Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 19 Machi 2014

madarasa walimu na vitabu bado changamoto

Shule ya sekondari Tongoni mkoani Tanga ina majengo mazuri, walimu 12, maabara, vitabu lakini kitaifa inashika nafasi ya tatu kutoka mwisho katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana. Shule hiyo, ina walimu 12 wengi wao wakiwa na elimu ya kiwango cha shahada ya elimu. Ina madarasa manane, madawati kwa kila mwanafunzi, maabara na vitabu vya kutosha. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 haijafaulisha mwanafunzi hata mmoja kwa kiwango cha daraja la kwanza, la pili wala la tatu. Daraja la kujivunia kwa shule hiyo kwenye mitihani ya kidato cha nne ni la nne na sifuri kwa watahiniwa wake. Sasa shule hiyo ina wanafunzi wapatao 123 kati yao wasichana ni 52 na wavulana 71. “Ni wanafunzi watatu tu kati ya 47 walioweza kufaulu mtihani wa kidato cha pili mwaka juzi … shule ikalazimika kuwatafutia wanafunzi hao shule nyingine ili waendelee na masomo. Waliobaki wakalazimika kurudia kidato cha pili,” alisema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mfaume Juma. Mwalimu Juma anasema mwaka jana, watahiniwa wa kidato cha nne walikuwa 37 wanafunzi saba kati yao hawakupata matokeo yao kwa kushindwa kukamilisha ada ya mtihani na 28 wakaambulia daraja sifuri. Ni wawili tu walipata daraja la nne. “Mwaka jana wanafunzi 28 walipata daraja sifuri katika mtihani wa kidato cha nne, saba matokeo yao yalizuiwa na Baraza la Mitihani la Taifa kwa kushindwa kulipa ada ya mtihani,” anasema Mwalimu Mkuu huyo. Miongoni mwa changamoto zinazoikabili shule hiyo, Mwalimu Mkuu anazitaja kuwa ni mwamko mdogo wa baadhi ya wazazi kuhusu umuhimu wa elimu hasa ulipaji wa ada na michango ya shule bado ni tatizo kubwa. Hatua hiyo, anasema inasababisha shule hiyo kushindwa kujiendesha kikamilifu asilimia 75 ya wanafunzi wanadaiwa ada. Changamoto nyingine ni ukosefu wa nyumba za walimu na mabweni kwa wanafunzi. Asilimia 70 ya wanafunzi wa shule hiyo huishi nje ya eneo hilo. “Kutokana na ukosefu wa nyumba za walimu na mabweni kwa wanafunzi baadhi ya wanafunzi wanachelewa kufika shule… kuna wanafunzi wanaoishi katika kisiwa cha Mwarongo ambacho ili kufika ng’ambo ya pili lazima wavuke kwa mashua.Wakati mwingine hutegemea hali ya upepo wa bahari siku ukivuma vibaya watoto wanashindwa kufika shuleni,” anafafanua Mwalimu Juma. Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wanasema, wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo kwa wakati au kuchelewa hasa siku ambazo hali ya upepo wa bahari ukiwa mbaya. “Mimi huwa naamka nyumbani saa 11 alfajiri, kuosha vyombo na kuchota maji baada ya hapo najiandaa kwenda shule, lakini ukifika Kivukoni ni lazima usubiri maji yajae ndiyo chombo kiweze kuvuka. Siku ambazo upepo ni mbaya mara kadhaa tulishawahi kuzama, hali iliyotulazimu baada ya kunusurika turudi nyumbani badala ya kwenda shule. Hii inatuumiza na kutuathiri sana kimasomo,” anasema Mariam Hassan mwanafunzi wa kidato cha kwanza shuleni hapo. Naye Zuberi Hamid, mwanafunzi wa kidato cha tatu shuleni hapo anasema, imekuwa ni kama kawaida kwao kutohudhuria vipindi viwili vya kwa asubuhi kutokana na hali ya usafiri kuwa ya mashaka na kimsingi hali hiyo imekuwa ni njia mojawapo inayochangia kufeli masomo yao. “Muda tunaoingia shuleni ni saa nne asubuhi unakuta vipindi viwili vya mwanzo vimekamilika. Pia muda tunaotoka shule nao hadi kuvuka na kufika nyumbani tunachelewa.Tukifika nyumbani muda unakuwa umekwenda sana hata fursa ya kujisomea inakuwa finyu sana, “ anasema Hamid. Baadhi ya walimu wanasema , shule hiyo yenye walimu 12 kati yao hakuna waliobobea katika masomo ya Biolojia, Fizikia na Hisabati hali inayowalazimu wanafunzi kufanya mitihani ya masomo hayo bila kufundishwa. “Kwa sababu ya kutokuwa na walimu wa Physics,Hesabu na Biology wanafunzi wanalazimika kufanya mitihani bila kufundishwa masomo hayo hili nalo ni tatizo sana,” anasema Thomas Simengwa, Mwalimu wa somo la Historia na Kiswahili katika shule hiyo. Omary Bushiri ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Tongoni anakiri kuwepo mwamko mdogo wa wazazi katika uchangiaji wa sekta ya elimu kijijini hapo sambamba na mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya wanafunzi wa shuleni hiyo. Bushiri ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, anasema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo pamoja na mambo mengine ni mawasiliano duni kati ya uongozi wa shule, wazazi na wanafunzi. “Ni ukweli kabisa kwamba maendeleo ya shule ya sekondari Tongoni yamekuwa yakididimia siku hadi siku lakini tatizo lipo kwa pande zote tatu kwa maana ya uongozi wa shule, wanafunzi, walimu na bodi ilishaomba uongozi wa shule kuandalia mkutano na wanafunzi lakini hadi leo jambo hilo halijafanyika ,“ anasema Bushiri. Anasema lengo la Bodi ya shule kutaka kukutana na wanafunzi wa shule hiyo ni baada ya kufahamishwa kuwa walimu wamekuwa na tabia ya kutoingia darasani kwa wakati na wengine kuishia njiani bila kufika shule na tabia nyingine ambazo ni kinyume cha maadili ya wanafunzi. “Wanafunzi walishalalamika kwamba walimu hawaingii darasani kwa wakati….lakini si hilo tu, pia wanafunzi wenyewe wana matatizo yao mengi tu ujana umewazidi na ndio maana tulitaka kuzungumza nao,” anasema. Anasema anashangaa wanafunzi kuchelewa shule kwa kisingizio cha usafiri wa mashua wakati kuna boti inayowasafirisha bila kikwazo chochote na kwamba hilo ni tatizo na uzembe wa ufuatiliaji wa wanafunzi kati ya uongozi wa shule na wazazi. Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tongoni, Luis Makame anasema wakazi wa kata hiyo hawana mwamko katika uchangiaji wa masuala ya elimu wakiamini kuwa elimu ya msingi inatosheleza kuendesha maisha ya watoto wao. “Kusema kweli, changamoto kubwa hapa ni uelewa wa wazazi katika kuchangia sekta ya elimu.Wengi wanaamini kuwa, kila mtoto ana riziki yake na kwamba elimu ya msingi inatosha kabisa kuendesha maisha ya watoto wao ya kila siku, “ anasema Makame. Kwa upande wao, baadhi ya wazazi wa Kata ya Tongoni wakizungumzia hali hiyo wanatupia lawama uongozi wa shule na kusema kuwa umeshindwa kuwafuatilia wanafunzi wao na baadhi wamekuwa na mienendo isiyofaa. Selemani Sharif ni mmoja wa wazazi, ambaye anasema kuwa, licha ya walimu kutoa malalamiko ya wazazi kutochangia ada kikamilifu, lakini nao wameshindwa kusimamia uendeshaji wa shule kwani hata wanafunzi nao wanalalamikia walimu kutoingia madarasani kwa wakati. “Sisi wazazi tunalaumiwa hatutaki kuchangia maendeleo ya shule, lakini walimu nao wanalalamikiwa na wanafunzi kutoingia madarasani na si hilo tu, uongozi wa shule umeshindwa kusimamia tabia za wanafunzi wao ambao tunawakuta vichochoroni wakati wa masomo na hiki kichaka ndiyo gesti yao, walimu wanakuwa wapi wakati huo hata wanafunzi wazurure ovyo,” anahoji Sharif. Naye Mwajuma Mwanajumaa anaiomba serikali kufanya mabadiliko ya uongozi wa shule hiyo kwa sababu wazazi hawaridhishwi na matokeo ya shule hiyo. “Shule hii wakati ikijengwa wananchi tuliichangia…kuitokana na umuhimu wake kama kweli hatupendi elimu ilikuwaje tulitoa nguvu zetu hadi ikajengwa…walimu na uongozi wa shule umetukatisha tamaa sana… sasa ili twende vizuri tunaiomba serikali iingilie kati suala hili,” anasisitiza Mwanajumaa. Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga ambaye pia ni Ofisa elimu Sekondari wa Jiji hilo , Bashiri Shelimo anasema hatua ya kwanza itakayochukuliwa ni kuuondoa uongozi mzima wa shule hiyo. Shelimo anasema, hatua ya pili ni kuhamisha walimu wa shule hiyo na kuwapeleka walimu wapya sambamba na kuunda upya bodi ya shule hiyo. Anasema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo hadi kufikia katika hali hiyo mbaya ni uongozi mbovu uliodumu kwa muda mrefu unaofanya kazi kwa mazoea. “Nina miezi kadhaa tangu nilipohamia hapa lakini kwa uchunguzi wangu wa awali nimeona kuna haja ya kuupangua uongozi wa shule hiyo. Bahati nzuri Mwalimu mkuu mwenyewe aliomba yeye na makamu wake wapumzishwe na tukaona ni sababu za msingi ili kuleta mabadiliko chanya kwenye shule ile,” anafafanua Ofisa elimu huyo. CHANZO: NIPASHE