Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 3 Oktoba 2013

Wanaorudia mitihani kidato cha pili watahadharishwa


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome
 
Wanafunzi 136,923 wa kidato cha pili wanaorudia mitihani, wapo hatarini kutimuliwa shuleni na kurudi mitaani ikiwa watashindwa kufaulu kwa mara ya pili baada ya serikali kuwapa nafasi ya mwisho mwaka huu 2013 kurudia.

Kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 74,020 na wasichana ni 62,903, ambao mwaka jana walifeli mitihani ya kidato cha pili na serikali kuamua kuwapa nafasi ya mwisho ili wajaribu tena mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema jana kuwa mwaka huu mitihani ya pili itafanyika kati ya Oktoba 7 hadi 21 na kwamba, jumla ya watahiniwa 531,457 wataifanya, wakiwamo wa shule binafsi na za serikali.

Alisema vituo vilivyosajili watahiniwa ni 4437, ikiwa ni ongezeko la vituo 140 sawa na asilimia 3.3 ikilinganishwa na vituo 4,497 vilivyosajiliwa mwaka jana.

Alisema sera ya wizara yake inasema mwanafunzi anayefeli mara ya pili mitihani hiyo ataondolewa shuleni kwa maana ya kuendelea na mfumo rasmi na kwamba, msimamo huo hautabadilika.

Ikiwa serikali itaendelea na msimamo huo, wanafunzi 136,923 waliofeli mwaka jana ikiwa pia mwaka huu watafeli watalazimika kurudi nyumbani kwa kuwa serikali haitawapokea katika mfumo rasmi wa elimu.

Profesa Mchome alisema wanafunzi watakaofeli kwa mara ya pili, labda wajaribu kujisomea wenyewe ili wafanye mitihani ya QT, ambayo mara nyingi hufanywa na watu wazima ama waende katika vyuo vya ufundi ikiwa Veta.

Watahiniwa wa mwaka huu, wasichana ni 270,734 (sawa na asilimia 50.9) na wavulana 260,723 (sawa na silimia 49.1), wakiwamo wanafunzi wenye ulemavu wa kuona.

chanzo. ippmedia.com