Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 21 Agosti 2014

Wanafunzi 28,000 elimu ya juu kukosa mikopo

Wanafunzi 28,037 watakosa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), hivyo kulazimika kusaka njia mbadala kama wanataka kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Idadi hiyo ni sehemu ya wanafunzi 58,037 ambao hadi kufikia Julai 31, mwaka huu walikuwa wamewasilisha maombi ya mikopo kwa ajili ya mwaka wa masomo 2014/15, huku bodi hiyo ikiwa na uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 30,000 pekee wa mwaka wa kwanza.

Idadi hiyo inafanya asilimia 49 ya waombaji wote kusaka vyanzo mbadala kama wanataka kuendelea na elimu ya juu nchini kwa mwaka ujao. HELSB imesema kuwa ina uwezo wa kutoa mikopo kwa asilimia 51.5 pekee.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salama jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisoba, alisema maombi yaliyopokelewa mwaka huu yameongezeka kutoka 53,239 mwaka jana hadi 58,037 sawa na ongezeko la asilimia tisa.

Alisema miongoni mwa waombaji wa mikopo, kundi la diploma ya ualimu wa sayansi ni 480 wakati wale wa shahada ya uzamili/uzamivu kwa vyuo vya ndani ya nchi wakiwa ni 276.

Kwa mujibu wa Mwaisoba, waombaji wa shahada kwanza kwa vyuo vya ndani ya nchi ni 56,922, wale wa shahada ya uzamili/uzamivu nje ya nchi wakiwa ni 126 na wale wa shahada ya kwanza nje ya nchi ni 233.

Alisema baada ya kufungwa rasmi kwa kipindi cha kupokea maombi ya mikopo, hatua inayoendelea kwa sasa ni uhakiki wa taarifa za waombaji kwa kuzipitia nyaraka mbalimbali zilizoambatanishwa na waombaji mikopo.

Nyaraka hizo ni cheti cha kuzaliwa, vyeti vya taaluma, vielelezo vya mdhamini, saini ya mwombaji na mdhamini wake na ushuhuda wa mwanasheria au hakimu kwamba vivuli vya nyaraka zilizowasilishwa kwenye bodi ni halisi.

Alisema mchakato wa uchambuzi na upangaji wa mikopo utakamilika baada ya majina ya wanafunzi waliodahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kujiunga na vyuo mbalimbali yanapowasilishwa rasmi kwenye bodi.

Kwa mujibu wa Mwaisoba, udahili wa wanafunzi unafanywa na TCU kwa mfumo wa pamoja wa udahili (CAS) unaotumiwa na vyuo takriban vyote vya elimu ya juu nchini. Alisema kwa vyuo ambavyo havimo katika mfumo wa pamoja wa CAS hutuma TCU majina ya wanafunzi, ambao vimewadahili ili wathibitishwe kabla ya kupatiwa mikopo.

“Taarifa za udahili ni muhimu katika zoezi la upangaji wa mikopo kwa kuwa zinatoa mwongozo wa gharama halisi za program za mafunzo,” alisema Mwaisoba.

Alisema wanafunzi wanaostahili na waliotimiza masharti na vigezo vya ukopeshaji ndiyo hupangiwa mikopo kulingana na bajeti iliyotengwa na serikali.

Mwaisoba alisema majina ya wanafunzi waliopata mikopo kulingana na udahili, yatatangazwa kwenye tovuti ya bodi na katika vyombo vya habari ili kuwataarifu wadau wote ikiwa ni pamoja na wanafunzi, vyuo vya elimu ya juu, wazazi na umma kwa jumla.

Alisema nakala za majina ya wanafunzi waliopangiwa mikopo zitatumwa kwenye vyuo husika.

Mwaisoba, alisema kwa kutambua umuhimu wa masomo ya sayansi na kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo hayo katika ngazi ya shule za msingi na sekondari, mwaka huu serikali imetoa fursa ya mikopo kwa wanafunzi watakaojiunga na masomo ya stashahada maalumu ya ualimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Alisema wanafunzi 5,000 wanatarajiwa kujiunga na stashahada hiyo maalumu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na kwamba, wote watanufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

“Kwa taarifa hii, bodi inapenda kuwataarifu wadau wote kuwa mchakato wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 unaendelea,” alisema Mwaisoba.

Aliwataka waombaji wa mikopo, wazazi/walezi na umma kwa jumla kutambua kuwa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uchangiaji wa elimu ya juu na hivyo iwapo kuna waombaji wanaoweza kujigharimia, wasiombe mikopo ili kutoa nafasi kwa wahitaji wengi zaidi.

Alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili HESLB ni pamoja na ucheleweshaji wa urejeshaji wa mikopo, ushirikiano hafifu kutoka kwa wadau katika urejeshaji wa mikopo na mazingira ya kijiografia kuweza kuwafuatilia waliokopa.

Hata hivyo, alisema HESLB ina uwezo wa kukusanya marejesho ya mikopo Sh. bilioni tatu kwa mwezi.

KUMALIZANA NA TAHLISO WIKI IJAYO
Kuhusu madai ya wanafunzi wa vyuo vitano ya kutaka wapewe Sh. bilioni 6.6 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, Mwaisoba alisema malipo hayo yanaandaliwa na kwamba, hundi za malipo hayo zinatarajiwa kupelekwa katika vyuo wiki ijayo.

Alisema wanafunzi wa vyuo hivyo walichelewa kulipwa kutokana na fedha kuchelewa kupatikana.Hali hiyo ilisababisha Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (Tahliso) kuitisha maandamano ya amani wiki iliyopita kwenda ofisi za Waziri Mkuu kushinikiza serikali kuwalipa fedha hizo.

Hata hivyo, maandamano hayo yalisambaratishwa na Jeshi la Polisi, lakini siku mbili baadaye, Tahliso ilitangaza tena kuitisha maandamano keshokutwa.

Kiwango hicho cha fedha kinachodaiwa na wanafunzi hao, kimo kwenye takwimu zilitolewa na Mkurugenzi wa HESLB wakati wakifanya mazungumzo juu ya hatma ya vyuo hivyo.

Vyuo hivyo, ambavyo havijapata  fedha hizo ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) Mwanza na Tabora, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji-Mbeya, Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMUCCO) na Chuo Kikuu cha Jordan Morogoro.    

CHANZO IPPMEDIA.COM