Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 18 Desemba 2013

Serikali yagomea CWT kuhusu kima cha chini cha mishahara


 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.Shukuru Kawambwa


Serikali  imesema haiwezi kuongeza vianzio vya mishahara kwa asilimia 53 kama Chama cha Walimu Nchini (CWT) kinavyotaka kwa kuwa fedha hizo ni zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Bungeni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso (Chadema).

Pareso alitaka kujua ni lini serikali italipa malimbikizo ya walimu yakiwamo yanayotokana na kupandishwa madaraja.

Pia alihoji serikali inapata kigugumizi gani kulipa nyongeza ya asilimia 50 ya mishahara kwa kadiri walivyokubaliana na CWT.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kufahamu mpaka sasa serikali imeshughulikiaje madai ya stahili za walimu hapa nchini.

Akijibu maswali hayo,  Dk. Kawambwa alisema serikali imejipanga kuondokana na madeni ya walimu.

Alisema zoezi linaloendelea hivi sasa ni uhakiki wa madeni ya serikali kwa ushiriki kikamilifu na CWT.

Hata hivyo, alisema madai ambayo CWT yaliyotaka nyongeza ya asilimia 53 kwa vianzia vya mishahara yanazidi bajeti ya mishahara yote ya watumishi wa serikali nchin.Kwa msingi huo alisema hakukuwa na namna ambayo serikali ingelipa.

Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikiongeza mishahara kwa walimu ambapo mpaka sasa imeshaongeza asilimia 30.9.

Aidha, alisema serikali na CWT wanaendelea na majadiliano kuhusiana na madai hayo ya walimu na tayari vikao vinane vimefanyika.

“Katika vikao hivyo, serikali iliahidi kutoa nyongeza ya wastani wa asilimia 14.62 ya vianzia vya mishahara ya walimu wakati CWT walishuka kutoka asilimia 100 hadi asilimia 53 ya nyongeza waliyokuwa wanadai,” alisema.

Chanzo Ippmedia.com