa akiwa hana fununu kabisa ya dhamira ya muitaji.
 
Anasema baada ya kufika nyumbani kwa mama yake huyo, alishangazwa kumkuta dada yake anayemfuata (jina linahifadhiwa) akiwa amefungwa mikono na miguu huku akilia kwa uchungu sana. Kilichomsikitisha zaidi ni kuona jinsi ambavyo dada yake alikuwa akivuja damu nyingi katika sehemu zake za siri.
 
Jambo hilo, lilimtisha sana Tansiana na kutokana na hamaki akapata wazo na maamuzi ya haraka ya kukimbia  kutoka nyumbani kwa mama yake mdogo  ili kujinusuru na hatari aliyoona kuwa inamkabili. Hata hivyo, hakufanikiwa kutimiza matakwa yake.
 
“Nilishtuka sana, kumuona dada akilia huku damu zinamtoka kwa wingi  sana katika sehemu zake za siri. Lakini nilivyotaka kukimbia mama mdogo  na bibi yule niliyemkuta pale nyumbani ambaye sikufahamu ametokea wapi wakanikamata na  kunifunga mikono na miguu kwa kamba,” anasimulia msichana huyo kwa masikitiko.
 
Baada ya kufungwa na kudhibitiwa kikamilifu ndipo bibi huyo asiyemfahamu akachukua kiwembe na kumkata kwenye sehemu yake ya siri kwa namna alivyojiridhisha na kusababisha atokwe damu nyingi kama ilivyokuwa kwa dada yake.
 
“Wakati  wananikata sikusikia maumivu sana kwa sababu nilikuwa na hasira sana kwa kile kitendo nilichokiona amefanyiwa dada yangu…ndipo  baada ya kupita muda kama kama saa moja hivi nikaanza kusikia maumivu makali sana kama roho inataka kutoka. Ndipo nikatambua namna gani watu wale walivyo wakali. Nilikuwa nimefanyiwa unyama wa hali ya juu bila ya ridhaa yangu. Nililia sana na kwa hakika nimemchukia sana huyo mama mdogo na sijui kama nitamsamehe,” anasema.
 
Akikumbukia zaidi anasema kuwa “wakati wananifanyia unyama huo, mama yangu mzazi alikuwa amesafiri kwenda Karatu na baba  hakuwapo nyumbani. Aliporudi alikuta tayari tumekeketwa.”
 
Anabainisha kwamba, ilimchukua takriban mwezi mmoja kuuguza kidonda hicho hadi kupona. Aina ya matibabu aliyokuwa akipewa anasema kuwa, ni kupakwa maziwa na mafuta ya taa mara mbili kwa siku.Yaani asubuhi na jioni kama dawa ya kuponyesha jeraha hilo. Alipata msongo mkali wa mawazo kuhusu tukio hilo baya kabisa na la ukatili wa kupindukia.
Baba yake, licha ya kutabua unyama waliofanyiwa, lakini hakuchukua hatua zozote dhidi ya wahalifu wale.
 
Anasema kuwa, miongoni mwa sababu walizoelezwa zilizolazimisha wachukuliwe hatua hiyo kukeketwa ni watoto wa kike kuwafanya waachane na vitendo vya uhuni kwa kile kinachodaiwa kuwa, wasipokeketwa wanakuwa na tamaa kali ya  kufanya mapenzi muda wote.
 
Hii ni kutokana na mila na desturi za kabila lao, kwamba iwapo binti hatakeketwa, basi ni dhahiri kwamba hatapata mume wa kumuoa na hatakuwa na heshima wala thamani anayostahili kupewa mwanamke kwenye jamii hiyo.
 
Kutokana na kitendo hicho, anasema kuwa ni dhahiri kwamba ameandaliwa kwa ajili ya kuolewa, hata kama jambo hilo litafanyika litakuwa ni kinyume cha ridhaa yake.
 
“Najua sasa hivi nasubiri tu kuolewa. Lakini ni kwamba watanilazimisha tu lakini mimi mwenyewe sipendi…napenda sana kusoma… natamani sana ajitokeze mtu wa kunisaidia katika hilo. Nipo tayari kabisa kwa hilo…na baada ya kusoma cha kwanza nitakachofanya ni kuhakikisha nazuia mila hii mbaya isiendelee kufanyika kwa wasichana wengine wa jamii hii. Kwa kweli inauma sana…tunateseka sana jamani,” anasema msichana huyo huku akibubujikwa machozi.
 
Msishana huyo, licha ya hatua ngumu ya maisha yake aliyopitia, lakini ana matumaini kuwa, siku moja atakuwa mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake, na kupiga vita mila na desturi ambazo zimekuwa zikitumika kumgandamiza mwanamke.
 
Aina hiyo ya maisha, ndiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kumfanya msichana huyo kuwa miongoni mwa wale waliokosa fursa ya kupata haki yake ya msingi hasa elimu. Alikuwa na ndoto za siku moja kupata elimu ili uwe mwanga wa uhakika kwa maisha yake na jamii yake inayomzunguka.
 
Pamoja na kukabiliwa na changamoto hiyo maishani, lakini binti huyo  katika familia yake ana msimamo wa kupenda elimu na kujituma kwa kazi za kifamilia na kwamba iwapo atatokea mfadhili yoyote atakayekuwa tayari kumchukua na kwenda kumsomesha  hata wazazi wake sasa wameutambua ukweli huo na kuwa tayari kumruhusu aende akapate elimu.
 
“Kamwe sitasahau unyama huu…nikipata elimu lazima niwe mwanaharakati wa kupinga unyama huu ,” anasema.
Mama mzazi wa binti huyo aitwaye Gyar Baa Isaya anasema kuwa wakati binti yake anakeketwa, alikuwa safarini na hakushirikishwa na mumewe kuhusu kufanyika kwa kitendo hicho.

Kimsingi anasema, alikuwa anafahamu kuwa siku moja binti yake atalazimika kufanyiwa mila hiyo kwa sababu ni utamaduni ambao hata yeye ameupitia na hakuwa na mamlaka ya kuupinga, kwani kwa kufanya hivyo, angeweza kumsababishia matatizo mtoto wake ikiwamo kutoolewa.

“Kusema kweli kwa mila za kwetu ili uonekane ni mwanamke ambaye umekamilika ni lazima ukeketwe…vinginevyo hupati mume na unaweza kupatwa na majanga makubwa  ikiwamo binti kuanza tabia mbaya kabla ya wakati wake…sasa watoto wangu wamelazimika kufanyiwa mila hiyo ingawa hawakuridhika nayo kabisa,” anasema mama huyo.

Naye  dada wa msichana huyo aliyeanza kufanyiwa ukatili huo, anasema kuwa sababu kubwa ya mdogo wake kushindwa kuendelea na masomo licha ya kuwa na ndoto za kufika mbali kimaisha ni ile hofu ya kuchekwa na wenzake hasa wakati wa kuoga wakimuona amekeketwa.

“Unajua mnapokuwa rika moja mnakuwa hamuoneani aibu kabisa, hata kama kuoga mtaenda wote, sasa wenzako wakikuona uko tofauti na wao kimaumbile wanakushangaa na wengine wanakucheka. Hali hii nilipokuwa nikimwelezea mdogo wangu ilichangia kumkatisha tamaa ya kusoma kwa hofu ya kuchekwa,” anasema dada huyo ambaye  ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule moja.

Hata hivyo anasema, kitendo walichofanyiwa kinadhihirisha udhalilishaji kwa mtoto wa kike na kwamba licha ya baba yao kuwa ni miongoni mwa wafugaji wenye tabia ya kuhamahama, lakini amedhamiria kuhakikisha kuwa anamaliza masomo yake.

“Baba yetu ni miongoni mwa wafugaji wenye tabia ya kuhamahama makazi, hali hii imetuathiri sana kielimu tena mimi ni nafuu kwa sababu naishi kwenye hosteli za shule. Mdogo wangu ndiyo amerudi nyuma kwani hadi sasa hasomi na  aliishia darasa la nne,” anasema dada huyo.
CHANZO: Ippmedia.com