Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 29 Januari 2014

serikali kusambaza tabuleti shule za sekondari nchini

Serikali inakusudia kutoa maelfu kwa maelfu ya tabuleti za kufundishia masomo mbalimbali kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari nchini kama njia ya ubunifu zaidi, ya kisayansi na ya uhakika ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

Ili kufanikisha mpango huo, Serikali inakusudia kuingia ushirikiano na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Opportunity Education Trust ya Marekani ambayo jana ilizindua mpango wa majaribio wa utoaji wa tabuleti hizo kwa wanafunzi na walimu wao wa shule za sekondari nchini.

Mpango wa Serikali wa kusambaza tabuleti kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari ulitangazwa juzi na Rais Jakaya Kikwete, alipokutana na kuzungumza na Joe Ricketts, mwenye taasisi ya Opportunity Education Trust na mmoja wa matajiri wa Marekani.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete alimweleza kwa undani Ricketts hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali yake kupania na kuboresha elimu tokea mwaka 2006, hatua ambazo zimechangia kupanua kwa kasi na kwa kiwango kikubwa wigo wa utoaji elimu nchini na changamoto ambazo zimezuka kutokana na upanuzi huo mkubwa.

Rais Kikwete alisema baadhi ya changamoto hizo ni ukosefu wa walimu na hasa wa masomo ya sayansi na ukosefu wa vitabu vya kufundishia, changamoto mbili kubwa ambazo zinatatuliwa na matumizi ya tabuleti.

“Mbali na upanuzi mkubwa wa nafasi za wanafunzi kupata elimu ya ngazi mbalimbali, pia tumepanua sana ufundishaji wa walimu. Mwaka 2005, vyuo vyetu vyote vilikuwa vinatoa walimu 500 sasa tunatoa walimu 12,000 kwa mwaka. Hivyo, tunaamini kuwa katika mwaka mmoja ama miwili ijayo, tutakuwa tumemaliza tatizo la walimu wa masomo ya sanaa,” alisema.

Hata hivyo, alisema bado nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi.

"Tuna upungufu wa walimu 26,000 na kwa mwaka vyuo vyetu vyote vinahitimisha walimu 2,100 tu," alisema.

Chini ya mpango huo wa majaribio wa kusambaza teknolojia hiyo ya kisasa, taasisi ya Opportunity Education Trust inatoa tabuleti 1,100 kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa sekondari katika shule 33.

Ricketts alimwambia Rais Kikwete: “Hapa tunafanya majaribio na Tanzania ni nchi ya kwanza duniani miongoni mwa nchi ambazo tunaunga mkono mipango ya maendeleo kunufaika na mpango huo wa majaribio. Ni azma yetu kuwa baada ya kuwa tumefanya tathmini ya mafanikio na changamoto za hatua hii ya majaribio, tutaupanua mpango huu kushirikisha shule nyingi zaidi kwa kushirikiana na Serikali kwenye mpango wake mkubwa wa kusambaza teknolojia hii katika shule zote za sekondari hapa Tanzania.”

Ricketts na wataalam wake pamoja na maofisa wa Serikali walianza kutekeleza mpango huo jana kwa kutoa tabuleti kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Wama Nakayama iliyoko mkoani Pwani.

Baada ya hapo, shughuli hiyo itahamia Zanzibar na Pemba, kabla ya Ricketts na wataalam wake kutoa tabuleti kwa shule zilizoko mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kagera na Morogoro.

Shule zinazonufaika katika mpango huo ni za Serikali na binafsi na kwa kuanzia masomo ambayo yanapatikana katika tabuleti hizo ni Hesabu, Jiografia, Historia na Kiingereza.
 
chanzo ippmedia.com