Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumapili, 16 Machi 2014

Baadhi ya wanafunzi wa kiume katika shule za msingi wilayani Kibaha, Pwani, wamejiingiza katika vitendo vya kujaamiana wenyewe kwa wenyewe na watu wengine kutoka nje ya shule na kufikia hatua ya kupasua kaptula zao makusudi ili kurahisisha vitendo hivyo. Shule hizo zipo katika mji wa Mlandizi mkoani humo na vimesababisha wanafunzi hao kuporomoka kimasomo kwa kuwa wanatumia muda mwingi kukaa machimbo ya mchanga na vichakani kwa ajili ya kufanya vitendo hivyo. Katika uchunguzi uliofanywa na NIPASHE imebainika vitendo hivyo hufanywa nyakati za asubuhi wakati vipindi vya masomo vinaendelea na jioni mara wanapotoka shuleni. Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, mahudhurio ya wanafunzi kwenye shule hizo yamekuwa ya kusuasua na kusababisha walimu kuwa na kazi ya ziada ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo. Uchunguzi huo umefanywa katika shule za msingi za Mtongani, Azimio na Jamhuri zote zipo ndani ya mji huo wa Mlandizi. HALI HALISI Katika hali inayoonyesha kuwa ni mbaya kwenye shule hizo, baadhi ya wanafunzi wameonekana kuathirika kisaokolojia na kupungukiwa na uwezo wa kimasomo darasani. Hata hivyo, afya za wanafunzi hao zipo hatarini kutokana na hofu ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwamo Ukimwi baada ya watu wazima kuhusishwa kuwaingilia. Baadhi ya walimu wa shule hizo walipozungumza na gazeti hili walikiri kuwapo kwa vitendo hivyo na kwamba vimeongezeka kwa kasi ya kutisha na kuwapa hofu. Walisema walengwa wa vitendo hivyo ni wanafunzi kuanzia darasa la tatu hadi la nne ambao mara nyingi wanalazimishwa kulawitiwa na wanafunzi wenzao wa madarasa ya juu. Aidha imedaiwa wanafunzi wengine wanafanyiwa vitendo hivyo na watu wazima wakiwa nyumbani kwao na kwenye mabanda ya kuonyesha picha za video nyakati za usiku. "Tatizo hili limekuwa kubwa, walimu tumejitahidi kupambana nalo kwa kiasi kikubwa lakini inaonyesha hatujafanikiwa," alisema Mwalimu Jamila Kipengele wa Shule ya Msingi Mtongani. Mwalimu Kipengele ambaye anaongoza kitengo cha taaluma, alisema vitendo hivyo vinafanyika katika maeneo hayo ambapo huko wanafunzi wanakutana mara wanapofanikiwa kutoroka wakati wa vipindi vya masomo. "Tunavyosikia huko machimbo wanakuwa watoto kutoka shule tofauti na kutendeana matendo hayo machafu, baada ya kugundua jambo hilo tuliamua kufanya msako mkali wa kuwakamata wote wanaohusika na kuwarudisha shuleni," alisema Kipengule. Kwa shule ya Azimio, Mwalimu Emmanuel Mwambeja ambaye anafundisha darasa la tatu, alieleza nusu ya wanafunzi 98 wa darasa lake hawaingii darasani katika vipindi vya jioni na badala yake wanaishia kwenye machimbo. Mwalimu Tetula Kessy wa Shule ya Msingi Azimio, ambaye yupo kwenye kamati ya kuzuia unyanyasaji wa watoto chini ya Plan Tanzania, alisema wanafunzi wengi wanajikuta wakiingia katika vitendo hivyo kutokana na kushawishiwa na watu wazima na kuangalia picha za ngono kwenye mabanda yaliyozunguka kila eneo kwenye shule hizo. "Tunapokaa na kuwauliza kwa nini wanafanya hivyo, wanajibu kwamba walikuwa wakifanyiwa nyumbani au wanaona kwenye vibanda vya video na wao wanajaribu kwa wenzao," alisema Mwalimu Kessy. WATOTO WAPASUA KAPTULA ZAO Katika Shule ya Msingi Jamhuri baadhi wanafunzi wameeleza upo wakati wanafunzi walifikia hatua ya kupasua kaptula zao upande wa nyuma ili kurahisisha kuingiliwa na wenzao. Baadhi ya wanafunzi ambao majina yao yanahifadhiwa, walisema wanafunzi hao walikuwa na kawaida kwenda kwenye korongo lililo jirani na shule hiyo na kisha kulawitiana. "Wanachana kaptula sehemu ya nyuma kwa kutumia wembe, tulikuja kugundua wanaporudi darasani wanakuwa katika hali tofauti ndipo tukaamua kuripoti kwa walimu," alisema mwanafunzi mmoja. Kauli za wanafunzi hao ziliungwa mkono na Mratibu wa Elimu Kata ya Kilangalanga, Thomas Tito, ambaye alisema amefanya juhudi kubwa kupambana nalo wakati alipokuwa Mwalimu Mkuu katika shule hiyo. "Nakumbuka nilipokuwa naongoza shule hiyo niliwakuta wanafunzi wamepasua kaptula zao kwa nyuma na wembe, nilipodadisi niligundua wanafanya mchezo huo hatari kwa sababu wanapotoka huko vichakani wanakuwa wamechafuka sana," alisema. Kufuatia hali hiyo aliamua kuripoti katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua lakini ilishindikana baada ya kuonekana watoto hao walikuwa wakilawitiana wenyewe kwa wenyewe. "Polisi walishindwa kuendelea kufuatilia na kuachia jukumu hilo uongozi wa shule, nilichofanya niliwaita wazazi kuwaeleza jambo hilo pamoja na kuwachukulia hatua ya kinidhmu wahusika," alisema mwalimu Tito. MABANDA YA VIDEO Hata hivyo, taarifa za uhakika zinaeleza kwamba kinachoendelea ndani ya mabanda ya video yaliyotapakaa kila kona ya mji wa Mlandizi, ni mambo ya kutisha. Imeelezwa kwamba ndani ya mabanda hayo, wamiliki wanaweka picha za ngono bila kujali muda wala umri wa wateja wao, kinachotokea wanaume watu wazima wanawachukua watoto waliokuwamo ndani na kuwaingilia kinyume na maumbile. Baadhi ya wanafunzi waliotoa ushuhuda huo (majina yamehifadhiwa) walisema mara picha hizo zinapoonyeshwa, wanaume hao wanawadanganya watoto kwa kuwapa pesa kidogo na kisha wanawapakata na kuwaingilia. "Kule watu wakubwa wanapakata watoto halafu wanawavua nguo kuwafanyia mambo mabaya," alisema mwanafuzi mmoja. Wanafunzi wengine mara baada ya kuangalia picha hizo, wakienda shuleni wanawachukua wanafunzi wenzao na kwenda kuwafanyia jambo hilo. "Tuna mwanafunzi mwezetu hapa shuleni (jina analitaja) amekuwa na tabia ya kuwaingilia wenzake kinyume na maumbile," alisema mmoja wa wanafunzi hao. Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Kipengele alisema kinachozungumzwa na wanafunzi hao ni jambo la kweli, tayari wamembaini mtoto huyo na kumchukulia hatua ikiwamo kuwaita wazazi wake. "Mwanafunzi huyu mahudhurio yake ni mabaya sana, tulipomfuatilia na kumbana sana alikiri kuhusika, na watoto waliofanyiwa vitendo hivyo walijitokeza tunaendelea kuwapatia ushauri nasaha,"alisema Mwalimu Kipengele. Aliomba serikali kuangalia upya utoaji vibali vya kuendesha biashara hiyo, kwani kuna hatari wanafunzi wengi wakaathirika na vitendo hivyo na kuambukizwa Ukimwi pamoja na kushuka kiwango cha elimu kwa ujumla. Hata hivyo wamiliki wa mabanda hayo wanapinga kauli hizo kwa kusema vibali vyao vimewapa masharti ya kutoonyesha picha za aina hiyo, endapo kuna watu wanafanya hivyo basi hawaendeshi biashara zao kihalali. Twaha Linde ambaye alikutwa akionyesha video katika banda lililojengwa jirani na shule ya Msingi Mtongani, alisema kwa upande wake hajawahi kuonyesha picha hizo. Pamoja na utetezi huo, ndani ya banda hilo walikuwapo wanafunzi zaidi ya 10 wa shule tofauti wakifuatilia picha, licha ya muda huo wa saa 6:00 mchana walitakiwa kuwapo darasani. WAZAZI LAWAMANI Walimu wamelaumu wazazi kwa kutokuwa na utaratibu mzuri wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao kila siku. Walisema hata wanapopewa taarifa ya watoto wao kutofika shule au kuhusishwa na tabia hizo wanawakingia kifua na kuwa wakali. "Inakuwa tabu pale tunapowapa taarifa wazazi juu ya tabia za watoto wao, mara nyingi wanakuja wakiwa wakali na kusema tunawaongopea, mara nyingi inabidi kutumia mbinu za kuwahoji mbele yao na wanapobaini kuna ukweli wanabaki wakilia," alisema Mwalimu Tito. Aliomba wazazi kuwa na taratibu ya kuchunguza tabia za watoto wao na kufuatilia maendeleo yao ya kielimu kwa ajili ya kuwajengea maadili mema. "Sisi tunasaidia kurekebisha pale wanapokuja shuleni, lakini wakiwa nyumbani hawana udhibiti na ndiyo maana hali hii inazidi kuongezeka huku wazazi hawana habari," aliongeza kusema. Hata hivyo Zuhura Yusufu (30) mkazi wa Mlandizi, alisema kinachosemwa na walimu wa shule hizo kina ukweli kwani wazazi wengi hawawajibiki ipasavyo katika malezi ya watoto wao. Alisema kuibuka kwa hali hiyo kutawazindua wazazi wenzake kwa kuanza kuwafuatilia watoto mara kwa mara OFISA ELIMU ANENA Ofisa Elimu wa shule za Msingi wa Wilaya ya Kibaha, Winfrida Mbuya, alipozungumza na NIPASHE Jumapili, alisema suala hilo limeenea katika shule nyingi na kuwa la kijamii kutokana na wanaohusika hutoka ndani ya familia. Alisema ofisi yake inaandaa tathmini ya jumla kujua ukubwa wake ili kuandaa mkakati wa ufuatiliaji kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kutoa elimu ya ushauri kwa watoto walioathirika. "Ni vizuri tukashirikiana pamoja kuwatambua watoto walioathirika ili waweze kupewa ushauri na wale waliohusika na unyama huo kuchukuliwa hatua za kisheria," alisema. RC: IMENISHTUA SANA Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwamtumu Mahiza, amesema ameshtushwa na jambo hilo, na kwamba atakahakikisha anakutana haraka na viongozi wenzake kulifuatilia. Alisema yeye kama kiongozi wa juu katika eneo hilo hataweza kuzungumza chochote kabla ya kukutana na wenzake. "Mimi nimeshtuka sana lakini sitaweza kusema kitu kwa sababu bado viongozi wenzangu ngazi ya Wilaya na Halmashauri sijakutana nao, nipe muda nitatoa tamko langu," aliongeza kusema.