Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumapili, 10 Novemba 2013

chama cha walimu kuidai tena serikali

Chama  Cha Walimu Tanzania (CWT) kimeipa serikali siku 60 za kukamilimisha madeni ya mishahara ya walimu ya Sh. bilioni 48 pamoja na kukamilisha majadiliano ya mishahara  ya walimu na chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa CWT, Gratian Mukoba, wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu maazimio ya mkutano mkuu wa Taifa wa walimu nchini uliofanyika mkoani Arusha  Oktoba 28-29, mwaka huu.
Mukoba alisema hatua hiyo ilifikiwa na chama hicho baada ya serikali kukaa kimya kwa muda mrefu bila kutekeleza ahadi walizokiahidi chama hicho juu ya madai ya walimu ya muda mrefu.
Alisema chama hicho kinaidai serikali zaidi ya Sh. bilioni 48, ambazo serikali ili ahidi kuzilipa Septemba mwaka huu, lakini hawakufanya hivyo badala yake ikasema  inafanya uhakiki kwanza wa madai hayo ili kukamilisha malipo hayo ambayo mpaka sasa hayajafanyika.
“Tuliendelea kukaa kimya tukisubiri serikali ikamilishe uhakiki wake na kutoa taarifa ya madai ambayo walimu wanaidai, lakini bado haikufanya hivyo, kwa hiyo na sisi baada ya kukaa kikao chetu cha walimu Taifa tukaweka maazimio haya,” alisema Mukoba.
Alisema wanatarajia kukabidhi barua ya notisi kwa Katibu Mkuu Kiongozi leo na hatua za kisheria zitafuata endapo serikali haitatimiza hayo ambayo wameyaorodhesha baada ya siku 60 kumalizika.
Alisema, maazimio mengine waliyoyaandika  kwenye barua hiyo ya notisi ni serikali iwe imebadilisha muundo wa walimu na wakaguzi ndani ya siku hizo 60.Azimio lingine  waliitaka serikali kukamilisha majadiliano na chama cha walimu kuhusu mishahara ya walimu ya mwaka ujao kwa mwaka  wa fedha wa 2013/2014.
“Haya yote na mengine ambayo sijakuainishia tunayataka yatekelezwe na serikali ndani ya siku hizi 60 tulizotoa na endapo serikali itaendelea kukaidi basi hatua zaidi za kisheria zitafuata na tutatoa msimamo wa chama kuwa nini kitafanyika,” alisema Mukoba.
NIPASHE lilimtafuta Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, jana ili kuzungumzia suala hilo, lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.Hata Naibu Waziri, Philip Mulugo, alipotafutwa simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.
 ippmedia.com