Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumapili, 1 Desemba 2013

Serikali kusaidia mikakati ya taasisi zinazosaidia elimu

Naibu Katibu Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zuberi  Samatama, amesema serikali itasaidia mikakati inayoibuliwa na taasisi mbalimbali za kiserikali katika kuboresha elimu ya msingi nchini.
 
Samatama alisema hayo, wakati akizindua kampeni ya uboreshaji wa elimu ya msingi Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam, inayofahamika kama Mnazi mkinda.
 
Alisema kampeni hiyo ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha wanafunzi wanakuzwa vipaji walivyozaliwa navyo, ni jambo la kuigwa kwani itawafanya watoto kuhudhuria masomo kwa muda wote.
 
Alisema serikali itahakikisha inaanzisha tuzo maalum kwa walimu wabunifu kwa ajili ya kuwapa moyo na kuwatambua.
 
"Kitu hiki mlichokibuni kitasaidia sana katika kuhakikisha wanafunzi wanapenda kusoma kwa sababu watatambua kile wanachokipenda kipo kwenye shule zao," alisema Samatama.
 
Alisema katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), umesababisha ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba kutoka kiwango cha asilimia 5.6 hadi silimia 75, mwaka jana.
 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Mwenda Hasara Maganga, alisema kampeni ya Mnazi mkinda, itawavutia watoto kwa kupenda shule na kuacha tabia ya ukwepaji.
"Kwa ujumla tatizo la machimbo halitakuwepo kwa sababu kila mtoto atapata kile anachopenda," alisema.
 
Baadhi ya vipaji vitakavyokuzwa katika kampeni hiyo ni pamoja na Hisabati, Sayansi, Teknohama, Dini na Sanaa ya maigizo, ngoma, muziki na sarakasi.
 
Afisa Elimu ya Msingi wa Manispaa hiyo, Elizabeth Thomas, alisema kampeni ya Mnazi mkinda imesambazwa kwenye shule zote pamoja na kuandaa kituo maalumu cha ukuzaji vipaji katika shule ya msingi Mnazimmoja.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

halmashauri Mbozi yashindwa kulipa pesa ilizowakopa walimu sh.milioni 200


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia
 
Chama cha walimu wilaya ya Momba na Mbozi, kimemuomba Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuwasaidia walimu kulipwa fedha zao zaidi ya Sh. milioni 200 walizokopwa na halmashauri ya wilaya ya Mbozi.
 
Fedha hizo zilikopwa kwa walimu mapema mwaka huu, zilikuwa michango ya walimu waliyokuwa wakikatwa kutoka kwenye mishahara yao kwa ajili ya kuweka akiba kwenye Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS).
 
Akiwasilisha malalamiko hayo kwa niaba ya walimu wote,  alisema walimu hao waliambiwa na halmashauri kuwa fedha hizo zimetumika kwa ajili ya shunguli zilizo nje ya shughuli za walimu.
 
Awali walimu hao wilaya ya Mbozi na Momba walikuwa wilaya moja kabla ya kugawanywa na kuwa mbili. Walipotaka kufahamu kuhusu fedha hizo waliambiwa zimetumika kuandaa sherehe za wafanyakazi (Mei Mosi) ambazo mgeni rasmi alikuwa Rais Jakaya Kikwete.
 
Wakionyesha kukata tamaa na madai ya malimbikizo ya madeni wanayoidai serikali zaidi ya shilingi bilioni moja kwa wilaya hiyo, pia walizidi kuvunjika moyo baada ya kutaka kuwasilisha kilio chao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia, na kukataa kuwasikiliza kwa madai kuwa serikali imeshamaliza matatizo yao.
 
Katika taarifa iliyosomwa na Nyanguye ilisema kuwa, Ghasia alimkataza Katibu wa Chama Cha Walimu, Emilia Mwakyoma aliyekuwa akisoma taarifa kwa kumtaka akae chini mara moja kwani hawezi kusikiliza madai ambayo yameshamalizwa.
 
Alisema hali hiyo ilisababisha walimu kushindwa kuwasilisha malalamiko yao siku hiyo, na hivyo kulazimika kuyawasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM, Kinana ili kuomba msaada kama wanaweza kusaidiwa.
 
“Tumekuja tu kujaribu kama tunaweza kusaidiwa kwani walimu tumeshasahaulika sana. Licha ya kusahaulika pia tunanyang’anywa haki zetu za msingi na Serikali na hatujui kama tutazipata na wala hatuoni wakumlalamikia tena zaidi ya kuishi kwa matumaini," alisema Nyanguye.
 
Akijibu malalamiko yao kwa mshangao, Katibu Mkuu CCM, Kinana alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Charles Mkombachepa kueleza matumizi ya fedha hizo za walimu, ambazo zinadaiwa kutumika kuandaa sherehe bila ya wakopwaji kutaarifiwa chochote.
 
“Unachotakiwa Mkurugenzi ni kuwaeleza walimu fedha zao umezitumia kufanyia nini, angalia bado wakiwa wana machungu ya madeni wanayoidai serikali, hivi serikali inatakiwa kukopa au kukopwa na tangia lini Mei Mosi zikaandaliwa na walimu? " alihoji Kinana.
 
Akijibu tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Mkombachepa, alikiri kutumia fedha hizo lakini kwa ajili ya kulipia huduma zilizotolewa na taasisi mbalimbali wilayani hapo.
 
"Katibu Mkuu, kweli fedha hizo zilitumika, lakini si kwa ajili ya Mei Mosi bali zilitumika kuandaa usafiri, kurekebisha magari na shughuli nyingine ambazo hazihusiani na walimu moja kwa moja," alisema Mkombachepa.
 
Mkombachepa, aliomba kuzilipa fedha hizo ndani ya miezi miwili kuanzia Desemba na kumaliza mwezi Januari mwakani, taarifa ambayo ilizidi kumkasirisha Kinana.
 
Kwa fedheha kubwa Kinana, alimtaka Mkurugenzi huyo kuacha kuwafanyia walimu usanii kwenye fedha zao ambazo wamezipata kwa taabu na kuagiza walimu hao kulipwa fedha zao haraka iwezekanavyo.
 
Aidha Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Asha Rose Migiro, aliahidi kuyashughulikia matatizo ya walimu kwa kufikisha taarifa za matatizo yao, ikiwamo malimbikizo  ya madeni wanayoidai serikali kwa viongozi wanaohusika.