Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumanne, 24 Septemba 2013

kurejea kwa elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne kwa shule kongwe

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Serikali imeanza kushughulikia utaratibu wa kurejesha utoaji wa elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne, katika baadhi ya shule kongwe nchini ili kurudisha ufaulu uliokuwepo na kuimarisha malezi ya watoto kuanzia elimu ya chini.

Jumamosi, 21 Septemba 2013

CCM yatoa miezi 6 kwa waziri wa Elimu kujiuzulu....Vinginevyo itamtimua kwa nguvu




CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kujiuzulu kwa kushindwa kulipa madeni ya walimu nchini.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pia ametoa muda wa miezi sita kwa Waziri huyo na Naibu wake Philip Mulogo kutekeleza hilo agizo hilo vinginevyo chama kitawatumia wabunge wake kuwatimua kwa nguvu.

Kwa mujibu wa taarifa za madeni zilizokusanywa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), hadi sasa walimu wanadai malimbikizo yao ya Sh bilioni 49 ambayo hajalipwa na Serikali.

Kinana alikuwa akihutubia mikutano ya hadhara jana katika wilaya za Bariadi na Busega.

Alisema CCM haiko tayari kuona walimu wakinyanyaswa wakati wana madai ya msingi.

Hivi sasa imejengeka tabia kwa baadhi ya mawaziri na watendaji wa wizara ya kuwadharau walimu na hata kuwanyanyasa huku wengine wakishusha utu na heshima ya walimu kwa kuwatukana, alisema.

Kinana ambaye yupo katika ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa alisema kwa mawaziri kushindwa kutatua kero za walimu, imefika wakati wahusika waondoke wenyewe na wasipofanya hivyo chama kitawaagiza wabunge wake wawafukuze kwa nguvu.

“Ninatoa muda wa miezi sita kwa Waziri wa Elimu na wasaidizi wake wakiwamo watendaji kuhakikisha wanalipa madeni ya walimu haraka. Haiwezeni hii ni nchi ya watu wote wakiwamo walimu wadharauliwe na hata kunyanyaswa kwa maneno ya matusi

“Hili hapana CCM haiko tayari kuona walimu kila siku wakipigwa danadana kutokana na uzembe wa watu waliokabidhiwa dhamana za kuongoza sekta ya elimu katika nchi yetu,” alisema.

MTANZANIA ilimtafuta Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch ambaye alisema hadi sasa madeni ya walimu yamefikia Sh bilioni 49 ambayo ni malimbikizo ya mishahara na mapunjo.

“Kila mara tunawaambia kuwa ni vema Serikali itafute Sh bilioni 100 katika fungu la dharura ili iweze kulipa madeni ya walimu na iachane nao lakini hawasikii,” alisema Oluoch.

Source: Mtanzania

Chikombe: Shule yenye walimu watatu wanafunzi 300

Nikiwa ziarani mkoani Lindi nafanikiwa kupita katika shule mbalimbali za msingi na sekondari. Lengo hasa lilikuwa ni kuangalia mazingira halisi ya shule hizo kama yanaweza kuleta tija kwa siku za baadaye?

Shule ya msingi Chikombe ndiyo kambi yangu ya kwanza katika ziara hii. Kwa kutumia usafiri wa pikipiki nafanikiwa kufika shuleni hapa saa tano asubuhi, nikitokea Lindi Mjini.

Mbele yangu ni uwanja mkubwa wa nyasi ukiwa na miti michache ya miembe. Kuna wanafunzi wachache wakiwa wamezagaa katika eneo hilo wakicheza mpira. Hii inaashira kuwa wako kwenye muda wa mapumziko.

Kadiri ninavyosogea nazidi kuwa karibu na majengo ya shule mbele yangu. Ni majengo mawili yenye hali tofauti. Moja ni jengo lenye madarasa mawili na ofisi moja ndogo ya walimu linaloonekana kuwa jipya kidogo.

Pia jingine ni jengo kuukuu lililojengwa kwa udongo na miti. Kwa kulitazama jengo hili unaweza kulifananisha na zizi la ng’ombe ama stoo ya kuhifadhia vifaa vya kilimo. Jengo hili lina vyumba vitatu vinavyotumika kama madarasa.

Upana wa chumba kimoja cha jengo hilo unaweza kuwa ni urefu wa madawati mawili na uchochoro wa kupita mtu mmoja katikati.

Wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza, la pili la tatu na la nne hutumia madarasa haya kama sehemu yao ya kusomea.

Kwa muda huu nilioingia nakuta wanafunzi wa darasa la kwanza wakiwa katika maandalizi ya kutoka shule.

Nafika kwenye ofisi ya walimu kwa ajili ya kujitambulisha na kupata mwenyeji wangu, ambaye ningepata mawili matatu kuhusiana na shule hiyo iliyo katika Wilaya ya Lindi Vijijini Jimbo la Mtama.

Mwalimu Hassan Halfan (54) ndiye alikuwa wa kwanza kukutana naye. Yeye ni mmoja kati ya walimu watatu katika shule hiyo. Kama ilivyo ada ya mgeni na mwenyeji alianza kwa kunipa historia ya shule yake.

“Shule ya Chikombe ilianza rasmi mwaka 2008 ikiwa na mwalimu mmoja ambaye ni mimi mwenyewe, nikiwa peke yangu niliweza kufundisha kwa miaka miwili bila usaidizi hadi mwishoni mwa mwaka 2009, alipokuja mwalimu mwenzangu,” alisema.

Mwaka 2010 idadi ya walimu iliongezeka na kufikia walimu watatu ambao tupo pamoja hadi hivi sasa.Changamoto kuu zinazoikabili shule hii

Kama ilivyo kwa shule nyingi zilizo katika Mkoa wa Lindi, Shule ya Chikombe inakabiliwa na matatizo lukuki kiasi cha kushindwa kujiendesha ipasavyo.Mradi pekee unaotegemewa katika shule hii ni ule wa shule ya awali, ambapo wazazi hulazimika kuwalipia watoto Sh300 kama ada ya mwanafunzi mmoja kwa mwezi.

“Pamoja na kuwekwa kwa kiasi kidogo cha ada, wazazi wanashindwa kuilipa na hivyo kuzidi kutupa wakati mgumu,” anasema mwalimu Halfani.

Anasema uchache wa walimu nalo ni tatizo linguine, ambapo walimu watatu waliopo wanalazimika kufundisha wastani wa vipindi 64 hadi 75 kwa wiki.
Jambo hili kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwapa mtihani walimu hao na hata kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

“Uchache wa walimu umekuwa ukikwamisha maendeleo ya shule yetu kwa kiasi kikubwa sana. Lakini ukiachikia mbali uchache huo, hapa shuleni kwetu kuna uhaba wa nyumba za walimu,” anasema.

“Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, tulilazimika kuwaondoa wanafunzi katika darasa moja ili kumpisha mwalimu mkuu ambaye alikuwa hana nyumba ya kuishi,” anasema mwalimu Halfan.

Jambo hilo lilisababisha msongamano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa, kwani madarasa manne yalilazimika kutumiwa na mikondo saba na wengine ilibidi wafundishiwe nje ya madarasa anasema mwalimu huyo.

Baada ya kuona ukubwa wa tatizo hilo, wanakijiji waliingilia kati na kwa pamoja walishirikiana kujenga nyumba moja ya mwalimu mkuu, ili kuwapa wanafunzi nafasi ya kushiriki masomo darasani.
mwananchi.co.tz

Alhamisi, 19 Septemba 2013

wasichana 11 shule ya msingi wapata mimba

WASICHANA 11 wa shule ya msingi iliyo Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay, wamepatikana kuwa wajawazito. Wanafunzi hao wa Shule ya Msingi ya Rangenya, iliyo karibu na Ndhiwa mjini wanajumuisha msichana mwenye miaka kumi aliye katika darasa la saba. Wawili kati yao tayari wananyonyesha watoto baada ya kujifungua hivi majuzi.

Wasichana wawili wako katika darasa la saba, huku kukiwa na mmoja katika darasa la nne na mwingine darasa la tano.Duru za kuaminika zilisema waliohusika kuwapachika watoto hao mimba ni mwalimu aliyeajiriwa na Chama cha Walimu na Wazazi (PTA), waendeshaji boda boda na vijana wanaotoka katika vijiji vya karibu.

Mwalimu huyo ambaye ni jamaa ya mmoja wa walimu wenye vyeo vikuu shuleni humo alipelekwa hadi kituo cha polisi mwaka jana, kwa kudaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa wanafunzi aliye katika darasa la saba.

Shughuli katika shule hiyo zilisitishwa kwa muda Jumanne baada ya Mkuu wa Elimu katika wilaya hiyo Maurice Jayora, na maafisa wake walipowasili kuanzisha uchunguzi.
Maafisa hao walitumia saa kadha asubuhi kuhoji walimu na wanafunzi kuhusu tukio hilo.

Mkuu huyo wa elimu aligutushwa na hali kuwa wasimamizi wa shule hiyo hawajawahi kufahamisha afisi yake wala ile ya afisa wa elimu katika eneo hilo kuhusu matukio hayo.“Nataka ifahamike kuwa mimi na maafisa wangu, tulifahamu kuhusu tukio hili kupitia vyombo vya habari. Hata afisa wa elimu katika eneo hili hakujulishwa,” alisema.

Masomo

Alithibitisha kuwa baadhi ya wasichana walioathirika bado wanaendelea na masomo na wanasaidia kwenye uchunguzi.“Baadhi ya waathiriwa ambao bado wako shuleni wanatupatia habari muhimu zitakazosaidia kwenye uchunguzi tunaofanya,” alisema.

Juhudi za kukabiliana na matukio kama haya pamoja na kuozwa kwa wasichana wenye umri mdogo katika maeneo ya Ndhiwa na Homa Bay hazijafua dafu kutokana na ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa wazazi. Uchunguzi umebainisha kuwa wakati wowote wanaohusika wanapokamatwa, baadhi ya wazazi huingilia kati na kupendelea kutohusisha mahakama kutatua masuala hayo.

Naibu wa Kamishna wa Kaunti Geoffrey Omonding amekuwa akionya maafisa wa utawala kuhusu athari iliyopo ikiwa matukio kama haya yatapatikana kuwa yanatokea katika maeneo wanayosimamia.

Jumanne, 17 Septemba 2013

CHAMA CHA HISABATI TANZANIA CHAPINGA (multiple choice) MITIHANI YA TAIFA YA HISABATI

CHAMA cha Hisabati Tanzania (MAT) kimeitaka Serikali kuliagiza Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), kuondoa mfumo wa majibu ya kuchagua (multiple choice) kwenye Mitihani ya Taifa ya Hisabati kwa shule za msingi nchini. MAT imesema mfumo huo unapunguza uwezo wa kufikiri na kutafuta majibu sahihi kwa wanafunzi na kusababisha taifa kupoteza vipaji vya somo hilo na kushusha viwango vya ufaulu nchini.
Mwenyekiti wa MAT, Dk. Sylvester Rugeihyamu alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa chama hicho jijini Mbeya.Dk. Rugeihyamu alisema mfumo huo hauna athari za kufikiri kwa mantiki kwa wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu lakini unapunguza uwezo wa kufikiri kwa wanafunzi wa shule za msingi kwa sababu bado wanahitaji mazoezi mengi ya kukuza uwezo wao wa akili.
Alisema mfumo huo unawafanya wanafunzi kubahatisha majibu badala ya kutumia uwezo wao wa akili hali inayodumaza vizazi vya Tanzania katika kumudu masomo yanayohitaji umakini wa fikra.
“Inawezekana huu mfumo ulianzishwa kwa lengo la kubana matumizi, lakini utadumaza watoto na taifa zima litarudi nyuma katika elimu, kwa kweli huu mfumo siyo mzuri kwa watoto wadogo,” alisema.
Dk. Rugeihyamu aliitaka NECTA na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuchukua hatua za kuacha matumizi ya mfumo huo kuliokoa taifa na hatari ya kuwa na vijana wasiokuwa na uwezo mzuri katika taaluma.
Dk. Rugeihyamu alisema mfumo huo pia umechangia kushuka kiwango cha ufaulu kwa somo la hisabati nchini tangu ulipoanza kutumika mwaka 2011 ambako kiwango cha ufaulu kilikuwa ni asilimia 39.36 lakini kikashuka hadi asilimia 18.74 mwaka 2012.
mtanzania.co.tz

Jumamosi, 14 Septemba 2013

JE MBUNGE WAKO ANAITHAMINI ELIMU

Agosti 11, 2013 tulifungua shule mpya ya msingi katika eneo la Kwebamba jimboni Bumbuli ambayo tumekamilisha ujenzi wake kwa juhudi za pamoja na wananchi. Kabla ya ufunguzi wa shule hii watoto walikuwa hawaendi kabisa shule katika eneo hili. Changamoto ni kuufanya mradi huu kuwa bora zaidi hasa kuwa na uwiano sahihi wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40 kwa darasa.

Agosti 11, 2013 tulifungua shule mpya ya msingi katika eneo la Kwebamba jimboni Bumbuli ambayo tumekamilisha ujenzi wake kwa juhudi za pamoja na wananchi. Kabla ya ufunguzi wa shule hii watoto walikuwa hawaendi kabisa shule katika eneo hili. Changamoto ni kuufanya mradi huu kuwa bora zaidi hasa kuwa na uwiano sahihi wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40 kwa darasa.
Ongeza kichwa

Jumanne, 10 Septemba 2013

MTIHANI DARASA LA SABA


SERIKALI mkoani Singida imesema haitasita kuwachukulia hatua wazazi watakaobainika kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu.

Inadaiwa kuwa baadhi ya wazazi hususani wale wa makabila ya wafugaji wamekuwa wakiwaambia watoto hao kuchora picha za ng’ombe kwenye mtihani badala ya kuandika majibu ili wasifaulu na kuchaguliwa kuingia Sekondari kwa ajili ya kuchunga mifugo na wasichana kuolewa.

Katika kipindi ambacho wanafunzi wa madarasa mengine wako majumbani kwa ajili ya likizo fupi, maandalizi yote muhimu kwa wale wanaofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yamekwisha kamilika.

Hata hivyo licha ya kuwaandaa vyema wanafunzi wao, baadhi ya walimu wanaonekana kuwa na hofu ya kufaulisha kutokana na kuwepo tuhuma za wazazi kutotaka watoto wao waingie Sekondari.

Katika moja ya mikutano ya hadhara kuhimiza shughuli za maendeleo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama anakiri kuwa tatizo hilo limekuwa sugu na kuathiri kiwango cha elimu mkoani Singida.

Pamoja na kukemea Mkuu huyo wa wilaya ya anatoa msimamo wa Serikali juu ya wazazi wa aina hiyo.
Singida ni moja ya mikoa ambayo imefanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba kwa miaka mitatu mfululizo baada ya kufaulisha chini ya asilimia 50, pamoja na mambo mengine moja ya sababu ikitajwa kuwa baadhi ya wazazi kutopenda wala kujua umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

Alhamisi, 5 Septemba 2013

WATANZANIA WATOA MAONI YAO TOVUTI YA WIZARA YA ELIMU



Ukifungua tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, pembeni kushoto kuna sehemu ya kupiga kura ya maoni kuhusu hali ya elimu nchini. Kwa maoni yaliyopo mpaka sasa, asilimia 42 ya waliotoa maoni yao-wana mtazamo kuwa hali ni mbaya; wakifuatiwa na asilimia 35 wenye mtazamo kwamba 'kuna kitu hakiko sawa'. Maoni hayo yasiyo ya kuridhisha-yanayofikia asilimia 77 yametumwa na wananchi na wadau mbalimbali wa elimu kwenye tovuti ya wizara ya elimu. Je, wizara inayatumiaje maoni haya ya wadau? Big Result ndiyo jawabu?

Jumanne, 3 Septemba 2013

KUWAFUKUZA WANAFUNZI WA KIKE WANAOPATA MIMBA NI KUKATISHA NDOTO ZAO


 
Hukumu ya hivi karibuni ya mahakama ya kikatiba imethibitisha kwamba shule haziwezi kuwafukuza wanafunzi kwa kupata uja uzito.Lakini Afrika Kusini bado inang'ang'ana kukabliana na suala hilo linalowaathiri wasichana 180,000 kila mwaka.


Daktari Jay-Anne Devjee ambaye ni mkuu wa afya ya akina mama katika hospitali ya King Dinuzulu anasema kwa mara nyingi hulazimika kuwazalisha wasichana kwa njia ya upasuaji, jambo linaloongeza hatari ya kuvuja damu na kuhatarisha maisha ya wazazi hao.
Msichana mwenye umri mdogo zaidi hapa ana umri wa miaka 14 na anaonekana kuzidiwa na uchungu wa uzazi kiasi cha hata kushindwa kuongea.
Phumla Tshabalala, mwenye umri wa miaka 16, anamshikilia mwanawe mchanga aliye na umri wa siku moja.Hii ni mara yake ya kwanza kujifungua na anasema ana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kumlea mwanawe peke yake.
Anaeleza hajamuona mpenzi wake kwa muda mrefu na licha ya kumuarifu kwamba amejifungua, hakuna mtu kutoka familia ya mpenzi wake aliyekuja kumjulia hali.
Anatoka katika familia maskini, Babake ndiye anayeilisha familia. Yeye ni binti wa mwisho kati ya mabinti watatu na wa kwanza aliyejifungua mtoto, jambo ambalo familia yake bado haijalipokea vyema.
Inakisiwa kuwa kila mwaka wasichana zaidi ya laki moja na themanini nchini Afrika Kusini hushika ujauzito. 180 kati ya wengine 1000, hupata kuwa wajawazito. 36% ya wasichana wenye mimba hufariki kila mwaka kulingana na takwimu za nchi hiyo wakati wanapojifungua.
Mifuko yao ya uzazi huwa bado haijakuwa vyema kiasi cha kubeba mimba na wengi huwa na wakati mgumu sana wanapojifungua , kulingana na daktari Jay-Anne Devjee.
Phumla anapanga kurudi shuleni kwa wakati muafaka ili aweze kufanya mtihani wa mwisho wa mwaka , lakini ana wasiwasi kuhusu vipi atakavyoweza kutimiza majukumu yote mawili ya kuwa mwanafunzi na mzazi pia.

Anasema laitani angesubiri hadi angekuwa mkubwa.

Lakini anajiona kuwa mwenye bahati kwa kuwa yeye na mwanawe ni wazima na wenye afya.
Madakatari wanasema kuna hatari ya kuzaa ukiwa una umri mdogo. Kwa mujibu wa baraza la utafiti wa sayansi ya binaadamu, viwango vya akina mama wanaofariki ni kubwa kwa wasichana kwa asilimia 36 ya vifo katika uzazi kila mwaka licha ya kwamba ni asilimia 8 pekee ya vifo hivyo ndivyo vinavyoripotiwa.
Utafiti unaashiria kwamba wasichana wengi hulazimika kuacha masomo ili kuwalea watoto wao na wengi wao hukosa kurudi kusoma baadaye.
Maafisa wa elimu wanasema katika shule ya upili wa Intshisekelo nje ya mji wa Durban, zaidi ya wasichana 20 walipachikwa mimba katika nusu ya kwanza ya mwaka.
Maafisa nchini humo wana wasiwasi kwamba huenda kushiriki kwa vijana katika ngono bila ya kinga kukaathiri vita dhidi ya HIV/Ukimwi. Mwalimu mmoja anasema mimba ni miongoni mwa sababu kuu pamoja na umaskini zinazochangia nusu tu ya wanafunzi wa kike kumaliza shule.
Kwa mujibu wa sheria, shule hazipaswi kufichua ni wanafunzi gani waja wazito na inasema baadhi ya wasichana huwa na kibarua kigumu cha kificha matumbo yao yanayozidi kukuwa ikwemo kuvaa nguo kubwa na pia kubeba mabegi yao ya shule mbele.
Sheria hiyo ya mwaka 1996 inasema wanafunzi hawapswi kufukuzwa kwa kuwa ni waja wazito lakini shule zinasema wanalazimika kuwafukuza kwa sababu hazijapewa mafunzo ya namna ya kuwasaidia wasichana hao waja wazito.