Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumanne, 1 Julai 2014

nini kinaendelea kwenye shule zetu?

Mwananchi 1 tu kati ya 10 ndiye anayefikiri kuwa watoto wengi wanaomaliza darasa la 2 wana uwezo wa kusoma na kufanya hisabati wa darasa hilo hilo (ngazi ya darasa la 2). Mbaya zaidi, wananchi 3 tu kati ya 10 (31%) wanafikiri kuwa watoto hawa wanapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuhesabu kwenye ngazi yao; ikimaanisha kuwa wananchi hawana matumaini kama kweli mfumo wa elimu utawafundisha watoto ujuzi na stadi wanazotakiwa kupata wakiwa shuleni.
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Nini kinaendelea kwenye shule zetu? Wananchi watafakari juu ya hali ya elimu. Muhtasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika kwa njia ya simu mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa ambao unauwakilishi wa kaya zote Tanzania Bara.
Muhtasari huu unachunguza hali ya shule zetu, ufundishaji na ujifunzaji pamoja na ushiriki wa wazazi kwenye elimu ya watoto wao. Licha ya matarajio ya chini kwenye mfumo wa elimu, wazazi mara nyingi hutimiza wajibu wao kuhamasisha na kusimamia ujifunzaji. Wanafunzi 7 kati ya 10 waliripoti kuwa wazazi wao hupitia na kukagua madaftari yao mara kwa mara.
Walimu wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanajifunza shuleni. Hata hivyo, hawawezi kufanya kazi hii kama walimu wenyewe hawaingii darasani. Wanafunzi 3 kati ya 10 walithibitisha kuwa mwalimu wao muhimu aliingia darasani vipindi vyote siku iliyopita. Wanafunzi 4 kati ya 10 (38%) waliripoti kuwa mwalimu wao hakuingia darasani siku nzima, na wanafunzi 3 kati ya 10 (28%) walisema kuwa, mwalimu aliingia baadhi ya vipindi tu vya siku hiyo.
Sauti za Wananchi iliuliza pia maswali kuhusu hali ya mazingira ya shule. Karibu wanafunzi wote (99%) wanafundishwa wakiwa madarasani, siyo nje, na wanafunzi 9 kati ya 10 (91%) hukaa kwenye fomu au dawati shuleni. Hata hivyo, ni nusu tu ya idadi ya wanafunzi (49%) waliosema hupewa chakula shuleni. Ingawa kukosekana kwa viti na madarasa kuna uwezekano wa kuathiri viwango vya kujifunza, watoto wanapokuwa na njaa wanakuwa na uwezo mdogo kupokea na kumiliki maarifa mapya.

chanzo twaweza tanzania

Tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike, serikali bado kigugumizi

kassim majaliwa
Nilikuwa nikisikiliza maelezo ya Mbunge Kasim Majaliwa, akiwa Bungeni, kuhusiana na suala la mimba za utotoni, na kama ni vizuri wanafunzi wanaopata mimba wasirudishwe au warudishwe shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Na kuwa kama  kurudishwa shule hakutakuwa ni mfano mbaya kwa wengine, au kutakuwa ni faida.

Mimi nataka kusema kuwa hakuna hasara yoyote kwa kumrudisha msichana shuleni baada ya kujifungua, na sababu ziko nyingi!
‘Kosa’ la mwanafunzi wa kike ni moja tu, kuwa na tumbo linaloweza kukaa mtoto, na kuonekana hadharani kuwa alijihusisha katika mapenzi na hakuweza kujikinga na hatimaye alipata mimba.

Na kuwa wale waliohusika (nasema ni wengi waliohusika) na kupatikana kwa mimba ya huyu msichana hawana tumbo kama hilo, au wamejitenga na uwajibikaji kwa kosa husika.

Kabla sijafika huko kwenye kutaja walio na makosa yaliyosababisha mimba, nataka niulize? Hivi kweli Tanzania, serikali na watu wake wako tayari kuendelea na maisha ya karne ya ishirini na moja wakiwa na watu wasiojua kusoma na kuandika, watu ambao wana elimu nusunusu, watu ambao hawana uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri?

Kisa ni kuwa msichana huyu amepata mimba akiwa mtoto- tena mimba ya utoto! Msichana huyu atakuwa ni mzigo kama asipoachwa aendelee na masomo, na hataweza kumudu maisha yake.

Katika nchi ambayo inataka kila mtu awe mjasiriamali, haiwezi kuruhusu kikundi cha watu wachache au wengi kuishi bila elimu, au elimu ya kutosha. Msichana huyu ataturudishwa nyuma kimaendeleo kama akiachwa asiendelee na shule kwa kosa dogo la mimba.

Waliohusika na kupatikana kwa mimba kwa huyu mtoto ni wazazi? Wazazi wajiulize kama walikaa na mtoto ambaye tayari amekua na kubalekhe, ili kumpa mwongozo bora wa maisha na umuhimu wa elimu kwake, na umuhimu wa urafiki na watu wa rika mbalimbali, lakini wakiwa waangalifu kuhusiana na suala la mapenzi? Au wazazi walitegea walimu, na walimu hawakuwajibika ipasavyo kwani walidhani kuwa wajibu wao ni kuwapatia elimu tu, ambayo ni masomo ya msingi bila kuhusisha stadi za mahusiano na maisha? Walimu wamekuwa wakiwalea watoto kwa muda wa kati ya saa 6 kwa siku hadi saa kumi na mbili, na wakati mwingine kwa miezi mitano hadi kumi kwa mwaka.

Hawa ni wazazi wa pili wa mwanafunzi huyu mdogo kwa umri, asiye na stadi kamilifu za mahusiano, na hawampatii mafunzo kuhusiana na hilo. Ukienda shule nyingi hakuna mfumo wa elimu ya unasihi ambapo mtoto anaweza kufika ofisini kwa mnasihi akihisi anasumbuliwa na mahusiano, au anataka kujiingiza kwenye mahusiano lakini hana uhakika na njia sahihi ya kuenda nayo.

Mtoto anajikuta akiishi kwa kubahatisha katika mahusiano ambao mengi yanaainisha ngono kama ndiyo msingi wa mahusiano. Na utaona hao hili lilimsababishia mtoto kupata mimba, ingawa eti lawama zinabaki kwa mtoto.

Watoto wanapotoka kwenye familia ya masikini, na kufika katika jamii ambako watoto wenzao wanakula vyakula vizuri, wana mali za kisasa, na wanaishi wakiwa na fedha zao wenyewe walizopewa na wazazi, siyo rahisi kujitoa katika mitego kama miongo ya kimalezi ya wazazi na ya shuleni ni hafifu au haipo.

Watoto hawa wanzongwa na mifumo ya habari na tamaduni pendwa ambavyo  vinawachagiza kujiingiza katika mahusiano au tabia ambazo zitawaingiza katika mahusiano bila kuwa na mwongozo sahihi.

Na watoto kama wageni katika dunia hii, wanapaswa kuwasaidia kuwaongoza watoto hao ili waelewe maana ya vitu wanavyokutana navyo. Watoto wanatakiwa kuongozwa, na wengi wa watoto waliopata mimba utotoni hawakuongozwa vizuri. Hawa walihusika kumpatia mtoto mimba, kwa sababu hawakutimiza wajibu wao!

Kinanishangaza zaidi pale ambapo aliyehusika na kudunga mimba anajulikana, au hata kama hajulikani, anaachwa aendelee na maisha yake, na mtoto wa kike ndiye anayebeba lawama. Kwa hili hatutofautiani na wale ambao mwanamke na mwanaume wakikamatwa wanazini, anayepigwa mawe na kuuawa ni mwanamke; mwanamke akibakwa, anayepigwa mawe na kufa ni mwanamke.

Wakati mwanaume, aliyehusika kumbaka, tena inajulikana kuwa ndiye aliyefanya hivyo, anaachwa aishi kwa raha na starehe akiendelea kuvizia wanawake  wengine wa kubaka.

Angalia jinsi vyombo vya habari vinavyohusika na kuwaambia watoto kuwa mapenzi kati yao inawezekana. Michezo ya kuigiza ya televisheni, redio, magazeti, na filamu, vyote hivi vinawaambia wanaume na wanawake kuwa mapenzi ya watoto kwa watoto, watoto na watu wazima, yanawezekana.

Kwa kifupi utaona kuwa waliohusika na kupewa mimba msichana ni wengi kutokana na tabia zao, ulegevu wao katika malezi na sera, lakini eti msichana ndiye pekee anabakizwa na kosa.

Huu ni uonevu. Ndiyo maana ninashangaa kusikia serikali inasita kumtambua mtoto wa kike kuwa ni kiumbe asiye na kosa!