Kurasa

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?

HARAKATI ZA MARAFIKI WA ELIMU NI NINI?
Ni harakati za watu wanaojali na wenye nia ya kuleta mabadiliko katika kuboresha elimu na demokrasia nchini. Harakati hizi zinawaleta pamoja wananchi wanaopenda maendeleo ya elimu na zinawapa fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika masuala yanayohusu elimu .Sera na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES) inasisitiza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wake.Hivyo wananchi wote wanawajibu wa kuchangia uboreshaji wa elimu na demokrasia nchini. kujiunga na harakati hizi za marafiki wa elimu ni bure na hakuna malipo yoyote wasiliana nasi kwa namba 0755 65 00 75 au 0786 65 00 75 au e-mail jmrchrd@yahoo.com tukuunganishe na marafiki wa elimu popote ulipo Tanzania

Jumapili, 1 Juni 2014

Matukio ya elimu katika Picha

TAFAKARI CHUKUA  HATUA YA KULETA MABADILIKO YA ELIMU NCHINI KILA MTOTO APATE ELIMU SAWA ISIYO NA UBAGUZI.


Elimu iwakumbushe vijana faida na hasara za ukoloni ( na Mtemi Gervas Zombwe)

Hoja yangu tangu wiki iliyopita ni kuwakumbusha vijana kufahamu vyema historia yao hasa kuhusu ukoloni na athari zake, ili wajipange vyema kutumia fursa zilizopo na kuendeleza jamii zao.
Nilisema kuwa baada tu ya mkutano wa Berlin uliofanyika Ujerumani mwaka 1885, bara lote la Afrika liliwekwa chini ya utawala wa matapeli wastaarabu, wanaojulikana kama Wazungu kutoka Ulaya.
Mtemi Zombwe
Sababu za kuja kwao na kukalia maeneo yetu, akili zetu, na utamaduni wetu zilidhihirika pale walipoanzisha mifumo yao ya uzalishaji na ukusanyaji wa mapato na malighafi.
Nilitaja baadhi ya athari za ukoloni kuwa ni pamoja na mauaji makubwa, unyanyasaji, kupora utajiri wa Afrika, kugeuza Waafrika kuwa vibarua wa dezo, ukatili, dhuluma, kuvuruga akili za Waafrika na kuua mifumo ya viwanda na teknolojia iliyokuwa imeshamiri katika jamii zetu.
Mbinu walizotumia kufanikisha utii na kuvuruga akili za Waafrika ni kupandikiza dini za kigeni na mafundisho mchanganyiko, huku wakinyang’anya ardhi za Waafrika, kuwaua ama kuwatesa.
Waliendelea kuwapa utumwa wa kiakili na mitazamo duni ili washindwe kufikiri vizuri. Wakawahimiza wawapende maadui zao (ambao ni wao wazungu), wakawahimiza wasamehe saba mara sabini(ili usihesabu viboko ulivyopigwa jana ukiwa uchi).
Waafrika wakaambiwa mila zao ni za kishetani (ili wafuate mila za wazungu wawatawale kirahisi). Na wakacholewa sanamu ya shetani mweusi inayotisha sana. Lakini malaika-wazungu, mitume-wazungu, watakatifu-wote wazungu.
Waafrika wakaogopa! wakaacha mila zao njema wakabeba mzigo wa mila za kishenzi zilizopakwa manukato ya kila aina ili zinukie na zivutie. Hizi ndizo zinazowatesa dada zetu kutamani uzungu kwa kuchubua ngozi zao, kudharau asili yao na hata uumbwaji wao.
Kila cha mzungu ni chema hata kama ni kinyesi na kila cha Mwafrika ni kibaya. Hili likamomonyoa maadili ambayo hadi leo tunayajutia. Wao kicheko!
Hata wasomi wakipelekwa Ulaya kwenda kupata maarifa, hawarudi na maarifa. Wanarudi na utamaduni wa kizungu, ufisadi wa kizungu, dharau za kizungu na ulevi wa kizungu. Maarifa wanayaacha huko huko. Wanarudi vichwa vyeupe vimejaa uzungu-na tamaa ya utajiri pasipo kufanyakazi.
Ndiyo maana kwa sasa tuna utawala wa kizungu, mienendo ya kizungu, lugha za kizungu, dini za kizungu, miujiza ya kizungu, nguo za kizungu, vyombo vya kizungu, na magonjwa ya kizungu.
Pia utamaduni wa kizungu, nyimbo za kizungu, viboko vya kizungu, dawa za kizungu, ufisadi wa kizungu, rushwa ya kizungu, taabu za kizungu, umasikini wa kizungu, Mungu wa kizungu na manabii wa kizungu, matusi ya kizungu, hata uzinzi wa kizungu. Hizi ndizo tunu za ukoloni tulizoachiwa.
Yaliyo mema ya Waafrika yakapotea, yakadharauliwa, yakabezwa na mizigo ya laana ikavijaza vichwa vya Waafrika hao wachache waliokwenda sambamba na mdundo wa mafunzo ya wazungu. Babu zetu wengi walipinga; lakini mwenye nguvu mpishe.
Siyo kila kitu waliachofanya wakoloni ni kibaya kwa Waafrika. La hasha! Yako mambo mengine mazuri kuigwa kwa kuoainisha na mahitaji yetu.
Kwa mfano, jitihada ya kufikiri, kubuni na kufanyakazi kwa bidii ni jambo jema linaloweza kuigwa. Ona kwa sababu ya shida walizopata, walithubutu kuondoka kwao maelfu ya kilomita kuja Afrika ambako hawakukuta pamba wala dhahabu zilizokuwa tayari. Bali wakikuta misitu mikubwa mapori ya kutisha wanyama wengi na udongo wenye rutuba.
Tena mapori mengi Waafrika waliyatumia kama kivuli katika shughuli za unyago. Na misitu mingine ilitumiwa kama sehemu za ibada na matambiko ya jadi.
Lakini wao wakakata nyasi na miti.Wakabuni mashamba na uchimbaji wa madini yaliyokuwa chini ya ardhi, ambayo hata Waafrika wenyewe hatukuyajua kama yapo. Wakathubutu kuchimba na kulima, wakafanikiwa.
Hilo likawezekana wakazoa utajiri mkubwa wakapekeka kwao. Bado huko huko kwao hawakuiacha pamba sebuleni, bali wakabuni mitindo mbali mbali ya usokotaji wa nyuzi ambazo zilikuja kutumiwa kuunda nguo za kila aina zilizouzwa kwao, Asia, Amerika na pia kwetu Afrika.
Mpira uliolimwa Congo wakabuni matairi ya magari wakapata pesa. Shaba waliichukua kwa wingi pale Zambia na Kongo wakabuni nyaya za umeme wakafanikisha umeme ukawaka Waafrika tukafurahia. Je, bila kufikri haya yangewezekana?
Hata wanasayansi wengi waliogundua kanuni na fomula nyingi zilizotumika kutengenezea vitu kama magari, ndege hawakuwa na vyeti vingi, bali kufikiri, kuthubutu na kubuni ndiyo siri ya mafanikio. Walitumia muda wao mwingi kufikiri na kubuni kikamilifu hadi wakaibuka na manufaa hayo makubwa yaliyoibadili dunia hii.
Kina Isaac Newton, Charles Darwin, Plato,Faraday, Garileo, James Watt, Abbot Lambert na wengine wengi ni mifano ya wafikirivu wakubwa ulimwenguni. Je, hawa walikuwa na digrii ngapi hadi wakaweza kufikiri?
Wakati sisi tunaiga uzungu badala ya maarifa na ubunifu, wenzetu Wachina na Wahindi wanaiga maarifa na ubunifu. Wachina wanachukua karatasi wanapaka rangi, wanabuni aina za mikunjo na kukunja karatasi linakuwa ua.
Wanaleta kwetu kama maua ya gharama sana. Tunanunua! Tembelea kwenye masoko duniani kote, bidhaa za Wachina zimetawala masoko, kutokana na kazi za wabunifu na watu wanaothamini kazi na kufikiri.

chanzo. mwananchi

vituko vya elimu kutoka Ruangwa, Lindi

Walimu wa kike wa shule za msingi wilayani Ruangwa mkoani Lindi, wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wa kike kutokana na wanafunzi hao kuwachukulia waume zao kama kulipiza kisasi kwa adhabu wanayopewa na walimu wao.

Kadhalika walimu wa kiume wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wakiume kwa hofu ya kuchomewa nyumba zao moto.

Mwalimu wa kike ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema aliwahi kutoa adhabu kwa mwanafunzi wa darasa la tano ambaye alimchukulia mumewe wa ndoa ili kumkomesha.

Alisema alimuonya mwanafunzi huyo bila mafanikio na kuamua kwenda kwa Afisa wa Ustawi wa Jamii ambaye alisaidia kunusuru ndoa yake.
Alisema kutokana na hali hiyo walimu wote wa kike wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wa kike.

Utafiti wa kihabari uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kuhusu ukatili, unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto, katika Wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi, umebaini kuwepo kwa hali hiyo.
Chama hicho kinafanya utafiti wa kihabari katika wilaya kumi za Tanzania Bara na Zanzibar.

Akiongea na NIPASHE, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkata kata ya Nandagala, Wilaya ya Ruangwa, Ismail Chikandanda, alisema kuna uadui mkubwa kati ya walimu na wazazi kutokana na kutokupenda watoto wao kupewa adhabu.

Chikandanda, alisema katika tukio moja wanafunzi walipigana, mwalimu alimchapa mtoto aliyeanzisha ugomvi lakini baada ya kipindi mwanafunzi alitoka darasani na kwenda kumuita bibi yake ambaye aliita wanakijiji wakiwa na silaha kumtafuta mwalimu aliyemwadhibu mwanafunzi huyo.

Mwalimu wa kiume ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema nyumba ilichomwa moto na wanakijiji baada ya kumwadhibu mwanafunzi wa kiume.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya Msingi Ruangwa, Sharifa Hassan, alisema kuwa tatizo kubwa linalowafanya wanafunzi kuwa na tabia mbaya ni kutokana na ngoma za jando na unyago wanazochezwa na kujiona wako sawa na wakubwa.

Afisa Elimu Kilimo na Ufugaji wa Wilaya ya Ruangwa Yussuf Chilumba, alisema tatizo kubwa ni wazazi kutokuwa na mwamko wa elimu, kwani hata wazazi wao hawakusoma hali inayowafanya kushindwa kusimamia maendeleo yao ya elimu,
“Wazazi wanawaomba wanafunzi wao wasifanye mtihani vizuri ili wasifaulu kwani watawapa shida ya kuwasomesha,” alisema Diwani wa kata ya Nandagala, Wilaya ya Ruangwa, Adrew Chikongwe, alisema kuwa ugomvi kati ya wazazi na walimu ameumaliza na kuanzia wakati huu kutakuwa na amani na hali ya elimu itaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na kuwahimiza walimu kuwafundisha kwa bidii watoto.

chanzo.Ipp media