Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumatatu, 9 Desemba 2013

wahitimu mzumbe wahimizwa kutumia elimu walioipata tulitumikia taifa vema

Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe mkoani Morogoro, wamehimizwa kutumia maarifa, elimu na stadi walizozipata chuoni hapo kuwa kichocheo cha maendeleo katika jamii inayowazunguka na ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa, amesema kwa kuhitimu kwao, kunawaweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutumikia taifa lao na jamii inayowazunguka.

Aliyasema hayo wakati wa mahafali ya 12 ya chuo hicho mjini hapa mwishoni mwa wiki.

Profesa Kuzilwa alisema wasomi hao sasa ni rasilimali watu inayotegemewa kuleta maendeleo ya nchi, hivyo akawaomba wakawe mfano bora kwa jamii inayowazunguka na kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanatimiza wajibu kwa taifa lao.

Jumla ya wahitimu 1,803 walitunukiwa vyeti mbalimbali, kati yao asilimia 46 ni wanawake na 54 wanaume.

Wahitimu 215 walitunukiwa astashahada, 1,153 Shahada ya Kwanza, 433 shahada ya uzamili na wawili shahada ya uzamivu.

Jumla ya wahitimu katika kampasi kuu ya Morogoro, Dar es Salaam na Mbeya ni 3,554, ukilinganisha na wahitimu 3,049 mwaka 2011/12, sawa na ongezeko la wahitimu 504 walihitimu katika mahafali hayo.

Alisema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 16 ambapo wahitimu 24 wamepata daraja la kwanza ikilinganishwa na 17 mahafali yaliyopita.

Pia alisema kutokana upungufu wa wanasayansi nchini, chuo kimeandaa program za shahada ya sayansi asili na tumizi kukabili hali hiyo na kuunga mkono Mpango wa Elimu ya Juu 2010-2020 wa vyuo vikuu kuongeza fursa za sayansi.

Mikakati ya kuanzisha program hizo inafanywa kwa  kushirikiana na vyuo vingine vikuu nchini na nje kama ilivyoainishwa katika mkakati wa tatu wa chuo wa 2012/13-2016/17 wa kuwa na mtizamo anuwai katika program zake.

Pia Chuo kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya Korea kinatarajia kuanzisha kijiji cha sayansi ambapo program mbalimbali zikiwamo za kompyuta zitaanzishwa chini ya kitivo cha sayansi na teknolojia.

Alisema pamoja na mafanikio na mipango iliyopo, Chuo kinakabiliwa na ufinyu wa bajeti ambayo haikidhi mahitaji halisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Daniel Mkude, alisema mhitimu kumaliza masomo siyo mwisho wa kujifunza, bali wazidi kujenga tabia ya kujisomea na kuchota maarifa.

“Taifa linawahitaji...mzidi kujisomea na kuendelea na hatua nyingine ya masomo,” alisema.

Alishauri wahitimu hao kujiepusha na tabia zisizofaa kwa vile taifa linapoteza rasilimali watu kutokana na baadhi hujiingiza katika matendo ya ulevi na kupoteza maisha wakiwa na umri mdogo.

Pia alisema wahitimu hao wanatakiwa kuwa mfano kwa jamii kwa kupiga vita ufisadi, wizi, mauaji ya vikongwe, imani za kishirikina, ukahaba, ubakaji, mauaji ya albino na utupaji wa watoto.

Mahafali ya Chuo Kikuu Mzumbe, pia yalihudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mkewe, Tunu ambao walishiriki kama wazazi na kushuhudia mmoja wa watoto wao akipata shahada yake.
 
Chanzo.  Ippmedia.com