Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Ijumaa, 29 Novemba 2013

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa vita nchini Syria vimesababisha kuharibu watoto kimwili na kisaikolojia.


Wakimbizi watoto walio katika umri wa kwenda shule ambao wamekimbilia katika nchi jirani wameendelea kukosa elimu na wanalazimika kufanyakazi ili kujikimu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limesema watoto wapatao 300,000 wanaoishi nchini Lebanon na Jordan huenda wakakosa masomo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2013.
Wengi wa ambao hawaendi shuleni wanakwenda kufanyakazi kwa muda mrefu wakipata malipo kidogo, wakiwa na umri mdogo wa hata miaka saba.
Zaidi ya nusu ya wakimbizi wa Syria milioni 2.2 ni watoto, wengi wakikabiliwa na hatari kubwa na hata nje ya eneo la vita.
Hatari hizo ni pamoja na athari za kimwili na kisaikolojia.
Akizindua ripoti hiyo, Kamishina wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Antonio Guterres alisema: "Kama hatutachukua hatua haraka, kizazi cha watu wasio na hatia kitaishia kufa kutokana na vita."
Utafiti huu ni mpya kabisa na unajaribu kuonyesha madhara makubwa kwa watoto kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vilivyodumu kwa miaka mitatu. Madhara hayo ni kwa watoto walio ndani na nje ya mipaka ya Syria.

chanzo bbc.com

Jumapili, 10 Novemba 2013

chama cha walimu kuidai tena serikali

Chama  Cha Walimu Tanzania (CWT) kimeipa serikali siku 60 za kukamilimisha madeni ya mishahara ya walimu ya Sh. bilioni 48 pamoja na kukamilisha majadiliano ya mishahara  ya walimu na chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa CWT, Gratian Mukoba, wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu maazimio ya mkutano mkuu wa Taifa wa walimu nchini uliofanyika mkoani Arusha  Oktoba 28-29, mwaka huu.
Mukoba alisema hatua hiyo ilifikiwa na chama hicho baada ya serikali kukaa kimya kwa muda mrefu bila kutekeleza ahadi walizokiahidi chama hicho juu ya madai ya walimu ya muda mrefu.
Alisema chama hicho kinaidai serikali zaidi ya Sh. bilioni 48, ambazo serikali ili ahidi kuzilipa Septemba mwaka huu, lakini hawakufanya hivyo badala yake ikasema  inafanya uhakiki kwanza wa madai hayo ili kukamilisha malipo hayo ambayo mpaka sasa hayajafanyika.
“Tuliendelea kukaa kimya tukisubiri serikali ikamilishe uhakiki wake na kutoa taarifa ya madai ambayo walimu wanaidai, lakini bado haikufanya hivyo, kwa hiyo na sisi baada ya kukaa kikao chetu cha walimu Taifa tukaweka maazimio haya,” alisema Mukoba.
Alisema wanatarajia kukabidhi barua ya notisi kwa Katibu Mkuu Kiongozi leo na hatua za kisheria zitafuata endapo serikali haitatimiza hayo ambayo wameyaorodhesha baada ya siku 60 kumalizika.
Alisema, maazimio mengine waliyoyaandika  kwenye barua hiyo ya notisi ni serikali iwe imebadilisha muundo wa walimu na wakaguzi ndani ya siku hizo 60.Azimio lingine  waliitaka serikali kukamilisha majadiliano na chama cha walimu kuhusu mishahara ya walimu ya mwaka ujao kwa mwaka  wa fedha wa 2013/2014.
“Haya yote na mengine ambayo sijakuainishia tunayataka yatekelezwe na serikali ndani ya siku hizi 60 tulizotoa na endapo serikali itaendelea kukaidi basi hatua zaidi za kisheria zitafuata na tutatoa msimamo wa chama kuwa nini kitafanyika,” alisema Mukoba.
NIPASHE lilimtafuta Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, jana ili kuzungumzia suala hilo, lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.Hata Naibu Waziri, Philip Mulugo, alipotafutwa simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.
 ippmedia.com

Jumatatu, 4 Novemba 2013

TAMKO LA HAKIELIMU KUHUSU UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU 4 NOVEMBA 2013.


Hivi karibuni serikali imetoa tamko kuhusu mfumo mpya wa upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi na ufaulu. HakiElimu na wadau wake imetafakari tamko hilo na kutoa maoni ya yafuatayo:

1. Hatujatambua lengo la serikali kuleta mabadiliko haya; hasa ikikumbukwa kuwa Tume ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mh. Mizengo Pinda haijawahi kuweka bayana taarifa yake kuhusu sababu za wanafunzi kutofaulu vizuri katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne. Wajumbe wa Tume hiyo wamekuwa wakitoa dondoo fupi fupi za matokeo ya kazi yao-kama vile Bungeni na katika hadhira nyingine za kitaifa; bila kutoa ripoti yenyewe. Je, kwa mabadiliko haya,wizara inataka kuwaaminisha Watanzania kwamba alama zilivyokuwa zimepangiliwa hapo awali,ndiyo sababu kuu ya wanafunzi kutofaulu vizuri?

2. Wizara imeeleza kwenye tamko lake kwamba imeshirikisha wadau mbalimbali katika kufikia uamuzi huo. Hata hivyo, katika orodha ya wadau walioshirikishwa inaonekana bayana kuwa asasi za utetezi hazikupewa nafasi. Baada ya kufanya mawasiliano na baadhi ya wadau wanaodaiwa kushiriki,wenyewe wamekiri kuwa ingawa walishiriki mawazo yao hayakuzingatiwa na hawakukubaliana kuhusu kushusha alama za ufaulu kufikia 20 kati ya 100.

3. Mpangilio wa alama zitakazotumika kuanzia mwaka huu unaleta tafsiri ya ndani kuhusu nia ya wizara kubadilisha alama hizo. Tafsiri hiyo ni kulazimisha kuona kwamba wanafunzi wachache zaidi wanapata daraja la 5 (ambalo limeanzishwa badala ya daraja sifuri); kukiwa na uwezekano wa kupunguza wanafunzi wanaopata daraja hili kwa asilimia 2.2% ukilinganisha na utaratibu uliotumika kwa matokeo ya mwaka 2012. Mpangilio huo mpya una uwezekano wa kuongeza kundi la wanafunzi wanaopata daraja la tatu na la nne kwa asilimia 12.1% kuliko utaratibu uliotumika mwaka 2012. Hata hivyo, alama hizo mpya zinaweza kupunguza uwezekano wa kupata daraja la kwanza na la pili kwa asilimia 11.9%. Serikali na wadau wengine wa elimu wanatambua bayana kuwa njia kuu ya kuboresha elimu na matokeo katika mitihani ni kuboresha utaratibu wa utoaji wa elimu. Kwa nini serikali, hasa katika kipindi hiki inataka kuona matokeo mazuri bila kuwekeza kwenye mipango ya kuboresha mfumo na utaratibu wa utoaji wa elimu? HakiElimu inatafsiri uamuzi huo wa serikali kama ni kukwepa ukweli na utaalamu; na badala yake serikali inatafuta njia ya mkato ya kuwafurahisha wazazi na wananchi ili wapunguze kelele.

4. Serikali imekubali kutumia asilimia 40 kutoka kwenye Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment, CA), ili ziunganishwe na alama 60 za mtihani wa mwisho. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa alama hizo zilikuwa zinachakachuliwa huko shuleni, na hata Baraza la Mitihani Tanzania mwaka huu walikiri hilo kutokea. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itatumia njia gani kuhakikisha kuwa zinapatikana alama sahihi toka shuleni zinazoendana na uwezo wa mwanafunzi? Je, kwa kiasi gani walimu wameandaliwa na kujengewa mazingira mazuri ya kufanikisha zoezi hili? Hata hivyo, serikali inapaswa pia kuwaeleza watanzania uzoefu wa nchi nyingine za Afrika katika matumizi ya alama za CA; wengine wanatumia asilimia ngapi? Ni muhimu kuwa na ushahidi kuwa kiwango cha CA tutakachokitumia kitaboresha utaratibu wa kutathmini wanafunzi; na kuwatendea haki badala ya kuwaghiribu au kuwaumiza.

5. HakiElimu inasikitika kuona wizara inalazimisha kila mwanafunzi atakayefanya mtihani wa kidato cha nne au cha sita awe amefaulu. Hiyo inathibitishwa na tafsiri ya alama ambazo zitatumika zinazoonesha kwamba kuanzia atakayepata alama sifuri mpaka mia moja atakuwa amefaulu kwa namna fulani. Kwa mfano, hata atakayepata alama kuanzia 0 mpaka 19 katika somo fulani atahesabiwa kuwa amefaulu, japo katika kiwango kisichoridhisha. Kwa nini wizara inakosa ujasiri wa kukubali kuwa mwanafunzi atakayepata chini ya alama fulani ahesabiwe kuwa hakufaulu?

6. Kwa upangaji huo mpya wa alama za ufaulu, Tanzania itakuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kwa kuwa na kiwango cha chini kabisa cha ufaulu katika elimu ya sekondari na kuna hatari kwamba kushushwa kwa alama za ufaulu kutapunguza ama kuondoa hamasa ya wanafunzi kusoma kwa bidii, kwa kuamini kuwa hawatafeli na cheti watapata tu. Kama wadau wote tunakubaliana kuwa nia ya kutoa elimu ni kuandaa Watanzania ambao watakuwa na maarifa na uwezo wa kushindana na wengine wanaosoma katika nchi nyingine Afrika.

7. HakiElimu pia inasikitika kuona kuwa wizara inapotosha malengo ya “Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now-BRN)” kwa kutafuta njia za mkato. BRN imeeleza bayana kuwa kati ya mikakati itakayotumika kupata Matokeo Makubwa katika elimu ni kuboresha mchakato wa kufundisha na kujifunza shuleni na kuboresha utaratibu wa utoaji wa elimu kwa kuweka bayana majukumu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya TAMISEMI. Wizara iwaambie Watanzania kuwa kwa kiasi gani upangaji huu wa alama utasaidia kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa maana ya kumjengengea mwalimu uwezo, mazingira mazuri na hamasa ya kufundisha na pia kutengeneza mazingira mazuri ya mwanafunzi kujifunza. Katika haya, je, ni kweli kwamba huu upangaji upya wa madaraja ni kipaumbele chetu namba moja? Si busara kushughulikia mpangilio wa alama na madaraja kwanza wakati mchakato wa kuboresha mfumo wa elimu ili kupata hayo matokeo mazuri bado uko chini. Kitendo hicho ni kukurupuka na kuruka hatua muhimu zinazoweza kuboresha elimu.

8. HakiElimu inawatahadharisha Watanzania, wakiwemo wazazi, wanafunzi na vijana wenye nia ya kurudia mitihani ili wapate vyeti; na serikali yenyewe kuzingatia ukweli kwamba: Elimu ni uwezo, SIYO cheti. Jitihada za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonesha wazi kuwa nia ni kuona matokeo mazuri hata kama matokeo hayo hayataendana na uwezo walio nao wanafunzi. Katika kutengeneza raslimali watu ya kutosha, Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine haina namna ya kukwepa kuhakikisha kwamba mfumo wa elimu unaandaa vijana au wananchi wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili wao wenyewe, jamii na Taifa kwa ujumla; pia kuwa na wananchi ambao watakuwa na ujasiri, tija na ubunifu, katika uzalishaji katika shughuli na fursa mbalimbali watakazozipata au kuzitafuta. Hali hii haipatikani kwa kuhangaika na alama za ufaulu kama kipaumbele. Tunahitaji kuhangaika na mfumo wa utoaji elimu utakaotusaidia kuleta mapinduzi ya kweli ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

HakiElimu inaishauri Serikali kusitisha matumizi ya alama na madaraja haya mapya. Irudi kwa wadau na ushahidi kuhusu uamuzi huu; huku ikitoa nafasi ya kuchukua maoni ambayo yanaweza kuboresha mfumo wa upimaji wa wanafunzi. Wakati zoezi hilo linaendelea, HakiElimu inaisisitiza Serikali kutumia matokeo ya tafiti mbalimbali na mipango iliyopo kushughulikia dosari na changamoto zinazorudisha nyuma elimu yetu, hasa zile zinazokwamisha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
Tamko hili limesainiwa na,

Elizabeth Missokia Mkurugenzi Mtendaji, HakiElimu

Big results now itafanikiwa kuongeza ufaulu lakini itaua ubora wa elimu

kwa mara ya kwanza leo Marafiki wa elimu musoma tumeweza kuzungumza na baadhi ya wanafunzi kuhusu mtihani wa taifa wa kidato cha nne, majibu tuliyoyapata kwa wanafunzi yanatia matumani sana kati ya wanafunzi 70 wa shule 5 tofauti hapa musoma tuliowahoji jinsi wanavyouona mtihani wanafunzi 65 wamesema mtihani ni rahisi wanafunzi wanafunzi 5 tu wamesema mtihani ni mgumu hii inaonyesha mwelekeo wa matokeo yajayo yanaweza kuwa mazuri zaidi ikilinganishwa na alama za ufaulu jinsi zilivyolegezwa marafiki wa elimu tunawatakia wanafunzi waendelee na mtihani na wazidishe bidii wapate division 1 maana ndio yenye unafuu kwao

Jumamosi, 2 Novemba 2013

kufutwa kwa division ziro je ni mpango wa kutekeleza Big results now

hivi karibini serikali imetangaza mabadiliko ya alama za ufaulu kama inavyoonekana hapo chini

A ni 75 hadi 100; huu ni ufaulu uliojipambanua
B+ ni 60 hadi 74; huu ni ufaulu bora sana
B ni 50 hadi 59; huu ni ufaulu mzuri sana
C ni 40 hadi 49; huu ni ufaulu mzuri
D ni 30 hadi 39; huu ni ufaulu hafifu
E ni 20 hadi 29; huu ni ufaulu hafifu sana
F ni 0 hadi 19; huu ni ufaulu usioridhisha

Kimsingi alama yoyote kuanzia sifuri hadi mia moja ni ufaulu wa aina flani;

Madaraja yatakuwa kama ifuatavyo;

Division One = pointi 7 hadi 17
Division Two= pointi 18 hadi 24
Division Three = pointi 25 hadi 31
Division Four= pointi 32 hadi 47
Division Five = pointi 48 hadi 49

Yaani mtu akipata E mbili na F tano, ana division four; au akipata D moja na F sita atakuwa na division four.

swali la msingi tunalopaswa kujiuliza ni je huu ndio utekelezaje halisi wa MATOKEO MAKUBWA SASA na kama ndio utekelezaje serikali haijaweka wazi na kuwaelimisha wadau juu kusudio hasa lililopelekea kupangwa kwa alama za ufaulu marafiki wa elimu tunaamini kwamba kupangwa kwa alama za ufaulu si suruhisho la matatizo ya elimu yanayokabili nchi ila tunaamini kuwa serikali ikitekeleza malengo yaliyobainisha kwenye vipaumbele vya mpango wa big results now elimu itafanikiwa kwa kiwango kikubwa sana.