Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatano, 9 Julai 2014

Tunataka wapate maarifa au wajue Kiingereza? makala ya Gervas Zombwe.

Tafiti zote duniani zinasema wazi kuwa binadamu yeyote anajifunza na kuelewa kikamilifu anapofundishwa kwa lugha anayoijua zaidi. Na uwezo wa kujenga utambuzi na kukuza vipawa umo ndani ya mila na desturi asilia zinazofungamana moja kwa moja na lugha mama inayomiliki maarifa na michepuo ya akili.
Kufundishwa kwa lugha asiyoielewa vizuri kunamzuia binadamu kumiliki maarifa ya kukuza michepuo ya akili. Kweli atasoma, atapata cheti, digrii, lakini maarifa na ubunifu viitabaki nje ya utambuzi wake.
Ndiyo maana nchi zote zilizoendelea wanafundisha watu wao kwa lugha zao. Huwezi kubuni kwa kutumia lugha ya jirani, huwezi kufikiri kwa kutumia lugha ya kukopa, kuwezi kuvumbua kwa kutumia lugha ya kigeni. Ni ndoto!
Mwalimu wa lugha, mtafiti na mtetezi wa lugha Profesa Martha Qorro, siku zote kupitia tafiti nyingi alizofanya amekuwa akisisitiza manufaa ya kutumia lugha ya taifa kufundishia vijana wetu.
Ili mwanafunzi afike ngazi ya juu kabisa ya uelewa, ni lazima maarifa yapitie kwenye lugha anayoijua vizuri. Vinginevyo atakuwa anajifunza juu juu tu na kuishia kwenye uelewa wa hatua ya mwanzo tu. Hatua za uelewa ziko kama ifuatavyo:
Hatua ya kwanza, uwezo wa lugha ya ‘kuombea maji’. Akilazimika kujifunzia lugha katika ngazi hii mzungumzaji inabidi akariri karibu kila kitu kwa kuwa ana uelewa mdogo. Huchukua muda mrefu kuelewa mambo madogo kwa kuwa lugha ni kikwazo. Haoni uhusiano kati ya maisha yake na mambo yale anayofundishwa au anayoelezwa shuleni. Masomo humchosha na mawazo huhama darasani.
Hatua ya pili, uwezo wa kumpa mtu maelekezo ya namna ya kufika sehemu fulani. Uelewa wa juu juu wa mambo yanayozungumzwa au kufundishwa kwa lugha hiyo. Tabia ya kukariri bado inaendelea, ingawa imepungua kwa kiasi kikubwa. Uwezo wa kuandika sentensi fupi fupi sahihi na kuuliza maswali rahisi. Kuna uwezekano mkubwa wa kutoelewa au kuelewa vibaya maana iliyokusudiwa. Uhuru wa fikra haupo!
Hatua ya tatu, uwezo wa kufikiri, kutafakari, kujadili, kuchambua na kuchanganua masuala na dhana mbalimbali yanayozungumzwa au kufundishwa kwa lugha husika. Mzungumzaji anakuwa na uwezo mkubwa wa kutumia lugha kama nyenzo ya kuvumbua mambo mapya. Ana uhuru wa kutumia lugha husika na yote atakayoelezwa katika kujikomboa kimawazo.
Katika hatua hii, lugha siyo kikwazo katika kuelewa, kupambana na changamoto za maisha. Hahitaji kukariri; bali hutumia uelewa wake katika kujibu maswali au kutoa maelezo juu ya yale anayoyaelewa. Ni katika hatua hii ya uelewa ndiyo wanafunzi wanapoweza kujifahamu, kujitambua, kuwa mbunifu, kutumia fursa, kujiendeleza, kutafiti na kutatua changamoto zinazomzunguka. Wanafunzi wetu wengi shuleni na vyuoni hawafiki hatua hii. Ushahidi unaonyesha shule za sekondari hawajifunzi na kupata maarifa kutokana na lugha. Kwa mfano, tafiti nyingi (Mlama na Matteru 1978, Criper and Dodd 1984, Roy-Campbell and Qorro 1987, Rubagumya, Jones and Mwansoko 1998, Qorro 1999, Mwinsheikhe 2003, Puja 2003, Brock Utne 2004, Vuzo 2005) zimeonyesha kuwa wanafunzi wengi katika shule za sekondari na vyuo nchini Tanzania wana uwezo wa hatua ya kwanza au ya pili ya uelewa wa lugha inayotumika kufundishia.
Kwa kung’ang’ania kutumia lugha wasiyoelewa, tunawafundisha wanafunzi wetu kushindwa! Wengi wao wanajifunza kutodadisi, kutofikiri, kutokuuliza maswali, kunakili na kukariri, kuwa waoga, kutojiamini, kukubali kila hali na kukata tamaa kwa kauli ya “yote maisha”. Ni vyema tukajiuliza, kuandaa vijana wasioweza kuelewa, kujadili, kufikiri, kuchambua na kuchanganua masuala na dhana mbalimbali zinazofundishwa ni kwa masilahi ya nani? Ni wazi kwamba tunahitaji elimu ya kujikomboa na kwamba ili kufanikisha elimu ya kujikomboa shuleni na vyuoni, ni lazima wanafunzi watumie lugha ambayo wao na walimu wao wana uelewa wa hali ya juu.
Katika hali ambayo wanafunzi wana uelewa mdogo wa lugha, wanafunzi wengi, hasa wasichana, huwa wanyonge na kwa muda mwingi hunakili maandiko ya mwalimu (mengine yakiwa na makosa) kwa kadri watakavyoweza kuyasoma. Maandiko hayo kwa sehemu kubwa wengi hawayaelewi.
Badala ya kujifunza masuala ya msingi, wanafunzi wanaishia kukariri maneno kwa lugha wasiyoelewa na muda mwingi unapotea na ari ya kusoma inapungua. Elimu hii ya kunakili na kukariri haiwapi uwezo wa kujikomboa bali huenda kinyume na makusudio.Kama tunataka maendeleo ya kweli, Waafrika ni lazima wachukue mamlaka juu ya taratibu zinazotumika kuendesha elimu yao. Lazima wafundishe watoto wao kwa lugha wanazoelewa ili kuwaandaa kuwa wadadisi wa kutafuta majibu ya matatizo yanayoikabili jamii. Ikumbukwe kuwa lengo kuu la elimu ni maendeleo siyo umahiri wa lugha fulani. Ni falsafa mbadala!