Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 13 Machi 2014

siri ya kufanya vibaya matokeo ya kidato cha 4 kwa shule za serikali

Miongoni mwa habari zilizoripotiwa katika gazeti hili jana ni pamoja na ripoti maalum iliyofichua baadhi ya sababu za kufanya vibaya kwa wanafunzi wa moja kati ya shule 10 za sekondari zilizoburuta mkia katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne uliofanyika mwaka mwishoni mwa 2013. Katika shule hiyo iitwayo Mvuti, iliyopo kwenye Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, ni mtahiniwa mmoja tu aliambulia daraja la tatu. Wengine watatu walipata daraja la nne huku 40 waliobaki wakipata daraja sifuri na mwishowe shule hiyo ikashika nafasi ya 3,251 kati ya 3,256 zilizokuwa kwenye kundi la sekondari zenye watahiniwa 40 au zaidi. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa shule ya Mvuti ina changamoto nyingi zinazokwaza maendeleo yao kitaaluma. Uwezo mdogo wa wanafunzi wanaoripoti katika shule hiyo, ukosefu wa vitabu vya ziada na kiada, tatizo la usafiri, njaa kwa wanafunzi na pia kukosekana kwa mkuu wa shule ni baadhi ya matatizo yanayoikwamisha shule hiyo. Sisi tunaona kuwa matatizo haya lukuki yanayoikabili Mvuti yanapaswa kutafutiwa ufumbuzi haraka. Ni wazi kuwa hatua sahihi zisipochukuliwa sasa, Mvuti na shule nyingine za umma zenye changamoto zinazofanana nayo zitaendelea kupata matokeo mabaya katika kila mwaka; jambo ambalo halipaswi kuachwa hivi hivi. NIPASHE tunajua kuwa nyingi kati ya changamoto zinazoikabili Mvuti na shule nyingine za aina yake zinaweza pia kushughulikiwa na uongozi wa shule husika. Halmashauri za manispaa na wilaya ambazo ni miongoni mwa wamiliki wa shule hizi, zinapaswa pia kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu, sawa na serikali kuu na wadau wengine wa sekta ya elimu nchini. Jambo muhimu ni kuwa na dhamira ya dhati kwa kila upande, kwa maana ya viongozi wa shule, wanafunzi, wazazi, serikali na wadau wengine. Kwa mfano, inaelezwa kuwa awali, Mvuti haikuwa na bodi kwa miaka miwili. Hili ni tatizo linalochangia kuwapo kwa matokeo mabaya kwani kupitia bodi, ndipo shule huwa na fursa nzuri ya kujiwekea malengo na kuyasimamia. Lipo pia tatizo la usafiri na njaa. Baadhi ya wanafunzi wa Mvuti hulazimika kupanda mabasi sita hadi nane kwa safari ya kutoka nyumbani kwenda shule na kurudi, achilia mbali safari nyingine ya kutembea kwa miguu umbali wa takriban kilomita nane kwa safari mbili kutoka katika kituo cha mabasi cha Mvuti hadi shuleni kwao. Matatizo ya aina hii huwakabili pia wanafunzi wa shule nyingine nyingi zilizo pembezoni mwa miji. Shule hiyo pia hukabiliwa na tatizo la kupokea baadhi ya wanafunzi wasio na uwezo darasani. Ripoti inaonyesha kuwa asilimia 70 ya wanafunzi walioripoti mwaka 2011 ili kuanza kidato cha kwanza walikuwa hawajui kusoma wala kuandika. Aidha, inaelezwa kuwa ni wanafunzi watatu tu ndiyo waliofaulu kwenye mtihani wao wa kidato cha pili miongoni mwa wale waliofeli sana mwaka huu na kuifanya shule ya Mvuti iingie katika orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya. Ni wazi kuwa kama taratibu zingefuatwa, shule hiyo isingepata matokeo hayo mabaya kwani wale waliofeli kidato cha pili wangepata nafasi ya kukariri darasa na wala siyo kuvushwa kirahisi na mwishowe kushusha ufaulu wa shule hiyo. NIPASHE tunaamini kuwa bodi ya shule ya Mvuti, kwa kushirikiana na wazazi wa wanafunzi na wadau wengine wa elimu, wanaweza kubuni utaratibu mzuri wa kukabiliana na tatizo la usafiri, maji na chakula kwa watoto wao. Mipango ya kujenga mabweni zaidi kwenye shule za pembezoni kama Mvuti ni muhimu. Aidha, Wizara ya Elimu inapaswa kuangalia vyema mfumo wake wa kuwapima watahiniwa wa darasa la saba ili wanafunzi wote wanaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wawe na sifa sahihi kwani ni vigumu sekondari hizi za kata kupata matokeo mazuri ikiwa zitaendelea kupokea wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika. Njia pekee ya kuzikomboa shule za kata kama Mvuti ni kushughulikia kero zilizopo. Kwa kufanya hivyo, nazo zitaimarika na kupandisha viwango vyao vya ufaulu.