Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Ijumaa, 28 Machi 2014

mwanafunzi bingwa wa hisabati na ndoto za udaktari

Unapomuona kabla ya kuzungumza naye, ni rahisi kuamini kwamba Sunday Mrutu (18) ana hulka ya usikivu, upole na kutafakari kabla ya kutamka ama kuchukua hatua yoyote. Ndivyo ilikuwa wakati nikijiandaa kumhoji, muda mfupi baada ya uongozi wa Shule za St. Anne Marie za jijini Dar es Salaam, kumtunukia Sh milioni tatu, kutokana na mafanikio yake katika mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka jana. Mkurugenzi wa Shule za St. Anne Marie, Jasson Rweikiza, Uanamtaja Mrutu kuwa kati ya wanafunzi wawili wa shule hiyo waliopata kati ya pointi saba na tisa za daraja la kwanza, yeye (Mrutu) akiwa na pointi saba. Kwa upande mwingine, Rwekiza akasema Mrutu alikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora nchi nzima, akishika nafasi ya sita, wakati aliongoza katika utahiniwa uliofanywa na Baraza la Mitihani, kama ilivyo kwa hisabati aliyopata alama 98 kati ya 100. Rwekiza anasema matokeo hayo na mengine hususani yaliyowahusisha wanafunzi 32 wa St. Anne na shule dada ya Brilliant, waliopata daraja la kwanza, yanajenga heshima kwa vijana hao na uongozi wa shule hizo. Tayari uongozi wa St. Anne Marie, Brilliant Sunshine, zote zikimiliwa na Rwekiza, zimetoa jumla ya Shilingi milioni 13.2 kwa wanafunzi waliopata daraja la kwanza. Zawadi hizo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mkurugenzi wa shule hizo, Rwekiza, kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka jana. Wanafunzi hao walipata kiasi tofauti cha fedha ambapo waliofaulu kwa kati ya pointi 15-17 walikuwa 14 na walizawadiwa Shilingi 200,000 kila mmoja. Wengine na kiasi cha fedha alizopata kila mmoja ni 13 waliofaulu kwa kati ya pointi 13-14 (300,000), wanafunzi watano waliofaulu kwa kati ya pointi 10-12 (500,000) na wawili waliopata kati ya pointi 7-9 (1,000,000). Hata hivyo, mwanafunzi aliyekuwa miongoni mwa wawili hao, SundayMrutu alipewa zawadi tofauti kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata katika mitihani hiyo. Mwanafunzi huyo alizawadiwa Shilingi 1,000,000 kwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora nchini ambapo alishika nafasi ya sita huku akiwa wa kwanza kwa upande wa wavulana. Pia Mrutu alizawadiwa Shilingi 500,000 kwa kuwa wa kwanza kwenye utahiniwa uliofanywa na Baraza la Mitihani la Taifa na kiasi kama hicho kwa kuongoza katika somo la hisabati nchi nzima, ambapo alipata alama 98. Rwekiza, akasema ingawa fedha hizo zinaweza kuonekana kuwa nyingi, lakini zitasaidia kuibua na kuhamasisha ari ya usomaji kwa wanafunzi wa shule hizo na nyingine nchini. “Tunalolifanya hapa kwa kutoa zawadi hizi za hamasa ni jambo la kawaida kwa kila mwaka, lengo kubwa hapa ni kuhakikisha watoto wetu wanaamini kwamba ahadi tunayowapa kuhusu kusoma kwa bidii zinatekelezwa,” anasema. Mrutu anathibitisha kwamba hisabati ni moja ya masomo anayoyamudu darasani, hali hiyo ikichochewa na umakini, usikivu na uelewa pindi mwalimu anapofundisha darasani. “Hisabati inaaminika kuwa somo gumu sana, lakini ninaamini kwamba kama mwanafunzi atakuwa msikivu, atatulia na kufuata mafundisho ya mwalimu, itakuwa kinyume chake….hisabati ni somo zuri na linaloeleweka kwa urahisi,” anasema. Mrutu anakumbuka namna alivyowafuatilia na kuwatii walimu wake waliowahi kumfundisha hisabati, akiwataja kwa jina moja moja kuwa Tarimo, Tino na Samuel. Wakati Mrutu akisema hivyo, wanafunzi wa shule kadhaa za sekondari wamekuwa wakilielezea somo hilo kama moja ya masomo yanayowashinda katika kusoma na kufaulu. KUHUSU UFAULU WAKE Mrutu anasema hadi matokeo ya kidato cha nne yalipotoka na kutaarifiwa kuhusu ufaulu wake, hakuamini kwa urahisi. “Nilifuatwa nyumbani (bila kumtaja mtu aliyemfuata) na kuambiwa kwamba nimefanikiwa vizuri sana kwenye mitihani yangu,” anasema. ANAPENDELEA UDAKTARI Mrutu anasema pamoja na kuwa na uwezo unaomfanya alimudu vyema somo la hisabati, kusudio lake ni kutaka kusomea Udaktari. “Ninajua hisabati ni somo muhimu lisilopewa kipaumbele sana kwa madaktari, ila mimi nafsi yangu ni kuona ninasoma kufikia kuwa Daktari wa binadamu,” anasema. CHANGAMOTO KWA WANAFUNZI SHULENI Mrutu, anasema ni jambo lililo wazi kwamba katika maisha ya takribani miaka minne ya kusoma sekondari ya awali, wanafunzi wanajenga urafiki na uhusiano wa karibu. Hata hivyo, anasema kinachotakiwa kwa mwanafunzi ni kuweka mipaka ya urafiki na uhusiano, kisha kusimamia dhamira, nia na utashi vinavyomuongoza. Anasema kukosekana kwa mipaka katika urafiki na uhusiano, ni miongoni mwa vyanzo vya kuibuka tabia zisizofaa, nyingi kati ya hizo zikitokana na kujifunza kunasababishwa na muingiliano wa kirafiki ama kimahusiano. “Sasa inapokuwa kwamba mpo marafiki wengi shuleni na huwezi kuwakimbia, ni vizuri mwanafunzi ukajiepusha na kuiga mambo, vinginevyo utajikuta unaachwa na wale uliokuwa unawaiga, kwa maana kila mtu ana mbinu zake,” anasema. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI