Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 13 Februari 2014

madiwani watafuta mbinu za kutokomeza ziro


MADIWANI wa Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama, wamehoji  watoto wanaosoma na kumaliza katika shule za sekondari za kata huku wengi wao wakiambulia kupata alama sifuri na kusababisha kubaki vijijini bila mwelekeo wa maisha.
Hoja hiyo ilikuja katika kikao cha baraza lao la madiwani wa halmashauri hiyo baada ya Diwani wa Chona, Mohamed Mwarabu (CHADEMA) kuhoji mpango wa kuwanusuru vijana hao ambao wengi wamejiingiza katika usanii wa nyimbo zisizokuwa na tija.
Mwarabu alisema sifuri kwa wanafunzi hao ni ukosefu wa walimu kwenye shule hizo  na hata wale wenye masomo ya Kilimo, Kiswahili na Kiingereza hawapo, hali inayofanya wanafunzi hao wamalize elimu ya sekondari sawa na wale waliomaliza darasa la saba.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Isabela Chilumba, alidai wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kupata alama sifuri hawako sawa na waliomaliza darasa la saba.
Chilumba alisema faida ya mwanafunzi aliyesoma sekondari ni nyingi, ambazo si kufaulu peke yake na kuwa hata kuanza maisha atakuwa na umri mkubwa kuliko yule wa darasa la saba ambaye huanza kupambana na maisha akiwa na umri mdogo.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Tabu Katoto, aliwataka madiwani hao suala la ukosefu wa walimu lisiwakatishe tamaa ya kusimamia ujenzi wa sekondari nyingine, kwani suala hilo litamalizika, kwa kuwa kila mwaka serikali inaajiri walimu.
Katoto alisema halmashauri yake inatarajia kufungua sekondari tatu katika mwaka huu wa fedha, mwaka 2014/2015 katika kata za Igunda, Nyankende na Sabasabini.