Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Ijumaa, 10 Januari 2014

Baba wa miaka 54 aoa mtoto wa miaka minane

Bunda. Polisi Wilaya ya Bunda, wanamshikilia baba mwenye umri wa miaka 54 kwa tuhuma kuoa mwanafunzi wa kike wa umri wa miaka minane.
Msimamizi wa Dawati la Jinsia katika Kituo Kikuu cha Polisi Bunda, Rita Charles alisema baba huyo mkazi wa Kijiji cha Nyaburundu wilayani Bunda alikamatwa jana akiwa anaishi na binti huyo (jina limehifadhiwa) kama mke wa nyumbani baada ya kutoa kishika uchumba kiasi cha Sh55,000 kwa wazazi wake.
Ilielezwa kuwa mwanaume huyo kabla ya kumwoa mtoto huyo aliyekuwa anasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Nyaburundu, alimchumbia kwa wazazi wake na kutakiwa atoe ng’ombe watano za mahari ndipo akatoa kishika uchumba hicho na mtoto huyo kuondolewa shule. “Tulifanikiwa kumkamata mwanamume huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema,” alisema Rita.
Alisema siku ya Mwaka Mpya, alichukuliwa na dada yake na kumpeleka kwa mume wake huyo ili aanze maisha ya ndoa.
Hata hivyo, alisema alipofika, usiku huo walilala kitanda kimoja wote watatu (baba muoaji, muolewaji na dada wa muolewaji) na kwamba mwanamume huyo alianza kufanya mapenzi na dada yake na baadaye akamgeukia ‘mkewe’ kuanza kumnyonya maziwa.
“Tulilala wote watatu na alifanya mapenzi na dada yangu, mimi akininyonya maziwa,” alisema mtoto.

chanzo. mwananchi

uandikishwaji wa wanafunzi darasa la kwanza baadhi ya mikoa kuna changamoto

Zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wapya wa darasa la kwanza mwaka huu limeanza na misukosuko ya aina yake. Baadhi ya maeneo nchini yamekumbwa na mgogoro mkubwa baina ya wazazi na walimu, chanzo kikitajwa kuwa ni pamoja na gharama ambazo kila mtoto hutakiwa alipiwe na wazazi wake kabla ya kupatiwa fursa ya kuandikishwa.

Taarifa zilizoripotiwa jana zilionyesha kuwa mjini Morogoro hali haikuwa shwari. Vurugu kubwa ziliibuka na mwishowe baadhi ya wazazi wanaodaiwa kuwa ni wenye itikadi tofauti za vyama walivaana mwilini.

Katika kisa hicho, inalezwa kuwa kila mzazi alitakiwa alipe walau Sh.50,000 ndipo kila mtoto aliyempeleka shuleni apate fursa ya kuandikishwa. Kwamba, baadhi ya wazazi wenye uwezo kifedha walilipia gharama hizo bila shida. Hata hivyo, wengine wakataka watoto wao waendelee kuandikishwa hata kama walikosa fedha hizo kwavile si sera ya serikali kuwabagua wananchi wake kwa kigezo cha pesa.

Inadaiwa kuwa sintofahamu hiyo ikakolezwa na itikadi za vyama baada ya mzazi mmojawapo anayedaiwa kuwa ni wa chama tawala kutetea ulipaji wa gharama hizo huku mwingine anayedhaniwa kuwa ni wa upinzani akipinga vikali. Mwishowe wawili hao wakavaana kwa nia ya kushikishana adabu. Walishindwa kukubaliana juu ya kutofautiana kwao.

NIPASHE hatukusudii kujadili ugomvi baina ya wazazi hao wa Morogoro. Na wala siyo lengo letu pia kuwa mahakimu na kueleza ni nani kati yao aliye sahihi. Bali, tunalichukulia tukio hili kuwa ni mfano wa kile kinachotokea katika maeneo mengi nchini.

Kwamba, katika kipindi hiki, baadhi ya walimu wakuu huwageuza wazazi kuwa mtaji. Huanzisha michango mingi kwa visingizio mbalimbali, lengo likiwa ni kuwakamua wazazi hadi tone la mwisho. Katika hili, sisi hatuoni kuwa ni sahihi. Siyo haki hata kidogo kuwabebesha wazazi mzigo mzito wa gharama za elimu kupitia rundo la michango inayoanzishwa kwa visingizio mbalimbali.

Kwa mfano, sisi tunaona kuwa kuwalazimisha wazazi kulipa Sh. 50,000 kwa kila mtoto ndipo haki ya kuandikishwa shule ipatikane siyo uamuzi sahihi. Tunaamini hivyo kutokana na ukweli kuwa mara zote, serikali yetu imekuwa ikisisitiza kuwa elimu ya msingi ni lazima kwa kila mtoto aliyefikisha umri wa kwenda shule. Tena, kadri ya ufahamu wetu, elimu hii hutolewa bure.

Abadan, michango ya aina yoyote ile haiwezi kuwa chanzo cha mwanafunzi wa darasa la kwanza kunyimwa haki yake ya kuandikishwa. Na ndiyo maana, kwa tukio la Morogoro, Mbunge wa Jimbo hilo aliingilia kati na kuwataka walimu kuwaandikisha watoto wote bila kujali kama wazazi wao wamelipa mchango wa Sh. 50,000 ama la. Ni kwa sababu elimu ya msingi ni ya lazima, na tena ni haki ya kila mtoto.

Isitoshe, kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali za elimu nchini, umri wa kuanza darasa la kwanza una ukomo wake. Kutomuandikisha mtoto aliyefikia umri wa kuanza shule ni kumpa adhabu asiyostahili kwani kuna uwezekano mkubwa wa kukataliwa katika mwaka unaofuata kutokana na kigezo cha kuwa na umri mkubwa. Matokeo yake, taifa litakuwa katika hatari ya kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika. Hili siyo jambo zuri hata kidogo.

NIPASHE hatupingi hatua ya wananchi kutakiwa kuchangia maendeleo yao, yakiwamo ya elimu. Hata hivyo, michango hii haipaswi kuwa chanzo cha kuongeza kwa idadi ya wasiojua kusoma na kuandika. Haipaswi vilevile kuwa chanzo cha kuligawa taifa kwa misingi ya wenye nacho na wasio nacho. Isitoshe, tunadhani kwamba sasa kuna kila sababu kwa viongozi wanaosimamia elimu kuingilia kati na kusimamia kwa vitendo kauli zao mbalimbali zinazosisitiza kuwa elimu ya msingi ni ya lazima kwa kila mtoto na kwamba, hakuna ada wala michango yoyote ya lazima.

Kuachia hali iendelee kuwa kama Morogoro ni hatari. Ni kuichafua serikali ambayo lengo lake zuri la kutoa elimu ya msingi bure linaelekea kutibuliwa na watu wachache walio na vipaji vya kubuni kila aina ya michango ili kuwakamua wazazi kwa maslahi yanayotiliwa shaka.

Michango mingi kama ya madawati, ya uji, ya ulinzi, ya nembo za shule na ya mitihani kwa shule za msingi haipaswi hata kidogo kutumiwa kwa maslahi ya wachache kwani athari za kuwa na taifa lililojaa watu wasiojua kusoma na kuandika ni kubwa sana na kamwe hazipimiki kirahisi.

Shime, michango hii katika uandikishaji wa wanafunzi wapya wa darasa la kwanza isitumiwe kubagua wasio na uwezo.

chanzo Nipashe