Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 4 Septemba 2014

Shule nyingi za msingi nchini zakabiliwa upungufu madawati

baadhi ya wanafunzi shule ya msingi mwisenge wakiwa wamekaa sakafuni
Shule nyingi za msingi zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati, hali inayotishia maendeleo ya elimu nchini.

Wakizungumza kwa njia ya simu kwa nyakati tofauti na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One Stereo, wakuu wa mikoa ya Iringa, Dodoma, Morogoro na Tanga, walithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo katika mikoa yao.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, alisema kwa njia ya simu kuwa licha ya mkoa wake kuwa unazalisha miti mingi ya mbao na uwapo wa shamba la miti la Taifa (Sao Hill), upungufu wa madawati upo, ingawa si mkubwa ukilinganisha na mikoa mingine.

Alisema tayari serikali ya mkoa wake imeshaanza kujipanga mapema kulikabili tatizo hilo hata kabla ya tamko la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku mkoa huo ukijiwekea mikakati ya kuhakikisha unatekeleza agizo hilo mapema mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, alisema mkoa wake una upungufu wa madawati kwa asilimia zaidi ya 40 kutokana na kutokuwa na vyanzo vizuri vya miti ya mbao suala, ambalo limekuwa ni changamoto kubwa.

Alisema ili kufikia malengo, wameanza na kuimarisha mfuko wa elimu na kwamba, wameweka utaratibu wa wilaya kuchangia Sh. 10,000 na nyingine kuchangia Sh. 5,000, kupitia mifugo ya kuku wanaopatikana kwa wingi katika mkoa huo.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alikiri mkoa wake kukabiliwa na uhaba mkubwa wa madawati, hasa katika shule za msingi na kwamba, kwa tathmini waliyoifanya ni upungufu wa kiasi cha madawati 91,000 kwa wilaya zote mkoani humo.

Tatizo la uhaba wa madawati limekuwa ni changamoto kubwa nchini kiasi cha kumfanya Pinda kutoa tamko la kuwataka wakuu wote wa mikoa kuhakikisha kila mmoja anamaliza tatizo hilo ifikapo Juni 30, 2015.

chanzo ippmedia,
picha. marafiki wa elimu musoma