Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumamosi, 25 Januari 2014

Elimu bora; silaha ya kupambana na adui umaskini

Mwanahabari mkongwe, Othman Miraj anasema umaskini uliokithiri nchini ni suala lililogubikwa na mambo kadhaa yaliyosongamana.
Ni kwa sababu hiyo anasema ili kuumaliza umaskini, kunahitajika mipango na mikakati anuai, badala ya kuegemea katika kile anachosema dawa mujarabu ya aina moja.
“ Kuushinda umaskini ni kuwa na mkakati wa kuugawa utajiri wa Taifa, mifumo ya kisiasa duniani, kupigwa vita kwa ufisadi na kuwepo kwa mfumo mzuri wa elimu,’’ anataja baadhi ya mikakati ya kupambana na umaskini.
Mfumo bora wa elimu
Siyo Miraji tu, utafiti na uzoefu vinaonyesha elimu ni mojawapo ya silaha kubwa na muhimu siyo katika mapambano dhidi ya umaskini wa mtu mmojamoja, lakini pia katika maendeleo ya nchi kijamii na kiuchumi.
Wachambuzi wa sera na masuala ya kijamii, Elizabeth Missokia na Gervas Zombwe katika chapisho liitwalo ‘Hali ya Elimu Tanzania’, wanasema katika dunia ya leo, ili kila mtu aweze kuboresha maisha yake ni lazima awe na elimu.
Elimu ndiyo inayomwezesha mtu kujitambua na kujimiliki yeye mwenyewe, kuzikabili changamoto zinazomsonga, kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake
Wanaongeza kusema kuwa ndani ya utandawazi, elimu isiyotosheleza, tafsiri yake ni umaskini zaidi; wakati elimu zaidi tafsiri yake ni maisha bora zaidi.
Ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo ni lazima iwe elimu bora, ambayo inalenga kumbadilisha mtu na kumwezesha kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda kazi, kuwa na mwenendo mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na ya jamii, wanaongeza kusema.
Umuhimu wa elimu hasa kwa mabadiliko ya mtu binafsi kuelekea mafanikio ya kijamii,unadhihiri pia katika kauli maarufu ya aliyekuwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyesema:
“........elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya mtu. Ni kupitia elimu ndipo binti wa mkulima mdogo anaweza kuwa daktari bingwa, kwamba mtoto wa kibarua wa mgodini anakuwa mkuu wa mgodi na mtoto wa kibarua wa mashambani anakuwa Rais wa Taifa kubwa”.
Elimu bora ni ipi?
Kwa kawaida, mfumo wa elimu bora huzaa elimu bora na hii ndiyo aina ya elimu tunayoitaka Tanzania kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi wake.
Swali kuu ni; elimu bora ni ipi? Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ahmed Kiwanuka anasema elimu bora ni ile inayomkomboa binadamu na kumwezesha kuchangia katika jamii na taifa kwa kazi atakazokuwa akizifanya.
“Lengo la kupata elimu ni kumkomboa mtu kutokana na utumwa wa umaskini. Inatakiwa elimu imwezeshe mtu kutumia fikra zake kuendesha maisha mara baada ya kuhitimu masomo yake,” anasema
Akirejea maneno ya Mwalimu Julius Nyerere, anasema mwanafalsafa huyo aliyekuwa mtetezi mkubwa wa elimu aliwahi kusema kuwa ukombozi wa watu maskini utatokana na kusoma.
“Ukimwelimisha mtoto wa masikini, utakuwa umeisaidia familia yake, jamii na hata Taifa kutokana na mchango atakaotoa baada ya kuelimika,” anaeleza Dk Kiwanuka na kuongeza:
“Wasomi wetu wanatakiwa kujitoa kwa jamii kuhakikisha wanatumia elimu walioipata kwa ajili ya wengine.Taifa lolote linalotaka kuendelea lazima liwekeza zaidi katika elimu kwa kuwasomesha watu wote bila kuwabagua.”
Naye Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, anasema elimu bora ni ile inayozingatia mambo muhimu matatu, ambayo ni maarifa, ujuzi na mtazamo.
“Ukiwa na mambo hayo mwanafunzi atakuwa anajitambua na ataelewa maisha ni kitu gani. Ndivyo vitu vitakavyomwezesha kujua namna ya kuitumia elimu katika maisha ya kawaida katika jamii inayomzunguka,” anasema Mukoba.
Vikwazo vya elimu bora 
Licha ya kuwepo kwa juhudi kadhaa zinazofanywa na Serikali na wadau wengine wa elimu zinazolenga kuimarisha elimu nchini, bado sekta ya elimu inakabiliwa na vizingiti kadhaa vinavyohatarisha utoaji wa elimu na hata mustakabali wa sekta kwa jumla.
Tafiti na uzoefu vinaonyesha vikwazo vikubwa vya elimu nchini ni pamoja na taifa kukosa dira maalumu kuhusu elimu na aina ya mafunzo au maarifa, ambayo wanafunzi wanapaswa kufundishwa au kujifunza kutegemea mahitaji ya wakati uliopo.
Dira ni mwongozo wenye malengo yanayolinda utoaji wa elimu kwa manufaa ya nchi na mtu binafsi.


Changamoto nyingine zinazotajwa na wataalamu wa elimu kupitia utafiti wao ni kasoro za mitalaa, ikiwamo baadhi yake kuwa na masomo yasiyotoa ujuzi wa maana kwa wahitimu, hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha.
Nyingine ni kuendelea kutumia lugha ya Kiingereza katika kufundishia shule za msingi, ambayo haifahamiki kwa wanafunzi na walimu wenyewe, uhaba wa walimu hasa katika masomo ya sayansi na hesabu, uwepo wa walimu wenye uwezo mdogo kitaaluma na kufundisha, uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na baadhi ya wanajamii kutojali elimu kwa watoto wao.

chanzo mwananchi

Mapenzi ya jinsia moja yalalamikiwa sekondari wasichana

Shule moja ya sekondari ya wasichana iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani,  imelalamikiwa na wanafunzi pamoja na wazazi kuwa mabinti wanajihusisha na vitendo vya ngono vya jinsia moja (usagaji).

Akizungumza na NIPASHE mmoja wa wazazi (jina linahifadhiwa)  alisema shule hiyo imepoteza sifa kwa kuwa kuna wimbi kubwa la wanafunzi wanaojihusisha na vitendo hivyo vya usagaji.

Alisema  mtoto wake alikuwa ameanza kidato cha kwanza mwaka jana na baada ya kumuandikisha ndipo baadhi ya watu walipomueleza kuwa shule hiyo kwa sasa ina sifa mbaya ya mchezo ‘huo mchafu.’

"Baada ya kuelezwa nikasema nitalifanyia kazi jambo hilo hivi karibuni katika kupekua madaftari ya mwanangu nakutana na kibarua cha mapenzi alichoandikiwa na msichana mwenzake niliumia sana na nilitumia nguvu kumbana bila hivyo asingeniambia," alisema

Alisema ilimbidi amhamishe binti yake na kujiunga na shule moja ya sekondari iliyopo mkoani Tanga kwa ajili ya kuendelea na masomo ya kidato cha pili mwaka huu.

Mzazi huyo alisema anashangazwa ni kwa nini hatua hazichukuliwi wakati suala hilo ni la hatari kwani watoto wao wataharibika kiakili pamoja na kimwili na wanaweza kuambukizana VVU na Ukimwi..

Alisema wakati mwanaye akisoma katika shule hiyo alikuwa akihudhuria vikao vya wazazi mara kwa mara na kwamba kila kikao walikuwa wakifukuzwa wanafunzi kutokana na mwenendo huo.

"Hili tatizo ni kubwa na kufukuzwa kwa mwanafunzi sidhani kuwa wanatatua tatizo nadhani hakuna usimamizi mzuri kwani wangeweza kudhibiti kwa haraka tatizo hilo kabla ya kuwa kubwa," alisema

Pia alisema ndugu yake imembidi amhamishe mwanae na kumtafutia shule nyingine kwa kuhofia binti yake  kurubuniwa kwani wanakuwa ni wadogo na hawaelewi chochote, hivyo inaweza kuwa rahisi kudanganywa na kuingia kwenye vitendo hivyo viovu.

Alisema kuwa hata kiwango cha ufaulu kwa sasa shule hiyo imeshuka kutokana na tatizo hilo kwa wanafunzi .

Hata hivyo, NIPASHE  ilizungumza na mwanafunzi mmoja ambaye anasoma katika shule hiyo kuhusiana na suala hilo ambapo alikiri kuwepo kwa jambo hilo na kueleza kuwa wanaofanya mchezo huo ni wa kidato cha tano na cha sita.

"Mimi hawajanifanyia ila najua wanaofanya mchezo huo ni wale walioko kidato cha tano na cha sita," alisema Pia kuna baadhi ya wazazi wengine wamekuwa wakilalamikia jambo hilo na kueleza kuwa ndugu zao imewalazimu kuwahamisha watoto wao kutokana na vitendo hivyo vinavyofanyika shuleni hapo.

CHANZO: NIPASHE