Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Ijumaa, 7 Machi 2014

kauli ya Kawambwa yawachefua walimu

waziri wa elimu dk. shukuru kawambwa
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimekerwa na kauli ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa , kuwa serikali inaendelea kujadiliana na taasisi za fedha juu ya namna ya kulipa deni la malimbikizo ya mishahara ya  walimu yanayofikia Sh. bilioni 61.

CWT  imesema kauli hiyo ya serikali ni kutafuta visingizio baada ya  kushindwa kutekeleza ahadi yake kuwa ifikapo Februari, mwaka huu deni la walimu litakuwa limelipwa.

Rais wa CWT, Gration Mkoba,  alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema majadiliano ya mishahara ya walimu yalitokana na mgomo wa  2012 baada ya kukaa kwenye meza ya majadiliano na serikali ilikubali kulipa deni na kuandaa utaratibu wa kupandisha walimu madaraja.

“Inasikitisha kuona majadiliano yanahusisha waandishi wa habari bila ya kujua kuwa kwa kauli yake waziri tayari  walimu wameingia kwenye mgogoro na serikali, lakini  nawasihi walimu wasubiri tamko rasmi la mgogoro,” alisema.

Mkoba alisema tangu serikali ilipoahidi kutekeleza madai yao, hakuna hata dai moja  lililotekelezwa  lakini imewashangaza kuona ikijinadi kuwa inaendelea na majadiliano ya kulipa deni hilo wakati majadiliano hayana tija kwa mwalimu.

Alisema Novemba, mwaka jana mkutano mkuu wa CWT ulitoa siku 60 kwa serikali kukamilisha taratibu zote la kulipa malimbikizo ya mishahara ya walimu nchini.

Pia Januari mwaka huu kwenye kikao cha Baraza  la Taifa la CWT kiliazimia kuwa ifikapo mwishoni mwa Februari, mwaka huu, ikiwa serikali itashindwa kulipa malimbikizo hayo litakuwa tayari kuongoza mgomo.
CHANZO: NIPASHE

bunge la katiba lakiuka katiba ya tanzania ibara ya 18

Bunge  la Katiba limeamua kuweka kitanzi kwa uhuru wa wananchi kupata habari za mchakato wa Katiba Mpya, kwa kuwazuia waandishi wa habari kuingia kwenye Kamati 12 za wajumbe wa Bunge hilo zitakazojadili Rasimu ya Katiba.

Mjadala mkali ulizuka kwa juzi na jana kwenye Bunge hilo, huku baadhi ya wajumbe wakitaka uhuru wa wananchi kupata habari uwapo kwa waandishi kuruhusiwa kuingia kwenye kamati na wengine wakiwamo wajumbe wa Kamati ya Kanuni na Kumshauri Mwenyekiti wakipinga vikali kwa kutaka waandishi wapewe taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kamati husika.

Kifungu cha 57 fasili ya kwanza ya Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, kinaeleza kuwa vikao vyote vya kamati vitakuwa vya faragha na hakuna mtu yeyote asiyekuwa mjumbe wa kamati, mtumishi wa Bunge au mtaalam aliyeitwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum atakayeruhusiwa kukaa katika sehemu yoyote ya ukumbi wa mikutano ya kamati wakati kikao cha faragha kinaendelea.

Fasili ya tatu, inaeleza kuwa bila kuathiri masharti ya kanuni hii Mwenyekiti wa Kamati ya mjumbe yeyote kwa idhini ya Mwenyekiti anaweza kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mambo yaliyojitokeza kwenye kikao cha kamati.

Baadhi ya wajumbe waliiomba kuwasilisha mapendekezo yao kwenye kifungu hicho, walitaka waandishi wa habari kuruhusiwa kwani kwa kuwazuia ni kwenda kinyume cha ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotaka kuwapo kwa uhuru wa kupata taarifa.

OLUOCH
Ezekiel Oluoch alisema anashauri vikao viwe wazi kwani hakuna jambo la siri la kujifungia kwani wananchi wana haki ya kujua kinachojadiliwa kwenye kamati na kwamba ni vyema kamati zikawa huru.

HALIMA MDEE
Halima Mdee alisema wenye jukumu la kuzitengeneza kanuni ni wajumbe na kwamba awali kamati ya kanuni na kumshauri mwenyekiti baada ya majadala mkubwa kamati ilipendekeza waandishi waruhusiwe kuingia kwenye vikao, na ikakubaliwa kwenye vikao vya kamati ambavyo vitakuwa na mijadala mikubwa na watakapokuja kwenye Bunge watafanya majumuisho kwenye manbo yaliyojadiliwa.

“Tulikubalina watu watakaokatazwa ni wananchi wa kawaida kutokana na
udogo wa kumbi, ila waandishi wa habari wakubaliwe, sisi ndiyo tunaopitisha kanuni na sisi tuliridhia ilikuwa ni matarajio yetu,”
alisema.

Alisema waliotajwa kwenye kanuni waruhusiwe kuingia na utaratibu utakaotumika uamuliwe na mwenyektii wa kamati kushauriana na makamu mwenyekiti.

“Waandishi wa habari waingie mnaogopa nini, mnaficha nini?...hii Katiba ni ya wananchi wana haki ya kujua kila kinachoendelea ndani ya kamati na nje ya kamati na kwenye ukumbi wa Bunge,” alisema Mdee.

MOSES MACHALI

Moses Machali alipendekeza fasili ya tatu ya kifungu hicho, ifutwe kwa kuwa inaweka kitanzi kwa uhuru wa wananchi kupata habari na hakimlazimishi mwenyekiti au makamu kutoa taarifa kwa waandishi wa habari.

Alisema vikao vyote vifanyike kwa uwazi bila kuzuia mtu ingawa hawataruhusiwa kushiriki kwenye mjadala wa kamati.

“Hao wanaosisitiza kura ya wazi halafu mnaogopa na kuwakataa waandishi wa habari mnaficha nini, sioni sababu ya msingi,” alisema Machali.

MARIA SARUNGI
Maria Sarungi alisema vikao vya kamati viwe wazi kwa waandishi wa habari kwa kuwa Rasimu ya Katiba itakwenda kwao kwa ajili ya kuipigia kura.

“Mwanzo wa Rasimu ya Katiba unasema kwakuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua...Katiba hii si ya kwetu tuliokaa humu ndani bali ya wananchi wa Tanzania, mchakato ulivyoanza ilianza kwa wananchi hadi tulipofika,” alisema.

FREEMAN MBOWE
Freeman Mbowe alisema Katiba inayotungwa ni ya wananchi na wanaowakilishwa ndani ya Bunge hilo wanataka kujua kila kinachoendelea ndani ya Bunge hilo.

“Tusifikiri tunahitaji kuridhiana sisi wenyewe tulioko ndani ya Bunge hili kuna Watanzania kwa mamilioni wa vyama na taasisi mbalimbali wanatisikiliza,” alisema.

Wakati wajumbe huyo anazungumza, baadhi ya wajumbe walipiga kelele na kuzomea hali iliyomlazimu kuacha kuzungumza na mwenyekiti kumsihi kuendelea, lakini Mbowe alisema: “Siwezi kuendelea wakati wajumbe wanapiga kelele.”

MAHALU

Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Kumshauri Mwenyekti wa Muda,Prof. Costa Mahalu, alisema kamati yake inapeleka mapendekezo kwa wajumbe na wenye maamuzi ni wajumbe na baadaye wanaagizwa kurekebisha mwafaka uliofikiwa na kuonyesha msimamo wao kwa pamoja.

Mjumbe wa Kamati, Bakari Khamis Bakari, alisema hakuna uhuru usiokuwa na kinga kulingana na maelezo ya maeneo husika na kwamba kamati italichukua suala hilo na kujadailiana ili kupata namna bora ya kuruhusu waandishi wa habari kuchukua habari.

George Simbachawene, mjumbe wa Kamati ya Kanuni na Kumshauri Mwenyekiti, alisema maoni ya kamati ni kuwa hisia na sababu wanazotoa wajumbe hao zilikuwapo kwenye kamati yao na walipenda waandishi waruhusiwe ili mchakato huo uonekane kwa umma wote.

“Kilichotushinda na kufikia uamuzi wa maoni hayo ni utekelezaji wake...kwa busara yetu tukaliwekea utaratibu kwenye fasili ya tatu, vyombo vyetu vya habari ni vingi, kamati iko ukumbi wa Msekwa asubuhi anakuja mwandishi anachukua anapeleka, habari zitakazokwenda juu ya hoja moja jambo moja zitakuwa hazijakamilika zitawachanganya wananchi na si kuwasaidia,” alisema.

Alisema waandishi watachukua habari kivyao na kuwachanganya wananchi na ndiyo maana wameamua mwenyekiti wa kamati atoe taarifa kwa waandishi.

DK. MWAKYEMBE
Dk. Harrison Mwakyembe alisema kitaaluma ni mwandishi wa habari na mwanasheria na kwamba anaona hakuna haja ya waandishi wa habari kuruhusiwa kuwepo kwenye kamati na badala yake wapewa taarifa na mwenyektii wa kamati husika.

Hata hivyo, baadhi ya watoa hoja, walipinga hatua hiyo huku wanaopinga waandishi kuingia kwenye ukumbi wakishangilia kwa kupiga meza kusisitiza waandishi kunyimwa kuingai kwenye kamati hizo, huku wachache wa vyama wa upinzani wakipinga uamuzi huo.

DK. TULIA ACKSON
Mjumbe wa Kamati ya Kanuni na Kumshauri mwenyekiti, Dk. Tulia Ackson, alisema hakuna uhuru usiokuwa na mipaka na kwamba kamati inapendekeza kifungu hicho kubaki jinsi kilivyo.

Hoja hiyo ilimalizika kwa wajumbe kupitisha kifungu jinsia kilivyo kuwa waandishi hawataruhusiwa kuingia kwenye kamati na badala yake watapewa taarifa na mwenyektii wa kamati.
CHANZO: NIPASHE