Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 6 Februari 2014

serikali inachangia kuua elimu nchini

SERIKALI imekuwa kama haioni maovu yanayofanywa kienyeji na watendaji wake  ndani ya sekta ya elimu.
Na kama inaona basi inaamua kufumbia macho.
Novemba 7, 2012, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Majaliwa Kassim, alisema bungeni kuwa ni kosa walimu wakuu kutoza fedha kwa watoto wanaoanza darasa la kwanza, lakini tozo limekithiri.
Majaliwa alionya mwalimu atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria, agizo ambalo serikali yenyewe kupitia watendaji  linaonekana kupigwa mweleka, huku wazazi wakishangaa kuwapo michango isiyoeleweka na mingine ilikubalika kupitia kamati za shule.
Imefika mahali sasa inaonekana wazazi wanafahamu sana umuhimu wa watoto wao kusoma ili baadaye walikwamue taifa  na familia zao, lakini watendaji wa elimu husika wamekuwa mzigo na kikwazo cha watoto hao kupata elimu.
Hivi karibuni mkoani Morogoro, wazazi walifikia kupigana wakigombea watoto waandikishwe ili wasome, lakini mbali ya ugomvi huo, lalamiko na kikwazo kilichotajwa, ni tatizo la tozo na michango kwa wanaoandikisha kufikia sh 50,000 kwa mtoto.
Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, katika uandikishaji huo, aliingia katika suluba kutoa ufafanuzi ili kuondoa utata baina ya wazazi na waandikishaji, ambapo malipo  ya sh 50,000 kwa mtoto anayeandikishwa, kunaashiria wakuu wa shule kuwa na mradi wa kutumbua fedha kupitia uandikishaji.
Kwa kuwa Kassim alishatolea ufafanuzi, Mwalimu Mkuu au yeyote anayekiuka agizo la michango kuwa atachukuliwa hatua kali, basi kwa hali ilipofikia hadi wazazi wanapigana na wengi wao kukosa kuandikisha watoto wakitumia tozo feki, waadhibiwe.
Ninasema hivyo kwa sababu walimu wakuu wakisaidiana na watendaji wa vijiji na kata, wanaamua kufanya lolote kuhusu elimu bila kupata hata ushauri.
Siku hizi imekuwa si ajabu, walimu wakuu na waratibu wa elimu wakikosa mapato, basi wakilala na kuamka utakuta wanapanga mipango ya kuhakikisha wanapata fedha, mojawapo ikiwa ni kutumia uandikishaji wa wanafunzi kama mradi wa kujipatia fedha.
Bila kufahamu uwezo na kipato cha wananchi wa hali ya chini, wamekuwa wakiwakandamiza na kuwanyanyasa wananchi, na wakati mwingine wanafikia kuwaweka ndani eti kwa sababu ya kushindwa kulipa michango hiyo.
Hapa ndipo ninaposema, aibu ya elimu Tanzania tujifiche wapi? Maana udhaifu wa sekta hii na mipango yake mibovu, haionyeshi mpango mkakati wowote unaowekwa ili kuwe na uwazi wa kuandikisha wanafunzi.
Ni mara nyingi tumeona walimu wakuu na waratibu wa elimu, wamekuwa tatizo kwenye elimu ndani ya vitongoji, vijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa na taifa, ambapo watendaji wamekuwa wakiamua mambo wanavyotaka bila kuwa na vigezo huku wazazi wakiteseka.
Tatizo jingine linalosababisha malumbano sekta ya elimu, ni Kamati za shule ambazo zimekuwa mizigo zikishirikiana na wakuu wa shule, kiasi kwamba wanakaa kupanga mambo wakiangalia uwezo na mishahara waliyonayo bila kutazama kipato cha wananchi.
Ifike mahali hawa nao wasifumbiwe macho maana badala ya kuwa kioo ndani ya elimu, wamekuwa giza kwenye elimu hiyo.
Hawana mbinu na mikakati ya kuwasaidia wazazi wamudu kusomesha watoto, ila mikakati ya tozo lao

chanzo tanzania daima

matatizo yanayomkumba mtoto wa kike kupata elimu bora

Kama kuna mikakati iliyobuniwa kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu nchini, ni pamoja na ujenzi wa shule za sekondari za kata.
Pamoja na udhaifu wa shule hizo kama unavyojulikana kwa watu wengi, angalau sasa watoto wengi wa kike wanapata fursa ya kukaa shuleni kwa miaka minne badala ya kuozwa na kuwa mama katika umri mdogo na kuwa mwisho wa elimu yao.
Hata hivyo, mkakati huu pekee haujawa mwarobaini wa changamoto zinazowakabili watoto wa kike katika safari yao ya kuelekea kupata elimu. Bado kuna tatizo kubwa la umasikini uliokithiri na unaokuzwa zaidi na janga la Ukimwi katika jamii ya Kitanzania kiasi kwamba baadhi ya wasichana wanaoingia shule za sekondari hawaendelei muda mrefu.
Hawa wanalazimika kuacha shule ama mwanzoni au katikati kwa kukosa ada ama mahitaji mengine ya shule. Watoto wengi ni yatima na katika maeneo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa na tatizo la Ukimwi hata ndugu na jamaa wamelemewa na mzigo.
Tatizo hili nimeliona Mkoa wa Iringa na sehemu nyingine nchini. Kama utafiti ungefanyika kujua ukubwa wa tatizo hili ingekuwa ni jambo jema. Kwa hiyo, Serikali haina budi kubuni mikakati ya kuwapa fursa wasichana wa kutoka familia maskini na mayatima kumaliza elimu ya sekondari na vyuo vikuu.
Huko nyuma kumekuwepo mifuko ya misaada kama ule wa Shirika la Kimataifa la Misaada la Sweden (SIDA) na mingine, lakini kuna baadhi ya viongozi serikalini walipenyeza watoto wao na waliostahili wakakosa fursa hiyo. Hii ni tofauti na enzi za Mwalimu Julius Nyerere sisi tuliotoka familia maskini tuliweza kusoma hadi chuo kikuu bila matatizo. Cha msingi ni kuwa na sera nzuri inayoelekeza namna ya kuwapa fursa wasichana.
Umbali mrefu
Shule nyingi vijijini ziko mbali na makazi ya watu, hivyo wasichana wanalazimika kutembea masafa marefu kwenda na kurudi shuleni. Umbali huu una athari na hatari zake kwa watoto wa kike. Kwa mfano, wengi huchoka na mwishowe inawaathiri kimasomo.
Vilevile, katika safari hizo ndefu wasichana wengine huchokozwa na wahuni au hata kubakwa. Baadhi ya wazazi na walezi wamepangishia vyumba watoto wao karibu na shule. Suluhu hii imesababisha wasichana kuwekwa kinyumba na wanaume wakware na wasichana wengi wamepata ujauzito.
Tatizo hili la umbali pia huathiri hata walimu wa kike wanaopangwa kufundisha shule zilizo mbali vijijini ambako huduma za jamii kwa mfano usafiri, maji, umeme, nyumba na nyinginezo muhimu ni shida. Vilevile, walimu wa kike wanafanyiwa vitendo vya kihuni ama na walimu wenzao au hata wanajamii wengine vikiwamo vitendo vya kishirikina.
Mila za jamii ya wafugaji
Ingawa wilaya nyingi wasichana wako shuleni (msingi na sekondari) na hasa ukiangalia takwimu kitaifa, lakini wasichana kutoka jamii za wafugaji wengi wako majumbani kutokana na mila na desturi zao. Katika maeneo haya kuna shule chache na watoto hutembea masafa marefu kwenda shule na kurudi nyumbani.
Makabila haya ingawa yana utajiri wa mifugo, lakini ni wagumu kuiuza ili wasomeshe watoto wao hususan wa kike. Kwa sababu hii serikali inahitaji kubuni mkakati maalumu kutatua tatizo la usawa ili watoto wote wa kike kutoka makabila yote wapate elimu.
Katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini, ipo sera maarufu Kiingereza kwa jina la ‘Re-entry’.
Sera hii huruhusu wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni kuruhusiwa kuendelea na masomo hadi wanapojifungua na vilevile kuwaruhusu kurudi na kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Sera hii imejadiliwa na kupeleka pendekezo Wizara ya Elimu kwa muda mrefu, lakini haijulikani ni lini itapitishwa na kuwa sera au sehemu ya sheria ya elimu. Wasichana wengi kutoka familia maskini hupata ujauzito na kuacha elimu rasmi baada ya ujauzito.
Wale wanaotoka katika familia tajiri baada ya kujifungua hupelekwa shule binafsi na kuendelea na masomo. Hata hivyo, suala la ujauzito kwa wasichana ni kwa sababu tu ya maumbile yao.
Kama wavulana nao wangeumbwa kuweza kubeba mimba sielewi nani angebaki huko shuleni!
Viongozi wengi ngazi za kufanya uamuzi ni wanaume, hivyo hawaoni kwamba suala hili linahitaji lifanyiwe uamuzi upesi ili kuwanusuru wasichana wengi wanaoathirika badala ya kuwaona au kuwaita ni malaya.
Nipendekeze kwamba, kama suala hili la kuwa na mifuko ya elimu kwa ajili ya wasichana katika ngazi mbalimbali za masomo hususan shule za msingi na sekondari linakuwa zito kitaifa, litolewe mwongozo au sera ili litengewe fedha katika ngazi ya Halmashauri.
Ellen Binagi ni mdau na mwanaharakati wa masuala ya elimu.
Amewahi kufanya kazi katika mashirika na asasi mbalimbli zinazohusiana na elimu.

makala kusoma kuhesabu tatizo kubwa kwa wanafunzi nchini

Tangu mwaka 2010, taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza kupitia mradi wake wa Uwezo, imekuwa ikifanya tafiti katika nchi za Afrika Mashariki zinazolenga kubaini uwezo wa watoto wa shule za msingi katika stadi za kusoma na kuhesabu.
Majaribio haya, yamekuwa yakihusisha masomo ya Hesabu na lugha za Kiswahili na Kiingereza kwa ngazi ya darasa la pili. Sampuli hujumuisha wanafunzi wa darasa la tatu na darasa la saba.
Sampuli ya washiriki
Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2010 watoto walioshirikishwa kwenye utafii huo walikuwa 37,683 mwaka 2011 wanafunzi 114,761 na mwaka 2012 wanafunzi walioshiriki ni 104,568.
Kwa upande wa kaya, mwaka 2010 zilishiriki kaya 18,952 mwaka 2011 zilikuwa kaya 59,992 na mwaka 2012 kaya. 55,191. Kwa wilaya, mwaka 2010 zilishiriki Wilaya 38, mwaka 2011 zilikuwa wilaya 119 na mwaka 2012 wilaya 126.
Shule zilizoshiriki kwenye utafiti uliofanyika mwaka 2010 zilikuwa ni 1,010 mwaka 2011 zilikuwa 3,709 na mwaka jana zikawa 3,624.
Mratibu wa Uwezo upande wa Tanzania, Zaida Mgalla anasema aghlabu majaribio hayo hutayarishwa kwa pamoja na wataalamu wa masomo kutoka vyuo vikuu, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na walimu wa masomo husika wa darasa la pili.
Matokeo 2010
Utafiti huu ulipofanywa mwaka 2010 ulionyesha kuwa, japo Kiswahili ni lugha inayozungumzwa kwa upana zaidi nchini, idadi kubwa ya watoto hawawezi kusoma kupitia lugha hiyo.
“Kwenye sampuli zetu, chini ya nusu (42.2 asilimia) ya watoto waliofanyiwa uchunguzi waliweza kusoma kwa hatua ya hadithi. Wakati watoto wote katika darasa la tatu wanapaswa kuweza kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, watoto chini ya mmoja kati ya watatu (32.7 asilimia) ndio wanaweza.
‘’Hata hivyo, hadi wanamaliza shule ya msingi, mtoto mmoja kati ya 5 hawezi kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, licha ya kumaliza miaka saba ya elimu ya msingi,”inasema sehemu ya utafiti huo.
Kwa upande wa Kiingereza, ripoti hiyo ya mwaka 2010 inaonyesha kuwa chini ya mwanafunzi mmoja kati ya 10 (7.7 asilimia) ndio anayeweza kusoma hadhithi ya Kiingereza ya ngazi ya darasa la pili

Wizara sita kufanyiwa tathmini `Matokeo Makubwa Sasa`

Mfumo  wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unatarajia kufanya tathmini katika wizara sita ili kuona ni kwa kiasi gani umefanya kazi na ripoti itakabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na kuwekwa kwenye mitandao.

Mtendaji Mkuu wa mfumo huo chini ya Ofisi ya Rais, Omari Issa, alisema tathmini ya mwaka mmoja itafanyika na taarifa kuwekwa wazi ili kila wizara ijipime na kuona kama imefikia malengo husika.

Alisema pia Februari 24, mwaka huu kutakuwa na mkutano na wafanyabiashara lengo likiwa ni kuwapa uwanja wa kueleza vikwazo vya kufanya biashara vilivyopo nchini kwa sasa ambavyo vinalalamikiwa.

Alisema chini ya mfumo huo ambao unmelenga kutatua matatizo yanayokwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo wengi wamesingizia kukosekana kwa fedha jambo ambalo alisema siyo kweli.

“Katika tathmini hiyo watabainisha matatizo ya wizara hadi wizara, mradi hadi mradi, uchambuzi wa kina utaonyesha nani apewe kiasi gani kwa ajili ya kutekeleza lipi…awali wizara ilikuwa inapewa kulingana na bajeti hata kama hawazitumii kwa wakati huo, lakini kwa sasa watapewa kulingana na utekelezaji,” alisema Issa.

Alisema mfumo huo umeweka utaratibu thabiti wa kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi katika maeneo ya kilimo, elimu, maji, nishati, uchukuzi na ufuatiliaji wa rasilimali, lengo likiwa ni kuwa na uwajibikaji wa kila mshiriki au taasisi katika utekelezaji wa miradi ya serikali ili kupata mafanikio haraka.

Kadhalika, Issa alisema mfumo umeanzisha kitengo cha kusimamia utekelezaji na ipo katika mchakato wa kuanzisha vitengo vya kusimamia utekelezaji katika ngazi za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ili kuongeza ufanisi wa kutekeleza miradi katika ngazi zote.

“Ili kufanikisha BRN, tunahitaji ushirikiano wa sekta binafsi ambayo italeta teknolojia, utaalamu wa menejimenti na mtaji, ili kuhamasisha ushirikiano huo tumeanzisha mchakato wa kurazinisha mfumo na taratibu za ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili tuhakikishe inatoa mchango wake stahili katika utekelezaji wa BRN,” alisema.

Alisema maeneo ya kimkakati ya kitaifa ni usambazaji wa maji salama vijijini ambako kwa kipindi cha miezi sita zaidi ya watu 300,000 wamepata maji, ulinzi wa chakula, elimu ya msingi na sekondari, kuimarisha usafirishaji wa bandari, reli na barabara katika kanda ya kati, upatikanaji na uzalishaji na utafutaji wa rasilimali fedha.