Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumapili, 31 Agosti 2014

Timu ya Haki Elimu uso kwa uso na afisa elimu (shule ya mwisenge)

afisa elimu bi. Beatrice Mkina akiteta kidogo na wafanyakazi wa Haki Elimu walipokutana shule ya msingi Mwisenge
maktaba ya kisasa iliyojengwa na Haki Elimu shule ya msingi Mwisenge

wanafunzi wasioona shule ya Mwisenge kujengewa kiwanja cha michezo


Afisa elimu Msingi manispaa ya Musoma Mjini Bi
. Beatrice Mkina alibainisha mpango wake wa kuwezesha shule ya msingi Mwisenge kujengewa kiwanja cha michezo kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavua wa macho.
siku ya ijumaa 29/8/2014 afisa elimu huyo aliitembelea shule ya msingi Mwisenge kwa minajili ya walimu wa shule hiyo kumpendekezea eneo zuri la ujenzi wa kiwanja hicho cha michezo
afisa elimu akiangalia eneo lililopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha michezo
afisa elimu katikati na baadhi ya walimu na wajumbe wa kamati ya shule
hii ni juhudi nzuri kwa serikali kuwakumbuka wanafunzi wasioona wa shule ya msingi mwisenge.
Afisa elimu kushoto na mjumbe wa kamati ya shule mwisenge

Alhamisi, 28 Agosti 2014

umoja wa marafiki wa elimu musoma (sauti zetu club) tumetimiza miaka 6

Marafiki wa elimu musoma
umoja wa marafiki wa elimu musoma tunaounda kikundi cha SAUTI ZETU CLUB leo tumetimiza miaka sita tangu kuanzisha umoja wetu mwaka 2008 tunamshukuru Mungu kwa kuendelea kutupigania na kuzidi kutuaminisha kwa jamii na viongozi pamoja na wadau wa elimu Musoma Mijini

Kwa pamoja tunaweza kuinua sauti za wanyonge

Jumatatu, 25 Agosti 2014

Hatimae shule ya kigera mbunge nyerere asema itajengwa kabla ya disemba mwaka huu

majengo ya shule ya kigera yaliyobomolewa na diwani bila kufuata utaratibu
hatimae Mbunge wa musoma mjini Mheshimiwa Vincent Nyerere katoa ahadi jana kwenye mkutano wa kuelezea mafanikio aliyofikia kwa miaka minne kuwa,
shule ya msingi Kigera iliyobomolewa na diwani wa kata hiyo ndugu Gabriel Ocharo Aenda kwa kile kilichogundulika kuwa ni kutokufuata utaratibu na kupelekea wanafunzi kukosa pahala pa kusomea ,

mbunge wa musoma mjini jana kamsimamisha Meya wa manispaa ndugu Alex Kisurura kujibu sakata la shule hiyo na kueleza kwamba ifikapo mwezi disemba shule hiyo iliyobomolewa vyumba sita vya madarasa na kupelekea wanafunzi kurundikana madarasani vitakuwa vimekarabatiwa tena kwa kiwango cha juu na kuahidi kuwa licha ya ukarabati pia watapeleka madawati mapya katika madarasa hayo.

sakata la kubomolewa madarasa hayo sita  mpaka sasa bado linaendelea mahakamani baada ya diwani huyo kufunguliwa kesi kwa kosa hilo la kobomoa madarasa hayo.

akizidi kuelezea waliyoyafanya kwa miaka minne ya uongozi wake mhe Nyerere kasema wamegawa computer 5 na projector kwa shule 3 wametengeneza madawati 1902  pamoja na mipango mingine mingi sana ikiwa ni pamoja na kujenga maabara ya kisasa shule ya sekondary bweri makatani na kujenga madarasa karibu kila shule ya sekondary

Alhamisi, 21 Agosti 2014

Wanafunzi 28,000 elimu ya juu kukosa mikopo

Wanafunzi 28,037 watakosa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB), hivyo kulazimika kusaka njia mbadala kama wanataka kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Idadi hiyo ni sehemu ya wanafunzi 58,037 ambao hadi kufikia Julai 31, mwaka huu walikuwa wamewasilisha maombi ya mikopo kwa ajili ya mwaka wa masomo 2014/15, huku bodi hiyo ikiwa na uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 30,000 pekee wa mwaka wa kwanza.

Idadi hiyo inafanya asilimia 49 ya waombaji wote kusaka vyanzo mbadala kama wanataka kuendelea na elimu ya juu nchini kwa mwaka ujao. HELSB imesema kuwa ina uwezo wa kutoa mikopo kwa asilimia 51.5 pekee.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salama jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisoba, alisema maombi yaliyopokelewa mwaka huu yameongezeka kutoka 53,239 mwaka jana hadi 58,037 sawa na ongezeko la asilimia tisa.

Alisema miongoni mwa waombaji wa mikopo, kundi la diploma ya ualimu wa sayansi ni 480 wakati wale wa shahada ya uzamili/uzamivu kwa vyuo vya ndani ya nchi wakiwa ni 276.

Kwa mujibu wa Mwaisoba, waombaji wa shahada kwanza kwa vyuo vya ndani ya nchi ni 56,922, wale wa shahada ya uzamili/uzamivu nje ya nchi wakiwa ni 126 na wale wa shahada ya kwanza nje ya nchi ni 233.

Alisema baada ya kufungwa rasmi kwa kipindi cha kupokea maombi ya mikopo, hatua inayoendelea kwa sasa ni uhakiki wa taarifa za waombaji kwa kuzipitia nyaraka mbalimbali zilizoambatanishwa na waombaji mikopo.

Nyaraka hizo ni cheti cha kuzaliwa, vyeti vya taaluma, vielelezo vya mdhamini, saini ya mwombaji na mdhamini wake na ushuhuda wa mwanasheria au hakimu kwamba vivuli vya nyaraka zilizowasilishwa kwenye bodi ni halisi.

Alisema mchakato wa uchambuzi na upangaji wa mikopo utakamilika baada ya majina ya wanafunzi waliodahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kujiunga na vyuo mbalimbali yanapowasilishwa rasmi kwenye bodi.

Kwa mujibu wa Mwaisoba, udahili wa wanafunzi unafanywa na TCU kwa mfumo wa pamoja wa udahili (CAS) unaotumiwa na vyuo takriban vyote vya elimu ya juu nchini. Alisema kwa vyuo ambavyo havimo katika mfumo wa pamoja wa CAS hutuma TCU majina ya wanafunzi, ambao vimewadahili ili wathibitishwe kabla ya kupatiwa mikopo.

“Taarifa za udahili ni muhimu katika zoezi la upangaji wa mikopo kwa kuwa zinatoa mwongozo wa gharama halisi za program za mafunzo,” alisema Mwaisoba.

Alisema wanafunzi wanaostahili na waliotimiza masharti na vigezo vya ukopeshaji ndiyo hupangiwa mikopo kulingana na bajeti iliyotengwa na serikali.

Mwaisoba alisema majina ya wanafunzi waliopata mikopo kulingana na udahili, yatatangazwa kwenye tovuti ya bodi na katika vyombo vya habari ili kuwataarifu wadau wote ikiwa ni pamoja na wanafunzi, vyuo vya elimu ya juu, wazazi na umma kwa jumla.

Alisema nakala za majina ya wanafunzi waliopangiwa mikopo zitatumwa kwenye vyuo husika.

Mwaisoba, alisema kwa kutambua umuhimu wa masomo ya sayansi na kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo hayo katika ngazi ya shule za msingi na sekondari, mwaka huu serikali imetoa fursa ya mikopo kwa wanafunzi watakaojiunga na masomo ya stashahada maalumu ya ualimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Alisema wanafunzi 5,000 wanatarajiwa kujiunga na stashahada hiyo maalumu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na kwamba, wote watanufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

“Kwa taarifa hii, bodi inapenda kuwataarifu wadau wote kuwa mchakato wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 unaendelea,” alisema Mwaisoba.

Aliwataka waombaji wa mikopo, wazazi/walezi na umma kwa jumla kutambua kuwa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uchangiaji wa elimu ya juu na hivyo iwapo kuna waombaji wanaoweza kujigharimia, wasiombe mikopo ili kutoa nafasi kwa wahitaji wengi zaidi.

Alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili HESLB ni pamoja na ucheleweshaji wa urejeshaji wa mikopo, ushirikiano hafifu kutoka kwa wadau katika urejeshaji wa mikopo na mazingira ya kijiografia kuweza kuwafuatilia waliokopa.

Hata hivyo, alisema HESLB ina uwezo wa kukusanya marejesho ya mikopo Sh. bilioni tatu kwa mwezi.

KUMALIZANA NA TAHLISO WIKI IJAYO
Kuhusu madai ya wanafunzi wa vyuo vitano ya kutaka wapewe Sh. bilioni 6.6 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, Mwaisoba alisema malipo hayo yanaandaliwa na kwamba, hundi za malipo hayo zinatarajiwa kupelekwa katika vyuo wiki ijayo.

Alisema wanafunzi wa vyuo hivyo walichelewa kulipwa kutokana na fedha kuchelewa kupatikana.Hali hiyo ilisababisha Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (Tahliso) kuitisha maandamano ya amani wiki iliyopita kwenda ofisi za Waziri Mkuu kushinikiza serikali kuwalipa fedha hizo.

Hata hivyo, maandamano hayo yalisambaratishwa na Jeshi la Polisi, lakini siku mbili baadaye, Tahliso ilitangaza tena kuitisha maandamano keshokutwa.

Kiwango hicho cha fedha kinachodaiwa na wanafunzi hao, kimo kwenye takwimu zilitolewa na Mkurugenzi wa HESLB wakati wakifanya mazungumzo juu ya hatma ya vyuo hivyo.

Vyuo hivyo, ambavyo havijapata  fedha hizo ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) Mwanza na Tabora, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji-Mbeya, Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMUCCO) na Chuo Kikuu cha Jordan Morogoro.    

CHANZO IPPMEDIA.COM

Jumatano, 13 Agosti 2014

Iringa shule yenye wanafunzi 600 ina mwalimu mmoja

Photo: TAFAKARI YA WIKI HII : Gazeti la RaiaTanzania limeripoti habari inayohusu shule ya msingi katika mkoa wa Iringa yenye wanafunzi 600  ikiwa na mwalimu mmoja tu (1), wakati huo huo Radio Uhuru imeripoti Shule moja mkoani Shinyanga yenye wanafunzi takribani 500 wana matundu mawili (2) pekee ya vyoo .Gazeti la Mtanzania pia limeripoti shule yenye wanafunzi 480 katika wilaya ya Serengeti ina madawati matano  tu (5).Muasisi wa Taifa letu , Mwalimu Nyerere alituasa ili nchi iendelee tunahitaji mambo manne SIASA SAFI, ARDHI, UONGOZI BORA NA WATU . Hakuna ubishi kwamba bado hatuna uongozi bora kwani imepita miaka 50 tangu Uhuru kukiwa na awamu nne za uongozi lakini changamoto kama hizi si ngeni miongoni mwa watanzania, Siasa yetu nayo bado ina madhaifu hilo halina ubishi. Leo tuachane na UONGOZI MBOVU NA SIASA MBOVU kabisa, tujiangalie SISI (WATANZANIA) kama wananchi  tujiulize tumefanya nini kuhakikisha tunaondokana na changamoto hizi? Je ni kwa kiwango kipi tumefanikiwa katika yale tuliyofanya katika kuleta mabadiliko ? Nini wajibu wetu watanzania katika kutatua changamoto hizi?. Hii ni aibu kwetu sote, kwangu mimi, yule na wewe. Tafakari na tujadili hatua zipi zichukuliwe kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa.TAFAKARI YA WIKI HII : Gazeti la RaiaTanzania limeripoti habari inayohusu shule ya msingi katika mkoa wa Iringa yenye wanafunzi 600 ikiwa na mwalimu mmoja tu (1), wakati huo huo Radio Uhuru imeripoti Shule moja mkoani Shinyanga yenye wanafunzi takribani 500 wana matundu mawili (2) pekee ya vyoo .Gazeti la Mtanzania pia limeripoti shule yenye wanafunzi 480 katika wilaya ya Serengeti ina madawati matano tu (5).Muasisi wa Taifa letu , Mwalimu Nyerere alituasa ili nchi iendelee tunahitaji mambo manne SIASA SAFI, ARDHI, UONGOZI BORA NA WATU . Hakuna ubishi kwamba bado hatuna uongozi bora kwani imepita miaka 50 tangu Uhuru kukiwa na awamu nne za uongozi lakini changamoto kama hizi si ngeni miongoni mwa watanzania, Siasa yetu nayo bado ina madhaifu hilo halina ubishi. Leo tuachane na UONGOZI MBOVU NA SIASA MBOVU kabisa, tujiangalie SISI (WATANZANIA) kama wananchi tujiulize tumefanya nini kuhakikisha tunaondokana na changamoto hizi? Je ni kwa kiwango kipi tumefanikiwa katika yale tuliyofanya katika kuleta mabadiliko ? Nini wajibu wetu watanzania katika kutatua changamoto hizi?. Hii ni aibu kwetu sote, kwangu mimi, yule na wewe. Tafakari na tujadili hatua zipi zichukuliwe kuhakikisha changamoto hizi zinatatuliwa.
 
 souce Haki Elimu
 

Jumanne, 12 Agosti 2014

wanaobeza juhudi za Mbunge Vincent Nyerere hawaitakii mema sekta ya elimu Musoma

Mbunge wa Musoma Mjini Vincent Nyerere na walimu wa shule ya Sec Kiara
siku ya leo napenda kuchukua fursa hii kuzungumzia japo kwa uchache juhudi za Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini Vincent Nyerere. kwa kile alichokifanya hivi karibuni kwa kugawa Computer pamoja na Projector kwa baadhi ya shule za Sekondari za hapa Musoma Mjini na kuahidi kugawa zingine hivi karibu
Sababu kubwa ya kuzungumzia suala hili ni baadhi ya wanasiasa wasioitakia mema sekta ya elimu kuendelea kudai kuwa hakukuwa na haja ya kugawa Computer kwa wanafunzi kwa wakati huu na badala yake angefanya kitu kingine na si kugawa computer.
harakati za marafiki wa elimu musoma tunapatikana hasa Kata ya kigera na katika Shule ya sekondari Kiara ambayo iko kata ya Kigera wamebahatika kugawiwa Computer 5 pamoja na Projector 1 na mbunge kuaidi kuwapatia tena Computer zingine 5

tatizo letu na wanaobeza juhudi za Mbunge huyu ni kwanini wao hawasemi ambacho mbunge angefanya kwa sasa kizuri zaidi ya kugawa hizo computer,
na Je hao wanaobeza watoto wao  wanasoma shule zetu za kata au wanasoma zile za St fulani  zenye kila kitu shuleni ikiwa ni pamoja na computer

kwa nini wanabeza maendeleo kwa watoto wa maskini , je si haki watoto wa maskini kuwa na computer mashuleni?

Je watoto wa maskini wa shule za kata wakifahamu kutumia computer ni jambo baya

sie marafiki wa elimu tunaamini kwamba hao watoto wa maskini wa shule za kata wana haki ya kumiliki computer mashuleni mwao kwani hata wakifeli kidato cha nne watakuwa na nguzo kidogo huenda wakawa masekretari kwani watakuwa walau na uzoefu wa kutumia computer
marafiki wa elimu tunapongeza juhudi za Mbunge huyu
na daima tukumbuke kuwa Elimu Ni taaluma isiyohitaji wanasiasa kuiharibu kwa siasa zao za kubeza mema yanayofanywa na mtu kisa tu si chama kile au itikadi ile

Tafakari chukua! hatua kiongozi bora ni yule anaethamini wapiga kura wake wa maendeleo ya elimu kwenye jimbo lake.

imeendikwa na Rafiki wa elimu
      Juma Richard Okumu

Jumatatu, 4 Agosti 2014

Miaka 30 kisiwa hakina shule, watoto 300 hawana pa kusoma


Mmoja wa kina mama wenye watoto kisiwani Kome Mchangani akiwa katika mizunguko yake ya kila siku kisiwani humo hivi karibuni.
Wakati taifa likiendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), hali ni tofauti kwa watoto zaidi ya 300 wanaoishi katika Kisiwa cha Kome Mchangani kilichopo kwenye Ziwa Victoria, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza baada ya kutojengwa shule kwa zaidi ya miaka 30.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kwa zaidi ya wiki mbili kwenye kisiwa hicho umebaini kuwa tatizo hilo halitokani na kuwapo kwa hamasa ndogo ya elimu kwa wazazi wa watoto hao; bali ni matokeo ya utekelezwaji wa Sheria ya Uhifadhi Misitu ya Mwaka 2002, katika kifungu cha 26 kinachokataza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa majengo ya kudumu.

Kisiwa cha Kome Mchangani ni miongoni mwa visiwa vya Ziwa Victoria vilivyotangazwa na serikali kuwa hifadhi ya misitu.

Kiongozi wa wakazi na wafanyabiashara wa mazao ya samaki katika kisiwa hicho, Tibenda Luhuya, aliiambia NIPASHE kuwa wamejitahidi kupigania uwapo wa shule na huduma nyingine za jamii kisiwani humo kwa muda mrefu lakini hakuna wanachoambulia zaidi ya kuambiwa kuwa sheria za nchi haziruhusu.

"Tunaelezwa kuwa eneo lote la kisiwa (cha Kome) halitakiwi kuwa na majengo ya kudumu na hivyo, serikali haiwezi kutujengea shule wala zahanati kwa sababu kufanya hivyo ni kuvunja hizo sheria," alisema Luhuya.

Hata hivyo, wakati shule na majengo mengine ya kudumu yakizuiwa, serikali imeruhusu kuwapo kwa jengo la kudumu la vyumba vitatu ambalo linatumiwa na Kikosi cha Usimamizi wa Fukwe (BMU).

"Bado tunaendelea kuisihi serikali kuwa itujengee shule kwa ajili ya watoto wetu ambao wanaishia kuvua samaki tu na kukosa elimu ambayo ni haki yao ya msingi," aliongeza.

Anasema kisiwa hicho kina wakazi zaidi ya 5,000 na kinahesabika kipo katika Kijiji cha Buhama, Kata ya Nyakasasa, Tarafa ya Buchosa. Umbali wa kutoka kisiwa hicho mpaka Kijiji cha Buhama ambako kuna Shule ya Msingi ni zaidi ya kilomita tano.

Akieleza zaidi, Luhuya anasema kwa zaidi ya miaka 30 tangu wavuvi na wafanyabiashara wa mazao yatokanayo na samaki walipoanza kuishi hapo hawajawahi kuwa na shule na hivyo, baadhi ya wazazi hulazimika kuwapeleka watoto wao kwa ndugu, jamaa na marafiki wanaoishi nje ya kisiwa hicho ili wakasome.

Hata hivyo, anasema zoezi hilo limekuwa gumu kwa kuwa baadhi ya wazazi wakishawapeleka huko (kwa ndugu zao), huwa wanawatelekeza na matokeo yake watoto hao wanarudi wenyewe kwa kuomba nauli na wengine kuingia ndani ya boti inazokwenda kisiwani humo bila ya kuwa na nauli.

WATOTO, WAZAZI WANENA
"Inaniuma sana kujikuta naishi bila kujua kusoma na kuandika. Wazazi wangu ni wavuvi na wote hawakusoma. Lakini na mimi nitaishia kuwa mvuvi nisiyejua kusoma na kuandika kama wao kwa sababu hapa kwetu (Kome) hakuna shule," ndivyo anavyoanza kueleza mtoto mmojawapo kisiwani Kome Mchangani, John (11).

Ibrahimu anasema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisikia kwamba kuna harakati zinafanywa za kuiomba serikali iwajengee shule. Lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na anaamini kuwa yeye na watoto wenzake wote kisiwani humo hawatapata fursa ya kujua kusoma na kuandika.

"Mimi inaniuma sana kwa kutojua kusoma... huwa ninawaona baadhi ya watu wanasoma magazeti na vitabu, hasa wanaotoka Mwanza kuja kununua samaki huku kwetu. Lakini mimi sijui kusoma wala kuandika.Ninachokijua zaidi ni kuvua na kufanya kazi ya kusomba dagaa kutoka ziwani kuwaleta nchi kavu," anasema Ibrahim.

Mtoto aitwaye Yona, mwenye umri wa miaka 10, anasema kutokana na kisiwa hicho kukosa shule, wazazi wake walimpeleka Mwanza mjini kwa rafiki yao ili akasome huko, lakini hilo halikuwezekana kwa sababu huko alikopelekwa, wenyeji hawakuipa shule nafasi na hata watoto wao (wa wenyeji) hawakuwa wakienda shule.

''Sasa nimerudi kwa wazazi wangu hapa kisiwani. Nimekaa wala sijui kama nitasoma... naendelea na kazi ya kibarua cha kusomba samaki kutoka katika mitumbwi ya wavuvi nyakati za jioni,'' alisema.

Tatu Kipile ni mmoja wa wakazi wa kisiwa cha Kome Mchangani. Anasema kuwa yeye ameshindwa kumpeleka shule mtoto wake anayeishi naye huko kutokana na kukosa fedha za kumsafirisha kutoka kisiwani humo na kumhudumia wakati anapokwenda kwenye eneo lenye shule.

"Nilihamia hapa (Kome) wakati mwanangu akiwa na miaka mitatu. Sasa ni zaidi ya mwaka wa tano niko hapa. Ninapenda sana mwanangu asome, lakini sina namna ya kufanya kwa sababu kisiwa hiki hakina shule na sina fedha za kumpeleka kwenye maeneo ya mbali yaliyo na shule za msingi," alisema mama huyo.

Hellen Cosmas alisema analazimika kumpangia chumba jijini Mwanza mtoto wake mwenye umri wa miaka 10 ili apate fursa ya kusoma, ingawa anasema bado kuna changamoto nyingi ya kutekeleza azima yake hiyo kwa sababu hana mwangalizi maalum.

"Hivi sasa nimemrudisha hapa kisiwani (Kome) kwa sababu mazingira ya kuishi Mwanza ni magumu. Hana mwangalizi na hivyo sasa niko naye hapa... haendi tena shule," alisema Hellen.

Sara Machera bado hajabahatika kupata mtoto. Hata hivyo, alisema kuwa hali iliyopo sasa ni ngumu kwa wazazi wa kisiwa hicho kutekeleza jukumu la kusomesha watoto wao kwavile hakuna shule. Aliongeza kuwa watoto wanaopelekwa kwa ndugu zao ili wasome ni kama huwa wanatelekezwa kwani uangalizi huwa mdogo.

Neema Abel ambaye pia bado hajapata mtoto anasema watoto kisiwani humo hukosa elimu kwavile hakuna shule na hivyo anaiomba serikali ifikirie kuwajengea shule ili kuokoa mamia ya watoto walio katika hatari ya kuwa wajinga, wasiojua kusoma wala kuandika.

VISIWA VINGINE
Tatizo la shule linalowakabilia wakazi wa kisiwa cha Kome Mchangani lipo pia katika visiwa vingine kadhaa vilivyomo kwenye Ziwa Victoria.
Mwanamama Agnes Joseph, mkazi wa kisiwa cha Ikulu alisema kuwa yeye ana watoto watano, na wote amewapeleka kwa mama yake ambako ni katika eneo lisilokuwa la kisiwa wilayani Sengerema ili wasome.

"Huwa ninawatembelea kila baada ya miezi miwili na kuwaachia fedha za matumizi... sitaki wanangu wakose fursa ya elimu," anasema Agnes.
Kiongiozi wa Kisiwa cha Ikulu Baharini, Juma, alisema watoto kukosa elimu na kuishia kuwa wavuvi kwa sababu ya kukosekana kwa shule ni janga kubwa kwao na taifa.

Alisema kwavile serikali inafahamu kwamba kwenye visiwa kuna mamia ya watu ambao ni Watanzania halisi, inapaswa kuchukua hatua sahihi ya kuwajengea shule.

Kiongozi wa Kisiwa cha Ito, Neema Elias, alisema eneo hilo lina wakazi (wavuvi) zaidi ya 500, lakini hakuna shule kwa ajili ya watoto wao.
Aliongeza kuwa tatizo la watoto kukosa elimu kwa sababu ya serikali kutokubali kujenga shule lipo pia katika visiwa vingine vingi miongoni mwa visiwa 35 vilivyopo katika Ziwa Victoria, hasa kwenye eneo la Wilaya ya Sengerema.

Alisema licha ya kukosekana shule katika eneo hilo, lakini pia wamepata maagizo ya serikali kwamba kamwe hawaruhusiwa kuishi kisiwani humo wakiwa na watoto wao.

"Hii siyo sawa.  Wazazi wanapozaa watoto wanalazimishwa kuwaondoa watoto kwa madai kwamba hakuna shule na tunatakiwa kuwapeleka kwa ndugu, jamaa na marafiki walio katika maeneo yenye shule, nje kabisa ya visiwa. Lakini hili limeshindikana... bado tunaishi na watoto wetu na matokeo yake wanakosa elimu," anasema.

OFISA ELIMU, MBUNGE
Akizungumzia tatizo la kukosekana kwa shule, Ofisa mtendaji wa Kata ya Nyakasasa, Mathayo Kanisiro alisema, eneo la visiwa hivyo ni msitu wa hifadhi na kwamba serikali imeagiza pasijengwe nyumba wala jengo lolote la kudumu.

Kanisiro alikiri kwamba hakuna namna ya kufanya, lakini amekuwa akistushwa na ukubwa wa tatizo kwani watoto wanaoishi na wazazi wao katika visiwa hivyo bila kupata haki yao ya msingi ya elimu imezidi kuongezeka.

Diwani wa Kata ya Nyakasasa, Avoid Geogratias, anasema eneo hilo la visiwa wanalokalia wavuvi na familia zao, lilitengwa kwa ajili ya hifadhi ya mistu miaka mingi iliyopita na kwamba, awali, wavuvi waliruhusiwa kuishi huko ili kulinda misitu huo dhidi ya watu waliokuwa wanapasua mbao.

Naye, kama ilivyo kwa Kanisiro, alisema hana namna yoyote ya kuwasaidia watoto hao ili wapate nafasi ya kusoma na kwamba, anajua kwamba watoto wamezidi kuwa wengi kama wanavyoongezeka wazazi wao (wavuvi).

Ofisa Elimu wa Wilaya ya Sengerema, Juma Mwajombe, alisema kuwa siku za nyuma kulikuwa na utaratibu wa wa wazazi kuchangishana fedha kisha kuwapeleka watoto wao kusoma nje ya visiwa. Lakini mpango huo ulifikia mwisho mwaka 2010 baada ya kutokea ajali ya kuzama kwa mtumbwi na wanafunzi 18 walipoteza maisha.

"Baada ya kutokea kwa ajali hiyo, zoezi hilo lilisimamishwa na hadi sasa watoto wengi wameendelea kuishi visiwani bila kupata elimu," alisema Mwajombe, aliyeelezea wasiwasi mwingine kuwa huenda misitu itakuwa hatarini kwa sababu baadhi ya wakazi wa visiwani wataona hakuna haja ya kulinda misitu wakati watoto wao wakikosa elimu kwa kutojengewa shule kwa sababu ya zuio litokanalo na sheria ya kulinda misitu.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Sengerema, Consolata Magaka, alisema serikali inafahamu shida wanayopata wazazi na watoto walio kweney visiwa kama Kome Mchangani, lakini hakuna namna ya kufanya.

Alisema serikali haiwezi kupeleka huduma za shule kwa kuwa wananchi hao wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi wako aktika eneo la hifadhi ya misitu.
Mbunge wa jimbo la Buchosa Wilaya ya Sengerema, Charles Tizeba, aliiambia NIPASHE kuwa, kama kuna mwananchi anayetaka kuendelea kukaa kisiwani (kama Kome) ambako ni hifadhi ya misitu, lazima amuondoe mtoto wake huko na kumrudidisha alikozaliwa ili ampatie fursa ya kusoma.

Alisema hawezi kuwatetea wananchi wake hao kujengewa shule visiwani, kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria ya misitu ambayo inakataza kuwapo kwa majengo ya kudumu.

Akizungumza na NIPASHE, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Focus Majimbi, alisema ni vigumu kujenga shule kwenye kisiwa cha Kome na visiwa vingine vya hifadhi ya misitu kwani sheria inazuia maeneo hayo (ya hifadhi ya misitu) kujengwa majengo ya kudumu. Aliitaja sheria hiyo kuwa ni namba 14, ya mwaka 2002, kifungu cha 26.

Majimbi alikiri kwamba suala la ukosefu wa elimu kwa watoto ni baya na lina athari kubwa. Alisisitiza kuwa, kwa kuzingatia sheria hiyo ya hifadhi ya misitu, maeneo ya visiwa hivyo hayatakiwi kujengwa shule wala jengo lolote la kudumu na kwamba serikali imeagiza kuhamisha watoto wote walioko huko ili wakasome katika maeneo mengine.

Hata hivyo, amri hiyo ya serikali ya kutaka watoto wanaozaliwa huko waondoshwe inakiuka sheria nyingine ya nchi; namba 21 ya mwaka 2009 ambayo inalinda haki za watoto wenye umri chini ya miaka 18.

Wilaya ya Sengerema ina ukubwa wa kilomita za mraba, 8,817 na kati ya hizo, kilomita za mraba 3,335 ni nchi kavu sawa na asilimia 38 na kilomita 5, 832 ni nchi kavu, sawa na asilimia 62.

Kwa mujibu sensa ya watu na makazi ya mwaka 2010, wilaya hiyo ina watu 662,166 na kati ya hao, wanaume ni 335,756 na wanawake ni 326,410.
CHANZO: NIPASHE

Ijumaa, 1 Agosti 2014

Waziri mkuu aagiza kumalizwa kwa tatizo la madawati

Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ameagiza wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha wanamaliza tatizo la uhaba wa madawati katika shule za msingi ifikapo juni 31 mwakani ikiwa ni kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha ili serikali inapoanza mwaka mpya wa fedha shule zote nchini ziwe na madawati ya kutosha.
Waziri mkuu Mizengo Pinda ambaye amewasili jijini Mbeya kwa ajili ya kuhudhuria kongamano ya uwekezaji katika mikoa ya nyanda za juu kusini ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Mbeya ambayo imeonyesha kuwa kuna tatizo kubwa la uhaba wa maawati katika shule za msingi.
 
Aidha waziri mkuu ameonyesha kutoridhishwa na ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi katika mkoa wa Mbeya, ambao mwaka jana wanafunzi wake wamefaulu kwa asilimia 48.5 ikiwa ni chini ya lengo la taifa la ufaulu wa asilimia 60, hivyo akatoa agizo kwa mkoa huo kuhakikisha unaweka mikakati itakayowezesha mwakani wanafunzi kufikia kiwango cha ufaulu ambacho kimewekwa kitaifa.

Waziri mkuu aagiza kumalizwa kwa tatizo la uhaba wa madawati

Waziri mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda ameagiza wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha wanamaliza tatizo la uhaba wa madawati katika shule za msingi ifikapo juni 31 mwakani ikiwa ni kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha ili serikali inapoanza mwaka mpya wa fedha shule zote nchini ziwe na madawati ya kutosha.
Waziri mkuu Mizengo Pinda ambaye amewasili jijini Mbeya kwa ajili ya kuhudhuria kongamano ya uwekezaji katika mikoa ya nyanda za juu kusini ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Mbeya ambayo imeonyesha kuwa kuna tatizo kubwa la uhaba wa maawati katika shule za msingi.
 
Aidha waziri mkuu ameonyesha kutoridhishwa na ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi katika mkoa wa Mbeya, ambao mwaka jana wanafunzi wake wamefaulu kwa asilimia 48.5 ikiwa ni chini ya lengo la taifa la ufaulu wa asilimia 60, hivyo akatoa agizo kwa mkoa huo kuhakikisha unaweka mikakati itakayowezesha mwakani wanafunzi kufikia kiwango cha ufaulu ambacho kimewekwa kitaifa.