Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumanne, 10 Juni 2014

kelele za Mbatia kuhusu ubora wa elimu je anasikilizwa?

james mbatia
Mbunge James Mbatia unajisumbua. Natambua uchungu ulio nao juu ya kudorora kwa sekta ya elimu, na natambua uhitaji wako wa mabadiliko katika sekta hii mapema inavyowezekana, lakini unajisumbua.

Sisemi kuwa ukate tamaa, na mimi sikati tamaa, ila naona unazungumza na watu ambao hawawezi kuelewa maana ya kile unachosema na kuhimiza. Nataka nieleza yafuatayo.

Mwaka jana ulipozungumza kuhusu mitaala, kuwa hakuna na kuwa sekta ya elimu inaendeshwa mzobemzobe kama Waluguru ambavyo wangesema, na kuwa vitabu vinavyotumika katika shule zetu havina uhakika wa ubora wake walikubeza, walikutukana, walikutenga, na kukuona mzushi.

Lakini wiki mbili baada ya kuahirishwa kwa Bunge, matokeo ya mitihani yakatoka, na kilichotokea, kuhusu kufeli kwa wanafunzi, Mungu tu anajua.
Mungu alikulipia na kuwaaibisha wale waliodhani kuwa ulikuwa mzushi, na ukarabati uliofanyika kuhusiana na matokeo hayo, na unaondelea kufanyika, sijui, ni suala la kuliombea taifa liondokane na pepo huyu ambaye hataki sisi tulioko serikalini tusikilize mawazo ya wananchi wenzetu.

Kuwa wananchi wenzetu wanapotushauri wanaonekana kuwa ni adui, na kuwa lengo lao sio kujenga ufanisi katika kutoa huduma bali kwa waliotupigia kura, bali kwa sababu wanataka kutujengea hoja tushidwe uchaguzi ujao.

Mbatia, unapokuwa na serikali ambayo wasiwasi wake ni kama itashindwa uchaguzi wa miaka mitano ijayo, na sio kama miaka mitano ijayo watakuwa na cha kuwaonyesha wananchi, katika orodha ndefu ya ahadi ndani na nje ya ilani ya uchaguzi waliyoinadi, sidhani kama unachokisema kitaeleweka.

Tumeona mwaka 2011, mara baada ya uchaguzi malumbano yakaanza ndani ya wanaserikali na walioko nje ya serikali, lakini wote wa chama kimoja, wakifanya maandalizi ya uchaguzi wa 2015.

Vikundi vya uchaguzi wa 2010 havikuvunjwa, kwa kweli vikaimarishwa na kampeni za uchaguzi kiaina zikaanza kwa makini kabisa, hadi walipoonyana wenyewe kwa wenyewe, lakini wale wenye masikio magumu wanaendelea bila kujali kitu.

Sasa hawa watu unapowaambia kuhusu kuimarisha sekta ya elimu unadhani inawezekana kweli, mawazo sio katika huduma bali katika kufanikisha chaguzi.

Mbunge Mbatia, maendeleo kwa wananchi kwa sasa, wewe unajua, sio kigezo cha kuchaguliwa. Hizo siasa zako ni za kizamani.

Sasa hivi unachaguliwa kwa sababu unaweza kutoa takrima, unaweza kuwanunulia watu ubwabwa wakashiba, ukawanunulia watu t-shirts, kofia na khanga, na kuwaimbisha nyimbo jioni wakala wakashiba.

Wananchi wa siku hizi hawaoni uhakiki wa utendaji wa walio madarakani kama ni kigezo, bali uwezo wake wa kutoa rushwa kwa wapiga kura. Sasa unapokuwa na uhakika wa kushinda kwa kutumia fedha na sio utendaji, unaanzaje kufikiria kuboresha elimu.

Elimu haikuwa kwenye ajenda wakati wa uchaguzi, ilitamkwa majukwaani kwa sababu mdomo haukosi cha kuzungumza ukikaa mbele ya kinasa sauti.

Kitu kingine ambacho unanishangaza James Mbatia ni kuwa huoni dunia inakwendaje?. Fasheni siku hizi ni kuhakikisha kuwa  watoto wanakwenda kusoma nje, na kama ni ndani basi katika shule za watu wakubwa, na wewe ukiwemo, nitashangaa kama haumo, kuwapeleka watoto kwenye English Medium, au sijui International Schools.

Unashangaa, mimi hapa ni waziri wa elimu, ofisa elimu, mkurugenzi wa elimu, mwalimu wa sekondari au mwalimu wa shule ya msingi, nimepewa dhamana ya kuhakikisha kuwa elimu inaboreshwa, na tulidhani kigezo kimojawapo ni kutuona sisi wenyewe tunawasomesha watoto wetu nje au ndani, lakini katika shule za serikali.

Lakini aka! Sasa kama tuliopewa dhamana ya kuboresha elimu tunakwepa shule zetu wenyewe, si ujue kuwa kuna jambo ambalo ni bovu tunaliona, na hatusemi ila tunawahamisha watoto wetu. Watoto wa masikini wajua wapi pa kuwapeleka wa kwao.

Kumeundwa kampeni kuwa wazazi wawagharimie watoto wao, badala ya kuimarisha shule za serikali, wanahimiza kuanzisha shule za binafsi.
Hivi kama kweli serikali ina nia ya kuboresha elimu, hao wazazi ambao wanalipa mabilioni ya fedha kwa ajili ya watoto wao, kama wangelipa robo tu ya hizo fedha kwenye shule za serikali kama ada, na serikali ikaweza kuboresha huduma na ubora wa, elimu, kungekuwa kweli na malalamiko dhidi ya sekta ya elimu?

Tungewaokoa wazazi wangapi ambao wanalipa ada kwenye shule ambazo hazina chochote ila utapeli. Lakini nadhani hatuwezi kufikiria kwa umakini.
Tunataka majibu rahisi kwa kitu kigumu, na hatutaki kufikiria kwa mkakati—strategically, bali kwa kuishi kama tulivyozoea.

Mbatia, tunahitaji kupungwa pepo huyu ambaye hataki kusikiliza vilio vya Watanzania kuhusu elimu.