Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 19 Desemba 2013

Waziri wa elimu adai yeye si waziri mzigo




Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ameamua kuvunja ukimya na kueleza kuwa yeye si waziri mzigo na wala hashtushwi na jina hilo kwani hawezi kuzuia maamuzi ya watu kumuita hivyo.

Dk. Kawambwa amesema yeye ni mchapakazi na tayari juhudi za kiutendaji katika wizara anayoiongoza zimeanza kuonekana.

Amesema kuwa suala la kuitwa waziri mzigo linatokana na yeye kuwa kioo na dira ya wenzake  katika wizara hiyo na hivyo majina kama hayo hayawezi kukwepeka na wala kuathiri utendaji wake na kujivunia kuwa yeye ni mmoja wa wasimamizi wa upatikanaji bora wa elimu hapa nchini.

 Waziri Kawamba aliamua kuvunja ukimya huo wakati akifungua kikao cha kazi cha maofisa elimu wa mikoa na halmashauri kinachojadili maendeleo ya elimu ya msingi hapa nchini pamoja na kufanya udahili wa pamoja katika matokeo ya darasa la saba.

"Kuna mtikisiko mkubwa katika wizara yetu na mengi yanasemwa wote mnasikia na Watanzania wanafahamu. Tupo katika safari nzito lakini ili gari liondoke, lazima kwanza litikisike, hivyo msiwe na wasiwasi tutafika salama tu," alisema Dk. Kawambwa.

Alisema anashangazwa kuitwa mzigo kwani kutokana na uwajibikaji wake katika wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, wamepata mafanikio makubwa hususani katika kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2013.

 Alisema kutokana na jitihada zake na kushirikiana na watendaji na wadau mbalimbali, kiwango cha ufaulu mwaka 2013 kwa wahitimu wa elimu hiyo ya msingi

kimeongezeka kutoka asilimia 31 mwaka uliopita hadi kufikia asilimia 50.61 mwaka 2013 ambao ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 19.89 ukilinganishwa na mwaka jana.

Waziri Kawambwa alisema jumla ya watahiniwa 844,938 walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi na kati yao 427,606 sawa na asilimia 50.61, wamefaulu kwa zaidi ya alama 100 kati ya 250 matokeo ambayo aliyaita ni mazuri.

Alisema kuwa kati ya watahiniwa hao waliofaulu, wasichana ni 208,227 sawa na asilimia 46.68 na wavulana ni 219,379 sawa na asilimia 55.01kitu ambacho kimeinua kiwango cha ufaulu.

Hata hivyo, alisema ufaulu huo bado haujafikiwa lengo la mpango wa Matokeo Makubwa Sasa la kufikia asilimia 60, lakini kutokana na jitihada na kipindi kifupi tangu mpango huo utangazwe, ni wazi kuwa kazi imefanyika na kustahili kupongezwa.

Jumatano, 18 Desemba 2013

Serikali yagomea CWT kuhusu kima cha chini cha mishahara


 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.Shukuru Kawambwa


Serikali  imesema haiwezi kuongeza vianzio vya mishahara kwa asilimia 53 kama Chama cha Walimu Nchini (CWT) kinavyotaka kwa kuwa fedha hizo ni zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Bungeni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso (Chadema).

Pareso alitaka kujua ni lini serikali italipa malimbikizo ya walimu yakiwamo yanayotokana na kupandishwa madaraja.

Pia alihoji serikali inapata kigugumizi gani kulipa nyongeza ya asilimia 50 ya mishahara kwa kadiri walivyokubaliana na CWT.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kufahamu mpaka sasa serikali imeshughulikiaje madai ya stahili za walimu hapa nchini.

Akijibu maswali hayo,  Dk. Kawambwa alisema serikali imejipanga kuondokana na madeni ya walimu.

Alisema zoezi linaloendelea hivi sasa ni uhakiki wa madeni ya serikali kwa ushiriki kikamilifu na CWT.

Hata hivyo, alisema madai ambayo CWT yaliyotaka nyongeza ya asilimia 53 kwa vianzia vya mishahara yanazidi bajeti ya mishahara yote ya watumishi wa serikali nchin.Kwa msingi huo alisema hakukuwa na namna ambayo serikali ingelipa.

Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikiongeza mishahara kwa walimu ambapo mpaka sasa imeshaongeza asilimia 30.9.

Aidha, alisema serikali na CWT wanaendelea na majadiliano kuhusiana na madai hayo ya walimu na tayari vikao vinane vimefanyika.

“Katika vikao hivyo, serikali iliahidi kutoa nyongeza ya wastani wa asilimia 14.62 ya vianzia vya mishahara ya walimu wakati CWT walishuka kutoka asilimia 100 hadi asilimia 53 ya nyongeza waliyokuwa wanadai,” alisema.

Chanzo Ippmedia.com

Alhamisi, 12 Desemba 2013

Wananchi wadai uwajibikaji mkubwa wa wabunge Wananchi wengi Tanzania Bara waunga mkono madai hayo na vifungu vingine muhimu katika rasimu ya katiba






Tarehe 4 Desemba 2013, Dar es Salaam: Zaidi ya theluthi moja (36%) ya Watanzania Bara wameshiriki
katika marekebisho ya katiba kupitia mikutano ya jamii, SMS, mahojiano, barua na barua pepe. Idadi
kubwa walishiriki kupitia mikutano ya jamii iliyoandaliwa na Tume ya Kurekebisha Katiba (CRC). Pia,
karibu nusu ya Watanzania Bara wanaweza kuelezea Katiba ni nini.
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza katika utafiti uitwao: Kurasimu Sheria Mama ya Nchi: Tafakari ya
Wananchi wa Tanzania Bara kuhusu Rasimu ya Katiba. Msingi wa utafiti huu mfupi ni taarifa kutoka
Sauti za Wananchi, utafiti wenye uwakilishi kitaifa, uliotumia simu ya mkononi, ngazi ya kaya katika
Tanzania Bara.
Taarifa zinaonyesha viwango vya juu vya ufahamu wa Katiba na ushiriki katika mchakato wa mapitio. Pia,
karibu watu saba kati ya kumi (67%) ya Watanzania Bara wanafahamu kuwa rasimu ya Katiba
ilizinduliwa, ingawa chini ya robo (23%) walijua jinsi ya kupata nakala ya Rasimu ya Katiba.
Moja ya maeneo makuu ya mjadala ni hali Muungano kati ya Bara na Zanzibar. Juu ya mada hii, utafiti
umegundua kuwa maoni yamegawanyika, nusu (51%) wakikubali na nusu (48%) wakikataa kuanzishwa
kwa Serikali tatu. Hata hivyo, walipoulizwa zaidi, idadi ya waliounga mkono Serikali tatu kwa Watanzania
wa Bara, ililingana na waliounga mkono Serikali moja, wote ni 19%. Sauti za Wananchi pia iliweza
kulinganisha matokeo haya na ya utafiti uliofanywa na Afrobarometer katika nchi nzima (pamoja na
Zanzibar) mwaka 2012. Mwaka 2012 karibu nusu (47%) ya Watanzania Bara walikataa mabadiliko yo
yote katika masuala ya Muungano, hata hivyo katika mwezi wa Julai mwaka 2013, robo (26%) ya
Watanzania Bara walikataa mabadiliko. Kinyume chake, moja kati ya kumi (8%) waliunga mkono
kuongezeka kwa uhuru wa Zanzibar mwaka 2012 wakati theluthi mmoja ya watu waliunga mkono jambo
hili mwaka 2013. Utafiti wa Sauti za Wananchi unafanyika Tanzania Bara tu, kwa hiyo uchambuzi huu
hauhusishi tawimu toka Zanzibar.
Kumekuwa na vifungu kadhaa katika rasimu ya katiba ambavyo vimekuwa vikijadiliwa kwa mapana
katika vyombo vya habari. Wananchi kwa kiasi kikubwa walikubaliana na rasimu katika yote haya. Karibu
wote (91%) ya Watanzania Bara wanataka kuwa na uwezo wa kumwondoa Mbunge wao kwa kushindwa
utendaji, hiki ni kielelezo cha wazi cha kutaka uwajibikaji; na ni hali iliyofanya kifungu hiki kupendwa
zaidi katika rasimu. Maeneo mengine ndani ya rasimu yaliyopata uungwaji mkono mkubwa toka kwa
wananchi ni:
Mgombea urais lazima awe na umri zaidi ya miaka 40 (84% wanakubaliana)
Mawaziri na Manaibu wao wachaguliwe na Rais na kupitishwa na Bunge (77% wanakubaliana)
Bunge lazima liundwe na wajumbe 75, wawili kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara, wawili kila
mkoa wa Zanzibari (76% wanakubaliana)
Spika na Naibu Spika, wanapaswa wasiwe viongozi wa vyama vya siasa kwa miaka mitano kabla
ya kugombea nafasi hii (72% wanakubaliana)
Mawaziri na Manaibu wao wanapaswa wasiwe madiwani, wabunge au wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi (70% wanakubaliana)
Wabunge wanapaswa kuwa katika ofisi kwa miaka isiyozidi 15 (70% wanakubaliana)
Wagombea huru waweze kuwania nafasi ya Urais na Ubunge (67% wanakubaliana)
Kuwe na tume Huru ya Uchaguzi, iliyoteuliwa na Rais (65% wanakubaliana)
Sauti za Wananchi pia iliwauliza Watanzania Bara kama waliunga mkono rasimu ya katiba. Pamoja na
kuwepo makubaliano ya jumla katika masuala muhimu, wengi wao wangepigia kura rasimu ya sasa.
Pamoja na hayo, theluthi mbili (65%) wanaamini kwamba Uchaguzi Mkuu ujao utafanywa kwa kutumia
Katiba mpya.
Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alisema “Kimsingi, katiba inapaswa kuandikwa kutokana na maoni
na amali za wananchi. Utafiti wa Sauti za Wananchi ni moja ya nyenzo muhimu inayotumika kupata
maoni ya wananchi kwa njia madhubuti na ya kisayansi. Ni matumaini yetu wale waliopewa jukumu la
kuandaa rasimu ya katiba watayasikiliza kwa makini.”
---- Mwisho ----
Kwa maelezo zaidi:
Risha Chande
Meneja Mawasiliano, Twaweza
e: rchande@twaweza.org | t: (255) (0) 656 657 559
Maelezo kwa Wahariri
Taarifa hii na data zilizomo zinaweza kupatikana www.twaweza.org, au www.twaweza.org/sauti
Twaweza ni jitihada ya miaka kumi zinazowalenga wananchi juu ya mabadiliko mapana katika
Afrika Mashariki. Twaweza anaamini kwamba mabadiliko ya kudumu yanahitaji kuanzia ngazi za
chini kwenda juu, na inataka kujenga mazingira na kupanua fursa za njia ambazo mamilioni ya
watu wanaweza kupata taarifa na kufanya mabadiliko kutokea katika jamii zao moja kwa moja
na kwa kuiwajibisha Serikali.
Unaweza kufuatilia kazi za Twaweza kupitia:
Mtandao: www.twaweza.org Facebook: Twaweza Tanzania Twitter: @Twaweza_NiSisi

Jumatatu, 9 Desemba 2013

wahitimu mzumbe wahimizwa kutumia elimu walioipata tulitumikia taifa vema

Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro, wamehimizwa kutumia maarifa, elimu na stadi walizozipata chuoni hapo kuwa kichocheo cha maendeleo katika jamii inayowazunguka na ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa, amesema kwa kuhitimu kwao, kunawaweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutumikia taifa lao na jamii inayowazunguka.

Aliyasema hayo wakati wa mahafali ya 12 ya chuo hicho mjini hapa mwishoni mwa wiki.

Profesa Kuzilwa alisema wasomi hao sasa ni rasilimali watu inayotegemewa kuleta maendeleo ya nchi, hivyo akawaomba wakawe mfano bora kwa jamii inayowazunguka na kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanatimiza wajibu kwa taifa lao.

Jumla ya wahitimu 1,803 walitunukiwa vyeti mbalimbali, kati yao asilimia 46 ni wanawake na 54 wanaume.

Wahitimu 215 walitunukiwa astashahada, 1,153 Shahada ya Kwanza, 433 shahada ya uzamili na wawili shahada ya uzamivu.

Jumla ya wahitimu katika kampasi kuu ya Morogoro, Dar es Salaam na Mbeya ni 3,554, ukilinganisha na wahitimu 3,049 mwaka 2011/12, sawa na ongezeko la wahitimu 504 walihitimu katika mahafali hayo.

Alisema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 16 ambapo wahitimu 24 wamepata daraja la kwanza ikilinganishwa na 17 mahafali yaliyopita.

Pia alisema kutokana upungufu wa wanasayansi nchini, chuo kimeandaa program za shahada ya sayansi asili na tumizi kukabili hali hiyo na kuunga mkono Mpango wa Elimu ya Juu 2010-2020 wa vyuo vikuu kuongeza fursa za sayansi.

Mikakati ya kuanzisha program hizo inafanywa kwa  kushirikiana na vyuo vingine vikuu nchini na nje kama ilivyoainishwa katika mkakati wa tatu wa chuo wa 2012/13-2016/17 wa kuwa na mtizamo anuwai katika program zake.

Pia Chuo kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya Korea kinatarajia kuanzisha kijiji cha sayansi ambapo program mbalimbali zikiwamo za kompyuta zitaanzishwa chini ya kitivo cha sayansi na teknolojia.

Alisema pamoja na mafanikio na mipango iliyopo, Chuo kinakabiliwa na ufinyu wa bajeti ambayo haikidhi mahitaji halisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Daniel Mkude, alisema mhitimu kumaliza masomo siyo mwisho wa kujifunza, bali wazidi kujenga tabia ya kujisomea na kuchota maarifa.

“Taifa linawahitaji...mzidi kujisomea na kuendelea na hatua nyingine ya masomo,” alisema.

Alishauri wahitimu hao kujiepusha na tabia zisizofaa kwa vile taifa linapoteza rasilimali watu kutokana na baadhi hujiingiza katika matendo ya ulevi na kupoteza maisha wakiwa na umri mdogo.

Pia alisema wahitimu hao wanatakiwa kuwa mfano kwa jamii kwa kupiga vita ufisadi, wizi, mauaji ya vikongwe, imani za kishirikina, ukahaba, ubakaji, mauaji ya albino na utupaji wa watoto.

Mahafali ya Chuo Kikuu Mzumbe, pia yalihudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mkewe, Tunu ambao walishiriki kama wazazi na kushuhudia mmoja wa watoto wao akipata shahada yake.
 
Chanzo.  Ippmedia.com

Jumatano, 4 Desemba 2013

Asakwa kwa kutorosha,kubaka mwanafunzi

Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili na unyayasaji wa kijinsia, mtoto mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) mkazi kijiji cha Chinangali mpakani mwa Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma, amebakwa na kulawitiwa kwa muda wa wiki mbili.

Akizungumza jana na NIPASHE, Mhudumu wa Shirika la lisilo la Kiserikali linalopinga ukatili wa kijinsia na watoto (Afnet) kwa kushirikiana na Tunajali, Mnemelwa Simba, alisema tukio hilo lilitokea katika kijiji hicho hivi karibuni.

Simba alisema wazazi wa mtoto huyo walifika kwa mhudumu huyo kuomba ushauri baada ya kuona mtuhumiwa wa ukatili huo akiwa hajachukuliwa hatua stahiki za kisheria na vyombo husika.

Alisema mtoto huyo, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari iliyopo Kibaigwa, amelazimika kusitisha masomo ili kupata matibabu kutokana na kufanyiwa ukatili huo.

Alisema mtoto huyo alifungiwa ndani ya nyumba kwa muda huo na mtuhumiwa aliyetambulika kwa jina la Hassan, ambaye ni mgeni katika kijiji hicho anayefanya vibarua vya ujenzi.

 “Mimi namjua huyu. Anatambulika kwa jina la Hassan. Na ni mgeni. Hata mwaka hajamaliza. Na mpaka sasa yupo, ni mtu na akili zake, aliyefanya kitendo hiki,” alisema Simba.

 Alisema wazazi wa mtoto huyo baada ya kumtafuta kwa muda mrefu, walitoa taarifa kwa ulinzi shirikishi ili kumtafuta.Simba alisema baadaye iligundulika kijana huyo akiwa na binti huyo, alimuhamishia katika Kijiji cha Ndurugumi.Alisema walipofika katika kijiji hicho walisikia amehama naye tena.

 Simba alisema mtoto huyo alikutwa katika Kijiji cha Ngomai kwa kaka yake na Hassan. Alisema Hassan alidai kuwa mtoto huyo alipelekwa na mdogo wake.

 Mama mzazi wa mtoto huyo, Suzan Fugusa, alisema ilikuwa siku ya Jumapili mtoto wake alimuaga anaenda kanisani kama ilivyo kawaida.
Alisema baada ya kuona muda umepita na mtoto huyo hajarudi kutoka kanisani walianza kumtafuta.

Fugusa alisema baada ya siku kadhaa kupita, walikwenda kutoa taarifa kwa ulinzi shirikishi na kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa.

“Baada ya kumtafuta katika hivi vijiji na kufanikiwa kumpata mkuu wa mtaa alisema suala hilo ni kubwa na kutuambia twende polisi ambako tulihojiwa na mtuhumiwa alikubali kuwa alimtorosha mtoto huyo,” alisema Fugusa.Alisema polisi waliwataka kwenda hospitali kufanyiwa vipimo.

Fugusa alisema walimpeleka, lakini kulingana na woga wa mtoto huyo, alishindwa kueleza ukweli kuhusu vitendo alivyokuwa akifanyiwa.

 “Baada ya kumpima ukimwi na mimba tukarudi nyumbani. Na mara baada ya kurudi akiwa na bibi yake, alienda kujisaidia.
Ndipo haja zote zikawa zinatoka kwa pamoja. Tukarudi hospitali tena. Tulipoona mambo tofauti, alipimwa akagundulika kweli aliingiliwa kinyume cha maumbile na kuanza matibabu ambayo anaendelea mpaka sasa,” alisema Suzan na kuongeza:

 “Tumetumia gharama nyingi kumtafuta mtoto wetu mpaka kumfuata. Na hii kesi ilishafika mahakamani isipokuwa hukumu imetolewa haraka kabla hatujapeleka ripoti ya pili ya daktari iliyogundua ameingiliwa na mtuhumiwa yupo nje hata hatuelewi tuanzie wapi. ”

Kwa upande wake, mtoto huyo alisema siku ya tukio alikuwa akitoka kanisani na kukutana na kijana huyo, ambaye alimwambia waende nyumbani.
Alisema baada ya kufika nyumbani kwa Hassan, alimzuia kurudi  nyumbani kwao na kumfungia ndani na kuanza kumuingilia kinyume cha maumbile kila kijiji walichokuwa wakienda.

“Kwa sasa naendelea na matibabu. Nimesitisha masomo mpaka nitakapopona. Maana niliumizwa. Bado nasikia maumivu makali,” alisema mtoto huyo.

Akizungumza kwa njia ya simu na NIPASHE,  Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibaigwa, Inspekta Beda Msoma, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
 Msoma alisema jalada lilifunguliwa kituoni hapo kwa hati ya mashitaka ya kubaka KBG/247/2013.

Alisema kesi hiyo ilikuwa na ushahidi wa kutosha na haelewi kwa nini mtuhumiwa ameachiwa huru, hivyo ataifuatilia kwa mpelelezi wake kuona kwa nini iliamuliwa hivyo.
“Hii kesi naijua ilivyokuja kuripotiwa. Nilifanya jitihada zote. Nikafanikiwa kuifikisha mahakamani ikiwa na ushahidi wa kutosha. Sasa nashangaa kusikia eti yupo huru.

Iliamuliwa vipi wakati ilikuwa na vithibitisho… Huyu binti nilimpeleka akafanyiwa councelling (ushauri) kwa madaktari wakishirikiana na ustawi wa jamii,” alisema Inspekta Msoma.

Alisema mtoto huyo alipimwa na kugundulika kuwa alibakwa.

Msoma alisema baada ya siku mbili, bibi ya mtoto huyo alirudi polisi na kudai kuwa ameona hali tofauti ndipo akapimwa tena na kubainika aliingiliwa pia kinyume cha maumbile.
CHANZO: NIPASHE

Jumatatu, 2 Desemba 2013

picha 5 zinazoonyesha choo tegemezi cha shule ya msingi Kiara na Nyang'omboli

choo cha shule ya msingi Nyang'omboli na Kiara
korido ya choo ilivyo
mashimo ya choo hicho hayana mifuniko
mashimo ya choo yakiwa wazi



choo kinavyoonekana


Jumapili, 1 Desemba 2013

Serikali kusaidia mikakati ya taasisi zinazosaidia elimu

Naibu Katibu Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zuberi  Samatama, amesema serikali itasaidia mikakati inayoibuliwa na taasisi mbalimbali za kiserikali katika kuboresha elimu ya msingi nchini.
 
Samatama alisema hayo, wakati akizindua kampeni ya uboreshaji wa elimu ya msingi Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam, inayofahamika kama Mnazi mkinda.
 
Alisema kampeni hiyo ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha wanafunzi wanakuzwa vipaji walivyozaliwa navyo, ni jambo la kuigwa kwani itawafanya watoto kuhudhuria masomo kwa muda wote.
 
Alisema serikali itahakikisha inaanzisha tuzo maalum kwa walimu wabunifu kwa ajili ya kuwapa moyo na kuwatambua.
 
"Kitu hiki mlichokibuni kitasaidia sana katika kuhakikisha wanafunzi wanapenda kusoma kwa sababu watatambua kile wanachokipenda kipo kwenye shule zao," alisema Samatama.
 
Alisema katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), umesababisha ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba kutoka kiwango cha asilimia 5.6 hadi silimia 75, mwaka jana.
 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Mwenda Hasara Maganga, alisema kampeni ya Mnazi mkinda, itawavutia watoto kwa kupenda shule na kuacha tabia ya ukwepaji.
"Kwa ujumla tatizo la machimbo halitakuwepo kwa sababu kila mtoto atapata kile anachopenda," alisema.
 
Baadhi ya vipaji vitakavyokuzwa katika kampeni hiyo ni pamoja na Hisabati, Sayansi, Teknohama, Dini na Sanaa ya maigizo, ngoma, muziki na sarakasi.
 
Afisa Elimu ya Msingi wa Manispaa hiyo, Elizabeth Thomas, alisema kampeni ya Mnazi mkinda imesambazwa kwenye shule zote pamoja na kuandaa kituo maalumu cha ukuzaji vipaji katika shule ya msingi Mnazimmoja.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

halmashauri Mbozi yashindwa kulipa pesa ilizowakopa walimu sh.milioni 200


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia
 
Chama cha walimu wilaya ya Momba na Mbozi, kimemuomba Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuwasaidia walimu kulipwa fedha zao zaidi ya Sh. milioni 200 walizokopwa na halmashauri ya wilaya ya Mbozi.
 
Fedha hizo zilikopwa kwa walimu mapema mwaka huu, zilikuwa michango ya walimu waliyokuwa wakikatwa kutoka kwenye mishahara yao kwa ajili ya kuweka akiba kwenye Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS).
 
Akiwasilisha malalamiko hayo kwa niaba ya walimu wote,  alisema walimu hao waliambiwa na halmashauri kuwa fedha hizo zimetumika kwa ajili ya shunguli zilizo nje ya shughuli za walimu.
 
Awali walimu hao wilaya ya Mbozi na Momba walikuwa wilaya moja kabla ya kugawanywa na kuwa mbili. Walipotaka kufahamu kuhusu fedha hizo waliambiwa zimetumika kuandaa sherehe za wafanyakazi (Mei Mosi) ambazo mgeni rasmi alikuwa Rais Jakaya Kikwete.
 
Wakionyesha kukata tamaa na madai ya malimbikizo ya madeni wanayoidai serikali zaidi ya shilingi bilioni moja kwa wilaya hiyo, pia walizidi kuvunjika moyo baada ya kutaka kuwasilisha kilio chao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia, na kukataa kuwasikiliza kwa madai kuwa serikali imeshamaliza matatizo yao.
 
Katika taarifa iliyosomwa na Nyanguye ilisema kuwa, Ghasia alimkataza Katibu wa Chama Cha Walimu, Emilia Mwakyoma aliyekuwa akisoma taarifa kwa kumtaka akae chini mara moja kwani hawezi kusikiliza madai ambayo yameshamalizwa.
 
Alisema hali hiyo ilisababisha walimu kushindwa kuwasilisha malalamiko yao siku hiyo, na hivyo kulazimika kuyawasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM, Kinana ili kuomba msaada kama wanaweza kusaidiwa.
 
“Tumekuja tu kujaribu kama tunaweza kusaidiwa kwani walimu tumeshasahaulika sana. Licha ya kusahaulika pia tunanyang’anywa haki zetu za msingi na Serikali na hatujui kama tutazipata na wala hatuoni wakumlalamikia tena zaidi ya kuishi kwa matumaini," alisema Nyanguye.
 
Akijibu malalamiko yao kwa mshangao, Katibu Mkuu CCM, Kinana alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Charles Mkombachepa kueleza matumizi ya fedha hizo za walimu, ambazo zinadaiwa kutumika kuandaa sherehe bila ya wakopwaji kutaarifiwa chochote.
 
“Unachotakiwa Mkurugenzi ni kuwaeleza walimu fedha zao umezitumia kufanyia nini, angalia bado wakiwa wana machungu ya madeni wanayoidai serikali, hivi serikali inatakiwa kukopa au kukopwa na tangia lini Mei Mosi zikaandaliwa na walimu? " alihoji Kinana.
 
Akijibu tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Mkombachepa, alikiri kutumia fedha hizo lakini kwa ajili ya kulipia huduma zilizotolewa na taasisi mbalimbali wilayani hapo.
 
"Katibu Mkuu, kweli fedha hizo zilitumika, lakini si kwa ajili ya Mei Mosi bali zilitumika kuandaa usafiri, kurekebisha magari na shughuli nyingine ambazo hazihusiani na walimu moja kwa moja," alisema Mkombachepa.
 
Mkombachepa, aliomba kuzilipa fedha hizo ndani ya miezi miwili kuanzia Desemba na kumaliza mwezi Januari mwakani, taarifa ambayo ilizidi kumkasirisha Kinana.
 
Kwa fedheha kubwa Kinana, alimtaka Mkurugenzi huyo kuacha kuwafanyia walimu usanii kwenye fedha zao ambazo wamezipata kwa taabu na kuagiza walimu hao kulipwa fedha zao haraka iwezekanavyo.
 
Aidha Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Asha Rose Migiro, aliahidi kuyashughulikia matatizo ya walimu kwa kufikisha taarifa za matatizo yao, ikiwamo malimbikizo  ya madeni wanayoidai serikali kwa viongozi wanaohusika.