Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatatu, 14 Aprili 2014

UTATA DIRA YA ELIMU NCHINI

Sekta ya elimu ilipata matumaini ya kupiga hatua mbele kimaendeleo baada ya serikali kuibuka na mpango wa ujenzi wa sekondari za kata mwaka 2010. Mpango huo ulilenga kuongeza nafasi za masomo ya elimu ya sekondari kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na umetoa fursa hiyo. Hata hivyo,
 matumaini hayo hayajafikiwa kama ilivyotarajiwa kiwa upande wa ufanisi katika uendeshaji shule hizo, nyingi zina uopungufu wa walimu,

baadhi hazina vyoo, vifaa vya kufundishia, ofisi na nyumba za walimu. Na kama hiyo haitoshi, serikali imekuja na mpango mwingine wa ujenzi wa madarasa makubwa kwa lango kama la mpango uliotangulia wa ujenzi wa sekondari za kata. Lakini tayari madarasa makubwa yanayojengwa yameibua msongamano wa wanafunzi, matokeo yake utoaji wa elimu kwa kutumia madarasa hayo ni kikwazo cha juhudi ya kuinua kiwango cha ubora wa elimu, hasa kunazia ngazi ya shule za msingi.
 Elimu ya msingi na pia ngazi ya sekondari imeathirika zaidi na tatizo hilo, kwa sababu linasababisha wanafunzi waliosongamana darasani kushindwa kuelewa wanachofundishwa. Mbali na wanafunzi kujisikia kama watu walioko jela au mahabusu, mazingira hayo yanapunguza uwezo wa walimu kufundisha kwa ufanisi, pia wananshindwa kujua tabia ya kilwa mwanafunzi. John Lupala wa Chuo Kikuu Ardhi Dar es salaam
, anasema kuwa madarasa yenye msongamano wa wanafunzi yanachangia walimu kushindwa kutekeleza vizuri malengo yao ya kutoa elimu kwa vitendo. Anasema mwalimu anayefundisha katika madarasa ya aina hii anatumia muda mwingi kufundisha somo lake na kuhakikisha kila mwanafunzi anayehudhuria kipindi chake ameelewa. Lupala anasema kwa upande mwingine,
 mwalimu pia anashindwa kusimamia suala nidhamu darasa lake linapokuwa limejaa wanafunzi, hasa kwa wanaokaa viti vya nyuma. “Madarasa ya aina hii yanahitaji jitihada kubwa ya mwalimu katika kudhibiti muda wa ufundishaji, kutokana na ukweli kuwa anatumia muda mwingi kufundisha mada moja,”anasema. Anasema uwiano halisi uliopo baina ya idadi ya wanafunzi na ukubwa wa madarasa unachangia unachangia kuwafanya walimu kukosa ari ya kufundisha.Anasema msongamano ni chanzo cha tatizo katika utendaji wa mwalimu, lakini pia suala hilo linaathiri zaidi tabia na usomaji wa mwanafunzi. “Usikivu wa wanafunzi darasani ni eneo mojawapo muhimu la kupewa kipaumbele, hasa kwa kuzingatia unaathiri ushiriki wake katika masomo.

Utafiti unaonyesha kuwa madarasa yenye watu wachache wanafunzi wanatumia muda mchache kufanya mazoezi yao na yanatoa nafasi kufanya mazoezi mengi zaidi,” anasema Lupala. Kwa mujibu wa Lupala, katika madarasa yasiyokuwa na msongamano, wanafunzi wanaelekeza akili zaidi katika kumsikiliza mwalimu wao, hii ni tofauti kwa madarasa yenye wanafunzi wengi. Anasema chimbuko la msongamano hauna uhusiano na ongezeko la wananfunzi, bali ni tabia ya ujengaji wa madarasa makubwa yenye wanafunzi wengi. “Katika mazingira ya aina hiyo, ni ndoto kutegemea kupata ufundishaji unaokidhi viwango,” anasema na kuongeza kuwa elimu kwa vitendo inaathirika zaidi.Jennifer Mhando, mwalimu wa shule ya msingi mkoani Lindi anasema kuwa madarasa yenye wanafunzi wengi yanasababisha mwalimu kushindwa kujua tabia ya mwanafunzi binafsi na wakati mwingine inamwia vigumu hata kuzungumza nao mmoja mmoja kutokana na ufinyu wa muda na idadi yao kuwa kubwa.
 “Darasa linapokuwa kubwa, wanafunzi huwa wanajenga tabia ya kutomsikiliza mwalimu aliye mbele yao kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo usikivu mdogo hasa kwa waliokaa viti vya nyuma ama waliokosa viti kabisa.” Jennifer. Kwa mfano, anasema wilaya yake ya Lindi vijijini kuna shule 123 za msingi zenye walimu 700 na kwamba hili linawafanya walimu kutumia mbinu zisizo rasmi katika ufundishaji wa elimu kwa wanafunzi wao. “Uwiano uliopo ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 125 kwa wakati mmoja ukiacha mikondo mingine. Inatuwia vigumu sana kusimamia utaratibu na wakati mwingine zoezi la kuweka kumbukumbu za wanafunzi linashindikana,” anasema. Jennifer anasema kuwa katika darasa lenye idadi kubwa ya wanafunzi hakuna upimaji mzuri wa maendeleo ya wanafunzi kutokana na ukweli kuwa mwalimu anaelemewa na kazi nyingi za kufanya, shughuli hizo ni pamoja na za kuhifadhi kumbukumbu ya kila mwanafunzi. Anasema asilimia 20 ya wanafunzi tu, ndiyo wenye uwezo wa kuuliza maswali na hili ni kutokana na ukweli kuwa mwingiliano mkubwa uliopo baina ya walimu na wanafunzi inawapa majukumu mengi, hivyo kufanya usahihishaji wa mazoezi mbalimbali kuwa mgumu. “Ujuzi wa mwalimu unaendelea kushuka kwa hana muda wa kusoma, kusikiliza na kubadilishana mawazo na wanafunzi na hivyo kumfanya mwalimu kutofahamu upekee wa mwanafunzi wake.” Anaongeza kuwa katika hali ya kawaida madarasa kama haya huwa na mwingiliano mkubwa baina ya walimu na wanafunzi, hivyo ni wanafunzi wachache tu ndiyo wanaopata nafasi ya kuuliza ama kujibu maswali. Anasema kuwa utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa mwalimu hana nafasi ya kumkagua mwanafunzi mmoja mmoja anayehitaji msaada wake na kuongeza kuwa kati ya wanafunzi 78, wanafunzi 20 tu ndiyo waliouliza maswali. “Utafiti unaonyesha kuwa wanafunzi wenye uwezo mdogo wa kuelewa wanadharauliwa kutokana na walimu wao kuwa na shughuli nyingi katika kufundisha na kuwasahau na hivyo kuwafanya wawe dhaifu zaidi,”anasema. “Kwa mujibu wa Jennifer madarasa yenye msongamano yana madhara makubwa kwa wanafunzi kutokana na ukweli kuwa unapunguza nafasi kwa shule kutoa elimu bora nchini.” Euphrasia Kileo, ni mwalimu wa shule ya msingi Ndara iliyopo mkoani Shinyanga, anasema ni vigumu kwa mwalimu kufanya uchambuzi wa wanafunzi binafsi kutokana na ukweli kuwa linahitaji muda. Anasema kuwa kutokana na wingi wao wanafunzi wachache wanapata msaada wa mwalimu pale wanapouhitaji na kuongeza kuwa kadri wanavyoendelea kushindwa wanajenga tabia ya kuchukia na kuamua kutoroka ama kukaa nje ya madarasa. “Tunapata wakati mgumu sana tunapotaka kusimamia na kufundisha madarasa yenye wanafunzi wengi kutokana na ukweli kuwa wakati mwingine tunashindwa kutumia mbinu mbalimbali za kufundisha,” anasema Euphrasia. Anasema hata mwalimu anapoamua kutumia mbinu mbalimbali za kufundisha inakuwa ngumu kwenye madarasa ya aina hii, elimu haiwafikii wanafunzi wote kwa kiwango kinacholingana. Anasema kuwa kutokana uwingi wa wanafunzi katika madarasa walimu wanashindwa kutumia mbinu za ziada kuleta ufanisi, kama vile kuwapa nafasi kubwa wanafunzi kuuliza maswali wakati wa kipindi.
 Anasema ufundishaji wa madarasa yaliyofurika wanafunzi pia siyo mzuri kwani unaweza kusababisha mzunguko wa hali hewa kutokuwa wa kawaida na wakati mwingine kusababisha maradhi ya kuambukiza kama vile uti wa mgongo. Anasema idadi kubwa ya wanafunzi isiyo na uwiano na uwezo wa darasa inaathiri uwezo pia wa wanafunzi kufuatilia kwa umakini kwa njia ya kusikia na kusoma, matokeo yake kiwango cha elimu nchini kinaendelea kubaki duni.
 “Ni vugumu kwa mwanafunzi kutumia vifaa kwa vitendo kwa sababu hakuna uwiano baina yao na vifaa vya kufundishia vinayotumiwa na mwalimu,”
 anasema Euphrasia Anaongeza kuwa uwiano wa idadi ya wanafunzi uliowekwa na wizara ya elimu na utamaduni wa 1:40, yaani mwalimu moja kwa wanafunzi 40 umetelekezwa na kwa maana hiyo hakutakuwa na mafanikio mazuri wala usimamiaji mzuri wa nidhamu na maendeleo ya wanafunzi kimasomo kwa jumla. Kibox: Uwiano uliopo ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 125 kwa wakati mmoja ukiacha mikondo mingine. Inatuwia vigumu sana kusimamia utaratibu na wakati mwingine zoezi la kuweka kumbukumbu za wanafunzi linashindikana”

 CHANZO: IPPMEDIA