Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 18 Septemba 2014

mwanafunzi ajinyonga na kuacha ujumbe unaowalaumu madaktari

Mwanafunzi, Ezra Gerald Wabamba, aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Ihungo, mkoani Kagera, amekatisha maisha yake kwa kujinyonga akiwa hospitalini na kuacha ujumbe mzito juu ya chanzo cha kifo chake.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gilles Muroto, mwanafunzi huyo alifikishwa hosptalini hapo Septemba 11, mwaka huu na kulazwa ili kupatiwa matibabu.

Alisema Ezra alijinyonga saa 1:30 asubuhi katika mti ulikuwa umbali wa hatua 73 kutoka kwenye wodi ya wagonjwa namba tatu aliyokuwa amelazwa, kwa kutumia shuka yake binafsi.

Alisema baada ya maiti yake kugundulika na kufanyiwa upekuzi kwenye mifuko yake ya nguo kulikutwa Sh. 3,900, funguo mbili za Solex na kipande cha karatasi chenye ujumbe.

Alisema ujumbe huo ulisomeka: “Haiwezekani binadamu kuhudumiwa kama mbwa, yaani nafika hospitali naeleza hali yangu halafu daktari ananiandikia kulazwa bila ya kupimwa, sasa sijui watatibu  nini?, kwa kweli siwezi kuvumilia yaani wenzangu wanasoma halafu mimi nimekalishwa tu hapa hospitalini bila ya kujua wananitibu nini, inaniuma sana  mpaka kufika hatua hii ya kujiondoa duniani, ni kwasababu ninaona wanachezea ndoto zangu, mimi siwezi kuona ndoto yangu inazimwa wakati ninatakiwa niwepo shuleni nikamilishe ndoto zangu, mjitahidi tukutane mbinguni.”

Mwanafunzi huyo alimalizia ujumbe huo kwa maeneo ya kiingereza yaliyosomeka: “ Respect my family and brother Henry.”

Kamanda Muroto alisema katika tukio hilo hakuna aliyekamatwa ila uchunguzi juu ya kifo cha mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma masomo ya mchepuo wa kemia, bailojia na jiografia (CBG) unaendelea, ili utaratibu wa kuukabidhi mwili wa marehemu kwa familia yake yenye makazi yake mkoani Tabora ufanyike.

Juhudi za kumpata Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Kagera, Dk. Thomas Rutachunzibwa, ili kupata ufafanuzi wa kifo hicho chenye mazingira tata hazikufanikiwa kutokana na kuwa nje kiofisi, ingawa Katibu wa hostali hiyo, Justus Benges, alithibitisha tukio hilo kutokea hospitalini hapo.

Alisema mwanafunzi huyo alikuwa akiendelea na huduma ya matibabu kutokana na kugundulika na ugonjwa wa malaria kali.

Mazingira ya kifo cha mwanafunzi huyo yameleta sintofahamu katika jamii ya wakazi wa mji wa Bukoba, huku baadhi  wakihusisha kuwapo huduma mbovu inayotolewa na hositali hiyo pamoja na lugha zisizorafiki kwa wagonjwa.

Imebainika kuwa marehemu tangu alazwe hospitalini hapo, alikuwa akihudumiwa kwa kupelekewa chakula na wanafunzi marafiki zake ambao walikuwa wakitoka shuleni.

chanzo Ippmedia.com

Ijumaa, 12 Septemba 2014

diwani kata ya kigera ahukumiwa kifungo miaka 3 kwa kosa la kubomoa madarasa

madarasa yaliyobomolewa na kuwaacha wanafunzi bila kuwa na pahala pa kusomea
diwani wa kata ya kigera mheshimiwa Gabriel Ocharo Aenda  amehukumiwa kifungo cha cha nje miaka mitatu na kulipa fidia ya milioni tano kwa kosa la kubomoa madarasa matatu yenye vyumba 6 vya madarasa katika shule ya msingi Kigera

Diwani huyo amekubwa na dhoruba hiyo baada ya kugundulika kubomoa madarasa hayo pasipo kufuata utaratibu. hivi karibuni ililipotiwa na kituo cha habari cha BBC katika kipindi cha haba na haba kuwa wanafunzi wa madarasa ya awali wa shule hiyo wamekuwa wakisomea katika moja ya jengo la ofisi kutokana na upungufu wa madarasa.
lakini suala hilo limechukua sura ya kisiasa zaidi baada ya MNEC Vedastus Manyinyi Mathayo kutoa ahadi hewa katika moja ya mikutano yake ya kisiasa kuwa atatoa mabati 100 kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo ambapo mpaka leo hajapeleka hata bati moja
hivi karibuni Mbunge wa Musoma Mjini  Vincent Nyerere na Meya Alex Kisurula katika mikutano yao ya kuelezea mafanikio na changamoto wameahidi wananchi wa kata ya Kigera kuwa madarasa hayo yatakarabatiwa kabla ya mwezi disemba mwaka huu.

wito wetu marafiki wa elimu musoma kwa viongozi :  ELIMU NI TAALUMA ISIYOHITAJI SIASA VIONGOZI WASILETE MCHEZO NA ELIMU YA WATOTO WA MASKINI.

Jumatano, 10 Septemba 2014

kila la heri wanafunzi wa darasa la 7 kwa mitihani yenu ya kumaliza elimu ya msingi

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Jenista Mhagama
Jumla ya watahiniwa 808,111 wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi leo, huku kati ya hao wavulana ni 378,470 sawa na asilimia 46.84 na wasichana ni 429,641  (asilimia 53.16).

Aidha, katika mtihani huo, watahiniwa 783,223 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili, watahiniwa 24,888 watafanya mtihami kwa lugha ya Kiingereza.

Kwa upande wa wasioona walioandikishwa kufanya mtihani ni 86 , wavulana 54 na wasichana 32, na watahiniwa wenye uoni hafifu wanaotarajiwa kufanya mtihani huo ni 714, kati yao  wavulana ni 371 na wasichana 343.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, alisema maandalizi yote kwa ajili ya mtihani yameshakamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, fomu maalum za OMR za kujibia mitihani pamoja na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo.

Mhagama alisema mtihani mtihani huo ni muhimu kwa taifa, wazazi na jamii kwa ujumla na kwamba masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii  mtihani ambao utafanyika kwa siku mbili mfululizo.

Alitoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na wilaya kuhakikisha taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo na kuwataka wasimamizi, walimu, wananchi na wanafunzi  kutoshiriki katika vitendo vya udanganyifu na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alhamisi, 4 Septemba 2014

Shule nyingi za msingi nchini zakabiliwa upungufu madawati

baadhi ya wanafunzi shule ya msingi mwisenge wakiwa wamekaa sakafuni
Shule nyingi za msingi zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati, hali inayotishia maendeleo ya elimu nchini.

Wakizungumza kwa njia ya simu kwa nyakati tofauti na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One Stereo, wakuu wa mikoa ya Iringa, Dodoma, Morogoro na Tanga, walithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo katika mikoa yao.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, alisema kwa njia ya simu kuwa licha ya mkoa wake kuwa unazalisha miti mingi ya mbao na uwapo wa shamba la miti la Taifa (Sao Hill), upungufu wa madawati upo, ingawa si mkubwa ukilinganisha na mikoa mingine.

Alisema tayari serikali ya mkoa wake imeshaanza kujipanga mapema kulikabili tatizo hilo hata kabla ya tamko la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku mkoa huo ukijiwekea mikakati ya kuhakikisha unatekeleza agizo hilo mapema mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, alisema mkoa wake una upungufu wa madawati kwa asilimia zaidi ya 40 kutokana na kutokuwa na vyanzo vizuri vya miti ya mbao suala, ambalo limekuwa ni changamoto kubwa.

Alisema ili kufikia malengo, wameanza na kuimarisha mfuko wa elimu na kwamba, wameweka utaratibu wa wilaya kuchangia Sh. 10,000 na nyingine kuchangia Sh. 5,000, kupitia mifugo ya kuku wanaopatikana kwa wingi katika mkoa huo.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alikiri mkoa wake kukabiliwa na uhaba mkubwa wa madawati, hasa katika shule za msingi na kwamba, kwa tathmini waliyoifanya ni upungufu wa kiasi cha madawati 91,000 kwa wilaya zote mkoani humo.

Tatizo la uhaba wa madawati limekuwa ni changamoto kubwa nchini kiasi cha kumfanya Pinda kutoa tamko la kuwataka wakuu wote wa mikoa kuhakikisha kila mmoja anamaliza tatizo hilo ifikapo Juni 30, 2015.

chanzo ippmedia,
picha. marafiki wa elimu musoma