Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Alhamisi, 18 Septemba 2014

mwanafunzi ajinyonga na kuacha ujumbe unaowalaumu madaktari

Mwanafunzi, Ezra Gerald Wabamba, aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Ihungo, mkoani Kagera, amekatisha maisha yake kwa kujinyonga akiwa hospitalini na kuacha ujumbe mzito juu ya chanzo cha kifo chake.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gilles Muroto, mwanafunzi huyo alifikishwa hosptalini hapo Septemba 11, mwaka huu na kulazwa ili kupatiwa matibabu.

Alisema Ezra alijinyonga saa 1:30 asubuhi katika mti ulikuwa umbali wa hatua 73 kutoka kwenye wodi ya wagonjwa namba tatu aliyokuwa amelazwa, kwa kutumia shuka yake binafsi.

Alisema baada ya maiti yake kugundulika na kufanyiwa upekuzi kwenye mifuko yake ya nguo kulikutwa Sh. 3,900, funguo mbili za Solex na kipande cha karatasi chenye ujumbe.

Alisema ujumbe huo ulisomeka: “Haiwezekani binadamu kuhudumiwa kama mbwa, yaani nafika hospitali naeleza hali yangu halafu daktari ananiandikia kulazwa bila ya kupimwa, sasa sijui watatibu  nini?, kwa kweli siwezi kuvumilia yaani wenzangu wanasoma halafu mimi nimekalishwa tu hapa hospitalini bila ya kujua wananitibu nini, inaniuma sana  mpaka kufika hatua hii ya kujiondoa duniani, ni kwasababu ninaona wanachezea ndoto zangu, mimi siwezi kuona ndoto yangu inazimwa wakati ninatakiwa niwepo shuleni nikamilishe ndoto zangu, mjitahidi tukutane mbinguni.”

Mwanafunzi huyo alimalizia ujumbe huo kwa maeneo ya kiingereza yaliyosomeka: “ Respect my family and brother Henry.”

Kamanda Muroto alisema katika tukio hilo hakuna aliyekamatwa ila uchunguzi juu ya kifo cha mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma masomo ya mchepuo wa kemia, bailojia na jiografia (CBG) unaendelea, ili utaratibu wa kuukabidhi mwili wa marehemu kwa familia yake yenye makazi yake mkoani Tabora ufanyike.

Juhudi za kumpata Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Kagera, Dk. Thomas Rutachunzibwa, ili kupata ufafanuzi wa kifo hicho chenye mazingira tata hazikufanikiwa kutokana na kuwa nje kiofisi, ingawa Katibu wa hostali hiyo, Justus Benges, alithibitisha tukio hilo kutokea hospitalini hapo.

Alisema mwanafunzi huyo alikuwa akiendelea na huduma ya matibabu kutokana na kugundulika na ugonjwa wa malaria kali.

Mazingira ya kifo cha mwanafunzi huyo yameleta sintofahamu katika jamii ya wakazi wa mji wa Bukoba, huku baadhi  wakihusisha kuwapo huduma mbovu inayotolewa na hositali hiyo pamoja na lugha zisizorafiki kwa wagonjwa.

Imebainika kuwa marehemu tangu alazwe hospitalini hapo, alikuwa akihudumiwa kwa kupelekewa chakula na wanafunzi marafiki zake ambao walikuwa wakitoka shuleni.

chanzo Ippmedia.com