Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumanne, 17 Mei 2016

walimu 35,411 kuajiliwa mwaka wa fedha 2016/2017

Walimu 35,411 nchini wataajiriwa katika shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Watakaokaidi kwenda kuripoti katika mikoa ya pembezoni, hawataajiriwa na serikali.
 
Hatua hiyo imeelezwa kwamba imetokana na serikali kupokea maombi mengi ya kazi kwa walimu, ambao mwaka jana hawakuripoti katika vituo walivyopangiwa pembezoni mwa miji kwa kutegemea kuajiriwa na shule binafsi, lakini hawakufanikiwa.
 
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) aliyetaka kufahamu serikali inafanya nini kwa walimu waliopangiwa kwenda mikoa ya pembezoni, ikiwemo Lindi na kwingineko, lakini hawakuripoti.
 
Jaffo alisema ni kweli kuna walimu wengi ambao hawakuripoti katika mikoa ya pembezoni. Alisema si Lindi peke yake, bali na mikoa mingine, ikiwemo Katavi na Kigoma.
 
Alisema kwa mwaka huu, wataajiri walimu 35,411, lakini ambaye hataripoti katika mikoa hiyo na kuishia mijini tu, hawataajiriwa tena serikalini, kama wanavyoomba tena baada ya kukosa katika shule binafsi

Ijumaa, 15 Aprili 2016

marafiki wa elimu musoma wasaidia jamii

kutokana na uhitaji wa jamii marafiki wa elimu musoma tumeona ni nafasi nzuri kujichangisha na kuweza kusaidia wanafunzi vifaa vya shule tazama picha za matukio pale marafiki tulipojumuika na jamii kuchangia tulichokuwa nacho
rafiki wa elimu Juma okumu akielezea dhana ya marafiki wa elimu

mwenyekiti wa mtandao wa marafiki wa elimu musoma Bi perus Masokomya akikabidhi vifaa hivyo







picha ya pamoja marafiki wazazi na wanafunzi




Alhamisi, 31 Machi 2016

marafiki wa elimu musoma kutoa msaada kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu

kutokana na dhana ya marafiki wa elimu ya kuhakikisha elimu bora kwa wanafunzi wote wa kitanzania, hivi karibuni mtandao wa marafiki wa elimu wameamua kujichangisha ili kuweza kukusanya vifaa vya shule kwa ajili ya kuweza kusaidia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu.

mpango huo wa marafiki wa elimu umelenga kusaidia wanafunzi 25 vifaa vya shule kama madaftari,kalamu mabegi na sare za shule.
mpango huo utatekelezwa tarehe 15/04/2016
kwa mdau atakaeguswa na mpango huu anaweza kuwasiliana na marafiki wa elimu musoma kwa nambari 0755 650 075
katibu msaidizi wa marafiki wa elimu Kaseja january akisoma machapisho

rafiki wa elimu Juma okumu pamoja na Godfrey Mjaya wakisoma machapisho kabla ya kikao kuanza

mwenyekiti mpya wa mtandao wa marafiki wa elimu musoma Bi Perus masokomya

rafiki elimu Daniel Richard akipokea michango ya marafiki

Kaseja January akihakiki vifaa vilivyopatikana

katibu wa marafiki wa elimu musoma Bi Rose Olimo

mlezi wa mtandao wa marafiki wa elimu musoma thomas bega aliyesimama

marafiki wakimsikiliza mwenyekiti wa mtandao

mwenyekiti wa mtandao akizungumza na marafiki

Jumatatu, 1 Februari 2016

Haki elimu yakusanya maoni kuhusu lugha ya kufundishia

shirika la Haki elimu linakusanya maoni ya wananchi kupitia mtandao wake wa twitter juu ya mapendekezo ya lugha ya kufundishia kama iwe KISWAHILI au KIINGEREZA unaweza kushiriki kwa kuwafuata kwenye ukurasa wao wa twitter kwa anwani ya  @hakielimu 

shiriki kwa kupiga kura yako je lugha ipi ungependa itumike kufundishia?

Jumatatu, 25 Januari 2016

shule ya msingi Mwisenge B yafanikiwa kupata darasa la tehama

darasa la tehama shule ya msingi Mwisenge B
wakati serikali ikiwa imetangaza na kuanza kutekeleza mpango wake wa kutoa elimu bure nchini shule ya msingi Mwisenge B ni moja kati ya shule zilizopata bahati nyingine tena ya kuweza kuboresha kiwango chake cha elimu kwa kuendana na mfumo wa kisasa zaidi wa kutumia computer tofauti na shule nyingi za msingi manispaa ya musoma mjini.
baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye chuma cha tehama
awali shirika lisilo la kiserikali la Haki Elimu liliweza kuichukua shule ya Mwisenge A na B na kuiingiza katika mipango yake na kuifanya shule ya mfano na kuweza kujenga Maktaba ya kisasa kabisa shuleni hapo pamoja na kukarabati madarasa ya awali (chekechea ( kwa kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuwapeleka walimu wa madarasa ya awali mafunzo.
mwalimu wa tehama shule ya msingi Mwisenge B
licha ya hayo shirika hilo pia limekuwa likitoa motisha kwa baadhi ya wanafunzi wanaofanya vizuri shuleni hapo hasa katika mpango uliouanzisha shuleni hapo wa vilabu vya masomo,ambapo vilabu hivyo vya masomo vimekuwa vikisaidia sana kuhakikisha vinamaliza kabisa tatizo la wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika shuleni hapo.
baada ya jitihada kubwa za shirika la Haki Elimu hivi karibuni wadau wengine wa elimu wamejitokeza na kuweza kuisaidia shule hiyo kwa kuipatia computer 17 pamoja na projector 3 na kuifungia shule hiyo huduma ya internet ya uhakika  jambo linaloonyesha nia ya kuitoa shule hiyo ilipokuwepo na kuipaisha zaidi kitaaluma .hivi karibuni kumekuwepo na mipango mbalimbali ya kuifanya shule hiyo kuwa kituo cha tehama kwa shule za msingi musoma mjini ,jambo litakalo kuwa zuri ikizingatiwa kuwa shule ya msingi Mwisenge ndipo aliposoma baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere.pamoja na iongozi wengine wakubwa kama kina jaji Sinde Joseph Warioba.








Alhamisi, 21 Januari 2016

Tamko la HakiElimu juu ya Sera Mpya ya Elimu ya 2014

JOHN KALAGE MKURUGENZI MTENDAJI  HAKI ELIMU
Ndugu Wananchi; Itakumbukwa kwamba Februari 13, 2015 Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ilizinduliwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete. Sera hii inaanza kutumika Mwaka huu (2016) wa masomo.
Sera hii, imefuta na kubatilisha matumizi ya sera nyingine za elimu zilizokuwa zikitumika kabla ya Mwaka 2015, zikiwamo Sera ya Elimu na Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo (1996), Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu (1999) na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ElimuMsingi (2007).
Lengo la Sera hii, linatajwa kuwa ni kushughulikia changamoto za ki-elimu ambazo zinajitokeza zikiwemo udhaifu katika mfumo wa elimu na mafunzo, uhaba wa walimu, uhaba wa zana, nyenzo na vifaa na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na changamoto katika ithibati na udhibiti wa ubora wa shule na vyuo katika ujumla wake ambavyo vimechangia katika kushuka kwa ubora wa elimu na mafunzo nchini.
Ili kufanikisha lengo hilo, Sera imependekeza hatua mbalimbali ikiwamo kupunguza miaka ya kupata elimu kutoka 18 (2+7+4+2+3+) hadi 16 (1+6+4+2+3); Kiswahili na Kiingereza kuwa lugha za kufundishia katika ngazi zote, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kutoa ElimuMsingi bila Ada sambamba na kupunguza michango ya wazazi shuleni.
Ndugu Wananchi; tukiwa miongoni mwa wadau muhimu katika kuhakikisha maendeleo ya elimu nchini, HakiElimu kama shirika ambalo linataka kuona elimu nchini ikiwa bora, yenye usawa na yenye kuwajengea uwezo wahitimu kukabiliana na changamoto za kimaisha na ushindani katika soko, tumepitia tumetathmini malengo na mapendekezo yaliyomo ndani ya Sera hiyo, na tungependa kutoa maoni au msimamo wa shirika kuhusu Sera hii mpya kama ifuatavyo:
Kuhusu ubora wa elimu
Pamoja na kuwa malengo ya sera yanataja kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa nchini inakuwa bora na ya viwango vya ushindani, sera imeshindwa kufafanua ni jinsi gani itahakikisha kuwepo kwa ubora huo. Katika uchambuzi tumeonesha kuwa tafiti nyingi zinakubali kuwa ili elimu inayotolewa iwe yenye ubora ni lazima taifa lijitahidi kuboresha mazingira ya ufundishaji na kuwekeza katika ubora wa walimu ambao ndio msingi wa elimu yenyewe.
Hata hivyo Sera hii imekuwa kimya juu ya suala la ubora wa walimu na mazingira yao ya kuishi na kufanyia kazi. Sera haitamki suala la kuboresha maslahi ya mwalimu.
Aidha, ili kuhakikisha ubora mashuleni, shule, taasisi na vyuo vinapaswa kufanyiwa ukaguzi kuhusu ufundishaji, ujifunzaji, mazingira n.k. Hata hivyo sera hii haitoi mwongozo maalumu kuhusu namna ubora wa elimu utakavyo tathiminiwa na jinsi ya kuimarisha ukaguzi. Itakumbukwa kuwa Idara ya Ukaguzi kwa kipindi kirefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto lukuki zikiwemo za uhaba wa bajeti na wataalamu. Takwimu zinaonesha kuwa hali ya ukaguzi nchini hairidhishi kwani ni takribani 40% tu ya taasisi za elimu ndizo hukaguliwa kwa mwaka..
Juu ya uwezo wa wahitimu kujiajiri,
Ndugu Wananchi lengo kubwa la mfumo wowote wa elimu duniani ni kuzalisha rasilimali watu. Pamoja na Sera hii mpya kuzungumzia kwa ujumla kuwa itaweka utaratibu utakaowawezesha wahitimu kuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira pamoja na kujiajiri; haitoi mwongozo ni kwa namna gani au hasa ni nini kitafanyika ili kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa.
Changamoto kubwa ya zao la rasilimali watu linalozalishwa na shule na taasisi zetu imekuwa ni uwezo hafifu. Ushindani katika soko la ajira umeiweka pembeni Tanzania kiasi kwamba katika kushindania kazi za kimataifa tunashindwa kufua dafu hata mbele ya wenzetu wa Afrika Mashariki mathalani kutoka Kenya, Uganda na hata Rwanda. Ripoti ya World Economic Forum Network Readiness Index (2012 inaonesha kuwa Tanzania inashika nafasi ya mwisho miongoni mwa nchi za ukanda wa Afrika mashariki kwa kuwaandaa wananchi wake kuwa rasilimali watu yenye ujuzi na maarifa bora. Sera kama mwongozo ilipaswa kutoa utaratibu wa jinsi ya kulikabiri tatizo hili la uwezo wa wahitimu ili kuwezesha kuwa na ujuzi na maarifa yatakayowafanya waweze kuajiriwa na kujiajiri kirahisi zaidi.
Kuhusu lugha ya kufundishia
Ndugu Wananchi; Sera Mpya imeruhusu lugha za Kiswahili na Kiingereza kutumika kama lugha za kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini. Tamko hili la kisera si tu ni ishara ya Taifa kutokuwa na msimamo juu ya lugha ya kufundishia and kujifunzia, lakini pia sera haijabainisha malengo mahsusi ya kutumia lugha mbili kufundishia katika ngazi zote za elimu . Uchaguzi wa lugha ya kufundishia lazima ulenge kuwawezesha wanafunzi kufundishwa na kujifunza ipasavyo ili kupata ujuzi na maarifa tarajiwa. Pia uchaguzi wa lugha ya kufundishia lazima ulenge kuwawezesha wahitimu wa kada mbalimbali za utaalamu kuweza kushindana katika soko la kitaifa na kimataifa Tunaishauri serikali kutathmini utekelezaji wa agizo hili la kutumia lugha mbili ikizingatiwa mambo mawili (a) urahisi wa upatikanaji wa maarifa ya mjifunzaji yanayokidhi soko la ajira na mwingiliano wa kijamii kati ya nchi na nchi.
Suala la usawa katika utoaji elimu,
Ndugu Wananchii; Pamoja na kuwa sera imetamka kuwa itahakikisha usawa katika elimu inayotolewa, bado haikueleza ni kwa namna gani hilo linaweza kufanikiwa wakati bado shule za umma zinakabiliwa na changamoto nyingi za mazingira ya kujifunzia na kufundishia ukilinganisha na shule binafsi.
Wakati wanafunzi katika shule za umma wakikosa walimu bora kutokana na walimu kukimbia malipo duni na mazingira magumu, wakikosa vitabu na maabara, wenzao katika shule binafsi wananufaika na mazingira mazuri, hamasa ya walimu, uwepo wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na hivyo kuwawezesha kufanya wafaulu vizuri katika masomo yao kuliko wanafuzni wa shule za umma.
Kwa kushindwa kushughulikia suala hili, sera imeshindwa kupendekeza mbinu za kuondoa matabaka ya kielimu nchini ambayo yanawagawa watoto wa masikini kusoma kwenye shule zenye mazingira duni ya kufundishia na kujifunzia na watoto wa wenye uwezo kusoma katika shule zenye mazingira mazuri. Ikumbukwe kuwa wanafunzi walioko kwenye shule za umma ni asilimia 94.7 ya wanafunzi wote walioko elimumsingi kwa takwimu za mwaka wa 2015.
Rai yetu ni kuwa, ili kuleta usawa katika ujifunzaji ni lazima serikali ikishirikiana na wadau wa elimu iboreshe mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za umma. Sera itoe mwongozo juu ya viwango maalumu vinavyohitajika kabla shule yeyote haijasajiliwa ili kuanza kutoa huduma elimu kama inavyofanya kwenye shule binafsi. Ni vyema pia viwango hivi vikahusisha kuwepo kwa miundombinu bora na ya kutosha vikiwamo nyumba za walimu, madarasa, vyoo, maji, maktaba, maabara na vifaa vyote muhimu vya kufundishia na kujifunzia.
Kuhusu ElimuMsingi bila Ada
Ndugu Wanahabari; Pamoja na kuwa wazo hili ni zuri na linaungwa mkono na wadau mbalimbali wa elimu ikiwamo HakiElimu, sera haikutoa utaratibu maalumu wa jinsi ambavyo tamko hili litafanikiwa. Serikali ni lazima ikumbuke kuwa kuwaweka shuleni watoto na wakajifunza ipasavyo kunahitaji gharama, tumeshuhudia utekelezaji wa sera ya elimu ya 1995 kupitia miradi ya MMEM na MMES ikishindwa kutokana uhaba wa bajeti.
Tayari serikali imeanza kutekeleza mpango wa kutoa elimu bila malipo kwa kuondoa ada na michango. Japo serikali imedhamiria kutoa 100% ya fedha za ruzuku kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa shule, bado kuna changamoto ya namna gani serikali itasaidia uboreshaji wa miundombinu shuleni ikizingatiwa kuwa shule hazipati fedha za shughuli za maendeleo na zimekuwa zikitatua matatizo ya miundombinu kwa kutumia michango ya wazazi. Tayari suala la elimu bila malipo limeanza kuleta mkanganyiko kwa wazazi na walimu wakuu hasa kuhusu uchangiaji wa kuboresha miundombinu ambao bado haujawekwa bayana na serikali. Serikali haina budi kuandaa mkakati utakaowezesha utekelezaji wa elimu bila malipo huku ikilenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katia shule zote za umma.
Ndugu Wanahabari; HakiElimu inapendekeza yafuatayo yawekwe kwenye miongozo ya utekelezaji wa Sera hii ili iweze kuleta tija na kusaidia kuboresha elimu yetu nchini.
Kama Taifa tunapaswa kutambua kuwa ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia unazifanya nchi na mataifa kuhusiana kwa karibu zaidi kuliko ilivyokuwa awali na hakuna taifa litakaloweza kuishi kama kisiwa. Ni muhimu Tanzania ikafanya tathmini hii na kuweka bayana msimamo wake kuhusu lugha tunayotaka kuitumia katika kuelimisha jamii na kizazi chetu kijacho. HakiElimu inaona kuwa njia pekee ya kutatua suala hili ni kuchagua lugha ambayo itaendana na uwekezaji ili kuwe na tija katika ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi ili wanafunzi wapate maarifa na ujuzi stahili na kuweza kushindana katika masoko ya ajira kimataifa
Suala la umri na miaka ya mwanafunzi kukaa shuleni lisipewe uzito kiasi cha kusahau jukumu la msingi la elimu nchini ambalo ni kuelimisha na kupandikiza weledi kwa watoto wetu. HakiElimu tunapendekeza badala ya kuweka uzito katika umri wa mwanafunzi, ni vema ikaangalia zaidi nini mwanafunzi anajifunza na vipi kinamsaidia katika kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Kwa kuwa Sera bado inaruhusu taasisi binafsi na wadau kushiriki katika utoaji elimu nchini, ni muhimu pia ikaweka utaratibu maalumu wa jinsi ambavyo shule za umma zitaboreshwa ili kuondoa tofauti ya shule za umma na binafsi na hivyo kuondoa matabaka kielimu.
Ubora wa elimu umekuwa ni changamoto ya muda mrefu sasa na ni muda muafaka kwa serikali kuandaa mikakati itakayowezesha kuboresha elimu yetu katika ngazi zote za elimu. Njia pekee ya kufanikisha hili ni kuwa na shule bora za umma ambazo zinahudumia wanafunzi wengi, kuwa na walimu bora na wenye hamasa ya kufundisha, kuwa na mifumo ya kufuatilia na kutathmini kiwango cha elimu katika ngazi zote na mifumo bora ya usimamizi wa shule.
Mwisho tunaipongeza Serikali kwa juhudi za kuhakikisha Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 inapatikana.Hii ni baada ya kuwepo kilio cha muda mrefu kutoka kwa umma na wadau wa elimu kudai kufanyiwa marekebisho kwa sera za elimu za zamani ambazo ni dhahiri zilikwishapitwa na wakati na hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto mpya za elimu.
Kupata nakala ya jarida lililobeba uchambuzi wa kina wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 tembelea http://www.hakielimu.org/publicatio...
Imetolewa na Idara ya Habari na Utetezi
HakiElimu
Mawasiliano: media@hakielimu.org